Sunday 2 October 2016

[wanabidii] Profesa Lipumba hakujiuzulu kwa bahati mbaya

BAADHI ya wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), wanaonekana kuridhishwa na kuunga mkono mwongozo wa Msajili wa vyama vya siasa nchini kuhusu uhalali wa uenyekiti wa Profesa Ibrahim Lipumba.

Katika maoni mbalimbali yaliyotolewa mojawapo ikawa ni ya mwanasheria msomi na Sahibu yangu wa siku nyingi tangu Mwenge Primary School na baadaye Isevya Secondary School, Stanley Kalokola, ambaye alitanabaisha hivi; "I don't believe in coincidence when it comes to Politics…jiulize kama ilikuwa ni bahati mbaya kwa Lipumba kujiuzulu na kama ni bahati mbaya kwa yeye kutaka kutengua uamuzi wake, jiulize timing pia,"

Kwa tafsiri isiyo rasmi, kwa maneno yake ya mwanzo aliyoyaandika kwa kimombo, amesema, "Linapokuja suala la siasa, yeye haamini katika sadfa (kutokea kwa mambo yenye kufanana au kuleta maana).

Pia katika muktadha huo, ametuasa kutafakari kunako muda ambao Profesa Lipumba amerejea chamani. Sasa nami kama mtu huru, nimejikuta nikipata machache ya kuchangia, hasa katika vipengele vya 'Timing', na Sadfa (Coincidence).

Yamkini kwamba, baada ya Lipumba kutofautiana misimamo ya kimaamuzi na Maalim Seif Shariff Hamad, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, hasa katika kumfanya Edward Lowassa, aliyekatwa jina na CCM na kutimkia CHADEMA, kuwa mgombea Urais chini ya mwamvuli wa UKAWA, akaamua kujitenga na maamuzi hayo kwa kuandika barua ya kuomba kujiuzulu wadhifa wake wa Uenyekiti wa chama cha CUF.

Huku 'mitaani' inasemekana kwamba, ile ilikuwa ni 'Timing' (ya Profesa Lipumba, aliyoifanya akiamini kwamba barua yake, kwa mujibu wa Katiba yao ya CUF, itawasilishwa kwenye mkutano mkuu ili wajumbe wa mkutano huo wapate kuijadili ili kuridhia ama kutoridia kujiuzulu kwake.

Alitegemea endapo mkutano ule utaitishwa kwa wakati, na barua yake kusomwa huku yeye akitakiwa kutoa ufafanuzi mahala patakapohitaji ufafanuzi wake, itaudhihirikia mkutano mkuu huo kwamba CUF – Bara kinakwenda kuistawisha Chadema huku chenyewe kikijimaliza kimyakimya kwa kuachiwa majimbo machache mno kwenye uchaguzi mkuu (kama ilivyofanyika), na hata kwenye hayo majimbo machache pia, zingelifanyika figisu za kuwabana mbavu (kama ilivyofanyika Segerea – kwa Mtatiro), nk.

Hivyo, kama mkutano mkuu ungaliziamini hoja za Profesa Lipumba, kwa yakini ingalikuwa kiama kwa Maalim Seif anayetuhumiwa kupanga na kubariki mpango huo.

Kwamba kwenye siasa hakuna sadfa, ina maanisha kwamba kujiuzulu kwa Profesa Lipumba hakukutokea kwa bahati-bahati tu, hivyo nami kwa mtiririko huohuo, sifikiri kwamba ilitokea kwa bahati mbaya Maalim Seif 'akaikalia' ile barua ya Profesa Lipumba badala ya kuitisha mkutano mkuu kuijadili ili kufikia maamuzi katika kipindi kilekile cha Uchaguzi.

Bila shaka ilikuwa ni 'Timing' ya Maalim Seif. Akaitia kwapani barua ya Profesa Lipumba, pengine baada ya kuiona hatari ya mkutano mkuu kutoa maamuzi magumu, hivyo akahepa. Kufikia hapo, ile 'Timing' iliyokusudiwa na Lipumba ikapea hewani mithili ya kishada kiendacho harijojo. Ikawa ni kicheko kwa Maalim, na maumivu kwa Lipumba.

Baada ya uchaguzi mkuu sasa, malengo ya Maalim Seif yakiwa yametimia kwa kiwango fulani, ndipo akatangaza uchaguzi wa kujaza nafasi ya mwenyekiti.

Si kwamba Maalim Seif hakufahamu kuwa katiba ya chama chake inataka kwanza barua ya aliyejiuzulu ikathibitishwe na mkutano mkuu ndipo mambo ya uchaguzi yafuate, hasha! Maalim alilitambua hilo.

Sasa, kwa kuwa Katiba haikuzingatiwa, kwa kuacha kuiwasilisha barua ya Profesa Lipumba kwenye mkutano mkuu, na badala yake Maalim akaanza kuandaa uchaguzi ilhali akijua dhahiri kwamba kujiuzulu kwa Profesa Lipumba hakujakamilika kisheria, ndipo ghafla Profesa Lipumba akaibuka kwa kuandika barua mpya ya kuitengua ile barua yake ya awali aliyoomba kujiuzulu.

Kwa kuwa Katibu mkuu hakupata kuuwasilishia mkutano mkuu, barua ya awali ya Profesa Lipumba kuomba kujiuzulu, na ghafla akapokea barua nyingine ya kuomba kuitengua ile barua ya awali ambayo haikujadiliwa wala kuufikia tu mkutano mkuu kama Katiba inavyotaka, hivyo sasa, mpira ukabaki kwake wa kwamba awasilishe barua zote mbili: ya ombi la kujiuzulu na ya kutengua ombi hilo, au asiwasilishe tena barua yoyote kwa kuwa ombi limekwishatenguliwa.

Mpira ukabaki kwa Maalim Seif; kitanzi shingoni, kisu mbavuni.

Kwa ustadi na utulivu, Maalim Seif akasikika akisema kwamba hana matatizo na Profesa Lipumba, na kwamba ni rafikiye mkubwa sana, hivyo, kama akitaka kurejea kitini watayaongea na kuyamaliza.

Kumbe mzee wa watu ana 'Timing' zake, akaibuka na kusema mkutano mkuu uko palepale, na kwamba baada ya ajenda ya kwanza ya kuijadili barua ya Profesa Lipumba na itafuata ajenda ya pili ya kufanya uchaguzi wa mwenyekiti mpya.

Unaweza kustaajabu Maalim Seif aliwezaje kujivika u-Sheikh Yahya Hussein kutabiri matokeo ya mkutano mkuu kwamba yatamkataa Profesa Lipumba kurejea kitini, kiasi cha kuendelea kutumia fedha za chama kuratibu ajenda ya uchaguzi ilhali anafahamu kwamba ikitokea wajumbe wa mkutano mkuu wamemtaka Profesa Lipumba aendelee na wadhifa wake, itakuwa amefanya ufujaji wa fedha za chama kwa kuzitumia kuandaa uchaguzi ambao utashindwa kufanyika? Ile nayo haikuwa bahati mbaya 'Timing'.

Kwenye mkutano mkuu, kila kambi ikijipanga vyema kutumia mbinu za 'Timing' ili kufanya hitima ya zoezi. Yakatokea yaliyotokea, sina haja ya kuyakariri tena hapa. 'Timing' za Profesa Lipumba kurudishwa na wajumbe wa mkutano mkuu na 'Timing' za Maalim Seif kumwondosha rasmi Profesa Lipumba kupitia wajumbe wa mkutano mkuu (hasa wa Zanzibar) zikavia kwa wote kukosa shabaha walizolenga, baada ya mkutano mkuu kuvurugika.

Kwa tabia zilezile za vyama vingi vya upinzani, haraka Maalim Seif akaitisha Baraza Kuu, na kuwasimamisha upesi wanachama na viongozi wa CUF walioonekana kukiuka amri zake; akiwemo Profesa Lipumba mwenyewe, Magdalena Sakaya, na wengineo, kabla hawajaleta madhara kwake. Ni 'Timing'!

Profesa Lipumba naye, kwa kushirikiana na waathirika wenziye, hakufanya ajizi wala zohali, akalipeleka suala lake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Fransic Mutungi ambaye ndiye mlezi wao wote. Majibu yakatoka kwamba kwa mujibu wa Katiba yao CUF, Profesa Lipumba angali Mwenyekiti halali wa Chama hicho.

Kama ilivyokuwa kwa Maalim Seif, alipofanya 'Timing' ya 'kuwashughulikia' wale aliowaona ni hatari mara baada ya mkutano mkuu kuvurugika na kuitisha Baraza Kuu, Profesa Lipumba naye baada ya kurejea kitini amefanya 'Timing' ya 'kuwashughulikia' wale wote alioona ni hatari kwake au pengine kwa mustakabali wa afya ya chama. Sasa wanashughulikiana kwa 'Timing' kubwa mno.

Kama ilivyokuwa kwa kina Sakaya, Lipumba, na wenzao, walipokuwa wakiiona ofisi chungu mara baada ya Maalim Seif kufanya 'Timing' ya kuwasimamisha, huku akina Julius Mtatiro, Mbarala Mharagande, na wenzao wakichekelea, sasa imekuwa zamu yao kuiona ofisi chungu.

Lipumba mara baada kurejea kitini, na kuanza kupangua safu ya wakurugenzi wanaoshutumiwa kuachilia umeya kwa CHADEMA kwenye majimbo ya Ubungo na Kinondoni.

Kama ilivyo katika michuano yoyote ile, baada ya hekaheka ya muda mrefu, wachuanaji huanza kuishiwa pumzi na kujawa na jazba kufuatia 'Timing' kugongana, kinachofuata hapo ni utasikia 'Bondia kaumwa sikio', mara 'mpira wa kichwa umepigwa kwa mguu' nk.

Kwa muktadha huu sasa, tunaanza kusikia 'wasanii' wetu wakirudia kuziimba tena nyimbo za zamani ambazo masikio yetu yameshachoka kuzisikia kwamba fulani anatumiwa na CCM, mara kahongwa fedha, mara msaliti, mara mamluki, nk.

Sasa, wakati Prof Lipumba na Maalim Seif wakienda sako kwa bako katika kucheza na 'Timing', huku tukishuhudia aliyecheka mwisho akijivunia 'Timing' zake badala ya yule aliyecheka mwanzo, nasi wapenzi wa burudani ya siasa tupeane burudani za mijadala ya staha na Timing badala ya chuki, ghadhabu.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment