Monday 29 April 2013

[wanabidii] Muungano uwepo, yafaa ukarabatiwe kwanza

Na Salim Said Salim, Mwananchi

Posted Aprili27 2013 saa 1:21 AM

Zanzibar. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni zao la kuungana kwa nchi mbili, Tanganyika na Zanzibar, ambazo ziliungana Aprili 26, 1964.

Lakini miaka 49 tangu kuwapo kwa Muungano huo, suala linaloulizwa na Watanzania, bara na visiwani ni je, Muungano umeimarika au unadhoofika? Yapo mawazo tofauti kutegemea na mtazamo wa mtu na vigezo anavyotumia kukiona kitu kimeimarika au kimedhoofika.

Kwa mtazamo wangu, Muungano unachechemea, yaani unakwenda ule mwendo unaoitwa ' kiguru cheche'.

Kilicho wazi ni kuwa Watanzania wanaelewa Muungano unakotoka hapa ulipo, lakini hawana uelewa wa uhakika ni wapi hasa unakoelekea.

Kila baada ya siku chache unasikia malalamiko mengi kutoka kwa watu wa pande zote mbili, bara na visiwani, juu ya muundo na namna Muungano unavyoendeshwa. Haya yote yamepewa jina la kero za muungano.

Malalamiko ya muungano
Hivi karibuni tumesikia bungeni mjini Dodoma malalamiko mapya. Nayo ni kuwa majimbo madogo ya Zanzibar yanapewa mafungu mawili ya mfuko wa jimbo wakati ya Tanzania Bara yakibakiwa na fungu moja.

Kinachosahauliwa ni kwamba hata wakati wa kuungana hakuna aliyekuwa hafahamu kwamba bara ni kubwa na Zanzibar ni ndogo, lakini pande zote mbili zilikubaliana kuwa washirika sawa wa Muungano. Madai mengine ni madai kuwa Watanganyika wananyimwa haki ya kumiliki ardhi visiwani na kwamba Wazanzibari wamejazana kwenye Bunge la Muungano wakati Watanganyika hawaruhusiwi kuingia kwenye Baraza la Wawakilishi.

Lawama au kasoro hizi zinakwenda sambamba na malalamiko ya Wazanzibari kwamba Watanganyika wamejazana katika taaasisi za Muungano zilizopo visiwani, kama vile, Benki Kuu (BOT), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)

Katika hili zimetoka kauli zilizojaa hasira hata ndani ya Baraza la Wawakilishi za kutaka TRA ifunge virago vyake na kuondoka Zanzibar kwa kile kinachodaiwa kuwapo ajenda ya kuua uchumi wa Zanzibar, hasa katika sekta ya biashara.

Kwa bahati mbaya yote haya yanaonekana kama yanapuuzwa na viongozi na unachokisikia ni kuwa viongozi wa pande mbili za Muungano wanalishughulikia suala hili kwa misingi ya utashi wa kisiasa.

Binafsi, Muungano ulipoundwa nilikuwa nakaribia umri wa miaka 18. Nilikuwa ninafanya matayarisho ya kwenda Prague, wakati ule mji mkuu wa Jamhuri ya Czechoslovakia (sasa Czech), kwa masomo ya uandishi wa habari, kazi niliyoianza nikiwa shule.

Taarifa kuhusu kuungana
Siku ile ya tarehe 26 Aprili, 1964, saa 10 jioni nilikuwa nimekaa kwenye kijiwe kimoja maarufu cha Mtaa wa Baraste Kipande, mjini Unguja, nikingojea zamu yangu ifike nicheze dhumna.

Alikuja mwalimu mmoja wa skuli, Mohammed Shatry na kueleza kuwa Zanzibar na Tanganyika zimeungana na mkataba wa muungano umetiwa saini mjini Dar es Salaam kati ya marais, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanganyika) na Sheikh Abeid Amani Karume (Zanzibar).

Wazee na vijana waliacha mazungumzo waliyokuwa nayo na michezo yote … bao, dhumna na karata ilisimama. Mjadala ulianza na wengi walishangazwa na habari zile.

Mtu mmoja aliyepigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia na kushiriki kujenga daraja la Mto wa Kwai (angalia filamu ya sinema ya Bridge over the River Kwai) kule Mynamar, wakati ule Burma, Mzee Maulidi aliyejulikana kwa jina la 'Kade Vondik' alisema: "Tumekwisha." Nini alichokusudia kulitegemea mtazamo wa mtu na tafsiri ya neno hilo.

Siku iliyofuata watu wengi walitumia muda mrefu kusikiliza redio na kusoma magazeti kujua habari za Muungano. Hapakuwa na sherehe zozote zile kuadhimisha kuungana kwa nchi hizi mbili. Siku chache baadaye palifanyika mkutano wa hadhara ambao kila pembe ya uwanja wa mkutano walikuwapo askari waliobeba silaha.

