Monday 1 April 2013

Re: [wanabidii] JESHI HILI JIPYA NI HATARI

Tatizo sio Boda boda tu, matatizo ya nchi hii ni mengi sana na Utawala unaona kama wao hayawahusu, kwa mfano kuna tatizo sugu la Dala dala kutanua na kusababisha foleni na usumbufu mkubwa hili nalo Serikali inaliangalia tu kama haliwahusu, kuna tatizo la vibaka kwenye mataa ambao juhudi na ubabe wako ndio utakuokoa ama sivyo unamalizwa nalo hili hawajal, kuna tatizo la ujenzi holela popote saa yeyote hili nalo jamaa wala hawana mda...kwa ufupi hii ni LAWLESSNESS STATE...Ni ubabe kwa kwenda mbele serikali ni kama haipo...



From: Joseph Beda Rupia <rupia.joseph@gmail.com>
To: wanabidii@googlegroups.com
Sent: Monday, April 1, 2013 2:19 AM
Subject: [wanabidii] JESHI HILI JIPYA NI HATARI

'Jeshi' la  bodaboda ni tishio kuliko…
 
Na Joe Beda
UKISOMA kitabu cha historia cha 'Western Civilization' utagundua kuwa ukimya uliofanywa na mataifa ya Uingereza na Ufaransa karibu kwa miongo miwili kuanzia mwaka 1920 ndio sababu ya kuzuka kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Viongozi wa mataifa hayo wa siku hizo walikaa kimya na kuitazama Ujerumani ikifanya mabadiliko ya ndani ya uongozi, ikiimarisha jeshi lake na hata ikianzisha na kutekeleza sera ya kujitanua (kutanua mipaka-expansionism).
Hilo lilikuwa kosa, lakini kosa kubwa ni pale mataifa hayo yaliponyamaza tena wakati majeshi ya Adolf Hitler yalipokwenda Hispania kupigana bega kwa bega na majeshi ya waasi yaliyoongozwa na Jenerali Francisco Franco dhidi ya serikali.
Ama kweli, mzaha mzaha hutumbuka usaha kwani vita hiyo ya Hispania ilitumiwa na askari wa Hitler kama maandalizi ya vita nyingine kubwa iliyokuja kujulikana kama Vita Kuu ya Pili ya Dunia, miongoni mwa majanga makubwa kuwahi kutokea duniani.
Ni wazi viongozi wa mataifa hayo walikiri kuwa walistahili lawama kwa unyamavu wao ambao baadaye ulikuja kupewa jina la 'Appeasement Policy' kwani walipotahamaki waligundua kuwa kitendo cha kumnyamazia Hitler na kumruhusu kufanya atakacho kilimwongezea uchu mbabe huyo wa kivita na sasa Ufaransa na Uingereza walilazimika kumpiga (kama si kupigana naye).
Hali hii ndio kama inayoonekana sasa nchini mwetu ambapo vijana wanaoendesha pikipiki za kubeba abiria wanaojulikana kama bodaboda wanatazamwa tu wakijifanyia watakavyo kana kwamba wanaishi kwenye dunia yao!
Hakuna anayepinga kwamba kwa kiasi fulani pikipiki hizi ni msaada mkubwa kwa wengi huku pia zikiwa ni suluhu kwa tatizo la ajira kwa vijana, lakini kwa mwenendo wanaokwenda nao kwa sasa, ninaamini kuwa hili ni bomu ambalo linaweza kulipuka wakati wowote.
Hapa sizungumzii ajali zinazosababishwa na waendesha bodaboda kwani ninaamini hilo limeshasemwa kiasi cha kutosha, lakini lipo jingine ambalo hakika linatisha, linakera na kusikitisha sana.
Waendesha bodaboda karibu wote wanafanana wakiwamo wa Dar es Salaam, Mbeya na Arusha. Inavyoonekana vijana hawa wamejiundia 'jeshi' lisilo rasmi na wakati wowote mmoja wao akikosewa iwe kwa makusudi au kwa bahati mbaya, hujikusanya na kulipa kisasi papo hapo!
Si ajabu kwa sasa kuwaona bodaboda wakimshambulia dereva wa gari na hata kutishia kuchoma moto gari kisa, dereva huyo kamgonga mwenzao. Hapo hawatazami nani mwenye kosa ila ni kulipa kisasi tu.
Si ajabu hata kidogo kuona gari likipewa 'escort' na waendesha bodaboda hata 100 kuanzia Kibaha hadi Dar es Salaam kushinikiza dereva ashuke ili wampige! Sasa wamefikia hata hatua ya kuua askari! Jamani, bodaboda hawa wasiachwe hivi hivi.
Mwaka jana nilishuhudia maofisa wa wakala wa kukusanya kodi ya mapato TRA mjini Morogoro wakipata wakati mgumu walipotaka kuwatoza kodi waendesha bodaboda. Vijana wale waligoma, wakajikusanya kama 300 hivi, wakalizunguka gari la mawakala wale wakitishia kuwapiga na kulichoma moto gari lao. Hawataki kutoa kodi hawa, wanavunja hata sheria na haki ya Mungu.
Ilibidi dereva wa lile gari aondoke na maofisa wake, lakini wapi! Bodaboda zile ziliendelea kulisakama gari lile, wakalisindikiza hadi Kituo cha Polisi Morogoro, kisha waendesha pikipiki wale wakaondoka zao huku polisi wakiwatazama tu. Ndio, waliwatazama tu kwani kuwachezea ni sawa na kucheza na moto. Wanaweza hata kuvunja 'armory' ya polisi, usicheze na bodaboda.
Nikajiuliza, jeuri hii wanaitoa wapi? Kwanini wagome kulipa kodi na kulisindikiza gari hadi kituo cha polisi? Ni nani alipaswa kupelekwa polisi, wao kwa kugoma kulipa kodi au mawakala wa TRA kwa kuwataka walipe kodi? Hii ni hatari.
Nililazimika kuzungumza na askari mmoja ambaye alikiri kuwa kwa sasa bodaboda hao ni jeuri na tishio hata kwa maisha ya walinda amani, lakini yeye akawatupia lawama wanasiasa.
Kwamba wao ndio wanaowalinda kwa kuogopa kuwa 'jeshi la bodaboda' likiwa tofauti na vyama vyao huenda wakakosa kura kwenye uchaguzi wowote ujao.
Nilijiridhisha baada ya muda mfupi niliposhuhudia waendesha bodaboda wakitumiwa kwenye maandamano ya kisiasa na kiongozi wao mmoja alikiri kuegemea upande wa chama fulani.
Mimi sina tatizo kwa wao kuwa na upande wa kisiasa, lakini wasiwasi wangu ni kwamba jeuri waliyo nayo inatisha na wanaweza kuamua kufanya lolote na chochote wakati wowote bila kuogopa sheria wala walinda sheria.
Kingine kilichozuka ni matumizi ya silaha na vitendo vya mauaji vinavyofanywa na waendesha pikipiki. Wiki kadhaa zilizopita, waendesha bodaboda wamehusika kwenye mauaji ya madereva kwa kutumia silaha!
Inakuwaje bodaboda wanamiliki silaha? Lakini pia waendesha pikipiki hawa wamekuwa wakishiriki vitendo vya uporaji kwenye benki, mawakala wa vocha na hata watembea kwa miguu na kisha kutokomea zao.
Nchi haiwezi kuendeshwa namna hii. Ni lazima itafutwe namna ya kuwadhibiti waendesha bodaboda kwani umoja wao ni tishio kwa usalama wa raia na hata wa taifa zima.
Kwanini hawataki kushirikiana na polisi na kuwakamata madereva wa magari yaliyowasababishia ajali? Jibu ni kwamba, wao pia wana makosa mengi na wakifika kituoni lazima kibao kitawageukia.
Wengi wao hawana leseni za kuendesha vyombo vya moto, wengine pikipiki zao hazina bima, wapo ambao vichwa vyao vina mzio (allergy) ya kofia (helmet) na wapo ambao hawalipi na hawataki kulipa kodi ya mapato.
Na hili la kodi si la kuachwa hivi hivi. Iweje idadi kubwa namna hii ya vijana wafanye kazi bila kulipa kodi? Nani awalipie? Ni kodi hizi ndizo zinazosaidia kupatikana huduma za kijamii na maendeleo ya nchi kwa ujumla, na ni wajibu wa kila Mtanzania kulipa kodi.
Lakini ni nani anayewalemaza vijana hawa? Ni Serikali? Ni jeshi la polisi? Ni vyama vya siasa? Au ni jamii nzima?
Hakika kuendeleza 'Appeasement Policy' kwa hawa bodaboda kutaitokea puani serikali yetu pale itakapobidi kutumia nguvu ya ziada kurekebisha mienendo yao.
Lazima sote kwa pamoja tutafute suluhu ya ubabe wa mabodaboda.
Mwisho
 
chanza: Gazeti la Rai; Machi 28-Aprili 3, 2013
--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 


0 comments:

Post a Comment