Saturday 4 May 2013

[wanabidii] Virusi vya Azimio la Arusha

Makala
Virusi vya Azimio la Arusha vyaniandama
Willy Mutunga
Toleo la 292
1 May 2013
  • Tutazungumziaje Shirikisho ikiwa Muungano wa kwanza Afrika unavunjika?

NILIKUWA mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya sheria katika Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1968 hadi mwaka 1971. Kisha nikarudi tena Kitivo cha Sheria mwaka 1973 ndipo nikahitimu shahada ya uzamili mwaka wa 1974.

Nilichangua Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa sababu nilikuwa nataka kuwa mwanasheria. Ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati huo kilichokuwa kinafundisha sheria. Chuo cha Makerere (Uganda) walifundisha madaktari na chuo cha Nairobi kilifundisha mengine. 

Kwa kweli nilikuja Dar es Salaam kama mwanafunzi wa Chuo cha Afrika ya Mashariki. Vile vile nilipenda sana kusafiri nje ya Kenya. Kipindi kile katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kulikuwa na vuguvugu kubwa ndani na nje ya Jumuiya ya chuo – mijadala juu ya Azimio, mijadala juu ya mfumo wa Ujamaa nchini na ulimwenguni, - sisi wanafunzi tulijitosa katika mijadala hiyo bila kujali nchi tulizokuwa tunatokea – kwa sababu hizi zilikuwa zama za Udugu wa Afrika na Ukamaradi wa kitabaka. Katika mijadala hiyo, tulifanya uchambuzi wa kina wa falsafa mbalimbali za maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Uchambuzi tulioufanya kuhusu mtazamo wa Kwame Nkrumah wa Ghana na Mwalimu Julius  Nyerere juu ya mustakabali wa nchi za Kiafrika ulitufanya tuamini kwa dhati kwamba binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja.

Hadi sasa bado ninaamini hivyo. Kwa kweli nikiwa Chuo Kikuu Mlimani niliwahi kumwona Mwalimu Nyerere mara nyingi. Niliwahi kuhudhuria mafunzo ya walimu waliojulikana kwa siasa ya mageuzi. Walimu kama Issa Shivji, Karim Hirji, Henry Mapolu, Walter Rodney, Clive Thomas, Giovanno Arrighi, Joe Kanywanyi, Mahamood Mamdani, Dani Nabudere, Kwesi Bothwey, Aki Sawyer, Yash Ghai,  Sol Piciotto na wengineo.

Vile vile wageni wengi walikuja Mlimani: viongozi wa Frelimo, ANC, Black Power, PLO, Polisario, wengi walialikwa na TANU. Nilishangilia sana siasa ya USARF na TYL. Wakati huo ndio nikamjua Issa Shivji kama mwanasheria ambaye alikuwa mwanasiasa.

Wanasheria wengi wakati huo walikuwa wanataka kusoma sheria bila kujali kiini cha sheria na vile sheria yenyewe inasaidia matabaka mbalimbali kunyonya na kudhalimu matabaka mengine. Nilisoma sana maandishi ya Shivji, sana sana niliporudi kusomea shahada ya uzamili.

Nilirudi Kenya mswaka 1974 na kufundisha sheria katika Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Nairobi. Katika Chuo Kikuu cha Nairobi nilianzisha  utaratibu wa demokrasia katika darasa. Niliwaheshimu wanafunzi; niliwapa nafasi ya kujieleza bila woga; niliwatia moyo walipofanya kazi kwa bidii na kuushangilia utafiti walioufanya. Binafsi nilifaidika sana na utaratibu huo wa kufundisha sheria. Nilileta usawa baina ya wanafunzi na mimi na kwa jumla wote tulifaidi.

Utaratibu huu mpya ulileta chuki baina yangu na walimu wenzangu ambao walipendelea utaratibu wa "upasta" wa kufundisha bila kuulizwa maswali na vile vile kuwachukulia wanafunzi wa sheria kama watoto. Ujeuri huu wa walimu ulipigwa marufuku na wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mashirika kama USARF na TYL. Mwaka wa 1979 tuliunda upya chama cha wafanyakazi wa Chuo Kikuu.

Nilichanguliwa Katibu Mkuu na nikajitosa katika siasa za wafanyakazi kwa  moyo na nguvu zangu zote. Pale Chuo Kikuu siasa za upinzani na mageuzi zilisikika. Awali, Bunge, vyama vya wafanyakazi, na mashirika mbalimbali ya jamii vilinyamazishwa na chama cha "Mama na Baba," yaani KANU lakini baadaye sauti ya ukinzani ilisikika kwa nguvu chuoni, jambo ambalo lilimuudhi Mtukufu Rais Daniel  Moi.

Punde si punde nilishikwa, pamoja na viongozi wa chama chetu, na kuwekwa korokoroni. Nilifungwa kizuizuni bila mashitaka kwa miezi 16. Nilipotoka kizuizini nilifanya kazi kama wakili kwa muda Nairobi kwa miaka mitano.

Nilifanya kazi na mashirika ya kupigania haki za binadamu ambayo wakati huo yalikuwa chipukizi. Baada ya miaka mitano nilienda zangu Canada nikahitimu shahada ya Uzamivu (PhD) katika sheria na kurudi Kenya kufanya kazi na masharika ya jamii. Nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Kenya. Mfumo wa vyama vingi ulikuwa umeanza na chama cha mawakili kiliunga mkono. Ni wakati huo vile vile chama cha mawakili kilipeleka kesi kubwa ya wizi wa pesa za umma, kesi inayojulikana kama Goldenberg.

Binafsi nilivutiwa sana na misingi ya Azimio (la Arusha), maadili na misimamo ya Mwalimu. Ukweli ni kwamba tangu wakati ule  nimekuwa mkereketwa wa Azimio na Mwalimu – najiita Nyerereist DAMU kama tunavyosema sisi Wakenya.

Misingi iliyonivutia sana hasa ni: Kwanza, ni usawa ambao umezungumziwa sana katika Azimio. Lakini dhana ya USAWA si mpya kwa wanasheria kama mimi kwa sababu ndio msingi wa hizi sheria za kibwanyenye tunazofuata – kitu kinachotofautisha dhana ya USAWA ya Mwalimu ni usawa ambao unaendana na HAKI kwa maana ya 'justice', na si haki ya kisheria tu (legal justice) bali ni haki ya kijamii kwa maana ya 'social justice'.

Na USAWA huu umewekwa kwenye Katiba yetu sasa (Kenya), Katiba ambayo nimeipigania kwa miaka 40. Nilipigania kazi hii ya Jaji Mkuu ili nipate nafasi ya kuimarisha USAWA ambao ni mageuzi yanayoletwa na Katiba.

Si kazi rahisi kwa sababu kuna Wakenya wangependa haki ya kisheria tu itawale. Bila shaka Mahakama ya Upeo Kenya ina jukumu la kuimarisha USAWA na tukifanya hivyo bila shaka tutashangiliwa kama Mahakama ya Wakenya wote na kuwapatia Wakenya nguvu za kupigania mageuzi na mapinduzi zaidi.

Jambo la pili lililonivutia sana ni usawa wa binadamu wote bila kujali rangi au kabila. Kwa mtu kama mimi ambaye nimezoea kuambiwa kila mara kwamba kuna ukabila nchini mwangu, jambo hili lilikuwa la msingi sana kwangu. Na kweli tangu wakati huo kuna ukabila Kenya.

Tunabaguana kwa rangi, kabila, eneo, kazi, umri, jinsia, dini.  Ni kwa kweli nimepigania usawa wa binadamu Kenya kutokana na msingi wa Azimio la Arusha. Na bado sijachoka wala sitachoka. Kupigania mageuzi na mapinduzi hakuna uchovu! Kwa kweli tukitekeleza Katiba yetu tunaweza tukajenga taifa jipya la Kenya. Hayo 'mapambano' yanaendelea.

La tatu, na hili lina umuhimu wa kipekee kwangu ni, umoja wa Afrika – Pan-Africanism. Ndiyo maana nilifurahi sana na kufarijika niliposikia kwa mara ya kwanza kwamba Chuo chetu kimeanzisha Kigoda cha Mwalimu kwa utambilisho wa Pan- Africanism – naambiwa na Wanakigoda kwamba Kiswahili cha Pan-Africanism ni Umajumui wa Afrika – asanteni kwa kupanua msamiati wetu.

Tunajua Mwalimu alipigania sana Shirikisho la Nchi za Afrika ya Mashariki. Bila shaka tangu niwe mwanafunzi hapa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam makaramadi wangu wamekuwa watu wanaopigania shirikisho. Tungali tunaendelea na jukumu hilo. Nilifurahi sana kualikwa na Taasisi ya Warioba (Tume ya Katiba Tanzania) kuzungumzia mambo ya Katiba na shirikisho.

Mwalimu wangu,  marehemu Nabudere aliandika vitabu viwili kuhusu shirikisho ambavyo hatuna budi kuvisoma kuanzia wanasiasa na watu wa mashirika mbalimbali, na wananchi wa Afrika ya Mashariki kwa ujumla wetu na hasa wale wanaotaka shikirisho.

Watanzania hamna budi kuhakikisha kwamba matatizo kuhusu Muungano wa Tanzania (Tanganyika na Zanzibar) mnayatatua kupitia Katiba yenu mpya. Tutawezaje kuzungumzia shirikisho ikiwa Muungano wa kwanza Afrika unavunjika (Tanganyika na Zanzibar)? Nawaomba sana ndugu zangu Watanzania mliangalie jambo hili kwa makini. Njia ni moja tu: Kuimarisha Muungano wa haki, usawa, maendeleo na siasa inayopendelea wananchi kwa jumla. Hivyo basi Muungano utakuwa taa kubwa ambayo tutaitumia kumulika njia ya kuleta Shirikisho na Umoja wa Afrika.

Jambo la nne lililonivutia sana ni namna Mwalimu Nyerere alivyoifanya Lugha ya Kiswahili kuwa nyenzo ya kuwaunganisha Watanzania. Pamoja na kutambua kwamba lugha za kigeni zina umuhimu wa kipekee katika uhusiano wa kimataifa, hasa katika nyanja za sayansi, teknolojia, diplomasia na biashara, Mwalimu Nyerere alitambua pia kwamba Lugha ya Taifa,  Kiswahili, ina nafasi ya kipekee katika harakati za kujenga umoja wa kitaifa na katika kueneza siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Kule kwetu Kenya, Lugha ya Kiswahili imekwishatambuliwa kikatiba kama Lugha ya Taifa tangu 2010. Undugu na utu wa Lugha ya Kiswahili niliujua Tanzania. Baada ya kuanza masomo Mlimani nilitamani kuliona Jiji la Dar es Salaam.  Basi nikapanda DMT. Kufika Ubungo mtu mwingine akapanda basi na tukakaa pamoja. Akaniangalia na kunisalimu; Ndugu hujambo, hawajambo nyumbani? Shemeji hajambo?

Mimi namwangalia tu, Ukenya wangu waniambia sijamwona, huyo jamaa kajuaje habari za jamaa zangu hata shemeji sikuwa naye siku hizo! Baada ya muda mfupi akaniuliza, Mkenya wee? Basi ndipo tukaanza mazungumzo, tukaachana Mnazi Mmoja. Naam, undugu na utu wa Lugha ya Kiswahili utatusaidia kuunda Shirikisho letu la Afrika ya Mashariki, inshalllah.

Kwa kweli: Virusi vya Azimio vimeniandama – ninajisikia raha kuwa mmoja wa waathirika wa virusi vya Azimio. Kusema ukweli, ninajisikia raha kuwa na AIDS,  sio kwa maana ya Acquired Immunity Deficiency Syndrome bali ni African Independent Development Syndrome.

Ndiyo, mimi ni kati ya wale ambao wanaamini kwamba hatuwezi kuendelea bila kujitegemea; na kamwe hatuwezi kuendelezwa na nchi za kibeberu – na ndiyo maana, tena, na katika hili, Mwalimu ni kiongozi mmojawapo ambaye alikuwa na sifa ya kipekee – sifa ya ujeuri wa Kiafrika; ujeuri wa kufanya maamuzi ya kujitegemea, ujeuri wa kupinga ukandamizwaji wa nchi za Magharibi. Laiti tungekuwa na viongozi kama Mwalimu katika nchi zote za Kiafrika, hali ya uhuru na utu wa Waafrika ingekuwa bora zaidi kuliko ilivyo sasa.

Ningependa kuwasihi vijana wote wa kiafrika, na hasa vijana wa ukanda wa Afrika Mashariki, kwamba: Anzeni kazi ya kuambukizana virusi vya Azimio kwa kasi na bila haya ili muweze kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya ubeberu. Ni vema pia kuwakumbusha vijana kwamba, ubeberu ni janga la kimataifa na kinga ya janga hili ni Azimio.

Mwalimu ameendelea na safari yake – tuliobaki hatuna budi kuziendeleza fikra zake – si kuziimba kama kasuku bali kuzitafakari kwa makini na kwa undani. Ndugu zangu, mimi binafsi ninaendelea kuzitumia fikra za Mwalimu kama mwongozo wangu – mimi ni Nyerereist DAMU DAMU.

Makala hii ni hotuba yake aliyotoa kwenye Maadhimisho ya Tamasha la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Aprili 2013, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment