Saturday 6 October 2012

[wanabidii] RE: MWALIKO KUHUDHURIA NA KUSHIRIKI SHEREHE ZA SIKU YA KIMATAIFA YA MTOTO WA KIKE DUNIANI JUMA TANO TAREHE 10/10/2012 VIWANJA VYA TGNP MABIBO

Wapendwa,                                                                                                    

 

 

              

RE: MWALIKO KUHUDHURIA NA KUSHIRIKI SHEREHE ZA SIKU YA KIMATAIFA YA MTOTO WA KIKE DUNIANI JUMA TANO TAREHE 10/10/2012 VIWANJA VYA TGNP MABIBO

 

Salaam kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)!

 

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ni shirika lisilo la kiserikali lenye dira ya kuwa na jamii ya Tanzania yenye usawa na haki kijinsia, wanawake walio na maendeleo maisha endelevu na haki ya kijamii. Ni shirika tetezi la haki za binanadamu, hususani haki za makundi yaliyoko pembezoni, ya wanawake, ya walemavu, ya wasichana, ya vijana, ya watu waishio na VVU/UKIMWI nk. Dhamira yake ni ukombozi wa wanawake kimapinduzi.

 

Kuhusu Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, ‘INTERNATIONAL DAY OF THE GIRL CHILD, ni siku ya kimataifa itakayosherekewa Oktoba 11 ulimwenguni kote.  Siku hii itasherekewa kwa mara ya kwanza duniani baada ya kupitishwa na kutangazwa na Umoja wa Mataifa  kupitia mkutano wake mkuu wa tareha 19/12/2011. Hii ni siku ya kutambua haki za wasichana na changamoto maalumu zinazowakabili kama wasichana ulimwenguni. Hii imetokana na kampeni za miaka mingi za wanaharakati wa Kanada na Amerukani. Siku hii,  imetengwa maalumu kwa ajiri ya wasichana kufanya  utetezi na kuchukua hatua wao wenyewe na kwa ajiri ya wenzao. “Tokomeza ndoa za utotoni”; ndio kauli mbiu ya siku hiyo.

 Lengo na madhumuni makuu ya siku ya mtoto wa kike ni kutangaza,  kuhamasisha na kuongeza uelewa  na  ufahamu juu ya,  na kutetea  haki za mtoto wa kike ulimwenguni.  Uamuzi wa Umoja wa Mataifa kutangaza siku hii ni ishara ya kutambua changamoto zao  na uwezo walionao wasichana. Pia Umoja wa Mataifa umeonesha dhamira yake ya kutokomeza mawazo mgando, ubaguzi, ukatili na tofauti za tabaka katika masuala ya kiuchumi yanayopelekea wasichana kupata vipato visivyo sawia.

 

Kwa kuungana na wenzetu duniani, TGNP, tumeamua kuisherekea siku hiyo katika semina yetu ya jinsia(GDSS) ya Juma tano tarehe 10/10/2012 hapa viwanja vya TGNP Mabibo karibu na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji.    Muda wa sherehe utakuwa ni masaa 2 tu. Tutaanza saa 9:00 alasiri na kumaliza saa 11:00 jioni. Mada ya siku hiyo; “Tokomeza ndoa za utotoni:kuza vipaji vya wasichana”. Pia kutakuwepo na jopo la wazungumzaji. 

 

Aidha napenda kukuhabarisha  kuhusu jukwaa la wazi kwa jamii maarufu kama ‘Semina ya Jinsia na Maendeleo (GDSS). Semina hii hufanyikia viwanja vya TGNP Mabibo karibu na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji Mkabala na Soko la Mabibo. Kwa kawaida, semina hii/jukwaa hili huendeshwa mara moja kwa wiki na huwa ni  siku ya Juma Tano saa 9 alasisri mpaka 11 jioni (kwa masaa mawili tu). Kulingana na Muktadha wa wakati huo, kwa kutumia mbinu mbalimbali, mada raghbishi hutolewa kwa  wanajamii ambapo masuala mbali mbali huibuliwa kwa mjadala na baadaye kumalizia na mkakati  wa nini kifanyike. Jukwaa hili linatoa fursa kwa wanajamii wote, wanawake kwa wanaume, vijana na makundi yote ya kijamii wakiwemo watu wenye ulemavu, waishio na VVU/UKIMWI, wanaharakati wa haki za binadamu na za wanawake. Bila kujali jinsi, umri, dini, itikadi za kisiasa, wanajamii huweza kukutana na kujadili mada mbalimbali za maendeleo na kutoa kero zao. Pia katika semina hizi washiriki hupashana habari mbalimbali, hujengeana uwezo, hujifunza, na kujenga mtandao wa vuguvugu la ukombozi wa wanyonge na makundi ya pembezoni.   

 

Hivyo, tunapenda kukualikeni, wanabidii nyote pamoja na mitandao yenu na marafiki, kuja kuhudhuria na kushiriki pamoja na Mtandao wa Jinsia Tanzania katika sherehe za siku ya kimataifa ya mtoto wa kike.

 

Mwaliko huu unatokana na kutambua juhudi na harakati zenu katika kuhabarishana na kupeana uzoefu katika nyanja mbalimbali za kijamii.

 

Kuhudhuria na kushiriki kwenu, kutawezesha mafanikio ya semina hiyo na siku ya mtoto wa kike duniani. Pia naomba kuzingatia kuwa usafiri wa kuja na kurudi ni wa kujitegemea. Huduma ya mkalimani wa viziwi itatolewa.

  

 Wako katika harakati za  kutetea haki za wasichana na kuinua vipaji vyao.

 

Asante.

 

 

 

Demetria Kalogosho

 

 

 

 

 

 

 

 

0 comments:

Post a Comment