Watanzania wenzangu, mwaka wa maamuzi umefika tena. Mwaka 2015, ni mwaka wa kufanya maamuzi makubwa ambayo yatakayoamua mustakabali wa nchi kwa miaka mingine mitano. Umefika wakati wa kujiuliza maswali muhimu sana na kutumia akili zetu na ufahamu wetu katika kufanya maamuzi. Tuachane na utamaduni wa kufanya mambo kwa mazoea au kwa ushabiki. Ni wakati sasa wa kujihoji na kujiuliza hivi tunahitaji nini? Tunataka kujenga Tanzania ya namna gani? Ni zipi changamoto na matatizo yanayotukabili kama Taifa? Ni yapi yanayokwamisha juhudi zetu katika kujiletea maendeleo na ustawi? Je tuna majibu? Ni chama kipi kina majibu ya matatizo yanayotukabili? Ni mgombea yupi ataweza kukabiliana na changamoto na matatizo yanayotukabili? Haya na mengine ni baadhi tu ya maswali ambayo kila mpiga kura anawajibika kujiuliza.
Watanzania hatuna budi kufahamu kuwa, toka uhuru tumekuwa tukipigana na maadui wanne. Maadui hawa ni ujinga, umaskini, maradhi, na rushwa. Ni hakika kuwa, pamoja na tambo nyingi sana, bado hatujaweza kushinda vita ya kupambana na maadui hawa. Na katika maeneo mengi tumekuwa tukipoteza hata yale machache ambayo tulianza kupiga hatua nzuri. Miaka 54 tumeshindwa kuwatokomeza maadui hawa. Katika miaka yote hii nchi yetu imekuwa chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) – TANU na ASP toka 1961 na CCM baada ya mwaka 1977. Katika kipindi chote hiki tumeona sera, mikakati, program ya kuondoa umaskni. Ni ukweli mchungu kuwa sera hizi na mikakati hii imeshindwa kuwaondoa maadui hawa. Tanzania imeshindwa kuondoa umaskni. Ukweli unabaki kuwa, Tanzania ni nchi maskini licha ya tambo za kukua kwa pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 7 tangu mwaka 2000.
Hali ya maendeleo ya Watanzania hadi sasa siyo ya kuridhisha. Ushahidi mzuri wa jambo hili ni ule unaotolewa na kipimo cha Maendeleo ya Binadamu (HDI). Kipimo cha HDI, hupima maendeleo ya binadamu katika nchi kwa kuzingatia mkusanyiko wa vigezo vya umri wa kuishi, elimu na kipato, kipimo cha chini huwa ni 0 na cha juu ni 1. Kwa kipimo cha 0.488, Tanzania imeshuka kufikia daraja la chini la nchi zenye kiwango kidogo zaidi cha maendeleo ya binadamu. Ipo nafasi ya 159 kati ya 187 duniani. Ripoti ya UNDP kuhusu Maendeleo ya Binadamu Duniani ya mwaka 2014 imeiweka Tanzania katika kundi la nchi zenye maendeleo ya binadamu ya kiwango cha chini. Kinachoshitusha ni kushuka kwa nafasi saba zaidi katika Kipimo cha HDI, ukilinganisha na mwaka 2013.
Katika ngazi ya mikoa, kipimo cha HDI kinaonyesha tofauti kubwa ya viwango vya maendeleo ya binadamu ndani ya Tanzania. Kushuka kwa nafasi ya maendeleo ya binadamu nchini Tanzania, kumethibitishwa pia na Kipimo cha Umaskini kwa Kutumia Vigezo Mbalimbali (MPI). Kipimo cha umaskini cha MPI ni kipimo cha maendeleo ya binadamu ambacho hupima kwa mapana ukosefu wa mahitaji muhimu kwa watu na kaya zao.
Ni wazi kuwa licha ya Ongezeko la Pato la Taifa kwa kiwango cha asilimia 7 katika muongo uliopita, kiwango cha umaskini kimepungua kidogo sana kutoka asilimia 33.3 mwaka 2007 hadi asilimia 28.2 mwaka 2012. Picha halisi ya umaskini nchini Tanzania inathibitishwa na hali ya umaskini inayoonyesha viwango vya chini vya maisha katika kaya nyingi. Pamoja na hilo, ni ukweli unaojulikana sana kuwa umaskini nchini Tanzania umekithiri huko vijijini ambapo viwango vya maisha ni vya chini ukilinganisha na kaya za mijini. Kwa mfano, wakati utumiaji wa umeme kwa ajili ya mwanga umeongezeka mara mbili kutoka asilimia 10 mwaka 2002 hadi asilimia 21 mwaka 2012, matumizi katika maeneo ya vijijini ni asilimia 8 (ukilinganisha na asilimia 49 katika maeneo ya mijini). Zaidi ya hayo, asilimia 67 ya kaya nchini Tanzania zinaishi katika makazi yenye sakafu za udongo, mchanga au kinyesi cha ng'ombe, wakati asilimia 63 hazina fursa ya kupata maji ya bomba kama chanzo kikuu cha maji ya kunywa. Vilevile, matumizi ya kuni kama nishati ya kupikia na ukosefu wa huduma za usafi kwa watu walio wengi bado ni tatizo. utapiamlo unaonekana kuwa miongoni mwa tishio kubwa kwa maendeleo ya binadamu nchini Tanzania. Upatikanaji wa vyakula muhimu na vyenye virutubisho vya kutosha haujaongezeka tangu mwaka 1997, na utapiamlo uliokithiri unakadiriwa kuwa ni sababu kubwa ya zaidi ya theluthi ya vifo vya watoto chini ya umri wa miaka 5.
