Monday, 31 August 2015

[wanabidii] Kweli fedha fedhea, Kaka yangu Mpendazoe leo anaposahau maandishi yake wakati wasomaji hatujasahau

Hatutaki mgombea urais anayekimbilia Ikulu

Fred Mpendazoe
Toleo la 402
22 Apr 2015
 
PLATO alikuwa kati ya wanafalsafa muhimu zaidi huko Ugiriki ya kale. Plato aliishi kati ya mwaka 427 hadi 447 KK. Alikuwa mwanafunzi wa Socrates na mwalimu wa Aristotle. Alibuni mawazo mengi ambayo yana maana hadi leo. Moja ya falsafa ya Plato ni kwamba mafilosofa ndio wanaofaa kuwa watawala wa nchi, maana wana sifa mbili muhimu. Kwanza wana uwezo wa kutawala na pili hawapendi kutawala.

Ni sheria ya mafilosofa kutawala kwa zamu . Na mtu zamu yake ya kutawala ikiisha, atafurahi sana kurudia shughuli zake za kifalsafa ambazo hasa ndizo anazipenda. Hivyo, Plato aliamini kwamba, zipo sifa kuu mbili au vigezo vya kumpata kiongozi awe rais, mbunge, diwani au nafasi yoyote ya kuchaguliwa.

Sifa ya kwanza ni lazima tunayetaka kumpa uongozi awe na uwezo wa kuongoza. Na sifa ya pili, mtu huyo sharti awe hataki kabisa kuwa rais, anatambua kuongoza watu ni utumishi na huyo ndiye watu wamfuate, wamshauri, wamwombe, ndipo atakuwa kiongozi bora, kwani atawaheshimu waliomwomba awaongoze. Na ataheshimu na kuiogopa dhamana aliyokabidhiwa.

Mwalimu Nyerere, katika kitabu chake, Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania, anasema wanasiasa kwa kawaida hupenda kutawala hata kama hawana uwezo wa kutawala. Kwa hiyo, wako tayari hata kuhonga ili wachaguliwe kuwa watawala au wako tayari kuchakachua kura ili watangazwe washindi na wakishachaguliwa au kutangazwa washindi hawatoki bila kulazimishwa.

Wanaotaka sana uongozi kwa gharama yoyote mara nyingi ni wanasiasa ambao hawana uwezo wa kuongoza. Hata hivyo, wapo wanasiasa wanaoutamani uongozi kisha wakawa viongozi bora, kama aliyekuwa Rais wa Marekani, hayati John F Kennedy, lakini nitahadharishe kuwa watu wa aina hiyo ni adimu sana duniani.
Kuna wakati Mwalimu Nyerere alikaririwa akisema kwamba alikuwa mwalimu taaluma aliyoipenda kwa kuichagua mwenyewe , lakini aliingia kwenye siasa kama ajali.

Hakutaka kuwa rais. Ilikuwa ni bahati mbaya kwake.
Katika makala yangu ya tarehe 15 April 22015 kwenye gazeti la Raia Mwema niliandika juu ya nini nilichoona kilikuwa ni chanzo cha nchi yetu kuyumba. Imebaki miezi takribani sita watanzania watachagua viongozi wao akiwemo Rais. Wananchi wana jukumu la kwanza kuhakikisha wanapata viongozi wazuri.

Hivyo ni mhimu wananchi waelimishwe ili waweze kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuongoza na wanaofaa. Katika makala hii ninapenda kutoa ushauri wangu kwa Watanzania tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 sifa muhimu wanazotakiwa wawe nazo wanaofaa kuwa viongozi. Ushauri wangu unaegemea katika falfasa ya Plato.

Watanzania mnashuhudia minyukano ya kuwania kuteuliwa kugombea nafasi ya urais ndani ya CCM na mbinu chafu zinazotumika leo kuelekea uchaguzi mkuu mwaka wa Oktoba 2015 ambazo Watanzania tunazishudia ni mbinu zilezile zilizotumika mwaka 1995 na 2005 na zinatumiwa na watu walewale na ni chanzo cha CCM kuanguka na taifa letu kuyumba. Wapo wana CCM wengi walionyesha nia ya kutaka kuchaguliwa kuongoza taifa letu.

Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa pia ameonyesha nia ya kutaka kugombea urais kupitia CCM. Zipo dalili za wazi kwamba CCM isingependa kumpitisha Lowassa kutokana na tuhuma za mbinu chafu. Wapo wanaomtetea kwamba hana tuhuma na wapo wanaoona kwamba tuhuma hizo ni za kweli. CCM imegawanyika.

Mgawanyiko huu umeingia hadi nyumba za ibada, vyuo vikuu, vyombo vya usalama nakadhalika. CCM nzima imegawanyika. Taifa limegawanyika. Sababu za kugawanyika kwa Taifa zinatokana na mbinu chafu zinazotumika wala si kwamba jamii inamhitaji sana Lowassa.

Makundi yanayotangaza kwamba anafaa na yanayokwenda kumshawishi kila mara baadaye yamedhibitika siyo kweli bali yametengenezwa na yamepewa fedha au yamenunuliwa. Ni ujinga.

Ningependa kusisitiza na tujiulize kwamba, Lowassa aliwania kugombea urais mwaka 1995 lakini akaondolewa na CCM kwa tuhuma za kutumia mbinu chafu ikiwemo kujilimbikiza mali. Mwaka 2007 akajiuzulu Uwaziri Mkuu kwa tuhuma za ufisadi. Kwa sasa anataka kugombea tena urais na bado anatuhumiwa na chama chake kwa kutumia mbinu chafu.

Kwa nini mwenzetu huyu, Edward Ngoyai Lowassa anataka sana kwenda Ikulu kwa gharama yoyote? Tunafahamu uongozi ni utumishi. Huwezi kung'ang'ania au kulazimisha kuongoza au kuitumikia jamii wakati huo huo jamii hiyo ina mashaka na uadilifu wako. Haiwezekani. Nyerere aliyekaa Ikulu miaka 24 alisema, kwa mtu muungwana kabisa Ikulu si pa kukimbilia. Hakuna biashara Ikulu.

Kwenye makala iliyopita ya tarehe 15 April 2015 kwenye Raia Mwema nilieleza kwamba kikao cha NEC cha mwaka 1995 kiliondoa jina la Lowassa kwa kuwa alikuwa na tuhuma za rushwa, kujilimbikizia mali na kupungukiwa na maadili, kinyume na katiba ya CCM na chama hicho kikawateua Benjamin William Mkapa, Cleopa David Msuya na Jakaya Mrisho Kikwete kuwa wagombea.

Ukweli kwamba kuna matajiri au watu wanaotumia pesa kumiliki siasa na uongozi katika nchi yetu, ni jambo lililo wazi. Mathalani, kulikuwa na matumizi makubwa ya fedha katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
Baada ya kutangazwa mshindi wa kiti cha urais katika uchaguzi huo, Rais Jakaya

Mrisho Kikwete, akizindua Bunge Desemba 30, 2005, alisema: "Yameanza mawazo kuwa uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha. Tusipokuwa waangalifu, nchi yetu inaweza kuwekwa rehani kwa watu wenye fedha za kununua uongozi au wanaoweza kupata fedha za kufanya hivyo, maana unaweza kufadhiliwa na mtu ili ununue uongozi, ni vema sasa tulishughulikie suala hili".

Nchi kuwekwa rehani kwa matajiri ni jambo la hatari sana, kwa maana serikali itaongozwa na matajiri na haitawajibika kwa wananchi. Demokrasia itakoma na udikteta utatawala. Jambo linalojitokeza hapa na ambalo ni matokeo ya matumizi makubwa ya fedha na rushwa kwenye chaguzi, ni kupatikana kwa viongozi ambao hawakuchaguliwa na wananchi bali walinunua uongozi au waliotoa rushwa kushawishi wapiga kura wawape uongozi.

Pia Mwalimu Nyerere, wakati wa uhai wake, aliwahi kuonya juu ya hatari ya watu wachache wenye pesa kujaribu kutafuta uongozi kwa manufaa yao. Alisema: "Tanzania halijawa taifa imara sana na adilifu kiasi cha kuruhusu matajiri kuingia kwenye uongozi wa nchi kama ilivyo Marekani na Ulaya. Wakati huo bado uko mbali sana na tukitaka kuuvuta kwa kamba huko ndiko kuliingiza taifa letu changa kwenye kiwango cha ufisadi kama ilivyo sasa.

Katika kitabu cha Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania, Mwalimu J.K Nyerere, alisema hivi: "Utajiri unaweza kupatikana kutokana na rushwa kwa watumishi wa umma au kutokana na wafanyabiashara ambao wanawania nafasi za kisiasa ili wawe wadeni wa rais aliyeko madarakani". Maana ya maneno haya ni kwamba kiongozi akipatikana kwa kupewa fedha na matajiri, atapaswa alipe fadhila kwa matajiri hao waliokifadhili chama chake au yeye mwenyewe wakati wa uchaguzi.

Serikali inayopatikana kwa rushwa haiwajibiki kwa wananchi. Hutumikishwa na matajiri walionunua uongozi na waliotoa rushwa. Serikali hiyo huwaabudu matajiri walioiweka madarakani, haiwezi kufanya maamuzi yenye maslahi kwa wananchi. Serikali hiyo hulinda maslahi ya watu wachache, haiwezi kuchukua hatua dhidi ya ufisadi.

Hivi karibuni tumeshuhudia uteuzi wa hovyo wa wakuu wa wilaya, pia siku za nyuma tumeshuhudia kwenye utawala wa Kikwete uteuzi wa kushangaza wa mawaziri , watendaji wa serikali na taasisi za serikali. Uteuzi wa ajabu kabisa hadi unajiuliza watoto wetu wanajifunza nini kwa watu wa aina hiyo wanaopewa dhamana kubwa wakati hawana uwezo na wamepungukiwa maadili?

Ni bayana walipewa dhamana hizo kwa kulipa fadhila kwani walikuwa kwenye mtandao uliomwingiza Kikwete madarakani. Mtandao wa sasa wa Lowassa ni mkubwa kuliko wa mwaka 2005 uliomwingiza Kikwete madarakani na fedha zinatumika sasa pia ni nyingi kuliko zile zilzotumika mwaka 2005. Je Watanzania tunategemea nini baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 ikiwa Lowassa atakuwa Rais?

Hivyo ninashawishika kukubaliana na wale wanaotabiri kwamba utawala wa Lowassa utakuwa mgumu kuliko wa Kikwete kwani utaendeleza yale yale ambayo Kikwete ameyafanya, mfano kulipa fadhila kwa wanamtandao waliomwingiza madarakani bila kujali uwezo wao wa kuongoza.

Rais wetu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM anao wajibu na nafasi ya kusaidia kutoa ufafanuzi na hatimaye kufikia maamuzi ya kuliponya taifa letu kama alivyofanya Mwalimu Nyerere. Nyerere alipotanguliza utaifa kwanza, akasema ukweli na maamuzi sahihi yakafanyika. A friend in power is a friend lost. Taifa letu kwanza urafiki baadaye. Kikwete amshauri Lowassa aache kugombea urais kwa ajili ya kuliponya Taifa letu.

Madhumuni ya makala hii ni kuendelea na ushawishi na ushauri wangu nilioutoa katika makala iliyopita kwa kuzingatia falfasa ya Plato na ushauri wa Mwalimu Nyerere alioutoa kwenye kitabu chake.

Tunamhitaji Mtanzania ambaye ana uwezo wa kuongoza lakini ambaye anajua Ikulu ni mahali patakatifu na hakimbilii au halazimishi kwenda huko kwa kujua ugumu wa kazi hiyo na si kazi ya kuomba kienyeji kwa matakwa yake binafsi. Tunahitaji mtu mwadilifu wa mkweli siyo kama watia nia wengine wanavyoigiza kukubalika na jamii na wanatumia uwezo wa kifedha kuutafuta urais.

Hivyo, ningependa kusisitiza ushauri wa Mwalimu Nyerere unaozingatia falsafa ya Plato kwamba ni muhimu wananchi waelimishwe ili waweze kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuongoza na wanaofaa na wasio na tamaa ya kwenda Ikulu kwa kuwahonga watu.

Ikulu ni mahali patakatifu na hakuna biashara Ikulu bali ni mahali pa kuwatumikia watu. Si kila tajiri ana uwezo wa kuongoza.

Chanzo Raia Mwema
Toleo la 402
22 Apr 2015

0 comments:

Post a Comment