Saturday 28 September 2013

[wanabidii] Nilivyoijadili hoja ya aliyeyafungua MWANANCHI, MTANZANIA

Kufungiwa kwa magazeti ya Mwananchi na Mtanzania, kulikofanywa na Mkurugenzi Idara ya Habari (MAELEZO) ambaye kwa sasa ni Assah Mwambene, kumenikumbusha makala niliyoiandika kwenye gazeti la NIPASHE la Mei, Mosi, mwaka huu, nikaandika hivi…
 
Nimpinge Mwambene wa MAELEZO, kumuunga mkono Msekwa wa CCM!
 
Na Mashaka Mgeta
1st May 2013
 
AKITAMBULISHWA kama Msemaji wa Serikali, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene, amehojiwa na kituo redio Clouds, kuhusu dhana ya uzalendo kwa taifa.

Mwambene amekuwa miongoni mwa mamia ya raia wa Tanzania wanaohojiwa na kituo hicho, hususani kupitia kipindi chake cha power breakfast kinachorushwa nyakati za asubuhi.

Mkurugenzi huyo wa idara nyeti katika kuielimisha na kuifahamisha jamii, akasema dhana ya uzalendo inapotea nchini, ikisababishwa na mambo kadhaa, mojawapo wapo ni kusemwa vibaya kwa Usalama wa Taifa.

Akasema wapo wanasiasa wanaosema vibaya Usalama wa Taifa na vipo vyombo vya habari vinavyoandika 'vibaya' kuhusu Usalama wa Taifa.

Baada ya Mwambene kuzungumza katika mahojiano yaliyofanyika Jumatatu wiki hii, alihojiwa pia Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)-Tanzania Bara, Pius Msekwa. Nitamuelezea baadaye.

Niweke wazi kwamba Usalama wa Taifa ni taasisi katika uhai wa taifa lolote duniani, hata kama itajengwa kwa mfumo na jina tofauti, umuhimu wake unabaki pale pale.

Niliwahi kuzungumza na mmoja wa maofisa waandamizi wa taasisi hiyo ambaye hivi sasa amestaafu, moja ya mambo aliyoyasisitiza ni uadilifu wake-Usalama wa Taifa.

Akasema kutokana na umuhimu wake unaoifanya kuwa mhimili asilia ambao taifa linasimama juu yake, ikitokea Usalama wa Taifa ukayumba, nchi haitabaki salama, lazima itayumba.

Hoja hiyo inajenga ukweli usiopingika, kwamba Usalama wa Taifa, kwa maana ya taasisi na watendaji wake wanapasa kuuishi uadilifu wa hali juu, ikibidi hata kupoteza maisha binafsi, ili mradi uadilifu uwe nguzo yao.

Hali hiyo si kwa sababu uendeshaji wake unategemea kodi za wananchi pekee, la hasha, bali asili, mapokeo, mafundisho, dira, mwelekeo, malengo na wajibu wao, unasimama juu ya kulifanya taifa liwe mahali salama pa kuishi.

Hayo yanapofanyika, umma utayaona, utayahisi na kuyakubali, kwamba taasisi hiyo inaiepeleka nchi katika mwelekeo unaostahili, hivyo njia pekee ni kuinga mkono, kuipongeza na 'kuikingia kifua' mahali popote na wakati wowote.

Lakini inapotokea zikajengeka hoja zenye mwelekeo wa kuhoji ufanisi wa taasisi hiyo, iwe kupitia kwa wanasiasa hasa wabunge ama vyombo vya habari, haina maana kama watu wanakosa uzalendo kama anavyotaka kuaminisha Mwambene wa Maelezo!

Ingekuwa ni suala la kutangaza hadharani undani wa utendaji kazi, mipango, mbinu, mikakati na rasilimali za Usalama wa Taifa, hapo ningekuwa wa kwanza kuwapinga, ikibidi kuwatemea mate, hata kama yasiwafikie, wanaoyafanya hayo.

Lakini kuhoji ufanisi, ikiwa Usalama wa Taifa kwa maana ya watendaji wake, unalipeleka taifa mahali panapo… ama pasipostahili, kwamba wanasimamia maadili, wajibu na madumuni ya kuwepo kwake, liwe kosa!

Binafsi, niliwahi kukutana na kijana wa kiume akiwa na rafiki yake wa kike yaani msichana niliyefahamiana naye, nikatambulishwa.

Baada ya utambulisho uliofanywa na msichana yule, rafiki wa kiume akajiweka wazi kwamba, anafanya kazi Usalama wa Taifa (akaitaja ofisi yake ilipo). Ilidhihirika kweli yupo katika taasisi na ofisi hiyo.

Swali lililoniijia akilini, ni kwa manufaa gani kijana yule aliamua kujitambulisha kwangu kwa kazi ninayojua haitakiwi kufanywa kirahisi namna hiyo, tena kwa mtu anayekutana naye kwa mara ya kwanza?

Na ikiwa amejitambulisha hivyo, inakuwaje katika utekelezaji wa majukumu yake, anayopewa na wakuu wake wa kazi kwa maslahi ya nchi?

Hilo linaweza kuwa moja ya mambo mengi yanayoidhoofisha taasisi hiyo, (pengine) kuanzia kwa kwa baadhi ya waajriwa vijana hadi maofisa waandamizi, ingawa ni kwa namna tofauti.

Ndio maana, anapozungumzia kwa juu juu, kwamba 'kuigusa' Usalama wa Taifa ni moja ya viashiria vya ukosefu wa uzalendo wa taifa, sikumuelewa nab ado sijamuelewa Mwambene wa Maelezo!

Kama nilivyoelezea awali, zipo taasisi muhimu kama Usalama wa Taifa alioutaja Mwambene, zinaopaswa kumilikiwa, kukubalika, kuungwa mkono na 'kukingiwa kifua' na umma, pasipo kujali tofauti za kijamii zilizopo.

Lakini kutokana na utendaji usioridhisha wa baadhi ya watumishi wa watendaji wake, Usalama wa Taifa kama zilivyo taasisi nyingine, zina haki ya kukosolewa ili zijitazame upya, kuliko kudhani imesimama, ikajikuta inaanguka.

Ndio maana ninarejea katika msisitizo wangu kwamba Usalama wa Taifa wana nafasi kubwa katika uhai na uendelezaji wa Tanzania iliyo salama. Waliopata fursa ya kuwa ndani yake, wanapaswa kulijua hilo, kulisimamia hilo na kuliendeleza hilo.

Ni kupitia uhifadhi wa maadili mema, misingi ya taifa, dira na mwelekeo wake, Usalama wa Taifa watalifikia kusudio hilo na kuwa 'chombo bora' kwa Watanzania wote.

Wakati nikilijadili hilo, niungane na Mzee Msekwa, alipoainisha baadhi ya mambo muhimu katika kujenga uzalendo ndani ya Tanzania.

Kupitia kipindi hicho cha Clouds, Msekwa akayataja kuwa ni usalama, ulinzi, maadili na upendo kwa vilivyo chini ya miliki ya umma.

Msekwa akasema wapo wanaoyatenda hayo katika kuhakikisha uzalendo unadumu na wapo wanaozembea ama kuyahujumu, akiwaita `walioptea'.

Nilimeamua kuyajadili maana kwa maana, ni ukweli usiopingika hata kwa sekunde moja, kwamba Tanzania inahitaji kurejesha uzalendo.

Uzalendo unahitajika katika maeneo na nyanja tofauti. Ingawa ni hivyo, tujiulize, sababu gani ziliufanya uzalendo uliokuwepo kiasi cha kuifanya Tanzania na Watanzania kuwia kwa umoja, kupotea?

Mambo gani ya kizalendo yalikuwepo na sasa hayapo, waliochochea yakapotea, walifanya nini vinavyopaswa kuepukwa ili uzalendo uerejee katikakati ya umma?

Tanzania yenye uzalendo inawezekana, tufunguke, tuache unafiki!

Mashaka Mgeta ni Mhariri wa Makala wa NIPASHE Jumapili na mchambuzi wa masuala ya siasa. Anapatikana kupitia simu namba +255754691540 ama barua pepe; mgeta2000@yahoo.com

 
 

0 comments:

Post a Comment