Hapo Mzee Karume aliwauliza waliohudhuria kama walifurahia hatua ya kuungana au vipi. Sauti zilipaa kwa kusema, "Tunautakaaa!"

Hofu
Baadhi ya watu waliiona hatua ya Mzee Karume ya kuwauliza wananchi kwa namna ile kama walikuwa wanautaka Muungano au vinginevyo kwenye mkutano ule ilikuwa na kasoro.

Kwanza, ilikuwapo dhana kuwa watu wangeulizwa kwanza kabla ya kuundwa kwa huo Muungano na siyo kuunganisha nchi na baadaye kuwauliza watu.

Pili, suala kama lile walihisi lilihitaji kupigiwa kura ya maoni. Tatu, ni kwamba mazingira yaliyokuwapo pale ya kila pembe kuwapo askari yalikuwa ya kutisha na kwa hivyo hayakumfanya mtu kujisikia kuwa huru kutoa hisia zake.

Zaidi ya hapo ni kwamba wakati huo watu wengi waliokuwa na mawazo tofauti na Serikali juu ya masuala mbalimbali walikuwa wakipotea kimyakimya, hivyo hakuna hata mtu mmoja ambaye angethubutu kupinga hadharani. Muungano ulipoundwa ulionekana zaidi kuwa wa kisiasa kuliko wa kiuchumi.

Siku ya pili au ya tatu nilikutana na baadhi ya mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi, baadhi yao sasa marehemu, waliniambia wameshtukizwa tu na kuundwa kwa Muungano.Wapo watu waliofurahia kwa kueleza huo ulikuwa mwisho wa kamata kamata ya watu iliyokuwa ikiendelea visiwani, lakini wapo walioona haikuwa jambo la busara.

Mengi yalizungumzwa na mjadala uliendelea kwa siku nyingi, lakini kwa sauti ya chini huku watu wakiendelea kupotea.

Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere siku moja alipokuja Zanzibar aliwaambia viongozi kwamba wakiwamaliza hao wanaowaita siyo wanamapinduzi watauana wenyewe kwa wenyewe.

Ukweli ni kwamba palikuwa hapana fununu ya Zanzibar na Tanganyika kuungana. Hata aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali , Wolfango Dourado, aliyekuwa Katibu wa Kwanza wa Baraza la Mapinduzi (Baraza la Mawaziri) na mawaziri wa Serikali ya Rais Karume wamenukuliwa wakisema hawakushauriwa juu ya kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika.

Dourado aliwekwa kizuizini wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere kwa kusema hakushauriwa Muungano ulipoundwa na kudai haukuwa halali.

Watanzania wanastahili pongezi
Sasa, Muungano huu uliopitia kila aina ya mikiki na dhoruba umetimiza miaka 49, wakati nchi nyingi za Kiafrika, Kiarabu na Asia zilizochukua hatua kama hii miaka ya nyuma zimeshindwa kuendelea kuungana kutokana na sababu za kisiasa na kiuchumi.

Watanzania tumekuwa tofauti, kwani pamoja na matatizo yote tuliyonayo ya kisiasa na kiuchumi bado tumeishikilia kamba iliyotuunganisha.

Kwa Watanzania wengi, bara na visiwani, suala la kuungana siyo tatizo. Kinachozusha mabishano na mivutano ni masuala gani ni ya Muungano na mambo gani yapo chini ya mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Malalamiko juu ya mfumo wa Muungano yamesikika mara nyingi na yanaendelea kusikika. Katika mchakato wa kutoa maoni ya Katiba Mpya, suala la Muungano lilitawala mjadala.

Zanzibar wapo wanaotaka muundo wa sasa wa Serikali mbili uendelee, wapo wanaosema uwe wa Serikali moja na wapo wanaopendelea mfumo wa shirikisho wa Serikali tatu.

Lakini, pia lipo kundi linalotaka Muungano wa mkataba na wapo wanaosema hawana haja ya Muungano. Hii ni kudhihirisha kuwa pamoja na kuwa wananchi wengi bado wangependa kuendelea na Muungano, lakini wakati umefika wa kuufanyia marekebisho ya kimuundo.

Wakati huu Watanzania wanapoandika Katiba Mpya, viongozi wasilififishe suala la Muungano, kama mjadala kuhusu muundo gani wa muungano wanaoutaka wananchi haujatosha, uendelezwe ili hatimaye tuwe na Muungano ulio madhubuti kuliko huu tulionao sasa.

Salim Said Salim ni mwandishi wa habari mkongwe, anayeishi Zanzibar, 0655 431890.

Chanzo:Mwananchi

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment