Saturday 6 October 2012

[wanabidii] Taarifa ya Kujiuzuru kwa Ismail Jussa

"Leo asubuhi nimewasilisha kwa Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mheshimiwa
Profesa Ibrahim Lipumba barua ya kuomba kujiuzulu nafasi ya Naibu
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) kwa upande wa Zanzibar ,
uamuzi ambao nimeomba uanze kutekelezwa rasmi tarehe 10 Oktoba, 2012.
"Nimechukua uamuzi huu baada ya kuzungumza na kushauriana na viongozi
wangu wa juu wa Chama ambao ni Mwenyekiti, Profesa Lipumba, Makamu
Mwenyekiti Mheshimiwa Machano Khamis Ali na Katibu Mkuu Maalim Seif
Sharif Hamad takriban miezi miwili iliyopita.

Nawashukuru baada ya kunitaka niwape muda wa kulitafakari
walinikubalia lakini wakaniomba nibakie hadi tutakapokamilisha baadhi
ya shughuli muhimu za Chama katika kipindi hichi. "Sababu kubwa
zilizonisukuma kukiomba Chama kiniruhusu niachie nafasi hii ni
kutokana na muda mrefu sasa kuhisi kwamba majukumu niliyo nayo ya kuwa
msimamizi mkuu wa utendaji wa Chama kwa upande wa Zanzibar na wakati
huo huo kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe
hakunipi fursa ya kujifaragua na kutumikia nafasi zote mbili kwa
ufanisi unaotakiwa.

Nataka kuona kazi ya kuibana Serikali ndani na nje ya Baraza ili
iwajibike zaidi kwa wananchi inaimarika zaidi. "Sambamba na sababu
hiyo ni kwamba nimekusudia kutumia muda mwingi zaidi kutoa mchango
mkubwa zaidi katika harakati za wananchi wa Zanzibar zinazoendelea za
kuhakikisha kuwa Zanzibar inarejesha mamlaka yake kamili kitaifa na
kimataifa itakayofuatiwa na kuwepo kwa Muungano wa Mkataba kati yake
na Tanganyika yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa. "Harakati
zinazoendelea Zanzibar kwa njia za amani na za kidemokrasia kwa
kutumia mchakato wa Katiba Mpya zinahitaji kuungwa mkono na kupewa
msukumo wa dhati na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochaguliwa na
wananchi wa Zanzibar kwenda kusimamia maslahi yao na ya nchi yao.

Nimetafakari na kuona kwamba nikiwa sina majukumu mengine ya
kiutendaji nitakuwa na muda kutosha wa kulifanya hili mimi na
Wawakilishi wenzangu tunaotoka CUF na CCM, vyama viwili vya siasa
vilivyomo Barazani. "Nafurahi kwamba leo nimetimiza azma yangu hiyo.
Pamoja na uamuzi huu, naendelea kubaki kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la
Uongozi la Taifa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa. "Nawahakikishia
viongozi na wanachama wenzangu wa CUF kwamba tutaendelea kushirikiana
pamoja katika shughuli nyengine zote za kisiasa za Chama na kwa pamoja
tutafanya kazi kuyatimiza malengo tuliyojiwekea. Naahidi kumpa
ushirikiano kikamilifu mwanachama yeyote atakayeteuliwa kujaza nafasi
ninayoiwacha.

" HAKI SAWA KWA WOTE "
ISMAIL JUSSA

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment