Saturday, 29 August 2015

[wanabidii] Lowassa kiboko

Lowassa kiboko
Na Saed Kubenea - Imechapwa 02 September 2008
Asaini mkataba pekee yake
Makamba: Tutaita Kamati Kuu

MKATABA wa kitegauchumi cha ujenzi wa jengo la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM) umechukua sura mpya baada ya wajumbe wa Baraza la Wadhamini mmoja baada ya mwingine, kumkana mwenyekiti wao, Edward Lowassa.

William Lukuvi, ambaye amepata kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika serikali, CCM na UV-CCM anasema, "Sijahajawahi kushiriki katika kikao kilichopitisha maamuzi ya ubia kati ya UV-CCM na muwekezaji."
"Sina chakuficha. Kama ningeshiriki ningesema. Sijashiriki, na hivyo ndiyo ninavyoweza kusema mahali popote pale. Kwamba mkataba ule siujui," anasema Lukuvi"

Hatua hii ya Lukuvi kukana mkataba inamweka pabaya Edward Lowassa aliyeweka saini mkataba huo.
Lukuvi anasema mkataba baina ya UV-CCM na muwekezaji ameuona kwenye gazeti. "Nilisoma katika gazeti lako, kwamba hamjanipata. Ahaa," anasema huku akiengua kicheko.

Akiongea kwa uchungu, Lukuvi anasema, "Mimi sijawahi kushiriki katika kupitisha maamuzi hayo. Hapa hakuna jambo la kuficha. Si tabia yangu kutenda mambo kwa kificho. Mimi ni muwazi …ndiyo maana nasema sijashiriki. Nahili nitalisema popote nitakapoulizwa."

Gazeti hili liliripoti mwezi mmoja na nusu uliopita, kwa mara ya kwanza, kuwa Baraza la Wadhamini la UV-CCM chini ya Lowassa lilisaini mkataba wenye thamani ya zaidi ya Sh. 30 bilioni, kati yake na makampuni mawili ya uwekezaji, bila wenye chama kujulishwa na kuridhia.

Mara baada ya taarifa hiyo, Lowassa alinukuliwa akitishia MwanaHALISI kwamba atalifikisha mahakamani kwa kile alichosema, "Limezoea kunizushia na kunichafua." Hadi sasa hajakwenda mahakamani na wala hajaleta malalamiko yake rasmi.
Lukuvi anasema ni vema ukafahamu kwamba "mimi sikushiriki. Katika vikao nilivyohudhuria,, hatukuwahi kujadili suala hilo. Nataka kila mtu abebe mslaba wake."

Lukuvi aliyepata kushina nafasi mbalimbali za uongozi katika UV-CCM tangu enzi za Youth League, ikiwamo Kaimu Katibu Mkuu wa UV-CCM kati ya mwaka 1992 hadi 1993, Mkuu wa Kitengo katika UV-CCM kati ya mwaka 1984 hadi 1989 anasema, "Ni kweli kwamba mimi ni mdau ndani ya UV-CCM. Lakini si katika mambo ya kuangamiza umoja wetu. Humo mimi simo."

Mjumbe mwingine, Dk. Mary Nagu ameliambia MwanaHALISI juzi Jumatatu, kwamba hajawahi kushiriki maamuzi ya kupitisha mkataba huo.
Dk. Nagu anasema, "Mimi ni msema kweli. Mimi nimehudhuria kikao cha juzi tu," kikao  ambacho kilifanyika wakati wa mkutano wa Bunge.

Anasema ndani ya kikao hicho ambacho kilifanyika mjini Dodoma wakati wa mkutano wa Bunge uliokwisha, aliwataka wenzake waache kufanya mambo gizani.
"Kama unazungumzia mkataba wa awali, mimi ni kama anavyosema Yusuf (Mjumbe kutoka Zanzibar) kwamba nimeona mkataba katika kikao kilichofanyika majuzi.

Kabla ya hapo mimi sikujua kama tayari mkataba umesainiwa," anasema Dk. Nagu.
Ni ndani ya kikao hicho, Dk. Nagu anasema, "Nikawaambia jamani haya mambo yaende kama yanavyotakiwa ili kuepesha yale yaliotokea katika UWT."
Anasema, "Nikawambia mtengeneze mambo haya vizuri, ili kuepesha yale ya UWT. Muandae  kila nyaraka na mtekeleze kila kinachotakiwa, kisha mpeleke katika vikao vinavyohusika."

Kabla ya hapo, Dk. Nagu anasema hajawahi kulisikia jambo hilo. "Labda kwa kuwa mimi huwa mara kwa mara nasafiri. Lakini hata kama ingekuwa hivyo, ningejulishwa. Mimi ni mjumbe halali, ningejulishwa," anasema kwa hali ya kulalamikia chama chake.

Kwa uchache tayari wajumbe watatu wamekana kuhusika na mkataba huo wa kinyonyaji, huku mjumbe mwingine ikidaiwa kulazimishwa na Lowassa kuwa shahidi wake. Duru za ndani ya UV-CCM zinamtaja mjumbe aliyelazimishwa kuwa ni Amos Makalla.
Taarifa zinasema Makalla aliitwa na Lowassa ofisini kwake na kuelezwa kwamba asaini mkataba huo.

"Unajua kwamba Lowassa alikuwa Waziri Mkuu na hakuna aliyetarajia kama angeanguka, zaidi ya kupanda. Katika mazingira hayo, Makala asingekuwa na ubavu wa kumkatalia Lowassa. Lakini ninavyojua Makalla hakubaliani na mkataba huu," alisema kiongozi mmoja wa UV-CCM aliyekaribu na Makalla.
Alipoulizwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba kuhusiana na hatua ya wadhamini kukana mkataba huo alisema, ""Kama haya unayonieleza ni ya kweli, basi kuna tatizo.
Makamba alielezwa na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake kwamba wajumbe karibu wote wa Baraza la Wadhamini ambao wameongea na MwanaHALISI wamekana kuhusika katika mkataba huo.

"Mimi ninamuhtasari wa kikao unaonyesha kuwa hawa watu walikutana na kujadili. Sasa kama kuna watu wanakana, tutawaita katika Kamati Kuu (CC) watueleze," alisema Makamba. 

Alisema mpaka sasa msimamo wa chama chake ni kupeleka mkataba huo katika kikao cha CC. "Huko ndiko tutakakwenda kuulizana," alisisitiza.
Alipoambiwa kwamba baadhi ya walionatajwa kushiriki katika kupitisha mkataba si wajumbe wa CC akiwamo Lowassa mwenyewe, Makamba alisema, "Ndiyo, lakini tutawaita."

Hata hivyo, Makamba hakusema kama tayari wameshajulishwa juu ya kuitwa kwao.
Wakati Makamba anasema mkataba wa ujenzi wa mradi unaokadiriwa kufikia Sh. 40 bilioni kati ya UV-CCM na mfanyabiashara Subhash Patel unafikishwa CC, kwa maamuzi ya mwisho, Baraza Kuu la UV-CCM, limesema halikuhusishwa katika suala la mkataba huo, huku Makamba na Lowassa wakidai kuwa mkataba haujafikiwa wala kuwekwa saini.

Mjumbe wa Baraza Kuu la UV-CCM na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Nape Nnauye alisema tarehe 22 Julai mwaka huu kwamba baraza la Lowassa halikuwa na madaraka ya kufikia maamuzi hayo kwa sababu "Baraza Kuu la UV-CCM, lenye mamlaka ya uamuzi wa mwisho, lilikuwa halijaridhia mkataba huo."
Mkataba ambao Makamba anasema unafikishwa kwenye CC, bado umejaa utata kutokana na kuwapo vipengele vinavyosema "mkataba huu ni sehemu ya mkataba ule."

Maneno hayo yanathibitisha hoja ya MwanaHALISI kwamba kilichosainiwa na Lowassa ni mkataba halisi na si makubaliano ya awali kama alivyodai yeye. Mbali na Lowassa wengine ambao wanaweza kutumbukia katika matatizo kutokana na mkataba huu, Mwenyekiti wa UV-CCM Emmanuel Nchimbi na Kaimu Katibu Mkuu Isack Francis ambao wanatuhumiwa kuwa vinara wakuu wa mkataba.

Nchimbi ndiye mwenyekiti wa vikao vyote vya UV-CCM; hajaonekana kuchukua hatua. Isack ni Kaimu Katibu Mkuu, wakati mkataba unasainiwa alikuwa Katibu wa Uchumi na Fedha wa UV-CCM.   

Katika hatua nyingine, kuna taarifa kwamba baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la UV-CCM wanakusudia kwenda mahakamani kushitaki Baraza la Wadhamini, iwapo Kamati Kuu ya CCM itaupitisha mkataba huo bila kushirikisha Baraza lao.

"Katika hili wala hatutanii. Kanuni za chama zinazuia wanachama kwenda mahakamani kwa ajili ya shughuli za kisiasa. Kanuni hazizuii kwenda mahakamani kutetea mali za chama," alisema mmoja wa wajumbe wa Baraza anayewakilisha wenzake ambaye hakutaka kutajwa gazetini.

Tayari Yusuph Mohammed Yusuf mjumbe wa Baraza la Wadhamini, anayewakilisha Zanzibar amekana kushiriki kupitisha mkataba huo uliosheheni utata.
Yusufu ambaye ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC), alisema, "Baraza la Wadhamini halijawahi kukutana kupitisha mkataba huo."

"Mimi ni mjumbe wa Baraza. Kama mkataba ni ule mlioandika kuwa ulisainiwa 2 Januari 2007, hakika siufahamu; sikuwahi kukutana na wenzangu na kukubaliana kusaini mkataba huo," amesema Yusufu.

Alisema yeye hafahamu na wala hakumbuki kama Baraza la Wadhamini chini ya Lowassa iliwahi kukutana na kukubaliana juu ya kusainiwa kwa mkataba huo.
Yusufu amesema walipelekewa mkataba na kuelezwa kuwa ni "maelewano" na kusema kuwa waliyapitia na "tukaagiza, kwa vile yalivyo sharti yapelekwe katika CC ya chama chetu.'

0 comments:

Post a Comment