Thursday, 6 October 2016

[wanabidii] Tulifanya uamuzi sahihi kumchagua Magufuli

MIRIAM, wewe ndiye binti yangu wa kwanza, sitaki kuelezea misukosuko ambayo mimi na mama yako tulipitia tulipokuwa vijana kabla wewe hujazaliwa. Hata hivyo, nataka uelewe kuwa maisha yamejaa ahadi nyingi na ni matumaini yetu utaishi kwa furaha na afya kwa vile tumeshaanza kuona mwanga wa nchi unayoishi.

Kama wazazi wengine, tungependa kuona unaishi maisha bora kuliko sisi wazazi wako.

Moja ya jitihada tulizofanya kuhakikisha unakuwa na maisha bora ni uamuzi tuliofanya wa kumchagua Dk John Magufuli kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano. Kabla sijafika mbali, Rais hakuishia kwenye ahadi tu lakini ametekeleza kwamba sasa watoto mnasoma bure hadi kidato cha nne.

Tulichagua kiongozi ambaye tuliamini atasimamia misingi ya haki na utu kwa watu wote. Hakika uamuzi wetu haukuwa wa kukurupuka, hatukushawishiwa na mtu, hatukupewa zawadi ya khanga wa tisheti ili tumchague kiongozi huyu.

Na hatukufanya uamuzi huo kwa sababu ya maslahi yetu binafsi bali kwa maslahi ya taifa kwa sababu sisi wazazi tuna jukumu la kuwanusuru watoto dhidi ya majanga mbalimbali yanayoikabili dunia kwa maslahi ya kizazi kijacho.

Tunaamini kila binadamu ana haki sawa na hii inajumuisha maisha na mustakabali wa kizazi cha sasa na kijacho. Nchi yetu sasa inaweka mipango ya kuboresha maisha ya watu wake sio tu kwa sisi tuliofanya uamuzi wa kumchagua kiongozi huyu lakini zaidi ni kwa ajili ya kizazi chenu na watoto wenu.

Miriam, sisi wazazi wako ni wafanyakazi. Kwa miaka yote ya utumishi wetu tumekuwa tukichangia pato la taifa kwa kulipa kodi kupitia mishahara yetu. Hata hiyo, nasikitika kukwambia kuwa mapato yanayotokana na kodi zetu hayakutosheleza kuiwezesha serikali kutoa huduma bora kwa watu wake.

Ndio maana tulikuhamisha kutoka ile shule ya Kata uliokuwa ukisoma mwanzo kwa kuwa ina upungufu wa walimu, vitabu na madawati. Ukosefu wa walimu na vitendea kazi ulisababisha mkifika shuleni badala ya kusoma mnacheza tu hadi muda wa kurejea nyumbani unapowadia. Ulikuwa ukirejea nyumbani ukiwa umechoka sana na hakuna la maana ulilojifunza.

Tukakupeleka kwenye hii shule unayosoma sasa, Mimi na mama yako tuliamini kuwa kwa kuwa ni shule ya madhehebu ya dini, watumishi na wamiliki bila shaka watakuwa wanaongozwa na nguvu ya kiroho achilia mbali maadili hivyo ungepata elimu bora kulingana na uwezo wa kipato chetu.

Tofauti na matarajio yetu kumbe shule hizi huendesha mambo yao kwa matakwa yao hata ada wanazotoza hazilingani na huduma wanayotoa.

Hata hivyo usihofu! Kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Dk Magufuli itawekeza katika elimu tutakurudisha ukasome katika shule za Serikali kwa kuwa tunaamini utapata elimu bora bila sisi wazazi wako kutoa michango wala ada.

Ndio maana hapo awali nilikwambia tumefanya uamuzi sahihi kuchagua kiongozi atakayesimamia haya yote ili kuboresha maisha hasa ya watu wa kipato cha chini kwa kuboresha huduma hasa za elimu na afya.

Afya bora ndio msingi wa maisha, leo hii jamii tunayoishi inapoteza watu wengi kutokana na vifo vinavyosababishwa na magonjwa ya milipuko ikiwemo malaria ambayo husababishwa na hali ya uchafu wa mazingira tunayoishi.

Pamoja na hayo lakini vifo vingi vimeendelea kugharimu maisha ya watu wengi vikisababishwa na magonjwa ya moyo, saratani, kupooza na magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi, kifua kikuu na mengine mengi.

Kwa kuwa kiongozi tuliyemchagua anatambua hilo, siku chache baada ya kuingia madarakani alifanya ziara ya kutembelea hospitali kuu ya taifa na kujionea hali mbaya za wagonjwa wakiwa wamelala chini kwa kukosa vitanda na wengine wakipoteza maisha kwa kukosa fedha za kununulia dawa.

Kiongozi wetu mahiri hakutaka kuchukua bakuli na kupita kwa wafadhili kuomba msaada. Alitumia ujasiri aliopewa na Mwenyezi Mungu akaagiza fedha zote zilizopangwa kutumika kwa ajili ya sherehe za kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais, zipelekwe hospitali kwa ajili ya kununua vitanda ili kuwaondolea adha wagonjwa wanaolala chini pamoja na kuboresha huduma ya afya.

Miriam, unaweza ukaona kama hili ninalokuhadithia ni simulizi tu la kusadikika lakini haya yametokea kweli na huyo ndio kiongozi ambaye mimi na mama yako tulifanya uamuzi wa kumchagua aongoze Taifa hili changa kwa maslahi ya kizazi hiki na kijacho.

Nilikuuliza tarehe 9 Desemba ni sikukuu ya nini hapa nchini ukaniambia ni Uhuru wa Tanzania, ndio maana nikacheka, sikumaanisha kukucheka ila nilifurahi kwa kuwa ulijibu kwa kujiamini.

Ni kweli mwanangu nchi yetu ilipata Uhuru tarehe 9 Desemba mwaka 1961, wakati huo ikiitwa Tanganyika na baada ya miaka mitatu iliungana na Zanzibar na kuundwa nchi inayojulikana kwa jina la Tanzania. Ni miaka 54 imepita tangu tumepata uhuru hata hivyo sina muda wa kutosha kukueleza kwa kirefu.

Mimi na mama yako tunaamini mtafundishwa vizuri hivyo utapata nafasi nzuri ya kumuuliza mwalimu wako na kujua mengi kuhusu siku hii muhimu katika historia ya nchi yetu. Ingawa nimekurudisha shule ya kata, naamini walimu watakufundisha vizuri. Kwa kuwa serikali imeamua kuwekeza katika elimu ya msingi hadi kidato cha nne hivyo kuanzia mwakani elimu mtapata bure.

Bila shaka walimu watafanya kazi yao vizuri zaidi kwa kuwa watalipwa maslahi yao kwa wakati na serikali itaweka vitendea kazi vya kutosha ili mpate elimu bora na sio bora elimu. Ila kuna jambo moja nataka uelewe kuhusu uhuru, miaka yote kumbukumbu ya uhuru ilisherehekewa kwa namna mbalimbali zikiwamo ndege za kivita kuruka kwa mbwebwe angani, gwaride na halaiki za watoto.

Wakati ukiwa mdogo tuliwahi kwenda uwanjani kushuhudia maadhimisho hayo sijui kama bado unakumbuka, ila inasemekana maonesho yale yaligharimu pesa nyingi ambazo ziliishia kulipia makandarasi wafanyabiashara wajanja na nyingine kuingia kwenye mifuko ya wadau. Mwaka jana mambo yalikuwa tofauti kabisa.

Kiongozi huyu tuliyemchagua mimi na mama yako alisema badala ya sherehe ni vyema tukafanya usafi wa mazingira ili kutafsiri kwa vitendo kaulimbiu yake ya Hapa Kazi Tu ambayo inaendana na falsafa za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuhusu Uhuru na Kazi.

Sizungumzii kiongozi mwingine bali Dk Magufuli ambaye wakati tunaenda kupiga kura za kumchagua, jirani zetu walitubeza kwa maneno ya kejeli kwamba tunaenda kuyaweka maisha yako na ya watoto wengine rehani.

Maneno yale hayakutukatisha tamaa, kwani tuliamini katika dhamira zetu kwamba tuko sahihi na pia ilikuwa ni kutumia demokrasia yetu kumchagua kiongozi tunayemtaka kwa maslahi ya maisha yako.

Kamwe tusingethubutu kuyaweka rehani maisha yako kwa kudanganywa na watu wachache wenye tamaa ya kuiba mali ya umma kwa maslahi yao binafsi na familia zao.

Utafika wakati ambao utaona wazi kuwa mimi na mama yako tumefanya uamuzi sahihi kumchagua Dk Magufuli kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa Taifa litakuwa kwenye mikono salama na hivyo wewe na watoto wako mtaishi maisha bora kuliko tulivyoishi sisi. Sasa hivi mwanangu, Rais Magufuli amesimamia vyema maadili serikalini na kwakweli amerejesha heshima ya utendaji kazi. Hakuna watu kufanya kazi kwa mazoea.

Lakini kuna watu wa ajabu sana, kwani pamoja na hatua za kutumbua majipu ambazoe amekuwa akifanya kuna wajanja wachache kule Kagera, walitaka kula pesa za maafa! Lakini Magufuli si mjinga, wamekwishatumbuliwa! Ahadi zake nyingi sasa zinatekelezwa.

Ndege alizoahidi ili kunusuru shirika la ndege na kuboresha safari za ndani na utalii tayari ziko kwenye ardhi yetu, ahadi ya kuhamia Dodoma katikati mwa nchi yetu imeanza kutekelezwa, zile barabara za juu zinajengwa mbali na usafari wa mwendo kasi...

Yaani ninaiona Tanzania yenye nuru kubwa mbele ya safari mwanangu. Vizazi vya sasa naona mtakuwa na maisha mazuri na yenye matumaini endapo tu mtazingatia uzalendo kwa nchi hii, mtafurahia maisha endapo mtajenga tabia ya kuepuka rushwa na ufisadi, na kupenda kufanyakazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo.

Mimi na mama yako bado tuko pamoja kumuunga mkono kiongozi huyu mahiri kwa kuhakikisha, "Hapa Kazi Tu!"

Baba Miriam
 

0 comments:

Post a Comment