Hali ya elimu nchini Tanzania bado hairidhishi; ubora wa elimu inayotolewa nchini Tanzania ni wa kiwango cha chini. Zaidi ya hayo, sekta ya elimu nchini inakabiliwa na ongezeko la wanafunzi wanaoacha shule, umahiri mdogo na kukosekana kwa ari na motisha kwa walimu. Ijapokuwa umma ulioelimishwa vema ni kichocheo cha mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya binadamu, ubora wa elimu nchini Tanzania hauridhishi. Wale wanaojitapa kuwa uchumi umekuwa ukiendelea kukuwa kwa zaidi ya asilimia 7 tangu mwaka 2000, hawasemi ni kwa nini kukua huko kwa uchumi hakuendi sambamba na kupungua kwa umaskini wa kipato?
Ufisadi na rushwa pia ni maadui ambao wameendelea kuliandama Taifa letu. Matumizi mabaya ya madaraka, uzembe, kutowajibika na kulindana. Haya pia ni madhila ambayo yameendelea kulidhoofisha Taifa letu. Tanzania ni nchi ambayo bado inanuka rushwa. Katika medani za kimataifa bado hatujaweza kufanya vizuri sana vita vya kupambana na rushwa. Matumizi mabaya ya fedha za umma yanadhihirika katika ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kila mwaka. Wizi wa fedha katika Halmashauri ni jambo la kawaida sasa. Ulipaji wa mishahara kwa wafanyakazi hewa ni jambo ambalo serikali ya CCM imeshindwa kulipatia ufumbuzi.
Kama Taifa tumeshindwa kutumia raslimali ambazo tumejaaliwa na Mola kwa faida ya Watanzania wote. Madini, gas, mbunga za wanyama na vivutio mbalimbali, bandari, misitu, bahari, mito na ardhi yenye rutuba, hivi vyote vimekuwa havina mchango wowote katika kuinua hali za wananchi ili waondokane na umaskini uliokithiri. Migogoro ya ardhi na mapigano kati ya wakulima na wafugaji na wananchi na wawekezaji limekuwa ni tatizo lisilokuwa na majibu. Viwanda vilivyojengwa wakati wa Baba wa Taifa vimekufa ama kuuzwa. Tatizo la ajira limezidi kuongezeka. Vijana wanahangaika mijini wakiwa hawana shughuli za kufanya. Hizi ni baadhi tu ya changamoto chache ambazo zinatukabli kama Taifa.
Kwa miaka 54 CCM walipewa ridhaa ya kukabiliana na changamoto hizi na ni wazi sasa kuwa wameshindwa kuwa na sera, mipango na mikakati ya kuweza kuondoa au kupunguza changamoto hizi. Watanzania, changamoto hizi na nyingine ambazo sikuzitaja, zinahitaji mabadiliko makubwa (radical reforms). Mabadiliko makubwa hayawezi kutoka ndani ya CCM. Mabadiliko makubwa yatatoka nje ya CCM. Watanzania, tufuatane pamoja ili tuweze kudurusu sababu ambazo zinathibitisha kuwa mabadiliko ya msingi hayawezi kutoka ndani ya CCM.
Chama chochote cha siasa duniani kilichokaa madarakani kwa miongo na karne nyingi huwa na sifa au maradhi yafuatayo; Kwanza, chama kama CCM huandamwa na saratani ya rushwa ambayo huenea kila mahali, katika ngazi zote za chama, na hata serikalini na hivyo kuikomesha ni ndoto. Njia pekee ya kukomesha rushwa na ufisadi ni kukipumzisha chama cha namna hii. Rushwa inakuwa ni sehemu ya maisha na jambo la kawaida. Hilo linadhihirika katika chaguzi zote za CCM za ndani ambazo zimekuwa zikifanyika katika miaka yote. Vyama vya namna hii, hubweteka, hujenga kiburi, jeuri na dharau na viongozi wake huamini kuwa wao ndio wanajua kila kitu, wao ndio wana akili sana, wao ndio wana hati miliki ya kutawala, wao ndio wapo sahihi na mikakati yao ni mizuri na wao hawafanyi makosa. Hali hii huwafanya wasiweze kujifunza aidha kutokana na makosa yao wao wenyewe au kujifunza kutokana na yale mazuri kutoka kwa wengine. Nafasi ya kujifunza kwao huwa hakuna na huendelea kufanya vile vile walivyokuwa wakifanya kwa miaka 54 na kutegemea matokeo tofauti!
Mathalani, jeuri hii ndio iliyowafanya wapitishe katiba pendekezwa wao wenyewe bila kujali kuwa vyama vya upinzani ni muhimu vishiriki ili viweze kufikisha sauti za wale ambao si wanachama wa CCM. Kwa jeuri waliamua kuweka kando mawazo ya wananchi yaliyopendekezwa katika Rasimu ya pili ya Tume ya Mzee Warioba. Kwa jeuri bila kujali muafaka na mazungumzo walipitisha miswada ambayo gesi na mafuta na ule wa makosa ya mtandaoni bila kujali mawazo ya wadau na wananchi ambao si wana CCM. Hizo ni sifa za chama ambacho kimekaa madarakani kwa muda mrefu.
Chama kilichokaa madarakani kwa muda mrefu hujenga tabia ya kulindana, upendeleo, majungu, fitna na kuendesha siasa za makundi na kuchafuana. Kwao wao shabaha yao si tena kutatua matatizo ya wananchi, bali kupata uongozi ili kuweza kumiliki raslimali na kuweza kupata kandarasi, mikataba ya kujipatia fedha na kipato. Haya yote yanadhihirika waziwazi ndani ya CCM na hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi. Chama cha namna hii hukabiliwa na uongozi mbovu ambao hautumii vikao kujadili masuala kwa uwazi ya kuyapatia majibu na ufumbuzi.
Chama kilichokaa madarakani kwa muda mrefu, hugubikwa na kadhi mbalimbali kama ambazo tumeziona katika Taifa letu. Hujenga matabaka na wateule ambao wao ndio hushika nyadhifa na kuwarithisha watoto wao. Chama cha namna hii huwa karibu sana na matajiri na kuwasahau masikini. Wale wenye kufanya makosa hulindwa (impunity) na kusafishwa na hakuna matokeo yoyote kwa vitendo vibaya wanavyovifanya. Chama cha namna hii hukosa uwajibikaji, ufanisi na hugubikwa na uzembe na urasimu ambao huwaletea adha na tabu kubwa wananchi.
Chama kilichokaa madarakani kwa muda mrefu, hakiwezi kurudi katika masuala ya msingi na kujiuliza ni wapi tunakosea, wapi tujirekebishe, wao huendelea kutafuta mbinu za kuendelea kukaa madarakani kwa gharama yoyote ile hata kama ni kwa wananchi kuendelea kuishi katika umaskini uliokithiri.
Vyama vyote vya siasa vilivyowahi kukaa madarakani kwa muda mrefu sana husumbuliwa na maradhi haya. Chama cha Wingereza cha Consertive kilichokuwa kikiongozwa na Margaret Thatcher na John Major, baada ya kukaa madarakani kwa muda mrefu sana, kilifikia hatua kilibweteka na kuwa na jeuri. Margaret Thatcher, Waziri Mkuu aliyekaa madarakani muda mrefu sana aliwahi kuwaambia Waingereza hakuna kitu kinachoitwa jamii. Kauli hii haikuwapendeza wengi sana. Mwaka 2002, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Conservative, Theresa May akiwahutubia wanachama wenzake, alisema ni muhimu Conservative ikafanya juhudi za kubadilika ili kisiwe chama kinachoenekana kina jeuri (nasty party). Chama cha KANU nchini Kenya kilifikia hatua ya kuwa na uozo, ubabe na kila aina ya madhila. Hivyo basi, ni kujidanganya kufikiri kuwa unaweza kuleta mabadiliko ndani ya mfumo wa chama kilichokaa madarakani kwa miongo mingi sana. Njia pekee ya kukisaidia chama cha namna hii ili kiweze kujiuliza maswali ya msingi na kurudi katika shabaha za msingi ni kukipumzisha ili kiwe chama cha upinzani. Hakuna namna nyingine.
Watanzania, tuna wajibu wa kihistoria, wa kuleta mabadiliko katika nchi yetu. Kuleta mabadiliko ya kiutawala, kuleta mapindinduzi ya kiuchumi, kuboresha elimu, afya, miundo mbinu, n.k. Hatuwezi kuyafanya haya bila kufanya mabadiliko makubwa, tunahitaji sera mpya, fikra mpya, chama kipya na namna mpya ya kufanya na kuendesha mambo yetu. Hili haliwezi kutoka ndani ya CCM. Wakati ni huu, fikiria na timiza wajibu wako.
0 comments:
Post a Comment