Friday, 21 October 2016

[wanabidii]

TANGAZO la muswada wa sheria ya uhalifu wa kimtandao (Cybercrime Bill) lililowekwa hadharani na serikali katikati ya mwaka jana liliniweka katika kipindi kigumu. Kwa upande, kama mmoja wa watumiaji wakubwa wa mitandao ya kijamii sambamba na kuwa miongoni mwa mabloga wa kwanza kabisa wa Kitanzania, ni muumini mkubwa wa uhuru wa habari.

Ninaamini kwa dhati kuwa uhuru wa habari ni haki ya msingi ya kila binadamu, iwe kueleza habari, kupata au kupatiwa habari.

Kwa hiyo kutetea muswada huo ambao baadaye ulipitishwa na kuwa sheria lilikuwa suala gumu kwangu. Nilitambua bayana kuwa muswada huo ukiwa sheria, ungeweza kutumiwa vibaya na vyombo vya dola kuwanyima wananchi uhuru wao kwenye habari na maoni.

Hata hivyo, nilikwishawahi kuwa mwathirika wa makosa ya kimtandao. Wakati fulani nilifikia hatua ya kutaka kujiondoa kwenye mtandao mmoja wa kijamii baada ya kuandamwa mfululizo pasipo sababu yoyote ile. Kwa hiyo, licha ya hofu kuwa muswada huo ungeweza kuzaa sheria yenye athari kwa uhuru wa habari na maoni, kwa kuzingatia uzoefu wangu mwenyewe nilivyonyanyaswa mtandaoni, ikanibidi tu niuunge mkono muswada huo.

Lakini pamoja na kuunga mkono hadi ulipopitishwa na kuwa sheria (Cybercrime Act), sijaridhishwa na ufanisi wake, ambapo sheria hiyo imeonekana kwa kiwango kikubwa kuwa na nguvu dhidi ya wanaofanya makosa ya kimtandao dhidi ya viongozi na sio dhidi ya wananchi wa kawaida.

Naendelea kuamini kuwa tatizo sio sheria hiyo bali utekelezaji wake. Na hilo ni tatizo letu takriban kwenye kila sheria. Laiti ikitumika vyema bila kubagua kati ya viongozi na wananchi basi kwa hakika itasaidia kufanya maisha yetu mitandaoni kuwa ya amani.

Nimekumbuka harakati za kuutetea muswada huo na baadaye sheria husika baada ya kubughudhiwa mno na jitihada zinazofanywa na kada mmoja maarufu wa chama kimoja cha upinzani huko nyumbani, ambaye kwa wiki kadhaa sasa amekuwa akifanya kila jitihada kutuaminisha umma kuwa Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Rais Dk. John Magufuli ni feki.

Miongoni mwa misingi ya hoja yake hiyo ni madai kuwa hajaona machapisho ya kitaaluma ya Dk Magufuli, kitu ambacho licha ya kuelezwa amegoma kukikubali ni kwamba uamuzi wa kuandika na kuchapishwa maandiko ya kitaaluma ni uamuzi binafsi, isipokuwa tu kwa wahitimu wanaobaki vyuoni kama wahadhiri.

Hiyo haimaanishi kwamba mtu aliyehitimu shahada iwe hiyo ya uzamifu, uzamili au ya kwanza, hapaswi kutoa machapisho ya kitaaluma kwa vile tu hatarajii kuwa mhadhiri. Tofauti kubwa ni kwamba wakati ni muhimu kwa 'wasomi' waliopo vyuoni kama wahadhiri kutoa machapisho ya kitaaluma, wanafunzi au wahitimu wa shahada hawalazimiki kufanya hivyo isipokuwa kwenye dissertation au thesis zao.

Lakini huyo kada wa upinzani hajaishia kwenye madai hayo tu bali amekwenda mbali na kudai kuwa rais aliandikiwa PhD yake. Kadhalika, amehusisha hoja yake hiyo na uteuzi wa msomi mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuwa mwenyekiti wa bodi moja ya taasisi ya umma, kama fadhila ya Dk Magufuli kwa Profesa aliyekuwa msimamizi wa PhD yake (na aliyemwandikia PhD hiyo).

Kijana huyo anadai kuwa kabla Serikali ya Dk Magufuli haijaanza uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma, aanze yeye kuhakikiwa PhD yake. Asichosema ni kuwa uhakiki huo wa PhD ya Dk Magufuli ufanyike vipi, Rais akiombe Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufanya uhakiki? Aiombe wizara kumhakiki? Au amwite kijana huyo athibitishe yeye mwenyewe? Na athibitishe nini kati ya chapisho la mwisho wa PhD (thesis) au cheti cha shahada ya uzamivu?

Kama mtu ninayefahamu vema kibarua cha kusaka shahada ya uzamivu, nilijaribu kumuelimisha kada huyo lakini akanigeuzia kibao kwa hoja zisizo na mashiko.

Kasoro kuu katika hoja ya kada huyo ni kutoa hukumu kabla ya kuweka hadharani uthibitisho wa hoja yake. Kwa kuwa yeye ndiye mwenye tuhuma, basi jukumu la kuzithibitha (burden of proof) kuwa PhD ya Dk Magufuli ni feki lipo mikononi mwake na sio kwa rais wetu.

Na jaribio lake la kujitetea kuwa anatumia haki ya kutoa maoni halina mashiko kwa sababu haki huendana na wajibu. Pasipo uthibitisho wa madai yake, anachokifanya kada huyo ni uzandiki, na hilo ni kosa kubwa linaloangukia kwenye uzito wa makosa ya ugaidi, uhujumu wa uchumi na hujuma (shughuli kuu nne za adui kwa mujibu taaluma ya usalama wa taifa)

Raia Mwema
 

0 comments:

Post a Comment