Thursday 4 October 2012

[wanabidii] MAMBO MUHIMU KWA MTUMIAJI WA KOMPYUTA

Kwa Njia moja au nyingine wewe umeshawahi kukumbwa na uhalifu wa mtandao au kama sio wewe basi mtu wako wa karibu au wote kwa ujumla , uhalifu unaohusisha mtandao umekuwa mkubwa na unapanuka kila siku kutokana na teknologia na vifaa mbalimbali .


Uhalifu wa mtandao unaweza kuzuilika au kupunguzwa endapo kila mtumiaji akiamua kuchukua nafasi yake vizuri haswa kwa kufanya yale muhimu yanayotakiwa ili yeye na wenzake waendelee kuwa salama zaidi .


Hapa chini ni mambo muhimu anayotakiwa kujua mtumiaji wa kompyuta haswa anapochomekwa kompyuta hiyo kwenye mtandao au anapotumia huduma za internet café sehemu mbalimbali .


ANGALIA UNACHOFANYA


Unapotumia kompyuta za internet café au sehemu za watu wengi ambazo zinatumika na kila mtu kuna mambo ya kuangalia .


Mfano angalia kitufe cha Keep me Signed in , Always Sign in , Remember me , Remember password , hakikisha unaondoa alama za pata kwenye vitufe hivyo kama ukiacha hivyo hivyo computer hiyo inaweza kukumbuka jina lako na neno lako la siri muda ujao na matokeo yake ni mtu kuingia kwenye anuani yako na kufanya anachotaka .


Wakati mwingine wahalifu wanaweza kutega program za kurekodi kile mtu anachofanya kwenye kompyuta hiyo , ni vizuri uhakikishe hakuna program hizo na kabla hujaondoka ujenge taratibu za ufuta rekodi za tovuti ulizotembelea na kurasa mbalimbali .


MITANDAO UNAYOHIFADHI TAARIFA ZAKO


Wengi wetu tumekuwa wahanga wa kuacha taarifa au kuweka taarifa hata zile nyeti kwenye mitandao haswa ya kijamii kama facebook , hi5 bila kujua kwamba taarifa hizi zinaweza kutumika dhidi yetu au dhidi ya watu wetu wengine wa karibu ni vizuri tupunguze taarifa au tuwe na taarifa muhimu tu ambazo hazimpi mtu nafasi ya kuchambua mengi na tuwe na utamaduni wa kujua wale tunaowapa taarifa kwa njia hiyo hiyo , Kama unaweka vitu kama CV tafadhali angalia jinsi CV hiyo na taarifa zake inavyotumika kwa wewe kuacha hapo .


UNATEMBELEA MITANDAO SALAMA ?


Kuna watu wanatumiwa linki kwenye barua pepe zao na kutembelea linki hiyo kwa kudhani wanatembelea tovuti ambayo ni sahihi au salama , kama umetumiwa linki ya kutembelea benki yako kwa njia ya mtandao fungua browser yako andika anuani ya benki yako kwa usahihi na ufanye unachotaka , kuna watu wameibiwa fedha au kuhamishiwa fedha zao kwa njia ya mtandao kwa kutembelea tovuti ambazo sio sahihi kwa kuaminishwa ni sahihi .

Hata kama una antivirus ambayo ni nzuri kiasi gani , hii haiwezi kukupa dhamana ya kutembelea anuani yoyote inayokuja kwako .


KUAZIMISHA SIMU ZA KISASA ( smartphones )


Unaweza kuwa hata na mtu wa karibu au rafiki tu akakuomba simu yako mara moja kama vile anapiga , hapo zamani watu walikuwa wanaweza kwenda na simu mbali kujaribu vitu kadhaa , siku hizi anaweza kufungua mtandao Fulani na kukuingizia program ya kurekodi mawasiliano yako ya simu bila ya wewe kujijua na saa nyingine hata kukupiga picha .


KUUZA KOMPYUTA /SIMU BILA KUFUTA TAARIFA


Kwenye miji mikubwa kuna biashara kubwa ya kuuza na kununua laptop , simu , zilizotumika , tujihadhari na biashara hizi bila kununua kifaa hicho kutoka dukani na sio mikononi mwa mtu maana hujui ameitoa wapi na imeingizwa vitu gani kwa ajili ya uhalifu .


Hata wewe mwenyewe unapoamua kuuza simu yako , kamera au laptop hakikisha unafuta taarifa zako zote au kama ulikuwa unahifadhi kwenye kifaa maalumu kama memory kard bora uuze kwa memory card mpya , au harddisk mpya kama ni zile zile zake mtu anaweza kutumia program maalumu kurejesha vile vilivyofutwa na kama ni taarifa zako za siri zinaweza kutumika dhidi yako .


Kama huamini nunua simu iliyotumika , kamera au kompyuta halafu fanya recovery utajionea maajabu ya mwaka .


MATUMIZI YA WIRELESS /BLUETOOTH


Unapokua safarini au sehemu ngeni usiyoijua ni vizuri ukazima wireless , kwenye laptop yako na simu zako , usipofanya hivyo unaweza kuumizwa kama ni uwanja wa ndege , hotelini au sehemu nyingine yoyote  maana kuna watu ambao hii ni kazi yao kutafuta kwenye njia rahisi kuiba , kuharibu au kuleta usumbufu Fulani .


Mfano hai .

Mwaka 2010 majasusi wa mossad walifanikiwa kuingiza virus ya kuharibu mfumo wa mawasiliano katika vinu vya nyuklia kwenye kompyuta ya balozi wa iran nchini uingereza alipokua kwenye mkutano nyeti muda huo wireless yake ilikuwa imewashwa .

 

Hapa Tanzania waziri mmoja aliwahi kufutiwa taarifa yake aliyokua anaenda kuwasilisha umoja wa mataifa huko uswizi baada ya kuwasha laptop yake uwanja wa ndege na kuruhusu uhalifu huo .


NENO LAKO LA SIRI /PWD SI SALAMA TENA


Wengi wetu tumewahi kukumbana na uhalifu wa kubadilishwa neno la siri tukafanikiwa kurudisha wengine hawawezi kabisa na taarifa zao ndio zinakuwa zimeshaishia hapo au kuibiwa kwa njia hiyo .


Wengi wetu tunatumia maneno ya siri yanayofanana na sisi au matumizi ya majina ya ndugu au vitu tunavyopenda na hata miaka ya kuzaliwa hii sio njema mtu anaweza kuotea akafanikiwa kukuingilia tumia maneno magumu na mchanganyiko wa namba na herufi kubwa na ndogo ambazo mtu si rahisi kufikiri au kuhisi .


ANUANI ZA BARUA PEPE ZAKO


Watu wengi bado wanapenda kutumia barua pepe za bure kama yahoo , hotmail , gmail na nyingine nyingi pale zinapovamiwa na kubalilishwa password hawajui wa kumlilia .


Unashauriwa usajili domain name yako rasmi iwe ya jina lako au kampuni yako na control yote inakua juu yako , hata mtu akivamia utakuwa na uwezo wa kurejesha kwa kuwasiliana na msajili tembelea www.tznic.or.tz kwa wale wa Tanzania .


Kama unatumia barua pepe za bure ni vizuri uwe na mbili au 3 za masuala mbalimbali usiweke kila kitu sehemu moja .


USI BOFYE / SHUSHA PROGRAMU USIZOZIJUA


Baadhi yetu tumewahi kwenda kurasa Fulani tukazipenda tukataka kuzishusha kwa ajili ya matumizi yetu , tafadhali omba ushauri kwanza au angalia review za program husika kabla hujaamua kuishusha na kuitumia wewe mwenyewe .


KUCHANGIA MADA KWENYE MITANDAO YA KIJAMII


Tafadhali uwe unachangia kile unachojua au kuwa na taarifa nazo sahihi na katika kufanya hivyo usipenda kushambulia watu na majina yao hata kama unajuana nao , kila unachoandika kinahifadhiwa kinaweza kutumika dhidi yako hata katika vyombo vingine vya dola kama mahakamani kukuhukumu .


MIKUTANO YA KUJUMUIKA ( YA MITANDAO YA KIJAMII )


Ni vizuri kwenda kujumuika kwenye mikutano kama hii ukiwa na taarifa ya kile kinachojadiliwa au kuongelewa na pia ujue angalau watu wengine wanaoenda , siku hizi zimeibuka tabia za ajabu za visasi , ubakaji , ulevi na ugomvi mbalimbali ambao chanzo chake ni michango kwenye mtandao ya kijamii .


UTUMIAJI WA SIMU KWENYE MTANDAO


Hakuna usalama wa asilimia kubwa pale unapotumia simu yako kwenye huduma mbalimbali za mitandao kama kununua bidhaa au kuangalia vitu kama gari etc , ni bora zaidi ukitumia kompyuta usalam unaweza kua mkubwa zaidi .


BORESHA KOMPYUTA YAKO KWA KUFANYA UPDATES


Kama unatumia antivirus au program yoyote ya ulinzi hakikisha iko salama , inafanya kazi saa zote na iko updated ili kuweza kujikinga na majanga mengi yanayoweza kutokea kwa kudharau program hizi za ulinzi kwa ajili yako .


Utumiaji wa program hizi za ulinzi kama antivirus na firewall sio kete ya kufanya chochote na kompyuta yako ,wakati mwingine zinaweza kushindwa kutekeleza baadhi ya vitu .


SERA / MIONGOZO YA MATUMIZI YA VIFAA VYA MAWASILIANO


Kampuni nyingi na mashirika hayana sera ya matumizi ya vifaa vya mawasiliano , matokeo yake ni mfanyakazi kutumia vifaa hivi vile anavyotaka , kutembelea tovuti yoyote anayotaka , kushusha chochote anachotaka na cha ukubwa wowote , kuandika chochote kwenye mitandao ya kijamii na mengine mengi .


Sera ya matumizi ni muhimu kwa maslahi ya kampuni , shirika , mtu binafsi na hata familia .


HAPA SI MWISHO , JISOMEE ZAIDI UELIMIKE UFAIDIKE

Katika mitandao ya kijamii kuna fursa nyingi sana za kuweza kumnyanyua mtu kibiashara , kielimu , taaluma , kujuana na watu na ndugu , tutumie fursa hizi kwa manufaa na sio kwa njia ya kuharibu kwa kunyima wenzetu fursa mbalimbali zilizopo .


Unapopata fursa nawe andika tuma kwenye mitandao ya kijamii watu wasome , wafaidike au wajadili .

 

YONA F MARO

10/5/2012 3:55 AM

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

0 comments:

Post a Comment