Sunday, 7 August 2016

[wanabidii]

KUNA hatari kwamba endapo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hakitajiangalia vizuri katika hali yake ya kupoteza mwelekeo ambao tunauona sasa hivi sasa kinaweza huko mbeleni kikaja na harakati nyingine za kuhamasisha watu kuandamana dhidi ya serikali au juu ya jambo fulani na wakaamua kuita harakati hizo 'Ukutiukuti'!

Tunaweza kuwaona siku moja wakishikana mikono na kuanza kuzunguka kwa pamoja huku wakitaka wengine nao washiriki kucheza na kurukaruka huku wote wakiimba "ukuti ukuti, wa mnazi wa mnazi, ukiingia upepo watetema!" Nina sababu ya kuhofia hili. Tulipokuwa watoto wadogo tulicheza michezo mbalimbali ambayo ilitufundisha misingi mbalimbali ya kimaisha. Kupitia michezo hiyo tulijifunza urafiki, kusaidiana, kushirikiana, kuwa mwangalifu, ujanja na hata mahusiano kati ya watu wa jinsia tofauti.

Kwa kadiri tulivyokuwa ndivyo michezo mbalimbali tuliipita tukaingia katika aina nyingine za michezo hadi kwenye shule na vyuo vya juu. Michezo ambayo tulicheza ni mingi na ilikuwa na aina yake ya ushindani; kuanzia Kombolela, Kula mbakishie baba, Kioo alikivunja nani, Banchikicha, Turinge Bayoyo, na michezo mingine mingi ya utotoni. Katika michezo yote hiyo, naamini ipo ambayo hadi leo ukikumbuka inakupa tabasamu kwani inakurudisha miaka ile ya kutokuwa na hatia na furaha ya maisha; mmoja wa hiyo ni huu wa 'ukutiukuti'.

Watoto kutoka mtaani au hata mtaa wa jirani walijikusanya pamoja mara nyingi baada ya michezo mingine yote kuisha wanashikana mikono katika mduara na kuanza kuimba huku wakizunguka na kuruka ruka. Huu ni miongoni mwa michezo iliyohusisha watoto wa kike na wa kiume. Wanapofika mwisho watoto wameanguka, wanacheka na kuagana au kwenda majumbani mwao wakiwa na furaha. Ni miongoni mwa michezo ambayo hata dada na kaka zao wakubwa waliweza kujumuika nao na hivyo kuendeleza mahusiano mazuri.

Siasa zetu sasa hivi zilipofika hasa kwenye chama kikuu cha upinzani nchini cha Chadema ni kuwa tusipoangalia wanaweza au tayari wamefikia mahali pa kuanza kuja na harakati kama burudani. Tangu walipoanza na Operesheni Sangara, Operesheni Mzizima, M4C, wengi tuliona hatari ya kampeni hizi zenye majina mbalimbali ambayo labda matokeo yake yanaweza kubishaniwa.

Kwa wanaojua, mimi sikuwahi kuwa shabiki wa lile dubwasha la Ukawa ambalo naamini lilichangia sana kuvuruga upinzani na mwelekeo wa upinzani kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Lakini kama vile ndugu zetu hawataki kujifunza au wamegoma kujifunza baada ya kikao chao kingine wameamua kuja na kampeni nyingine au operesheni nyingine ambayo sasa wameamua kuiita 'Ukuta' ukiwa ni Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania.

Kimsingi, wameamua kuja na operesheni ya kupinga uongozi wa Rais Magufuli. Nina uhakika wa kutosha kati ya operesheni zitakazoshindwa vibaya ni hii. Kwa sababu wakati ile nyingine kwa kiasi ziliakisi hisia za Watanzania wengi na zilibeba kwa kiasi maudhui ya matamanio yao hii ya sasa ni operesheni ya wasomi wachache (the few elite) ambao wanaamini kinadharia na kwa sababu zao za kisomi kuwa Magufuli ni dikteta. Wanaamini hivi na wanataka watu wa kawaida ambao hawaoni huo udikteta wa Magufuli waunge mkono.

Operesheni hii itafeli kwa sababu, mamilioni ya Watanzania waliokuwa wanalalamikia watoto wao kukosa madawati leo wanaona madawati yanatengenezwa na kupatikana kwa wingi, waliokuwa wanalalamikia watu kutokuwajibika au kuwajibishwa wanaona watu vigogo wanawajibishwa kila kona, na wale ambao walikuwa wanataka kuona serikali inasimamia vizuri watendaji wake wanaona hilo linatokea tena bila kupepeseana macho.

Wale ambao wanafikiri kuna haki ya kuonekana kwenye runinga mubashara (live) na kuamua kugoma kwa sababu hawaonekani mubashara wanaweza kupata shida. Wananchi wa kawaida wanajua ipo haki ya kujua (right to information) lakini hakuna haki ya kuonekana. Kuandamana kutaka watu waonekane mubashara wakati watu wanapata nafasi ya kujua hata bila kuona kwa wengine ni kuanza kuchanganya mambo.

Wale ambao kwa muda mrefu walikuwa wanataka mafisadi washughulikiwe bila huruma leo hii wanaanza kupinga serikali ambayo imeanzisha na kutenga fedha tayari kwa ajili ya mahakama maalumu ya kushughulikia wahujumu uchumi na mafisadi. Sasa unagoma ili kiwe nini? Serikali iache mpango huo? Unagoma ili serikali isihamasishe ujenzi wa madarasa mapya na kwa haraka? Unagoma ili watu wabovu na wasio na weledi wasiendelee serikalini? Unagoma ili tuendelee tulikokuwa?

Ndio maana hofu yangu ni kuwa tusipoangalia baada ya harakati hizi kushindwa; ndugu zetu wapendwa hawa wanaweza wakaja na operesheni "Ukutiukuti". Hii itakuwa ni operesheni ya aina yake, watu wataambiwa wasimame pamoja kuonesha umoja lakini ni umoja katika kuzunguka duara! Tatizo la kuzunguka duara ni kuwa halikomi! Binafsi ningependa kuiona Chadema inarudi na kuwa chama cha siasa na kufanya mambo yake kama Chadema, na kupitia taasisi zake.

Hizi operesheni zake mbalimbali siyo tu zinapoteza muda mrefu lakini pia zinatishia zaidi uhai wake kama chama cha siasa na kwa vile viongozi wake hawajawajibishwa kwa madudu yao ya mwaka jana, basi wanaweza kabisa kwenda kuipoteza Chadema kuelekea 2020. Na wasije wakadhani kumlaumu Magufuli kwa madudu yao kutawapatia simanzi kwa wananchi; Magufuli amechaguliwa na kuungwa mkono na watu ambao walikuwa wanatamani mabadiliko ya kweli. Atahukumiwa na wananchi hao ifikapo 2020.

Na mabadiliko hayo watu wameyaona; hayahitaji kupewa jina la operesheni. Ni matumaini yangu baada ya kutoka M4C hadi Ukawa na kutoka Ukawa hadi Ukuta, wana-Chadema na wale wenye kuamini siasa za upinzani watakuwa wamechoka na hawatokuwa tayari kuimbishwa tena Ukutiukuti au Kumbaya my Lord Kumbaya! Kwani, tukianza kufanya siasa kama burudani, wananchi na watu wanaotuamini wanaweza waka wanasubiria kama watu wanaosubiria wimbo mpya wa Diamond, Ali Kiba na wasanii wengine.

0 comments:

Post a Comment