Monday, 31 August 2015

[wanabidii] ‘Mbwambo, simamia ukweli hata ukibaki peke yako’

'Mbwambo, simamia ukweli hata ukibaki peke yako'

Johnson Mbwambo

Ndugu Mbwambo, nashukuru uliyoyasema kuhusu Edward Lowassa kwamba hafai kuwa rais wa nchi hii, na Watanzania wasitarajie mabadiliko yoyote makubwa chanya kama watamchagua kuwa rais.
Kila anayejaribu kujitokeza kuonyesha mapungufu ya uadilifu ya Lowassa anaambiwa kuwa ana 'chuki binafsi' naye kama wewe unavyoambiwa hivi sasa. Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na mimi hakuna aliyekuwa na tatizo au chuki binafsi na Lowassa pale Dodoma mwaka 1995 jina lake lilipokataliwa kugombea urais.

Mwalimu Nyerere na Mzee Ali Hassan Mwinyi wote walimstahi sana Edward Lowassa wakati ule. Hata mimi niliyopata kuandika, mwanzoni mwa mwaka huu, kwenye gazeti lenu la Raia Mwema kuhusu Edward Lowassa nilijitahidi sana kutoweka yote hadharani. Kwa hakika, nilishangaa sana hivi karibuni kwa Mzee Ngombale sasa kuwa mtetezi mkubwa wa Edward Lowassa; maana walikosana naye baada ya kumtuhumu kwa ufisadi, na Mwalimu Nyerere ndiye aliyewasuluhisha. Huo ndio ukweli ambao wengi hawaujui.

Lakini Mbwambo usikate tamaa. Rais wa zamani wa Marekani, Abraham Lincoln, aliwahi kusakamwa na kutengwa kwa sababu ya msimamo wake. Lakini yeye aliwajibu waliomtenga kwa kusema hivi: If there is anything that links the human with divine it is the courage to stand by a principle when everbody reject it.

Kwa hiyo Mbwambo, usijali kuandamwa. Simamia ukweli hata ukibaki mwandishi peke yako anayeuona ukweli kuhusu Lowassa. (Samwel Kasori – Katibu Myeka wa zamani wa Nyerere - simu 0716-267879). 'Hatutafuti rais mtakatifu – hayupo'

Bw. Mbwambo, nikiri wazi mimi ni mmoja wa wasomaji wa makala zako kila unapoandika, na nakubaliana na mengi usemayo kama sio yote. Hata sasa nakubaliana na mawazo yako kuhusu Lowassa kwa kiasi fulani ila nakushauri epuka kuwa hakimu.

Nimepata bahati kutembelea nchi nyingi za Afrika na Ulaya lakini nimeishi zaidi Angola. Najua siasa za Angola sio kwa kuambiwa bali kwa kujionea mwenyewe. Wengi wenu haswa nje ya Angola mliaminishwa sana kuwa Savimbi alikuwa ndiye tatizo, na haswa kupitia vyombo vya habari ambavyo kimsingi vinamilikiwa na serikali. Mpaka sasa Angola vyombo vya habari ni vya serikali isipokuwa radio moja tu ya Kanisa Katoliki ambayo kimsingi ni serikali tu kwa Angola.
Savimbi kuwa mbaya ni nusu ya ukweli kwa sababu Dos Santos mwenyewe amewanyamazisha na ameua wengi waliotofautiana naye nchini Angola, na hicho ndicho chanzo cha uhasama kati yao kwa muda mrefu ingawa vyombo vya habari vinafunika ukweli huo.

Do Santos na binti yake Isabela sasa ni matajiri kweli kweli (utajiri haramu wakati wananchi ni masikini wakutupwa). Nikirejea ya hapa nchini, na haswa kipindi hiki cha uchaguzi mkuu niseme kwamba huwa siweki tumaini kwa mgombea yeyote. Ukweli ni kwamba; kwanza, Afrika hatuna viongozi - tuna watawala. Pili, Afrika watawala wanapenda siasa lakini hawafanyi siasa bali ni ujanja, wizi, ubinafsi na ulafi tu. Hata Tanzania ni hivyo hivyo.

Kwa muda mrefu tumeaminishwa kuwa Lowasa ndiye fisadi. Yamesemwa mengi kuhusu yeye lakini hakuna hata mmoja ambaye ameweza kusimama akaleta ushahidi. Ni simulizi, ni ngonjera na siasa uchwara. Wakati umefika tuweke maneno katika vitendo. Watanzania tuamke. Tuwawajibishe hawa watawala ili kuua mfumo wote mbovu wa kifisadi ili tupate viongozi badala ya watawala. Hili litawezekana tu nje ya CCM.

Mbwambo, Hatutafuti rais mtakatifu - hayupo. Maana kutaka hilo ni mpaka Yesu arudi. Hata njia ya ukombozi aliyopitia Mandela, Nyerere na Nkrumah haikuwa nyofu (takatifu). Yako mengine ya ovyo yalifanyika sembuse ya Lowassa.
(Davis Lewis Msechu – dmsechu@gmail.com (link sends e-mail)). Lowassa 'unpredictable' Magufuli 'unreliable'

Shikamoo Mzee Mbwambo. Nimetoka kusoma makala yako muda si mrefu. Nimeielewa. Na hasa katika suala la kutokata tamaa. Leo naomba nitoe rai kwa vyombo vya habari hasa vya redio na luninga. Kwa mtazamo wangu, vyama vyetu vimetuwekea mbele yetu wagombea urais ambao si bora. Binafsi ninawaweka katika makundi mawili ya 'unpredictable' – Edward Lowassa na 'unreliable' John Magufuli.

Sasa basi, pamoja na hali hiyo, kuna msemo mmoja nilijifunza katika moja ya tamthiliya za kizungu kuwa no matter what, the future is ahead of us'. Naamini hii ndo hali tuliyonayo Watanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.

Kuwa haijalishi ni watu gani wametuwekea hapo mbele ili mmojawao tumchague kuwa rais wetu ajaye, na bila shaka mmoja wao ndiye, bado the future is ahead of us. Tukisema tususe au tuchague kwa mantiki ya 'potelea mbali' au kufuata mkumbo, tutaumia wenyewe mbeleni. Tukikata tamaa bado the future is ahead of us; kwa maana kwamba bado uchaguzi utafanyika na mmojawao atakuwa rais.

Na hapo ndipo ninapogeukia vyombo vya habari kwamba vitusaidie wapigakura kumfahamu mgombea aliye nafuu kidogo kati ya hao wawili. Sisemi kwamba vitushawishi tumchague nani. La hasha. Ninasema vifanye japo mambo haya mawili kwa ajili na kwa niaba ya Watanzania. La kwanza ni vyombo vya habari viwahoji hawa wagombea. Viwaulize maswali magumu juu ya mustakabali wa nchi. Maono yao juu ya nchi yetu na namna watakavyotekeleza hayo maono lazima vifahamike. Waulizwe juu ya doubts zozote zinazowazunguka na wanaowazunguka.

Jambo la pili ambalo vyombo vya habari vinaweza kulifanya ni kutujuza juu ya wagombea wetu. Ukweli ni kwamba pamoja na mihemuko yote iliyopo sasa, sisi wananchi hatuwajui kiundani wagombea hao wawili. Vyombo vya habari vitusaidie katika hilo na vitakuwa vimetekeleza wajibu wao. Nitoe mfano wa huyu mgombea anayevutia mashabiki wengi – Edward Lowassa. Nasema ni 'unpredictable' (hatabiriki). Katika miezi mitatu hii amekuwa akitoa kauli hii na kufanya tofauti.

Kwa mfano, aliahidi angeongelea kuhusu Richmond kwenye mkutano wake wa Arusha lakini hakufanya hivyo. Akasema hataondoka CCM hata iweje lakini akahama. Tutamuamini vipi katika yale anayo – na- atakayotuambia? Tuamini vipi katika ahadi zake au tutarajie kurukwa na kugeukwa akishakuwa rais?

Magufuli naye ni 'unreliable' (haaminiki). Simuoni kama ni mtu mwenye uwezo wa kubadili hali ndani na nje ya CCM. Kwake chama kwanza kama alivyosema wakati wa uteuzi wake. Alisahau kuwa 'nchi kwanza' na chama baadaye.

Kwa ufupi, vyombo vya habari badala ya kushabikia tu, viwamulike hawa wagombea wawili ipaswavyo ili tuwafahamu na kupiga kura kumchagua ambaye ni nafuu kidogo tukiwa na uelewa wa kutosha juu yao. (Condrad Mariki - 0753 423264)


Ya Dk. Slaa na Profesa Lipumba

Ndugu Mbwambo, nimesoma makala yako moja hivi karibuni kwa makini. Pamoja na umahiri wa uandishi wako, kuna mambo kadhaa ambayo nadhani hujayazingatia. Jambo la kwanza aliyesema dhamira inamsuta ni Lipumba peke yake, kwa Dk. Slaa hakuna anayejua anafikiri nini. Pili, ukumbuke kuwa hawa wawili wote ni watu waliokuwa wanautamani sana urais na nadhani walijiaminisha kuwa hakuna mwingine isipokuwa wao.

Sasa, wao ni binadamu. Huenda wameumizwa na kukosa kwao urais ndiyo maana wameumia kwa ujio wa Edward Lowassa katika Ukawa. jambo jingine kubwa ninalowashangaa ni wao kushiriki kwenye maamuzi na kura ikapigwa halafu wanajitenga na maamuzi ya vikao walivyoshiriki! Hapa wameonyesha udhaifu mkubwa sana.

Kwa waungwana mnapokubalina kwenye kikao mkitoka then you have to surrender your opinion. Kama kwa mfano Slaa angetaka kuwa na mawazo yake angesusia kikao ili kumbukumbu iwe sahihi. Mpaka nitakapoelewa vinginevyo, hao wawili mimi nawaona kama wasaliti wa mapambano. Waachwe waende wajifie wenyewe kisiasa.

(Mathias Mbalinga)

Maskini huhamaki tajiri akimkaribia
Ndugu Mbwambo, nimesoma makala yako kwenye Raia Mwema toleo lililopita nikakumbuka kitu fulani. Ilitokea zamani mfalme Ujerumani akitoa nishani ya uvumbuzi muhimu wa injini ya gari aligundua kuwa anayeipokea kumbe hakuwa mjerumani bali ni mfaransa aliyeishi huko.

Mfalme yule hakuamini, lakini baadaye wajerumani walifaidika mno na uvumbuzi huo. Kwa hiyo, ni sahihi ulichoandika jana. Wapiga kura wengi bado watazingatia ukanda wakati wa kupiga kura badala ya kuzingatia maslahi mapana ya taifa (kama kweli yapo).


Ndugu yangu Mbwambo, bila kuwa mnafiki, ni ukweli usiofichika kuwa Watanzania na Waafrika kwa ujumla bado tu wapuuzi. Na haipo njia ya kukwepa bara letu kukaliwa na wazungu kiuchumi. Tusali tusisali haitasaidia.
Na usisahau pia kwamba maskini anakuwa na hamaki tu pale anapokuwa karibu na mwenye mali; vinginevyo umaskini ni hali iliyotulia – haina msukosuko (poverty is a stable state of life on its own.

Kwa maana hiyo, wewe Mbwambo unaweza kwenda kijijini na kuwahubiria wanavijiji juu ya umaskini mkubwa unaowakabili na jinsi ya kujitoa humo lakini wao watakukodolea tu macho na kukushangaa! Ndo maana wanamfuata Lowassa kwa maelfu bila kujijua, na hata uandike nini kuwafumbua macho hawatajifunza kitu!
(Msomaji wako - Simu 0754 – 898227)

Kama Lowassa ni 'mwarobaini' Monduli kafanya nini?
Na leo tena kaka Mbwambo nimekusoma. Na hongera zako nyingi. Wanaokutukana na kukulalamikia wameshindwa kuwaza. Mie niliwaza hata kabla ya Lowassa kwenda Chadema na nikasema hafai kuwa rais wetu mpya.
Ukweli ni kwamba hana maono na hana hata msingi mmoja anaousimamia. Historia haimuonyeshi kuwa ni nabii ingawa watu wamempa 'unabii' na amekuwa ni ideology kwa sasa.

Lakini hawa Watanzania wanaomshabikia Lowassa wamekuwa sawa na wale watu wazima wanaohubiriwa na mchungaji mmoja huko Afrika Kusini na bila kufikiri kukubali kula majani, nyoka, na hata kuvua nguo! Hawana tofauti na wafuasi wa Kibwetere waliochomwa moto na kufia kanisani.

Hivi karibuni niliwauliza watu wanaomshabikia swali hili: Lowassa amefanya nini kwao Monduli? Je, Monduli kajenga kiwanda cha nyama? Kajenga kiwanda cha maziwa au jibini? Jibu ni 'hapana'.
Wamasai wa Monduli ni wafugaji; je amewabadilisha kiasi cha kuwafanya wafuate ufugaji wa kisasa? Jibu pia ni 'hapana'. Isitoshe, Wamasai wanalalamika kila siku kuhusu matatizo ya ardhi yanayowakabili; Je, Lowassa amewasaidia vipi katika suala hilo? Hata hapa jibu ni 'hajawasaidia'.

Lowassa anadai eti yeye ni mtu wa kuleta 'mabadiliko'. Si angeanza kwanza 'kuibadili' Monduli yake kabla 'hajaibadili' Tanzania nzima? Ukweli ni kwamba hata alipokuwa waziri wa ardhi aligawa viwanja kwa rafiki zake akina Ladwa wakajenga hoteli ya Golden Tulip. Ni kipindi hicho cha uwaziri wake pia kipande cha Gymkhana kilimegwa na kujengwa Serena Hotel. Je, alishughulikia migogoro ya ardhi ya wananchi wa kawaida? La hasha.

Kuhusu Mchakato wa Katiba, Lowassa wala hakuwahi hata kufungua mdomo wake kueleza msimamo wake ndani au nje ya Bunge. Leo anaungana na timu ya Katiba (Ukawa) ambayo hata, nina uhakika, hajui walitaka nini! Lowassa yuko busy kupanga mikakati ya kuwa rais na siyo kuielewa na kuiendeleza nchi hii Wanaomzunguka wanazungumzia sera zake zipi? Kwamba wakiingia ikulu watafanya nini? Nijuavyo, maswahiba wake tayari wameshajigawia madaraka na miradi kana kwamba tayari wameshinda uchaguzi!

Inasikitisha kwamba Watanzania (kwa wiki hizi nne) wameshindwa kuyaona yote hayo, na wanamshabikia tu kwa kufuata mkumbo kama vile hawana akili nzuri. Lakini nina hakika watayagundua makosa yao hayo huko mbele ya safari. Usichoke Mbwambo kuwaambia ukweli.
(Aloys Bahebe - aloys@aloysassociates.com (link sends e-mail))

Chadema unafiki mbele kwa mbele.
Mbwambo, wewe ni mwandishi makini na mwandishi huru, na kwa sasa mmebakia wachache sana katika nchi yetu hii. Kila ninaposoma makala zako naona mtu mwenye fikra, mtu huru, mtu msema ukweli na mchambuzi makini.
Kuna wasiopendezwa na hayo unayoyaandika, lakini ukweli ni kwamba baadhi ya viongozi wa juu wa Chadema ni wanafiki na wasaliti wakubwa. Itakuwa vigumu kuendelea kuwaamini watu wa aina hiyo hata baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba kumalizika. Hisia zangu ni kwamba chama hiki kitasambaratika baada ya matokeo ya Oktoba 25.

Nakutia moyo uendelee kuwafumbua macho Watanzania hata kama baadhi hawapendi unachokiandika. Kuna waandishi, kupitia safu zao, niliwaamini kuwa ni watu makini na huru, lakini baada ya kuona wanagombea ubunge na misimamo yao imebadilika, nimepoteza imani nao. Sasa mmebaki wachache mnaoaminika - kazeni buti tusimipoteze na nyinyi.
(Padri Daudi Andrea Msofe – Same. Simu 0756 – 449929).

*Ndugu zangu, imenipendeza toleo hili kuchangia nanyi mawazo haya ya baadhi ya wasomaji wangu kama walivyonitumia kwenye sms na emails zao juu ya niliyokuwa ninayaandika kwenye safu hii hivi karibuni kuhusu ugombea urais wa Edward Lowassa. Yatafakarini.

Chanzo Raia Mwema, Toleo la 420 ,28 Aug 2015

0 comments:

Post a Comment