Friday 24 May 2013

[wanabidii] Uchambuzi Wa Habari: Goma Wanalilia Amani, Sisi Tumechoka Kuihubiri..!

Ndugu zangu,

Pasipo haki na usawa hakuna amani, lakini, katika jamii yeyote ile,  uwepo wa amani na utulivu ni msingi mzuri katika kutafuta haki na usawa, kwa njia ya majadiliano.

 Leo asubuhi kwenye televisheni ya Aljazeera ameoneshwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon  akiwa Goma, DRC. Pale Uwanja wa Ndege  wa Goma wameonekana akina mama wakiwa na mabango. Walikuwa  wakimlilia Ban Ki Moon awasaidie kurejesha amani na utulivu katika Goma na DRC. Kwamba wamechoka na vita.

Kwenye mitaa ya Goma wakaonekana  pia vijana wakiwa na mabango wakifikisha ujumbe wa kulilia amani kwenye msafara wa magari ya Umoja wa Mataifa. Vijana wengine wakaonekana wakiyagonga kwa mikono madirisha ya magari yaliyowabeba maofisa wa Umoja wa Mataifa.  Wanataka amani. Wamechoka na vita.

Hapa nyumbani kwenye magazeti yetu ya leo kumepambwa na picha za kuhuzunisha za vurugu za Mtwara.  Picha ya kuhuzunisha kabisa ni ile yenye kuwaonyesha akina mama na watoto  kwenye Hospitali ya Mkoa ya Ligula. Wamefika hapo kupata hifadhi. Wamekimbia vurugu. Wamekimbia mshikemshike ya polisi.

Inasikitisha, ni kwa vile tumesoma pia taarifa ya mama mja mzito anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi. Hakika, inasikitisha kuwaona watoto wenye kupitia hali hii ya mashaka makubwa.

Mara nyingi, kwenye hali ya vita na hata vurugu, ni akina mama na watoto wenye kuteseka sana. Maana, kuna hata wenye kudhalilika kwa kubakwa.

 Ndugu zangu,

Nchi yetu bado ni ya amani na utulivu. Tusifanye yale yatakayopelekea kuitumbukiza nchi yetu kwenye dhahma ya vurugu na machafuko.  Na kwa viongozi wetu, watangulize busara na hekima katika kushughulikia kadhia hii ya Mtwara na nyinginezo.

Na tunaamini, kuwa ya Mtwara ni ya kwetu wenyewe. Yanatuhusu sote na yanazungumzika. Na media yetu pia ifanye kazi yake katika kutoa taarifa sahihi zisizo za kishabiki. Iwezeshwe ifanye kazi ya kutoa Elimu ya Uraia juu ya suala hili la gesi.

Maana, pamoja na umuhimu wa kuripoti matukio ya vurugu,  hakuna faida ya kuripoti kwa namna ya kushabikia,  habari za vurugu na machafuko huku tukiacha kutoa elimu juu ya suala zima la gesi na mipango iliyopo.

Hivyo, kwa kuanzia, Serikali ichukue jihada za makusudi na za haraka za kukaa chini na wadau wenye kuhusika ikiwamo  WaTanzania wa Mtwara bila kuwasahau wazee wa Mtwara na vyombo vya habari.

Na hakika, tusipoyapa mazungumzo nafasi yake stahiki katika kutatua  kadhia hii, basi, hatari iliyo mbele yetu ni kuhatarisha amani  yetu ambayo wengine hata leo hii asubuhi tumewashuhudia kule Goma, DRC, wakiililia. Nasi tunaonekana kuwa tumechoka kuihubiri!

 Maggid Mjengwa,

Iringa.
0754 678 252
http://mjengwablog.co.tz

 

 

 

 

 

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment