Sunday 29 September 2013

[wanabidii] Neno Fupi La Usiku; Chumvi Ni Upatanishi...!



Ndugu Zangu,

"UNAPOTAKA kusema, tumia yako hekima.
Neno liwe la heshima. "- Remmy Ongala.

Naam, usiku umeingia. Nitazungumzia 'Chumvi '. Ndio, nataka kusema kuhusu chumvi. Chumvi ni maisha, chumvi ni siasa.

Afrika hatunyimani chumvi, hata kama tuna uadui wa chui na paka. Naam, chumvi ni upatanishi. Na tupatane katika chumvi. Wanadamu tumeumbwa kukosea. Tunakosea ndio maana tunajifunza. Ni nani asiyefanya makosa? Na kwa mwanadamu, kusamehe ndilo jambo lililo bora kabisa kulifanya kwa mwanadamu mwenzio aliyekukosea.

Ndio, kwa wengine chumvi kwao wataona ni kitu kigogo sana. Hapana, Afrika chumvi ni kitu kikubwa. Sukari na utamu wake hauzidi utamu wa chumvi. Kwanini?

Maisha yaso chumvi si maisha. Ndio maana Serikali zote Afrika huheshimu bei za chumvi. Ukimwona raia wa nchi anaanza kulalamikia bei ya chumvi, basi, hizo si ishara njema.

Mwanadamu waweza kuwa na kila kitu nyumbani. Lakini, ukikosa chumvi nyumbani , basi, huna kitu! Chumvi ni mwandani pia, au?

Haya, umenunua nyama, vitunguu, nyanya na vingine. Jikoni unakaangiza. Kumbe! Unakumbuka, kuwa umesahau. Nyumbani huna chumvi.

La haula! Giza limeshaingia, utakitafuta hata kibanda cha masikini, ukaombe chum… Shii! Usiku kuna mwiko wa chumvi. Usiku usiseme chumvi, sema ' dawa ya mboga'.

Na unajua maana yake? Wazee wetu walikuwa na busara sana. Aliyesahau kuwa na chumvi nyumbani alikumbushwa kwa kupewa ' tabu kidogo' katika kuipata. Maana, chumvi ni muhimu nyumbani.

Ndio, chumvi ndio dawa ya mboga. Nyama ulokaangiza haiwezi lika bila chumvi ati! Kama kuna ' nyama ya ulimi', basi , chumvi ndio ' asali ya ulimi'. Na chumvi ina kawaida yake. Ikiharibika ndo basi tena, ni ya kutupwa hiyo. Chumvi haioshwi.

Na mwanadamu chunga ulimi wako. Neno lako ni chumvi. Fikiri kwanza kisha ulitamke, usitamke kisha ukafikiri. Neno baya ni sawa na chumvi iliyoharibika. Haiosheki, ikasafishika, na ikabaki kuwa chumvi.

Na mwanadamu akisemwa amekula chumvi nyingi ina maana ameishi miaka mingi. Amefaidi maisha. Binadamu aweza kupitisha siku bila kula chenye sukari.

Lakini, hakuna siku ipitayo kwa mwanadamu bila mdomoni mwake kumeza kitu chenye chumvi. Na kama si chakula, basi mate, nayo yana chumvi!

Na nikisema chumvi ni tamu kuliko sukari nani abishaye?

Mh! Chumvi!

Ni Neno La Usiku Huu!

Maggid,
Iringa.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment