Sunday 30 June 2013

[wanabidii] Huu ndio unyama wa JWTZ kwa CUF, Mtwara

MATESO NA UKATILI MKUBWA ALIOFANYIWA NAIBU MKURUGENZI WA OGANAIZESHENI UCHAGUZI NA BUNGE WA CUF TAIFA MHE. SHAWEJI MKETO NA VIONGOZI WENGINE WA CUF MKOANI MTWARA.
A. Muhtasari
Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika kambi yao ya Naliendele yamewafanyia mateso makubwa viongozi wa CUF akiwemo Mheshimiwa Shaweji Mketo, Naibu Mkurugenzi wa Oganaizeshani, Uchaguzi na Bunge ambaye alipigwa mpaka akazimia na kuchomwa sindano na kemuwekea drip 3 kabla hajazinduka saa 10 alfajiri. Rais Kikwete asitishe mara moja vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu unaofanywa na askari Mkoani Mtwara. Taarifa ninayoitoa inatokana na maelezo na utafiti uliofanywa na Naibu Katibu Mkuu, Julius Mtatiro niliyemtuma kwenda Mtwara kufuatilia kukamatwa kwa Mketo na wenzake.
B. Shughuli halisi alizofanya Mhe. Mketo alipofika Mtwara Mjini;
Jumatano tarehe 26 Juni 2013 Mkurugenzi wetu wa Oganaizesheni Uchaguzi na Bunge Mhe. Shaweji Mketo alitumwa na Chama chetu kuhudhuria kesi inayowakabili viongozi mbalimbali wa CUF katika mahakama ya Mtwara Mjini (Kesi inayomkabili MHE.KATANI AHMAD KATANI na wenzake).
Mhe. Mketo alipotoka mahakamani alifanya kikao na wanachama wa CUF Mtwara mjini ambao walimueleza unyanyasaji na ukatili mkubwa ambao wanajeshi na polisi wanawafanyia wananchi wa Mtwara. Palitolewa taarifai ya mwanamke mmoja aliyenajisiwa na ambaye aliripoti tukio husika katika kituo cha polisi cha Msimbati kilichoko Mtwara na alipeleka polisi hadi ushahidi wa mipira ya kiume iliyotumika kumfanyia unyama huo lakini polisi hawakuchukua hatua yoyote hadi leo.
Mhe. Mketo na viongozi wengine waandamizi watano walielekea maeneo ya kijiji cha Msimbati ambako mwanamke huyo amesitiriwa baada ya unyama huo. Mzazi wa binti aliyebakwa anajulikana kwa jina la SELEMANI BIN OMARI. Mhe. Mketo na viongozi aliokuwa nao walifika kijiji cha Msimbati na kukutana na mwanamke aliyebakwa mbele ya familia yake, waliongea naye kwa kina na mwanamke huyo alieleza kila kilichojiri;
C. Maelezo ya mwanamke aliyebakwa yaliyotolewa na mwanamke husika mbele Mkurugenzi Mketo tarehe 27 Juni 2013;
Siku ya tukio mwanamama huyo ambaye ameeleza ana umri wa zaidi ya miaka 40 lakini kimaumbile anaonekana kama ana miaka 20 – 25 alikuwa anawasha moto nyuma ya nyumba yao huku mama yake mzazi akisuka mkeka sehemu ya mbele ya nyumba yao. Ghafla akaona wanajeshi watatu wameingia nyumbani kwao. Mwanajeshi mmoja akamuuliza anawasha moto wa nini, akawajibu anataka kupika. Yule mwanajeshi akamwambia "twende kwanza ndani" na akamshika na kumvutia ndani. Askari Yule akamuingiza katika mojawapo ya vyumba na kumrusha kitandani kwa nguvu.
Wale askari wengine wawili, mmoja akalinda upande aliokuwepo mama yake mzazi akisuka mkeka na mwingine akalinda mlango wa upande ambako mwanamke huyu alikuwa anawasha moto. Mule chumbani, askari Yule alimlazimisha kufanya mapenzi na juhudi zake za kupinga hazikusaidia kwani alitishiwa kuwa akipiga kelele atapigwa sana. Askari Yule alisisitiza kuwa baada ya kumridhisha atampa shilingi elfu tatu 3,000/-. Kwa sababu ya kumzidia nguvu na kumtishia kumuua, askari husika alifanikiwa kutoa pakiti ya mpira wa kiume na kuuvaa na kumuingilia kwa nguvu. Baada ya kitendo kile askari Yule alivaa nguo akaungana na wenzie waliokuwa wakilinda milango yote miwili wakaondoka huku mbakaji akiacha pakiti ya mipira ya kiume ene la tukio.
Baadaye familia ya mwanamke huyu ilitoa taarifa kwa mwenyekiti wa Kitongoji chao anayetokana na Chama Cha Wananchi CUF na mwenyekiti akawataka waende wakaripoti polisi. Waliripoti kituo cha Polisi Msimbati wakapewa nyaraka ili waelekee hospitali. Walipokwenda hospitali, daktari alifanya vipimo na kuwajulisha polisi na ndugu kuwa mwanamama Yule amebakwa na kwamba kuna michubuko ya wazi katika sehemu zake. Baada ya ripoti hiyo kutolewa, polisi waliichukua na hadi leo haijulikani iko wapi.
D. Kutishiwa familia ya mwanamke aliyebakwa, kutekwa na kuteswa kwa daktari aliyempima na kuthibisha kitendo alichofanyiwa;
Mwanamke husika na familia yake wameendelea kutishiwa sana na askari jeshi. Mwenyekiti wa Kitongoji wa CUF amehojiwa mara kadhaa na wanajeshi na daktari aliyefanya uchunguzi ule alivamiwa nyumbani kwake na wanajeshi usiku wa kuamkia tarehe 27 Juni 2013 akakamatwa na kupelekwa kwenye kambi ya jeshi ya Naliendele na kuteswa hadi majira ya alfajiri. Alikuwa anateswa ili asijihusishe tena na namna yoyote ya kutoa ushahidi kwa mtu yeyote kuhusu uthibitisho wa tukio la ubakaji uliofanywa na askari wa jeshi.

E. Safari ya Mhe. Mketo na Viongozi waandamizi kutoka Msimbati kurudi Mtwara Mjini na kutekwa na wanajeshi kulivyotokea;
Kati ya saa 11.30 – 12.00 jioni walifika eneo la kilometa tatu kabla ya kuingia mjini (Eneo la njia pacha). Magari mawili ya kijeshi moja likiwa aina ya TATA na lingine likiwa DEFENDER ya jeshi yaliziba barabara. Ilibidi gari ya mhe. Mketo iliyokuwa ikipeperusha bendera ya chama chetu isimame (Gari hii ni aina ya NISSAN PATROL yenye namba T 866 BGW – Mali ya Chama Cha Wananchi CUF). Askari jeshi zaidi ya 50 waliivamia gari aliyokuwemo Mhe. Mketo na viongozi waandamizi na kuanza kuwapiga bila sababu na kisha kuwarusha kwenye karandinga la jeshi. Viongozi waliotekwa kwa kushtukizwa walikuwa ni;
1. Shaweji Mketo – Naibu Mkurugenzi wa Oganaizesheni Uchaguzi na Bunge,
2. Salum Hamis Mohamed – Mwenyekiti CUF Mtwara Mjini,
3. Ismail Hamis Jamal – Mwenyekiti CUF Mtwara Vijijini,
4. Ismail Bakari Njalu – Mwenyekiti wa vijana(JUVICUF) Mtwara Mjini,
5. Said Issa Kulaga – Katibu CUF Mtwara Mjini,
6. Kashindye Kalungwana – Dereve wa CUF Ofisi Kuu.
Baada ya kuwateka waliwapeleka katika kambi ya jeshi ya NALIENDELE ambako walishikiliwa kwa jioni, usiku mzima na asubuhi ya tarehe 28 Juni 2013. Baada shinikizo la kuwaachia nililolitoa, wanajeshi waliwaachia viongozi wote majira ya saa 5 asubuhi kwa kuwakabidhi kwa RPC wa Mkoa wa Mtwara ambaye hadi anakabidhiwa viongozi hao alikataa kabisa kutoa ushirikiano kwa chama, kila alipopigiwa simu alijibu yuko vikaoni na kuwa hawezi kuongea. Majira hayohayo, RPC aliondoka na viongozi wote 6 hadi makao makuu ya jeshi la polisi Mtwara na kisha wakaanza kuhojiwa na kisha wakapelekwa mahakamani.
F. Mashtaka waliyosomewa mahakamani;
Majira ya tarehe 28 Juni 2013 saa 10 jioni walifikishwa katika mahakama ya wilaya ya Mtwara Mjini na kusomewa mashtaka matatu katika kesi ya jinai namba 137 ya mwaka 2013;
1. Shtaka la kwanza ni Njama za kutenda makosa kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 ambapo inadaiwa kwamba tarehe 27 Juni 2013 katika eneo la barabara ya Msimbati ndani ya wilaya ya Mtwara Mjini katika mkoa wa Mtwara wote kwa pamoja walipanga njama za kutenda makosa.
2. Shtaka la pili ni Kusanyiko lisilo halali kinyume na kifungu cha 74(1) na 75 cha Sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 na kwamba shtaka hilo pia linakwenda kinyume na kifungu cha 43,44 na 45 cha Sheria ya Polisi na Polisi wasaidizi kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 ambapo inadaiwa kwamba tarehe 27 Juni 2013 katika eneo la barabara ya Msimbati ndani ya wilaya ya Mtwara Mjini katika mkoa wa Mtwara wote kwa pamoja walifanya kusanyiko ambalo si halali ambalo lilisababibsha kuvunjika kwa amani na kuleta hofu kwa wananchi.
3. Shitaka la tatu ni kupanga na kuchochea ufanyaji wa makosa kinyume na kifungu cha 390 cha Sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 ambapo inadaiwa kwamba tarehe 27 Juni 2013 katika eneo la barabara ya Msimbati ndani ya wilaya ya Mtwara Mjini katika mkoa wa Mtwara wote kwa pamoja waliwachochea wananchi wa Mtwara kutenda makosa.
Walipokana makosa hayo dhamana iliwekwa wazi lakini kwa sharti la kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye mali isiyohamishika na atakayewasilisha hati iliyothaminiwa ya mali husika ambapo thamani ya mali atakayowasilisha iwe ni shilingi milioni 20 na kuendelea.

G. Kushindwa kukamilisha masharti magumu ya dhamana na kukataliwa kupokelewa gerezani;
Kutokana na hali halisi kuwa Mtwara Mjini haina hati zilizothaminiwa kwa wananchi wengi mawakili na wanachama wetu hawakuweza kufanikiwa kukamilisha sharti hilo hivyo viongozi wetu walipelekwa gereza kuu la Mtwara mjini hadi hapo masharti ya dhamana yatakapotekelezwa. Askari magereza walipowakagua walikataa kuwapokea kwa sababu kwamba "magereza haipokei wagonjwa" kwani magereza walithibitisha kupigwa na kuumizwa kikatili kwa wahusika wote sita. Iliwapasa Askari polisi kuondoka nao wote katika gari la polisi na kuwapeleka hospitali ya mkoa wa Mtwara majira ya saa 12 jioni. Hospitalini madaktari walijionea kipigo kikubwa walichopata maeneo mbalimbali ya miili yao, pamoja na hayo madaktari walieleza kuwa hospitali ya Mkoa haina dawa kwa ajili ya matibabu. Ilimpasa mhe. Mketo kutakiwa kutafuta fedha za matibabu kwa hivyo alitafuta na kupata pesa za madawa na kuwapa madaktari ili watuhumiwa wote wapate matibabu.
