Sunday 7 August 2016

[wanabidii]

SERIKALI imepiga marufuku mihadhara ya siasa ili kuleta utulivu utakaoiwezesha kuhudumia wananchi vizuri zaidi, lakini Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa upande wake, kinaona hatua hiyo inakinyima haki ya kufanya mihadhara kwa wanachama na wafuasi wake. Hoja zote zinajadilika na ukizipima, kila moja ina uzito wake.

Nikianza na upande wa Serikali ya Awamu ya Tano, kama nilivyodokeza hapo juu, imezuia mikutano ya kisiasa ya hadhara kwani uchaguzi mkuu umekwisha na sasa ni wakati wa kuchapa kazi. Lakini mikutano ya ndani au ya wabunge kwenda kushukuru wapiga kura wao haijazuiwa.

Hoja ya serikali ina mashiko kwamba ni wakati wa kuipa wasaa itekeleze ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyowafanya wananchi wakaichagua. Kwamba baada ya kupatikana Rais, tunatakiwa sasa tuwe wamoja, tuzungumze lugha moja, tuvae sote viatu vya 'hapa kazi tu', tukosoe kwa kuleta mawazo mbadala ambayo ni mazuri zaidi, lengo likiwa ni kusukuma nchi yetu mbele na si vinginevyo.

Dhana ni kwamba hata ukileta wazo mbadala ambalo lingeweza kuharakisha maendeleo, wananchi watakusikia na utakuwa unajijengea mtaji wa kupata kura katika chaguzi zijazo bila kuhitaji maandamano, kwani wananchi hawa si wajinga, wanajua pumba na mchele.

Kwamba kama serikali inaimba wimbo wa elimu bure, inaimba wimbo wa kumaliza tatizo la madawati, inadhibiti matumizi ya hovyo katika sekta ya umma, inatumbua majipu ambayo yametusumbua kwa muda mrefu basi busara inaelekeza kwamba sote, bila kujali itikadi zetu za kisiasa au za kidini tungeiunga mkono kwa sababu hakuna ubishi kwamba hayo ni mambo yenye manufaa kwa kila Mtanzania.

Mimi ningetegemea kuona, kwa mfano, Chadema inakuwa mstari wa mbele katika kuipiku serikali iliyoko madarakani kwenye halmashauri au majimbo inayoyaongoza kwa upande wa wabunge kwa kufanya vizuri zaidi katika kutatua kero za wananchi yakiwemo hayo mambo ya madawati, kuhamasisha ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule zetu na huduma nyingine lukuki za kijamii.

Serikali hii inadai kwamba kuendelea kuruhusu mikutano ya hadhara ni kuwachanganya wananchi, kuifanya nchi iwe kama iko kwenye uchaguzi wakati wote badala ya sasa kujikita katika shughuli za maendeleo. Wachambuzi wanaangalia hata nchi zilizotutangulia kidemokrasia kama Marekani na Uingereza, ambapo baada ya uchaguzi hakuna tena kutapakaa kwa mikutano ya kila siku ya hadhara ya upinzani.

Huko watu hugeukia kazi na kukutana kwenye majukwaa maalumu kama vile Bunge ambako ndiko utasikia sera mbadala na mitazamo mbadala ambayo inaweza kuisaidia serikali iliyoko madarakani. Kwa upande wa hoja ya Chadema, kama nilivyodokeza hapo juu inaweza kujadiliwa. Hoja hiyo ni kwamba moja ya kazi kuu ya chama cha siasa ni kutoka na kwenda kujiuza kwa wananchi. Kwamba mihadhara na hotuba ndio uhai wa chama cha siasa na kazi ya wanasiasa ni kuzungumza.

Lakini nimekuwa nikijiuliza, Je, mihadhara ya wapinzani imekuwa na afya kwa Watanzania wote? Kwamba ni mihadhara inayowasaidia walioko madarakani kuboresha zaidi utawala wao, kujifunza na kupata mawazo mbadala au ni mijadala ya kupinga kila kitu na wakati mwingine kwa lugha zisizo na staha na hivyo kuwa kero.

Ni baada ya serikali kuzuia mihadhara ya kisiasa ili kupata utulivu wa kuwatumikia Watanzania na Chadema kuona kama hatua hiyo siyo sahihi, je, namna ya kuonesha kutokubaliana na uamumzi wa serikali ni kupambana nayo kwa kuvunja amri au kuna njia nyingine za kufikia mwafaka kama vile mijadala au kwenda mahakamani?

Lakini swali la msingi ambalo wengi tumekuwa tunajiuliza kila tunapoangalia mwenendo wa Chadema tangu ilipoanza kuongozwa na Freeman Mbowe, ni kama hizi operesheni zake kama ile ya Sangara, maandamano na kususia vikao vya Bunge zimekuwa na faida yoyote kwa chama hicho katika kujijenga kisiasa? Hivi karibuni , Chadema ilipotangaza nia ya kufanya mikutano ya hadhara nchini kote kuanzia Septemba Mosi, kuna ambao wameipa ushauri wa bure na sijui kama wataufanyia kazi.

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi ambaye ni mlezi wa vyama vya siasa, ni miongoni mwa watu waliozungumzia uamuzi huo wa chama. Amesema amepokea kwa masikitiko makubwa tamko hilo akisema kimsingi Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992 kifungu (2) (c) inakataza chama cha siasa kutumia au kuhamasisha matumizi ya nguvu au vurugu kama njia ya kufikia malengo yake kisiasa.

Anasema kifungu cha 9 (2) (f) kinakataza chama cha siasa kuruhusu wanachama au viongozi wake kutumia lugha ya matusi, kashfa na uchochezi ambayo inaweza kusababisha kutokea uvunjifu wa amani. Ndipo akasema: "Tamko la Chadema ni ukiukwaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa. Aidha, hii si mara ya kwanza kwa Chadema kutumia lugha za namna hii za kuhamasisha uvunjifu wa amani."

Ni katika muktadha huo, Jaji Mutungi anavitaka vyama vya siasa kuwa na ustahimilivu kwani siasa haitaki hasira. Nao wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuanza na Profesa Kitila Mkumbo anasema vyama vya siasa vina wajibu wa kulinda misingi ya demokrasia lakini pia vina haki ya kupigania kufanya shughuli za siasa ingawa si kwa mapambano. Naye Dk Bashiru Ally anasema kauli ya kufanya mikutano nchi nzima ni vyema ikafafanuliwa, kuhojiwa au kutafsiriwa kwani hakuna mahali utaratibu, sheria na kanuni zinafuatwa kiholela.

Anasema uholela haujengi demokrasia bali ni chanzo cha chuki na hata kuumiza, hivyo ni vyema yawepo mazungumzo ili kufikia mwafaka na kama yupo asiyeridhika aende mahakamani. Kwa upande wake, Dk Benson Bana anasema kukaidi agizo linalotolewa na vyombo vya dola sio jambo jema na kwamba ni vyema kuheshimu kwani ndio njia ya kukuza demokrasia. Anafafanua kwamba mpango wa maandamano siyo suluhisho la maridhiano ya kisiasa na badala yake utaleta vurugu na kuchochea uvunjifu wa amani.

"Kutumia ubabe hakuwezi kuzaa mwisho mwema kwao, wangeweza pia kutumia Bunge lakini walilikwepa, hivyo si njia za kiungwana kufanya mikutano hiyo kwa nchi nzima na watambue kuwa hawatoungwa mkono," anasema Dk Bana. Mbali na mawazo hayo ya wasomi, lakini nimekuwa nikijiuliza maswali haya. Hivi karibuni, nilimsikia aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho, Edward Lowassa, akisema ataisaidia Chadema kutoka kwenye 'uharakati' akimaanisha kuachana na mambo kama maandamano na migomo na hivyo kuja na siasa za kistaarabu zaidi.

Je, amekutana na masikio yasiyosikia la mwadhini wala mkimu swala? Na je, Chadema haikujifunza chochote kutokana na andiko linaloaminika kwamba lilikuwa sababu ya kutimuliwa kwa akina Kabwe Zitto, Profesa Mkumbo na Samson Mwigamba kwenye chama hicho? Andiko hilo lilionesha dhahiri kwamba operesheni za maandamano hazijakisaidia chama hicho kisiasa.

Katika waraka wao walioita wa mabadiliko, akina Mkumbo waliandika hivi: "Ni dhahiri kwamba uongozi uliopo umeishiwa mbinu... Kuchoka kwa uongozi wetu kunaonekana dhahiri katika mipango na mikakati ya taasisi ya miaka kadhaa. Mfano mwaka 2008 uongozi ulianzisha mkakati wa operesheni Sangara. Hiyo ilifanyiwa kazi katika mikoa kadhaa na hatimaye ikafa kimya kimya.

Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kulianzishwa matembezi ya maandamano ambayo nayo yalikuwa yakipeleka ujumbe kwa watu na yalipangwa kufanyika mikoa yote na wilaya zote... kisha nayo yakafa kifo cha mende. Kisha mwaka 2012 ikaanzishwa operesheni ya mabadiliko maarufu kama Movement for Change (M4C).
Hiyo ilikuwa inakwenda kwenye mikoa na timu kama nne hivi ambazo kwa ujumla zilitathmini hali ya mtandao na uongozi wa taasisi, kuhamasisha umma kwa njia ya mikutano ya hadhara, kuingiza wanachama na kusimika uongozi na hatimaye kufanya mafunzo kwa viongozi.

Hiyo ikafanyika Mtwara na Lindi, Morogoro na kisha ikaenda kufia Iringa. Kitendo hiki kwa peke yake, cha kufeli kwa kila mkakati unaoletwa na viongozi wetu katika hatua za utekelezaji unaofanywa na wao wenyewe waleta mkakati ni kiashiria tosha kwamba uongozi uliopo umechoka..." Labda Chadema hii ni sikio la kufa!

0 comments:

Post a Comment