Saturday 22 June 2013

[wanabidii] Ujenzi wa minara ya simu

Minara ya simu haijengwi kwa matakwa ya serikali
Suala la ujenzi wa minara ya simu limekuwa likipotoshwa na wanasiasa kwa muda mrefu sana. Ujenzi wa mnara wa simu mahali fulani hutegema wingi wa watumiaji wa simu katika eneo husika. Mara nyingi, taarifa kuhusu ukubwa wa uhitaji na ulazima wa ujenzi wa mnara katika eneo husika hutokana na wingi wa maombi ya wateja wanaopiga simu kitengo cha Huduma kwa Wateja wakiomba ujenzi wa mnara katika sehemu wanayoishi na kuendesha shughuli zao za kila siku. Taarifa hizi kukusanywa na kitengo cha ujenzi wa minara na kuhifadhiwa na baadaye huchakatwa na kutumiwa kama kigezo cha kuamua ni wapi mnara ujengwe. Hata hivyo, kabla ya kufikia uamuzi wa kujenga mnara wataalamu wa mawasiliano hutembelea eneo husika na kujiridhisha kama kuna ulazima wa kujenga mnara mahali hapo.
 
Pamoja na wingi wa maombi yanayopokelewa na kitengo cha Huduma kwa Wateja kutumiwa kama kigezo cha ujenzi wa mnara, kigezo kingine muhimu kinachotumika kuamua kujenga mnara eneo fulani ni idadi ya watu na watumiaji wa huduma za simu katika eneo husika. Pia shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa na wananchi waishio mahali hapo huzinagatiwa. Kampuni ya simu haiwezi kujenga mnara wa simu, ambao hugharimu mamilioni ya shilingi, kwa ajili ya wateja wachache ambao matumizi yao ya huduma za simu hayawezi kutosha kuufanya mnara ujiendeshe.
 
Tukumbuke kwamba mnara unatakiwa kufanya kazi wakati wote bila kujali kama kuna umeme au la. Na kwa yale maeneo yasiyokuwa na umeme, kampuni hulazimika kuingia gharama za ziada kununua majenereta makubwa kwa ajili ya kuendeshea minara. Na si hayo tu, kuna suala la ulinzi na usalama wa miundombimu ya minara pamoja na  na gharama za ununuzi wa mafuta ya kuendeshea hayo majenereta. Ukichanganya hizi gharama zote, utaona ugumu wa kujenga mnara mahali penye idadi ndogo ya watumiaji wa huduma za simu.
 
Nimefanya kazi kwenye kampuni moja ya simu hapa nchini kwa muda wa miaka ipatayo tisa. Kwa hivyo, ninao uzoefu wa kutosha kuhusu mchakato wa ujenzi wa minara ya simu za mikononi. Minara ya simu haijengwi kwa amri wala utashi wa kisiasa kwani ujenzi wa minara ni ghali kuliko watu wengi wanavyoweza kudhani. Ujenzi wa mnara mmoja huweza kugharimu hadi shilingi bilioni moja!
 
Wakati bajeti ya Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano ikiwasilishwa bungeni hivi karibuni, nilimsikia mbunge mmoja akimuomba Waziri awajengee wananchi mnara wa simu katika jimbo lake kwani ni muda mrefu wananchi wake wamekuwa wakipiga simu wakiwa wamepanda mitini au milimani. Mbunge huyo alilalamika hadi akalia machozi! Haya nayaita 'machozi ya kisiasa' au 'machozi ya mamba' ambayo hutumika kupata huruma za wapiga kura.
 
Hakuna hata siku moja ambayo Waziri anaweza kuingilia suala la ujenzi wa mnara wa simu kwa wapiga kura wa jimbo fulani. Makampuni ya simu sio mali ya serikali na hayaendeshwi kwa kodi za umma. Hujiendesha yenyewe kwa kuwekeza kwa faida na kwa umakni wa hali ya juu. Kama ingekuwa uendeshaji wa makampuni haya unafuata siasa, yangekuwa yameishajifia kitambo sana. Hizo siasa zao labda wazipeleke kule TANESCO na kwenye mashirika mengine ya serikali yanayoendeshwa kisiasa. Sijawahi kusikia serikali ikituma pesa za maendeleo kwenye makampuni ya simu. Sasa iweje wajipendekeze kudai kwamba watawajengea wananchi minara ya simu?
 
Nawakumbusha wanasiasa kuacha kuwapaka mafuta wapiga kura wao kwa mgongo wa chupa huku wakijua kwamba hawana mamlaka wala uwezo wa kuyaamrisha makampuni ya simu kujenga minara mahali wanapotaka. Suala la kuahidi kuwajengea wananchi minara ni uongo wa kisiasa usiokuwa na tija yoyote kwa ustawi na maendeleo ya wananchi. Pia naomba kuwatahadharisha wananchi wauepuke utapeli huu wa kisiasa. Akili za kuambiwa changanyeni na za kwenu. Tafakari, chukua hatua!

0 comments:

Post a Comment