Friday 21 October 2016

[wanabidii]

UAMUZI wa Ikulu kufuta mialiko ya viongozi mbalimbali kushiriki kuzima Mwenge wa Uhuru mkoani Simiyu umefichua namna fedha za umma zinavyotafunwa kupitia malipo ya masurufu (imprest) Raia Mwema likielezwa kuwa saini moja ya kiongozi katika kitabu cha wageni wizarani au idara yoyote ya serikali inaweza kufanikisha uchotaji wa hata shilingi milioni moja.

Raia Mwema limeelezwa na vyanzo vyake mbalimbali kwamba umekuwa ni utamaduni mkongwe kwa viongozi wengi wa umma kufuja fedha kila wanapokuwa na safari za kikazi na wamekuwa wakifanya hivyo kupitia masurufu na kwa ustadi mkubwa wamekuwa wakikwepa kunaswa katika kashfa za udanganyifu.

Masurufu ni malipo ya fedha kwa watumishi wa umma kwa ajili ya kufanya kazi maalumu na sehemu ya fedha inayobaki baada ya kazi husika kukamilika hutakiwa kurejeshwa au hata ile iliyotumika hutakiwa kuthibitishwa kwa risiti ama uthibitisho mwingine wa nyaraka.

Mbali na mchezo huo mchafu kupitia malipo ya masurufu, Raia Mwema pia limeelezwa namna Rais Dk. John Magufuli alivyoshituka 'dakika' za mwisho kuelekea kilele cha siku ya kuzima Mwenge wa Uhuru huku tayari mialiko ikiwa ilikwishakusambazwa na kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo na baadhi ya waalikwa wakiwa ama wamekwishafika mkoani Simiyu au wakiwa njiani kwenda.

Ufisadi wa masufuru

Inaelezwa kwamba kwa viongozi wa umma, hasa waandamizi kwa ngazi ya kitaifa, kila wanapopata safari hulipwa masurufu ambayo mara kwa mara, wengi hushinikiza walipwe kiwango cha juu.

Baada ya kulipwa masurufu hayo Raia Mwema limeelezwa, kwa mfano, katika tukio la majuzi la kwenda Simiyu kuzima Mwenge wa Uhuru, kiongozi, mbali na kulipwa posho yake ya kawaida, hulipwa imprest inayoweza kufikia hata mara tano ya jumla ya posho anayolipwa na baada ya hapo, kazi inabaki kwake namna atakavyohalalisha matumizi ya imprest yote hiyo (bila kurudisha chenji).

"Kiongozi anaweza kutoka mkoa fulani kwenda Simiyu, kabla ya kwenda Simiyu, atajipitisha kwanza Dar e Salaam ambako hana shughuli maalumu na muhimu, anaweza hata kwenda pale Wizara ya Elimu, akasaini daftari la wageni hata kwa mlinzi na hiyo inamsaidia kuthibitisha kwamba alikuwa Dar es Salaam kikazi, atalala Dar es Salaam kwa siku kadhaa kwa kadiri ya saini zake– hapo ataweza kuhalalisha malipo ya siku hizo na matumizi mengine.

"Baada ya hapo akiwa anakwenda Simiyu njiani anaweza kufika ofisi nyingine ya serikali katika mikoa ya njiani, huko nako atasaini daftari la wageni kuonyesha kwamba alikuwa kikazi katika ofisi fulani. Anaweza kufanya hivyo katika maeneo mbalimbali kwa kufika katika ofisi za umma.

"Sasa kama watu wa ufuatiliaji wanataka kujiridhisha kwamba alikuwa maeneo hayo kikazi ili asirejeshe masurufu, inakuwa rahisi kupata ushahidi. Watakwenda kukagua madaftari ya wageni katika wizara au idara husika za umma, watakuta tarehe fulani alifika hapo na huko kwingine pia watakuta alifika katika tarehe husika. Kwa hiyo tayari fedha za umma zitakuwa zimepotea bila kazi ya maana," kinaeleza chanzo chetu cha habari.

Jinsi alivyoshituka Magufuli

Raia Mwema limeelezwa kwamba hadi mialiko inatolewa, ilikuwa inaeleweka kwamba utaratibu wa utoaji mialiko hiyo ungekuwa katika mfumo wa kawaida.

Katika mfumo huo, waalikwa katika shughuli ya uzimaji Mwenge wa Uhuru ni kila Mkuu wa Mkoa ambaye katika hafla hiyo huwakilisha mkoa wake. Mbali na mkuu wa mkoa, mwingine ambaye kutoka kila mkoa hupatikana kwa kuteuliwa na mara nyingi huwa mkuu mmojawapo wa wilaya katika mkoa husika. Kwa hiyo kila mkoa hutoa wawakilishi wawili kusafiri kuhudhuria uzimaji mwenge.

"Safari hii hali imekuwa tofauti, karibu kila mkoa umetoa watu zaidi ya 10, mikoa mingine watu zaidi ya 20," kinaeleza chanzo chetu cha habari.

Hali hiyo inathibitishwa na taraifa ya Oktoba 12, mwaka huu, kutoka Ikulu, kuhusu uamuzi wa Rais Magufuli kuagiza viongozi wote wa serikali walioalikwa kuhudhuria sherehe hizo za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kutohudhuria sherehe hizo.

Katika agizo hilo, Magufuli aliwataka waliokwikushalipwa fedha za posho na safari kwa ajili hiyo kuzirejesha.

Katika kuthibitisha 'utitiri' wa viongozi walioalikwa, taarifa hiyo ya Ikulu iliyotolewa na na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, ilieleza; "Viongozi waliotajwa ni pamoja na wakuu wote wa mikoa, wakuu wote wa wilaya, wakurugenzi wote wa mamlaka za serikali za mitaa, mameya na wenyeviti wote wa halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya pamoja na watumishi ambao huambatana nao wakiwemo madereva na wasaidizi wao ambao kwa idadi hufikia takribani 1,500.

Taarifa za taasisi mbalimbali za uchunguzi, hasa ile ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali za (CAG) kwa muda mrefu sasa zimekuwa zikifichua namna fedha za umma zinavyotafunwa.

Kwa mfano moja ya ripoti zilizowahi kuwasilishwa bungeni na CAG iliweka bayana namna fedha za serikali kupitia masurufu zinavyotafunwa.

Katika moja ya ripoti hizo za CAG iliyoishia Juni 2013 ilielezwa jinsi masurufu ya takriban shilingi 288,923,451 yalivyoshindwa kuonyeshwa katika taarifa za fedha za idara mbalimbali za umma, kwa mujibu wa kanuni namba 103 (1) ya kanuni za fedha za umma ya mwaka 2001.

Kanuni hiyo inataka masurufu hayo kurejeshwa mara tu baada ya shughuli iliyokusudiwa kukamilika.

Aidha, imekuwa ikielezwa mara kwa mara na CAG kuhusu kuwapo kwa kasoro katika kuzuia udanganyifu serikalini, kwa kurejea viwango vya kimataifa vya ukaguzi (ISSAI 1240) ambavyo vinafafanua kuwa "udanganyifu ni kitendo cha makusufi kinachofanywa na mtu moja au zaidi ndani ya menejimenti na wale wanaohusika na uongozi, wafanyakazi au watu wa nje, wakishiriki kwa njia ya udanganyifu ili kujinufaisgha kwa njia zisizo halali.

Raia Mwema

Maoni yangu

Hakika watanzania hatukukosea kumchagua Dr. Magufuli, sijui leo ingekuwaje kama tungemchagua yule mwingine mwenye kashfa tata za ufisadi na utajiri ambao anashindwa kuutolea maelezo.

ASANTE MUNGU KWA KUTUNUSURU NA JANGA WATANZANIA KWA KUTUPA RAIS MAGUFULI

0 comments:

Post a Comment