H. Maelezo ya jumla ya Mhe. Mketo juu ya matukioa aliyohudhuria Mtwara siku ya kesi ya kina Katani aliyayoyatoa mbele ya Mtatiro alipomtembelea gerezani 29 Juni 2013;
Naibu katibu Mkuu wa CUF Mhe. Mtatiro na mawakili walifika Mtwara jumamosi tarehe 29 Juni 2013 na alifika gerezani na kuonana na mhe. Mketo na kufanya naye mazungumzo chini ya ulinzi mkali. Mhe.Mketo alieleza kwa kina tukio zima lilivyokuwa;
Alieleza kuwa wao walipofika Mtwara siku ya alhamisi tarehe 27 Juni walihudhuria mahakamani katika kesi inayomkabili mhe. KATANI AHMAD KATANI (Mwenyekiti wa JUVICUF taifa). KATANI na wenzie kadhaa wakiwamo viongozi wa NCCR Mageuzi wanashtakiwa katika kesi moja yenye mashtaka ya aina moja na nambari ya kesi moja. Cha ajabu katika kesi hii iliyoitwa kwa kutajwa tu siku hiyo, hakimu wa mahakama ya wilaya aliiahirisha hadi tarehe mbili tofauti wakati kesi ni moja na washtakiwa walishtakiwa pamoja. Mhe. Katani aliambiwa atahudhuria mahakamani tarehe 27 Julai 2013 huku wenzake kina Uledi wa NCCR Mageuzi walitakiwa kuhudhuria mahakamani tarehe 29 Julai katika kesi ileile moja na mashtaka yaleyale, hii ina maana kuwa mahakama imetangaza tarehe mbili ambazo watuhumiwa katika kesi moja watahudhuria kila watuhumiwa tarehe yao. Hatuelewi kwa nini mahakama imefanya hivi, mawakili wetu wanashughulikia.
Baada ya ahirisho hilo Mhe. Mketo na viongozi wengine walikusanyika ndani ya ofisi ya CUF wilaya ya mtwara mjini na kufanya kikao kifupi na naada ya hapo walifunga safari ya kwenda kijiji cha MSIMBATI ili kukutana na mwenyekiti wa CUF ambaye alipaswa kuwapeleka kwa familia ya mwanamke aliyebakwa. Walipomaliza kuongea na familia hiyo na mwanamke husika, walirekodi ushahidi na waliingia kwenye gari kurudi Mtwara mjini.
I. Maelezo ya kuvamiwa, kuteswa, kutekwa na wanajeshi hadi kukabidhiwa kwa polisi keshoye(Maelezo ya Mhe. Mketo aliyoyatoa mbele ya Mtatiro):
Kilometa tatu kutoka mjini ndipo walipokuta barabara imezibwa na magari ya jeshi huku wanajeshi zaidi ya 50 walio na silaha nzito zikiwemo bunduki za kijeshi wakiwasubiri. Waliposimamisha gari tu milango yao ilifunguliwa kwa nguvu. Askari mmoja mwenye bunduki alirusha ngumi ambayo mhe. Mketo aliipangua, kuona hivyo askari Yule akahoji kwa nini Mketo amepangua ngumi yake, wakati anataka kujibu askari mwingine alimpiga na kitako cha bunduki katika shavu la kushoto. Katika sekunde chache ambazo walisimama wote walipigwa sana, Mwenyekiti wa VIJANA Mtwara Mjini alipigwa na kuchanika sehemu za usoni. Wote sta walibebwa juu juu na kutupwa katika karandinga la jeshi na kuamriwa kulala chini kisha wakapelekwa kambi ya jeshi ya NALIENDELE.
Walipofikishwa NALIENDELE walianza kupigwa na kuteswa sana. Mketo alishuhudia mateso ya kikatili mbayo hakuwahi kuyaona maishani. Walivuliwa nguo zote na kulazwa kifudifudi na kumwagiwa maji ya baridi na kupakwa chumvi kisha walianza kupigwa usiku kucha kwa kutumia mikanda ya kijeshi, ngumi mateke na fimbo maalum za ngozi za wanyama na miti maalum.
Baadaye wanajeshi wale watesaji walianza kuwapiga mateke ya nguvu maeneo ya usoni, tumboni na kichwani. Kwa bahati mbaya Mketo alipigwa sana katika ubavu wake wa kulia ambapo amewahi kufanyiwa oparesheni kubwa miezi kadhaa iliyopita. Alipoona anapigwa sana eneo hilo akaona awaombe askari jeshi hao wampige maeneo mengine lakini eneo hilo wamhurumie kwa sababu amefanyiwa oparesheni. Kusikia vile, askari wale walimgeuza kwa nguvu na kuanza kumpiga mateke ya nguvu zaidi katika eneo lile hadi alipoteza fahamu majira yale ya jioni. Baada ya kupoteza fahamu askari wale walikuja na kuanza kumchoma sindano (ambazo hazijulikani zilikuwa za nini), kisha walimtundikia dripu tatu za maji. Mketo alizinduka majira ya saa 10 alfajiri ya ijumaa ya tarehe 28 Juni 2013 na alijikuta ana dripu, hakuelewa ni ya nini. Baadaye wanajeshi walikuja na kuitoa, wanajeshi walipoondoka aliwauliza wenzie zile dripu ni za nini, ndiyo wenzie wakamjulisha kuwa alitundikiwa dripu usiku kucha.
Alfajiri hiyohiyo askari jeshi wale walirudi, wakamlaza kifudifudi mhe. Mketo na kuanza kumpiga sana kwa fimbo katika miguu yake, walimpiga kwa saa nzima hadi walipochoka na kuondoka. Baadaye alianza kusikia maumivu makali maeneo yenye upasuaji (ubavuni na tumboni), anasema anahisi kuna matone ya maji au vitu laini yanadondoka ndani kwa ndani katika eneo alilofaniwa upasuaji mkubwa. Hali haikuishia hapo tu, baadaye na hadi sasa anasema kila akienda msalani anajisaidia choo chenye damu nyingi huku hana msaada wa matibabu zaidi ya yale yasiyo na vipimo yanayoendelea gerezani.
Mketo anasema wenzake watano ndio waliopigwa kuliko yeye, anasema kuwa "wenzake ndo wamepigwa kipigo cha mbwa", kwa sababu hawakupoteza fahamu usiku ule. Anaeleza kuwa usiku kucha walipigwa kwa zamu na mafungu ya askari jeshi waliokuwa wakiingia kwa zamu kwa idadi kadhaa. Wanawapiga viongozi wetu kwa nusu saa hadi saa nzima kisha wanaondoka na kuja wengine. Askari wengi waliowatesa walionekana kuwa walinyweshwa pombe ili waifanye kazi ile bila huruma, Mketo anasema usingeongea na askari wale wakakuelewa lolote. Kazi yao ilikuwa "ni kupiga tu, ukiweka kichwa wanapiga, ukiweka tumbo wanapiga, ukiacha jicho wazi wanapiga tu", kwa hiyo namna ilokuwepo ilikuwa ni kulala kifudifudi na kuacha mwili upigwe watakavyotaka.
Dereva Kashinde Kalungwana alipigwa na kuumizwa sana ikiwemo eneo la mkono ambao anasema maeneo ya kiganya ni kama umekufa ganzi hadi leo. Pamoja na sindano anazochomwa hadi sasa hauhisi mkono wake, hivyo umefungwa kwa "crip bandeji" na ameubeba akikata tamaa. Hospitalini hawakumjulisha lolote na hakupata matibabu yoyote ya maana, alipewa madawa ya kumeza tu.
Kulipoanza kucha ndipo mhe. Mketo na wenzake waliacha kupigwa. Baadaye waliingia wakubwa wa jeshi kutoka kwenye kambi ile na kuwasalimu na kuwapa pole na kuwajulia hali. Baadaye majira ya asubuhi alikuja Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara (RPC) na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) . Kina Mketo walichukuliwa na kupelekwa katika chuma maalum na kuwakuta viongozi wa jeshi la Ulinzi wa kambi ile na Mkoa wa Mtwara wakiwa pamoja na RPC na RCO. Walihojiwa kwa muda katika kikao hicho kisha wanajeshi wakawakabidhi kwa polisi wale majira ya saa 5 asubuhi na wakapelekwa polisi chini ya ulinzi mkali wa polisi na kuhojiwa na kisha tena kufikishwa mahakami na kusomewa mashtaka hayo hapo juu na kurudishwa gerezani.
Pesa zao mbalimbali, laptop, simu na viatu hadi sasa havijulikani vilipo. Vilichukuliwa wakati wa kipigo kile cha askari jeshi na hata wakati Mketo anaondoka pale kambi ya jeshi alipewa viatu viwili tofauti kwa kila mguu kwani viatu vyake halisi havijulikani viko wapi. Anakumbuka kuwa viatu vyake vilivuliwa kwa nguvu na mmoja wa askari wakati wamelazwa kifudifudi.
Pamoja na hali hiyo, Askari magereza wana maelekezo kuwa mtu yeyote asiwaone kina Mketo na wasipelekwe mahali popte kwa ajili ya jambo lolote nje ya Magereza kwa sababu maalum. Kuwaona lazima kupatikane kibali maalum, haya ndo maelekezo aliyopewa mkuu wa gereza kutoka kwa mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ambaye ni mkuu wa mkoa, sababu inayotolewa ni kuwa Mketo na wenzie ni watu hatari sana na kwamba ati "upelelezi utaharibiwa ikiwa watatembelewa mara kwa mara na watu mbalimbali".
J. Maelezo ya Jeshi la Polisi Mtwara na Hali halisi ya mambo;
Mtatiro alipofika Mtwara alimtafuta RPC wa Mtwara bila mafanikio. Alibahatika kumpata RCO na kuongea naye siku ya jumamosi 29 Juni 2013. RCO alidai kuwa viongozi wa CUF hawakupigwa na kwamba wako salama. RCO alikiri kuwepo kwa tukio na taarifa za kubakwa au kunyanyaswa kijinsia na wanajeshi (hana uhakika) lakini anasisitiza kuwa "mwanamke aliyebakwa ndiye hataki kuendelea na mashtaka na kwamba polisi walipoongea naye pamoja na kutotaka kuendeleza mashtaka dhidi ya wabakaji wake, ati mwanamke huyo aliwajulisha polisi kuwa hajabakwa!"
Ukiangalia mwenendo wa matukio yote hayo kuanzia "kuvamiwa na kutekwa kwa nguvu na wanajeshi, kupelekwa kambi ya jeshi badala ya polisi, kuteswa kinyama usiku kucha, kuja kusalimiwa na wakuu wa kambi ya jeshi asubuhi, kuja kwa RPC na RCO asubuhi husika na kukubali kwao kuwapokea watu waliopigwa kiasi kile, RPC na RCO kukubali kupika mashtaka ya kusadikika na kuwabambikizia viongozi ambao hawakufanya mkutano wowote Mtwara, wala kuchochea jambo lolote Mtwara, wala kuvunja amani yoyote Mtwara, kukiri kwa RCO juu ya kuwepo tukio na taarifa za ubakaji wa mwanamke Msimbati(pamoja na RPC kukubali na kukana kwa wakati), yote haya ni kielelezo cha uvunjifu mkubwa wa katiba ya nchi, uvunjifu mkubwa sheria zinazoongoza ukamataji wa raia na kuwashtaki, uvunjifu mkubwa wa protokali za kijeshi na majukumu ya jeshi la ulinzi na polisi, uvunjifu mkubwa wa haki za raia na ni ushenzi na unyama usiomithilika ambao sasa majeshi yetu kwa Baraka za serikali, wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama, wakuu wa mikoa na mamlaka zao, na wakuu wailaya na mamlaka zao wamekubali haya yatendeke na yaendelee kutendeka. Kutekwa, kuteswa na kubambikiziwa kesi kwa viongozi wetu na wananchi wa Mtwara ni mipango iliyo wazi ya vyombo vya dola na mamlaka za serikali na wala si jambo la bahati mbaya".
Aidha tarehe 29 Juni 2013 Mtatiro ametembelea wakazi kadhaa walioteswa katika kambi ya Naliendele wakiwemo watumishi wa serikali ambao wanaugulia vidonda na maumivu makali vitandani. Wengi wao wametishiwa kuwa wakienda hospitalini majeshi yatajua na kwamba yatawafuata mahospitalini na kuwarudisha kwenye kambi ya mateso.
Kwa bahati mbaya sana – vyombo vya habari, mashirika ya haki za binadamu na asasi za kiraia havifuatilii kabisa matukio haya mabaya nay a kutisha yanayoendelea Mtwara. Hii inakamilisha ule usemi kuwa "mikoa ya kusini imetengwa na haipati huduma na haki za msingi ambazo binadamu wanastahili". Baadhi ya waandishi wa habari tulioongea nao Mtwara wanaonesha kuwa na wao wanasakwa na wanajeshi ikiwa wataripoti matukio haya. Tumewauliza mbona wakiwa Arusha hata kama ni katikati ya mabomu na vipigo bado wanaripoti habari. Wanachojibu ni kuwa Arusha si Mtwara.
K. Hatua muhimu za kuchukua;
Tunatoa wito kwa Mahakama kuwapa dhamana mara moja viongozi wetu waliopigwa na kubambikiziwa kesi ili wapate matibabu. Maisha ya viongozi wetu yako hatarini. Mketo alifanyiwa operesheni kubwa mwaka jana na inaonekana kuna damu inavuja ndani ya mwili wake (internal bleeding). Wengine wamepigwa zaidi ya Mketo hatujui madhara makubwa waliyoyapata.
Tunawasiliana na Mawakili wetu na asasi za haki za binadamu kuelewa hatua za kisheria tunazoweza kuchukua dhidi ya Jeshi la Wananchi kuwateka nyara na kuwatesa viongozi wetu.
Vile vile tunawasiliana na Mawakili kujua hatua za kisheria za kuchukua dhidi ya Jeshi la Polisi la kushiriki katika kubambikizia kesi watu ambao wamekamatwa na kupigwa na askari wa Jeshi la Wananchi.
Tunawasiliana na asasi za kiraia zinashughulikia Haki za Binadamu na Haki za Wanawake kumsaidia mama aliyebakwa kisaikolojia na kuhakikisha waliohusika wanafikishwa mahakamani ili wanajeshi wanaobaka wajue kuwa hawako juu ya sheria.
Jeshi la Wananchi linajijengea uhasama mkubwa na raia wa kawaida mkoani Mtwara. Hii ni hatari kwa usalama na amani ya kweli ya nchi yetu. Utaratibu wa wanajeshi kukamata kupiga na kutesa wananchikwenye kambi ya Naliendele usitishwe mara moja. Mkuu wa Mkoa ambaye ni afisa wa jeshi mstaafu hana mahusiano mazuri. Anawadharau, kuwabeza na kuwaona ni waswahili wasiokuwa na maana. Anajenga uhasama mkubwa kati ya wananchi na serikali.
Tukio hili la utesaji la raia ndani ya Kambi ya Jeshi la Wananchi ukiliunganisha na matukio mengine kama vile utesaji wa Dr. Ulimboka, kutekwa nyara na kuteswa kwa Mwandishi wa Habari Absalom Kibanda, kulipuliwa bomu katika mkutano wa hadhara wa CHADEMA katika viwanja vya SOWETO, Arusha na matukio mengine kunadhihirisha hatua za awali za kusambaratika kwa dola (Failed State). Rais Kikwete akiendelea kuyafumbia macho mambo haya na kuruhusu vitendo vinavyofanywa na Jeshi la Wananchi katika Kambi ya Naliendele taifa linaweza kusambaratika.

Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti,
Jumapili, 30 Juni 2013.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment