Sunday 12 August 2012

[wanabidii] Re: Tamko la DKt. Lwaitama kuhusu habari ya "Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe"

Tamko la Prof. Shivji kuhusu habari ya "Shivji, Lwaitama wataka
Muungano uvunjwe"
09/08/2012
JUU YA MUUNGANO: TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Nimeshitushwa na gazeti moja la kila siku  (Tanzania Daima la tarehe7
Agosti 2012) lilonipandikizia maneno katika kichwa chake cha habari
kwamba 'Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe'. Siwezi nikamsemea
Dr. Lwaitama lakini kwa upande wangu sijasema wala kumaanisha kwamba
'Muungano uvunjwe'.

 Mosi, kwamba wasomi, wakiwemo wanahabari, wana jukumu zito la
kutokupinda  ukweli wa kihistoria kwa lengo la kuhalalisha mtazamo na
msimamo wao kuhusu  Muungano. Nikatoa mfano wa jinsi Merehemu Sheikh
Karume anavyodekezwa  katika msimamo wake juu ya Muungano. Wasemaji
hapa bara wanamsifu kwa kuwa  muasisi mwaminifu na mshabiki mkubwa wa
Muungano tangu mwanzo. Huko  Zanzibar, wasemaji hawachoki kumnukuu
Mzee Karume kuwa tangu mwanzo yeye  hakutaka Muungano isipokuwa
alikuwa anafikiria Shirikisho.

Wanaendelea kusema kwamba aliposaini Mkataba wa Muungano, Mzee Karume
alifikiri kwamba anasaini Shirikisho la Serikali tatu, lakini kutokana
na kiwango cha  elimu yake hakuelewa vizuri mantiki na maana ya
alichokuwa anasaini.

Nikaendelea kueleza kwamba maelezo haya yote mawili hayaungwi mkono na
ushahidi wa kihistoria. Ukweli ni kwamba, Mzee Karume aliingia katika
Muungano kutokana na hesabu zake mwenyewe za kisiasa. Muungano kwake
ulikuwa njia ya kuondoa upinzani, au upinzani tarajiwa, wa utawala
wake. Yaani ilikuwa ni tendo la mwanasiasa yeyote yule kudumisha
utawala wake (political survival).

Na kwa watawala wote wa Zanzibar waliomfuata, wakiwemo wa upinzani,
ndivyo ilivyokuwa. Wamekuwa wakitumia mwavuli wa muungano wakati
utawala wao uko hatarini na kushawishi wananchi wao dhidi ya muungano
wakitafuta umaarufu wa kisiasa.

Nikitoa mfano nikasema kwamba kuna taarifa kwamba chama kimoja huko
Zanzibar kinapandikiza pendekezo la 'muungano wa mkataba, sio wa
katiba' bila ya kueleza waziwazi maana yake. Ukweli ni kwamba huwezi
ukawa na muungano wa mkataba bila kwanza kuuvunja muungano. Kwa hivyo,
wanachoshawishi moja kwa moja ni kuuvunja muungano. Basi waseme hivyo
badala ya kujificha nyuma ya pazia la 'muungano wa mkataba'.

Jambo la pili nililorudia ni kwamba tuliangalie suala zima la muungano
kwa mtazamo na maslahi na matakwa ya Umma wa Zanzibar na Umma wa
Tanzania bara, hususan matabaka ya hali ya chini. Katika hali yao
kimaisha – kiuchumi na kisiasa – hakuna tofauti kati ya wananchi wa
Zanzibar na wananchi wa Tanzania bara. Uduni wa hali yao ni uleule;
ukosefu wa ajira ni uleule; kutokuwa na mfumo wa dhati wa demokrasia
unaojali walalahoi ni kulekule.

Kwa hivyo, umuhimu kwao ni mshikamano wao kuboresha mifumo ya uchumi
na siasa. Wasiburuzwe na wanasiasa na vyama vyao kwa maslahi yao
binafsi ya muda  mfupi ya kudumisha, au kuingia kwenye, utawala.

Jambo la mwisho nililogusia ni kwamba kiini cha suala la muungano si
idadi ya serikali (mbili au tatu) bali ni mgawanyo wa madaraka
(distribution of power) kati ya  dola la Zanzibar na dola la Muungano.
Na katika hili kila muungano duniani ni wa kipekee kutokana na hali
halisi yao ya kihistoria na uwiano wa kisiasa. Sisi pia
tukiwashirikisha wananchi kikamilifu na tukaelewa vizuri matakwa yao
tunaweza kubuni muundo wetu wa muungao ambao ni wa kipekee bila kujali
idadi ya serikali.

Nimeona niweke wazi mtazamo wangu kwa sababu ya baadhi ya vyombo vya
habari kuwa na hulka ya kupotosha mambo kutokana na ushabiki wao bila
kujali madhara  yanayoweza kutokea.

Mwishoni ningependa kusema kwa dhati kwamba uvunjaji wa muungano
hauwezi kuwa kwa manufaa ya walio wengi. Ukweli ni kwamba unaweza
ukasambaratisha  nchi na jamii zetu pande zote mbili za muungano.
Tukianza kubaguana kati ya Watanganyika na Wazanzibari, tutaendelea
kubaguana kwa msingi wa Uislamu na  Ukristo, na Usukuma na Uchaga,
Uarabu na Uafrika, weusi na weupe bila kikomo.


Kama alivyosema Mwalimu, ukishaonja nyama ya mtu basi utaendelea
kumtafuna.


Issa Shivji
Profesa wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Agosti 8, 2012

On Aug 12, 10:13 am, Yona Maro <oldmo...@gmail.com> wrote:
> 11/08/2012
>
> *JUU YA MUUNGANO: TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI ***
>
> Nimesikitishwa na aina ya uandishi wa habari  uliojiweka wazi  katika
> taarifa iliyonukuliwa kuandikwa na  mwandishi  wa gazeti moja la kila
> siku  (Tanzania Daima la tarehe7 Agosti 2012), Datus Boniface.  Huyu
> mwandishi, pamoja na wahariri wake walioruhusu habari hiyo kuchapwa
> walithubutu kusema uongo kuwa  eti " Dk Lwaitama, Prof. Sheriff na Prof
> Shivji waliushambulia Muungano.." Tena, mwandishi huyu na wahariri
> walioruhusu habari hiyo ichapishwe  wakaenda mbali zaidi na kutumia
> kichwa  cha habari kilichosema eti 'Shivji, Lwaitama wataka Muungano
> uvunjwe'.
>
> Nafahamu Prof Shivji tayari ameisha toa tamko juu ya upotoshwaji wa hali ya
> juu uliobebwa na kichwa cha habri hiki na makala nzima ya mwandishi huyu
> mwenye aina yake ya ujuzi wa kuandika habari, Datus Boniface. Mimi katika
> tamko langu sitojisemea mimi tu kama alivyosema Prof. Shivji katika tamko
> lake. Nitajaribu kueleza kile ambacho nilidhani kilizungumzwa na kila
> aliyechangia katika Mazungunzo ya yale ya Kifungua Kinywa       ( Breakfast
> Talk), Jumatatu tarehe 6 Agosti 2012, yaliyofadhiliwa na Baraza la Habari
> Tanzania( MCT).
>
> Wakwanza kuzungumza alikuwa Prof Abdul Sheriff na aliainisha kile
> alichotaka kibainike kama historian a sababu za kuwepo Muungano katika ya
> Tanganyika na Zanzibar. Alieleza kile alichotaka kieleweke kama mapungufu
> ya  kisheria katika mchakacho wa kuwepo Muungano. Pia alieleza kile
> alichotaka kieleweke kama Muungano kukosa kuwa na uhalali wa kisiasa (
> political legitimacy) kutokana na ushirikishwaji hafifu wa viongozi wa
> Serikari ya mapinduzi wa wakati huo  na wananchi kwa ujumla. Akahitisha
> maelezo yake kwa kusema Wazanzibari walio wengi sasa hivi wamefikishwa
> mahali ambapo wanatamani kutumia mchakato wa kuandika katiba mpya
> uliozinduliwa hivi karibuni unaoongozwa na Jaji SJoseph Sinde Warioba
> kujaidili Muungano kwa kina na kuingia kwenye maridhiano mapya  juhuu ya
> kama Muungano uendeleee kuwepo na kama ndiyo kwa mfumo wa serikali ngapi.
> Ilikuwa wazi kuwa Prof Sheriff alikuwa hafikiri kuwa walikuwepo Wazanzibari
> wengi waliokuwa tayari kuendelea na Muungano wa serikali mbili kama wa
> sasa.  Si kumsikia mahali popote ambapo Prof Sheriff alitamka kuwa eti
> anataka Muungano uvunjwe, yeye kama yeye. Sasa hyu mwandishi Datus Boniface
> halipata wapi ujasiri wakumlisha mwanataaluma ya historia  huyu wa
> Kitanzania, hata kama ni Mzanzibari pia? Ni uandishi wa habari wa aina hii
> ni wa kusikitisha.
>
>  Aliyezungumza wa pili alikuwa mimi, Dkt Azaveli Lwaitama.  Mimi kazi yangu
> ilikuwa kujibu hoja za mzungumzaji mkuu ( Discussant) ambaye kwa kweli
>  alikuwa Prof. Abdul Sheriff peke yake.  Kwanza nilimkosoa ndugu yangu
> Mtanzania mwenzangu Prof Abdul Sheriff kwa kuomba wote tukubali kuwa
> viongozi wetu waliotuunganisha kuzaliwa taifa letu la Tanzania walikuwa
> watu walioongozwa na dhamira safi  iliyojimbuka katika kuwa waumini thabiti
> wa itikadi ya *Umajumui wa Kiafrika ( Pan Africanism)* ya kutaka
> kuwaunganisha watu wa dola zetu hizi waliokuwa wamekusanywa pamoja na
> wakoloni na kupachikwa majina kama Tanganyika na Zanzibar bila ridhaa ya
> wakazi walikuwa ndio  wengi wa sehemu hii ya Bara la Afrika wenyewe.
> Nikaeleze jinsi mbavyo *mwelekeo wa viongozi hawa haukuwa wa kufungwa sana
> na matakwa ya kisheria bali na kile walichokiamini kingesadia kufanikisha
> lengo la kuwaunganisha Waafrika* wote bila kujali kabila ( tribe) au uzawa
> ( race).  Nikatolea mfano wa jinsi Mwalimu Nyerere alivyoshirki katika
> kuimiza kuungana kwa Shiraz Association na African Association kuzaa Afro
> Shiraz Party ( ASP) tarehe 5 Februari 1959, siku na mwezi ambavyo mwaka
> 1967 vilikuja kuwa siku na mwezi  wa kuzaliwa Azimio la Arusha , na mwaka
> 1977 vilikuja kuwa ni siku na mwezi kilizaliwa Chama cha Mapinduzi kutokana
> na  kuunganisha Tanganyika African National Union ( TANU) na Afro Shiraz
> Party ( ASP).
>
> Nilisisitiza kuwa leo tunaweza kuyaona wazi mapungufu makubwa katika *taratibu
> za kisheria* zilizogubika mchakato wa kuunda Muungano lakini si vizuri
> kukataa Muungano kutokana na mapungufu haya ya kisheria tukasahau kuwa
> Muungano uliundwa kwa *sababu za dhamira ya kuunganisha Washiraz, Waafrika,
> Waarabu, Wahindi na Wazungu  na kuwaweka pamoja kama Waafrika waumini wa
> Umajumui wa Kiafrika (Pan Africanism),* wawe wa dola lilosimikwa na
> wakoloni la Zanzibar au dola lililo simikwa na wakoloni la  Tanganyika.
> Mwalimu Nyerere na Mzee Abedi Karume walisukumwa na kutaka kuunda taifa ya
> Kiumajui wa Kiafrika jipya la TANZANIA, baada ya kuona Mzee  Jomo Kenyata
> wa Kenya  na Ndugu  |Milton Obote wa Uganda   hawakuwa tayari kwa wakati
> huo, mwaka 1964, kuunda dola jipya ambalo lingeongozwa na itikadi ya
> vuguvugu la utaifa wa Umajumui wa Kiafrika ( Pan Africanist nationalist
> movement) la Shirikisho la Afrika Mashariki. Kwa waasisis hawa wa Muungano
> taratibu za kisheria hazikupewa kipaumbele bali dhamira safi ya kutenda
> liloonekana kuwa la manufaa kwa wananchi walio wengi  wa sehemu hii ya
> Afrika. Tukumbuke  kuwa Mzee Karume na Mwalimu Nyerere walikuwa wanafanya
> kazi katika mazingira ya kivuli cha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 1964
> mwezi mmoja baada ya Uhuru wa Zanzibar tarehe 9 Desemaba 1963 uliopatikana
> kwa kufuata taratibu za kisheria lakini matokeo yake yakapinduliwa kijeshi
>  tarehe 12 Januari 1964 kwa vile taratibu hizo za kisheria zilitumika
> kukwepa kupatikana kwa ridhaa ya kisiasa ya walio wengi katika kupatika
> Uhuru ule wa Zanzibar wa Desemba 1963 !!
>
>  Nilitumia muda kuelezea jinsi ambavyo tabaka la mabepari uchwara Tanzania
> Bara na Tanzania Zanzibar lilivyokuwa na ushawishi mkubwa juu ya uongozi wa
> serikali ya Muungano na serikali ya Zanzibar. Nikaanisha kuwa hii ndiyo
> ilikuwa sababu kubwa ya watetezi wa Muungano wa Serikali Mbili, ambao
> walikuwa ni wenye kufuata nyayo za Mwalimu Nyerere  kama mimi vile ni
> wana-Umajumui wa Kiafrika,  kukikri sasa kuwa ukitaka kulinda Muungano
> katika mazingira ya sasa lazima kukuballi kuwepo kwa Muungano wa serikali
> Tatu. Nilitumia muda mrefu zaidi nikieleza kufurahishwa kwangu na
> mwanasiasa kijana wa chama cha Chadema, Mheshimiwa Zito Kabwe,  kuelezea
> kuunga mkono kwa dhana ya kutafuta kuulinda Muungano kwa kuridhia kuwepo
> kwa  Muungano wa serikali Tatu.  Kwanza, kutakuwepo Serikali ya  na Bunge
> la Muungano. Serikali ya Muungano itakuwa  ndogo, yenye kushughulikia mambo
> ya Muungano machache yasiyozidi manne au matano yahusuyo *mambo ya ndani* (
> yaani uhamiaji, uraia, polisi), *mambo ya nje* ( yaani ulinzi wa nje na
> mahusiano ya kimataifa),  *uratibu wa mambo ya fedha na mipango ya
> uchumi*( yaani sarafu, sera ya uwekezaji. mambo wa ushuru na kodi),
> na
> *miundo mbinu* inayoitaji uwekezji mkubwa( teknohama, uzalishaji na
> usambazaji umeme, usafiri wa bahari na maziwa, reli, na anga).  Hata haya
> mambo ya muungano mengi yake baadaye yatashugulikiwa na Jumuia ya Afrika
> Mashariki kadili itakavyo kuwa inaimarika kuelekea kuwepo kwa Shirikisho la
> Afrika Mashariki.
>
> Pili kungelikuwepo serikali mbili za Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar
> zilizo sawa kila moja ikiongozwa na  Waziri Mkuu na kila moja ikisimamiwa
> na Baraza la Wawakilishi.  Mheshimiwa Zito alipendekeza katika uchanguzi
> mkuu kuwepo uchanguzi wa Rasi na Rais Mwenza wa Serikali ya Muungano  na *
> Wabunge* *wa Bunge la Jamuhuri* *ya Muungano* pamoja na Uchanguzi wa *Wajumbe
> wa  Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Tanzania Bara *na *Wajumbe wa
> Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Tanzania Zanzibar* . ( Mwandishi wa
> gazeti la Jamhuri Deodatus Balile alipendekeza Tanzania Zanzibar iitwe
> Tanzania Visiwani!). Lengo hapa litakuwa kuzidi kuimiza  kuukubali
> utambulisho wa  *kujiita Mtanzania* iwe mtu ni mkazi wa Tanzania Bara au
> Tanzania Zanzibar na kufifisha mwelekeo wa kubanguana kwa misingi ya
> Utanganyika na Uazanzibari.
>
>  Kwa lengo hili hili la kushamilisha utambulisho wa Utanzania, na *kufifisha
> mwelekeo wa kubanguana kwa misingi ya Utanganyika na Uazanzibari*, Mawaziri
> Wakuu wa Seriakali za Tanzania Bara an Tanzania Zanzibar watateuliwa na
> vyama vyama husika kutegemea ni chama kipi au vipi vitakuwa vimepata viti
> vingi au kura nying katika changuzi za Wajumbe wa  Baraza la Wawakilishi
> husika.  Kutokuwepo uchanguzi wa wakuu wa serikali ya Tanzania Bara na
> Tanzania Zanzibar kutasaidia kupunguza polepole ushabiki na hamasa za
> kisiasa zinazojikita kwenye utanmbulisho wa Utanganyika  au Uzanzibari.
> Haya yote lengo lake litakuwa kutafuta njia za sasa za kuendelea kuwaenzi
> waasisi wa Muungano, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume,  ambao dhamira yao
> ilikuwa nzuri ya kuunganisha Waafrika wote bila kuwabagua kwa misingi ya
> kabila, rangi, dini, uzawa au upande wa bahari ya Hindi mtu alikokuwa
> anaishi kwa sasa au hapo nyuma.
>
> Nilisisitiza umuhimu wa itikadi  ya Umajumui wa Kiafrika kwa  kusema hata
> kama itatokea ushawishi wa tabaka  lenye kutaka kuvunja muungano
> wakawashauwishi Wazanzibari kwa sasa kuridhia kuuvunja muungano  basi
> Watanzania Bara waendelee kujiita Tanzania Bara kama Wasudan Kusini
> walivyoridhia kuiita Sudan Kusini ili utambulisho wa Kiumajumui wa Kiafrika
> wa Sudan ubaki kwenye utambulisho wa wote, Kusini na Kazikazini, kuendelea
> kujiita Wasudani!!!! Sielewi uandishi wa Datus Bonaface  ni wa aina gani
> uliomruhusu kusuka manano kutoka  kwenye mchango wangu  hapo juu  wakusema
> eti 'Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe' au eti " Dk Lwaitama, Prof.
> Sheriff na Prof Shivji waliushambulia Muungano.." Inasikitisha sana kuwepo
> waandishi wa aina hii na wahariri wanaoruhusu uchapishwaji wa uongo wa
> kiwango hiki !!!
>
> Wachangiaji kadhaa walifuata mchango wangu kabla ya Prof Shiji kutoa
> mchango wake ambao ameuleza vizuri sana  katika  tamko lake kuhusu
> upotoshwaji wa hali ya juu ulifanywa na mwandishi Datus Bonaface pamoja na
> wahariri walioruhusu  habari hii ya uongo kuchapishwa.  Laiti wahariri wale
> wangeomba ushaidi wa kanda ya kilichozungumza wangegundua mara moja kuwa
> mwandishi Datus Bonaface ni mwandishi wa ajabu kweli kweli.  Naliambatisha
> Tamko la Prof. Shivji kama alivyolitoa, ni wazi Prof. Shivji kamwe
> hakutamka mahali pale chochote cha kuhalisha kusema eti  eti 'Shivji,
> Lwaitama wataka Muungano uvunjwe' au eti " Dk Lwaitama, Prof. Sheriff na
> Prof Shivji waliushambulia Muungano.." Inasikitisha sana kuwepo waandishi
> wa aina hii na wahariri wanaoruhusu uchapishwaji wa uongo wa kiwango hiki
> !!!
>
> *Mwl. Azaveli Feza Lwaitama*
>
> *Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Jukwaa la Dira Afrika Mashariki*
>
> *&*
>
> *Mhadhiri Mwandamizi Mstaafu,*
>
> *Kitengo cha Falsafa,
> Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.*
>
> *Kerezesia_mukaluga...@hotmail.com*
>
> *+255784432696*
>
> *+255782807728*
>
> *
> Agosti  11, 2012 *

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment