Monday, 30 September 2013

[wanabidii] THE COMMEDY YA DR. ULIMBOKA IMEISHIA HAPA!

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemhukumu kwenda jela miezi sita au kulipa faini ya sh 1,000, raia wa Kenya, Joshua Mulundi, ambaye alikuwa akikabiliwa na kosa la kutoa taarifa za uongo.
Mulundi alidaiwa kutoa taarifa za uongo kwa ofisa wa polisi katika Kituo cha Polisi Oystebay jijini Dar es Salaam, kwamba yeye na wenzake walikodiwa kwenda kumteka na kumjeruhi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi, Alocye Katemana, akisema kuwa kesi hiyo ilikuja jana kwa ajili ya upande wa Jamhuri kumsomea maelezo ya awali mshitakiwa huyo.
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, alimsomea maelezo ya awali mshitakiwa na baada ya kumaliza, mshitakiwa huyo alikiri kutenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha 122 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Kabla ya Hakimu Katemana kutoa adhabu yake aliutaka upande wa Jamhuri uzungumze lolote kama wanalo, ambapo Wakili Kweka alidai kuwa anaiomba mahakama itoe adhabu inayostahili.
Kwamba, kwa mazingira ya kesi hiyo, hali iliyojengeka katika jamii kuhusu sakata la kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka ni tete na kuwa si vema kwa mtu mzima kama huyo kutoa taarifa za uongo polisi.
Aidha, kwa upande wake Mulundi, alieleza kuwa yeye ni raia wa Kenya na kwamba lengo na madhumuni ya kuja Tanzania ni kuja kufanya biashara ya kuuza nguo.
Alidai kuwa Juni 27, mwaka jana akiwa Arusha, alitekwa na mtu asiyemfahamu na kumwamuru afanye kila jambo atakalomtaka, kwamba yeye alikubali kufanya yote aliyoamriwa na mtu huyo ambaye alikuwa na silaha.
"Mheshimiwa hakimu kwa kuwa nilikuwa naogopa vitisho hivyo nilifanya kama alivyokuwa akinielekeza na baadaye mtu huyo aliyekuwa ameniteka akanipeleka hadi Tanga sehemu ambayo sikuwa nimewahi kufika.
"Akanieleza kuwa yeye ni Mkristo na kwamba ananituma kwa Mkristo mwenzie na akanipa taarifa hizo nizipeleke kwa Mkristo mwenzake na taarifa hizo ndizo zilizosomwa hapa mahakamani na mwendesha mashitaka wakati akinisomea maelezo ya awali," alisema.
Alidai kuwa alikwenda hadi katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo Kawe, Tanganyika Parkers na kumkuta Mchungaji Joseph Kiliba ambaye yule mtekaji alimwagiza amfikishie taarifa hizo.
Mulundi aliongeza kuwa alimpelekea taarifa zile mchungaji kama alivyoelekezwa lakini baada ya hapo alijikuta anakamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Oystebay, ambako alirudia taarifa ile na kisha kufunguliwa mashitaka.
Akitoa adhabu yake baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili, Hakimu Katema alisema kwa kuwa mshitakiwa amekiri kosa kabla hata mashahidi wa Jamhuri hawajaletwa kutoa ushahidi wa kesi hiyo, mahakama yake inamhukumu kwenda jela miezi sita au kulipa faini ya sh 1,000.
Hata hivyo mwandishi wa habari wa Radio Times, Chipangula Nandule, aliyekuwapo mahakamani hapo alijitolea kumlipia faini hiyo.
Lakini sekunde chache baadaye askari polisi walimkamata Mulundi, wakidai ni raia wa Kenya, hivyo wanamshikilia ili waweze kuandaa taratibu za kumrejesha nchini kwao.
Agosti 6, mwaka huu, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), alimfutia Mulundi kesi ya kujaribu kumuua na kumteka Dk. Ulimboka.

Source: TANZANIA DAIMA

0 comments:

Post a Comment