Saturday 4 May 2013

[wanabidii] THRD-Coalition inapinga kukamatwa kwa Watetezi wa haki za binadamu Bahi

TAMKO LA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU (THRD-COALITION) KUPINGA KUKAMATWA KWA MTETEZI WA HAKI ZA BINADAMU WILAYA YA BAHI 
BB DOMINIC HAULE NA WENZAKE SITA


Mtandao wetu umezipokea kwa majonzi habari za kukamatwa kwa mwanachama wake na Mtetezi wa Haki za Binadamu BB Dominic Haule na wenzake sita. Waliokamatwa ni Mpumba Mwaruko, Juma Kamunya, Charles Munyakongo, Ayubu Mukosi, Matereka Ndoru, na Champunga Mburi Mutinya.

Taarifa tulizozipokea kutoka eneo hilo zinasema Bw Haule na wenzake wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa kutimiza majukumu yao kama raia wema wanaotaka kuona kwamba utawala wa sheria na haki unazingatiwa. Kwa mujibu wa vyanzo vyetu hivyo vya habari watetezi hao wakiwamo waandishi wa habari walikuwa wanafuatilia mambo yaliyokuwa yanalalamikiwa na wananchi ambayo ni pamoja na kutozwa michango mikubwa bila kuona manufaa ya kile wanachochangia.

Baadhi ya maeneo yaliyokuwa yanaathiriwa na ukiukwaji huo wa haki za binadamu ni Kijiji cha Chali Isanga, Wilayani Bahi ambalo ni eneo lililo chini ya uangalizi wa Utetezi wa Haki za Binadamu wa Bw BB Dominic Haule. Vyanzo vyetu vinaeleza kwamba ukiukwaji huo ni pamoja na watu kutozwa hadi shilingi la saba kwa mtu mmoja kwa ajili ya michango hiyo kulingana na idadi ya mifugo aliyonayo.

Pia kulikuwa na fedha zilizokuwa zimechangwa kwa ajili ya ujenzi wa choo cha shule pamoja na Wadi ya Kujifungulia akina mama kijijini hapo bila kukamilika. Katika ujenzi huo jengo hiloliliezekwa kwa mabati ya zamani na kupakwa rangi huku ikielezwa kuwa ni mapya jambo ambalo wananchi walilipinga.

Pia katika hatua hiyo ilibainika kwamba baadhi ya vifaa vya ujenzi vimeuzwa na baadhi ya viongozi wa kijiji kwa watu wasiohusika na katika kutaka kufukia habari hiyo wakaamua kuzuia waandishi wasijue chochote

Mnamo tarehe 24 Aprili Bw BB Dominic alitafuta mwandishi wa habari na kwenda naye kijijini na wakati wakiwa kijijini hapo katika kazi ya uchunguzi walikutana na wananchi waliowapa ushirikiano na kuwaonyesha baadhi ya vifaa vya ujenzi wa zahanati vilivyoibwa na viongozi na kuuzwa kwa watu wasiohusika.

Wakati wakihojiana na wanavijiji hao, alifika Afisa Mtendaji wa Kata (WEO), na kuanza kuhoji uhalali wa mwandishi wa habari kufika kijijini hapo ambapo alimtaka aonyeshe kitambulisho chake cha kazi.

Huku akiwa ni mwenye hasira kali na kwa woga wa kuumbuliwa katika vyombo vya habari alikitupa chini kitambulisho hicho na akakipiga teke kisha kumpiga ngumi mwandishi huo wa REDIO KIFIMBO na kusababisha kupoteza baadhi ya vifaa vyake vya kazi.

Kitendo cha kupigwa kwa mwanahabari Maliki Selemani kiliwakera wananchi na hasa baada ya kuona kwamba waliyemtegemea kulinda amani ndiye anakiuka haki za binadamu na kumpiga mwandishi asiye na hatia. Na hapo ikatokea purukushani kati ya wanakijiji na mtendaji huyo. Baada ya tukio hilomtendaji huyo wa Kata ya Chali Isanga alitoweka katika mazingira ya kutatanisha na siku ya pili yake alifika akiwa na askari na kuanza kuwakamata baadhi ya wananchi.

Inadaiwa kukamatwa huko kunafuatia agizo la Mkuu wa Wilaya ya Bahi Bi Betty Mkwasa, hadi sasa Mtetezi BB Dominic na wananchi wengine sita wamekamatwa, kufunguliwa shitaka la uchochezi na kusababisha vurugu kijijini. Baada ya kukamatwa walipelekwa Dodoma mjini kwa uchunguzi zaidi kutokana na tukio hilo.

Baada ya kufanyika jitihada wakiwa katika kituo cha Bahi na kwa kuhofia kwamba kitendo cha kuendelea kumkamata mwandishi wa habari kingeleta kelele nyingi mwandishi huyo aliachiwa na kubakizwa Mtetezi wa Haki za Binadamu BB Dominic na wananchi hao sita. Mpaka sasa wahusika bado wako kizuizini na hawana msaada wowote na kwa taarifa tulizonazo wamebambikiziwa kesi nyingine ya kujeruhi.

RAI YETU

  • Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu haujaridhishwa na mazingira ya kukamatwa kwa mwanachama wake na wananchi waliotajwa kwa sababu kwa mujibu wa katiba yetu, kila mwananchi anahaki ya kupata taarifa sahihi za mapato na matumizi ya serikali katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na vijiji halmashauri za wilaya na serikali kuu. Lengo likiwa ni kuzingatia uwazi ambayo ni nguzo muhimu katika kulinda utawala bora.
  • Tunalitaka Jeshi la polisi Mkoani Dodoma na Wilayani Bahi watimize majukumu yaokisheria na kuacha kutumika na baadhi ya viongozi was serikali wasiojua misingi ya utawala bora na haki za binadamu.
  • Mtandao wa Watetezi unalitaka Jeshi la Polisi kuwaachia huru watetezi hao kwani makosa waliyotuhumiwa kwa malengo ya kuwaridhisha watawala katika eneo la Bahi yanaruhusu dhamana.
  • Tunawataka viongozi wote wa serikali wenye nia mbaya dhidi ya watetezi wa haki za binadamu hapa nchini kuacha mara moja kutumia vyombo vya dola kuwakandamiza watetezi wa haki za binadamu.
  • Pia Mtandao unawasihi viongozi wote waheshimu kazi za waandishi wa habari kwani kitendo cha Afisa Mtendaji wa Kata kumpiga ngumi mwandishi wa habari na kukanyaga kitambulisho chake ni kunyume na utawala bora na kuingilia uhuru wa habari.


Onesmo Olengurumwa

MRATIBU MTANDAO WA
WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU.

---

Board of Directors:
Dr. Helen Kijo Bisimba, Kharous Mpatani, Martina Kabisama, Tike Mwaipabipile, Joseph Parsambei, Saed Kubenea, Hamisa Mmanga and Ernest Kimaya.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment