Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania na Rais wa Taasisi ya Women for Africa Foundation, Mama Maria Tereza Fernandez de la Vega, akisalimiana na maofisa wa ulinzi na usalama mara baada ya kuwasili katika bandari ya Nansio, Ukerewe hivi karibuni kuzindua mradi wa kilimo cha viazi lishe unaofadhiliwa na taasisi yake ya inayoshughulikia maendeleo ya Wanawake wa Afrika.
Mama Getrude Mongella (waliosimama katikati mwenye blauzi nyekundu) akifafanua jambo kwa Mkamu wa Rais mstaafu wa Hispania na Rais wa Taasisi ya Women for Africa Foundation, Mama Maria Tereza Fernandez de la Vega, wakati walipotembelea mradi wa kilimo cha viazi lishe wilayani Ukerewe. Kushoto kwa Mama Mongella ni Bi. Leocadia Vedastus, ambaye ni mshiriki kiongozi wa mradi huo.
Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania na Rais wa Taasisi ya Women for Africa Foundation, Mama Maria Tereza Fernandez de la Vega, akiangalia bidhaa zilizo mbele yake ambazo zinatokana na viazi lishe katika kuongeza mnyororo wa thamani. Hii ni wakati alipokwenda kuuzindua mradi huo wilayani Ukerewe katika Mkoa wa Mwanza.
MRATIBU wa mradi wa akinamama wapambanao na mazingira wa Green Voices, Alicia Cebada, amesema kwamba wamefarijika na mradi huo kwa kuwa umeonyesha mafanikio makubwa nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara yao ya kutembelea miradi mitano kati ya 10 inayotekelezwa na wanawake wa Tanzania,hivi karibuni mratibu huyo kutoka taasisi ya Women for Africa Foundation, alisema hawakutegemea kama miradi waliyoianzisha akinamama hao ingeweza kufanikiwa katika kipindi kifupi tangu kuwapatia mafunzo.
"Ni kipindi kifupi tangu wanawake hawa walipopatiwa mafunzo nchini Hispania, lakini kwa hakika miradi waliyoibuni imeonyesha mafanikio, ni endelevu, rafiki wa mazingira na italeta tija kwao na taifa kwa ujumla," alisema Alicia.
Aidha, alieleza kwamba, changamoto pekee ambayo ipo mbele yao ni kuhakikisha miradi hiyo inasimama na kuwafundisha wanawake wengi kadiri wawezavyo ili kuhakikisha wanajiletea maendeleo katika maeneo yao kiuchumi na kijamii.
"Tumewaona wanawake wa Ukerewe wanavyolima viazi lishe na kuongeza mnyororo wa thamani, tumewaona wanawake wa Kijiji cha Kitanga huko Kisarawe wakiongozwa na 'Malkia wa Muhogo' Abia Magembe, tumewatembelea akinamama wanaofuga nyuki kupambana na ukataji wa misitu huko Kisarawe, pia tumewaona wanawake wa Morogoro namna wanavyokausha mboga na kuwa na uhakika wa akiba ya chakula, na hapa (Bunju) tumeshuhudia jinsi kilimo cha uyoga kilivyo na faida, ni miradi mizuri, endelevu na rafiki mkubwa wa mazingira," alisema.
Alicia Cebada na Anna Salado wakiangalia namna ya mifuko ya kupandikizwa uyoga inavyohifadhiwa kwenye mapipa wakati walipotembelea kilimo cha uyoga Bunju hivi karibuni.
Picha ya pamoja na akinamama wafugaji nyuki katika misitu ya Pugu na Kazimzumbwi wilayani Kisarawe.
Alicia alisema kwamba, taasisi yake inaangalia uwezekano wa kuwaongezea nguvu akinamama wa Green Voices katika awamu ya pili ya mradi baada ya kuridhishwa na mafanikio ya majaribio ili waweze kukabiliana na changamoto walizonazo.
Hata hivyo, aliipongeza serikali ya Tanzania kwa kuunga mkono mradi huo na akasema hiyo inawapa nguvu hata wanawake wanaoshiriki na ni dalili njema kwamba wengi wanaweza kujifunza na kuitekeleza miradi kama hiyo na kubuni mingine yenye manufaa kwa jamii.
"Tumeona jinsi serikali ilivyo bega kwa bega na wanawake hawa katika sehemu zote tulizotembelea, hii inaonyesha kwamba miradi waliyoibuni siyo yao pekee bali ya jamii nzima na itawahamasisha wanawake wengi zaidi kujifunza na kuitekeleza katika maeneo yao," alisema.
Kauli ya Alicia imekuja muda mfupi baada ya rais wa mfuko huo, Mama Maria Tereza Fernandez de la Vega kuzuru nchini kushiriki uzinduzi wa mradi huo Julai 11, 2016 ambapo ulizinduliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan.
Mama Samia aliahidi wakati wa uzinduzi kwamba serikali yake itahakikisha inakuwa bega kwa bega kusaidia miradi hiyo iwe endelevu ili kuunga mkono juhudi za utunzaji wa mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kuongeza uhakika wa chakula, kuwakwamua wananchi na umaskini pamoja na kuongeza ajira, hasa kwa wanawake.
Kwa upande wake, Mama Maria Tereza, ambaye ni makamu wa rais mstaafu wa Hispania, alieleza kufurahishwa kwake na jitihada za akinamama wa Tanzania na kusema kwamba taasisi yake inaangalia namna ya kuwasaidia zaidi.
"Tumefarijika sana na jitihada hizi, tumesikia changamoto zinazowakabili na tutaangalia namna gani ya kuwasaidia kuzikabili katika awamu ya pili ya mradi huu wa Green Voices," aliwaeleza akinamama wa Ukerewe mbele ya wananchi waliokusanyika katika eneo la Shule ya Bukongo.
Mkurugenzi wa ubunifu wa taasisi hiyo, Noellia, aliwapongeza wanawake wanaotekeleza miradi hiyo kupitia Green Voices na kuwataka waendelee kushikamana ili kusonga mbele huku akiwapa moyo kwamba changamoto zilizopo zinaweza kutatuliwa.
Noellia alisema kwamba, kuonekana kwa changamoto ni dalili njema kwamba kumbe miradi hiyo inatekelezeka ikiwa changamoto hizo zitafanyiwa kazi.
"Kama unabaini vikwazo basi ni dalili kwamba kumbe vikifanyiwa kazi unaweza kusonga mbele, msikate tamaa," alisema wakati alipozungumza na wanawake wafuga nyuki wilayani Kisarawe.
Naye mkurugenzi wa mawasiliano wa taasisi hiyo, Ana Salado, alipongeza namna vyombo vya habari vilivyojitahidi kuripoti mafanikio ya wanawake hao na kusema kwamba hali hiyo imesaidia kuihamasisha jamii kushiriki kutokana na ukweli kwamba miradi yote iliyobuniwa na akinamama hao ina tija kwa taifa zima.
Jumla ya wanawake 15 wa Tanzania walipatiwa mafunzo ya wiki mbili jijini Madrid, Hispania mapema mwaka huu ambapo 10 kati yao walikwenda kuanzisha miradi mbalimbali wakati watano ni wanahabari ambao wamekuwa wakiripoti maendeleo ya miradi hiyo.
Mratibu wa mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela Balisidya, amesema kwamba mradi huo unatekelezwa katika mikoa sita ya Tanzania Bara ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Kigoma, Mwanza na Kilimanjaro.
Anawataja wanawake walioanzisha miradi hiyo – miradi na mikoa watokayo vikiwa kwenye mabano – kuwa ni Regina Kamuli (Mkuranga, Pwani – Majiko Banifu), Abiah Magembe (Kisarawe, Pwani – Usindikaji wa Muhogo na Mtama), Magdalena Bukuku (Kinondoni, Dar es Salaam – Kilimo cha Uyoga), Mariam Bigambo (Dakawa, Morogoro – Ufugaji wa Nyuki), na Esther Muffui (Morogoro – Ukaushaji wa Mboga na Matunda).
Wengine ni Farida Makame (Kilimanjaro – Majiko ya Umeme-Jua), Leocadia Vedastus (Ukerewe, Mwanza – Kilimo na Usindikaji wa Viazi Lishe), Monica Kagya (Kisarawe, Pwani – Ufugaji wa Nyuki), Sophia Mlote (Kinyerezi, Dar es Salaam – Kilimo Hai cha Nyanya na Mbogamboga), na Evelyn Kahembe (Uvinza, Kigoma – Kilimo cha Matunda).
Kupitia miradi hiyo, zaidi ya wanawake 300 wamepatiwa mafunzo mbalimbali huku program nyingine za mafunzo kwa vitendo zikiendelea katika makundi yao.
Anna Salado akifurahi pamoja na akinamama wa Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe. Wanawake hao wanajihusisha na mradi wa usindikaji wa muhogo na mtama.
Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Milikieli Mansweat Mahiku, naye aliongozana na viongozi wa taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika, Anna Salado (kushoto) na Alicia Cebada (wa pili kulia) kukagua kilimo cha mboga mboga katika Kata ya Mzinga kwenye manispaa hiyo. Wa tatu kushoto ni Mratibu wa Mradi wa Green Voices Tanzania, Secelela Balisidya, na aliyeinama ni mshiriki kiongozi wa mradi wa ukaushaji mboga na matunda wa Mzinga, Esther Muffui.
Kuendelea kwa miradi hiyo kumeonyesha dalili njema hasa baada ya serikali kuahidi kuiendeleza kwa kushirikiana na wanawake hao, ikiwa ni pamoja na kuangalia fedha za maendeleo kupitia mfuko wa wanawake na vijana katika kila halmashauri.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Estomih Chang'a, alikwenda mbali zaidi baada ya kuwashauri wananchi wa wilaya hiyo kujikita katika kilimo cha viazi lishe ili kuongeza akiba ya chakula na kukabiliana na baa la njaa.
"Ninashauri wananchi wote wa Ukerewe kulima viazi lishe kwa sababu mbali ya kuongeza akiba ya chakula, lakini vinaongeza pato la familia na taifa hasa vikichakatwa ili kutoa bidhaa mbalimbali," alisema.
Naye mjumbe wa bodi ya taasisi hiyo, Balozi Getrude Mongella, akizungumza katika uzinduzi huo kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Bukongo mjini Nansio, aliwaomba watendaji wa serikali kusimamia kidete mradi huo ili kuondoa njaa katika visiwa vyote vya wilaya ya Ukerewe.
Alisema kwamba, kuanzishwa kwa mradi huo wilayani humo siyo tu kutawakwamua wanawake na wananchi wote, lakini pia kunaifanya Ukerewe kuwa kiini cha usambazaji wa zao hilo katika maeneo mengine ya Mkoa wa Mwanza.
"Ninawaomba watendaji wa serikali ya wilaya hamasisheni zao hili lilimwe katika visiwa vyote na kama ilivyokuwa zamani ambao mbegu zote za pamba zilitoka Ukerewe, basi tengenezeni na zalisheni mbegu za kutosha msambaze katika wilaya nyingine za Mkoa wa Mwanza.
"Naamini mkoa wote ukilima zao hili njaa haitakuwepo na wanawake wanaweza kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo wakiziuza zitawakwamua kiuchumi," alisema.
Naye Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mh. Selemani Jaffo, ambaye pia ni Mbunge wa Kisarawe, amesema yuko tayari kushirikiana na wanawake wanaosindika muhogo katika Kijiji cha Kitanga pamoja na wilaya nzima ya Kisarawe kuhakikisha wanajikwamua kiuchumi kutokana na zao hilo.
Aidha, Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Milikieli Mansweat Mahiku, alisema atahakikisha anasimamia kwa bidii ili teknolojia ya ukaushaji wa mboga na matunda isambae kwa wanawake wote wa manispaa hiyo.
Aidha, aliahidi kwamba, yeye na madiwani wenzake watahakikisha asilimia 10 ya fedha za maendeleo katika halmashauri wanapatiwa wanawake na vijana wanaofanya miradi endelevu yenye tija na inayolenga kutunza mazingira kama wanavyofanya wanawake hao wa Mzinga.
"Sasa hivi bajeti ya maendeleo ya halmashauri imeongezwa hadi asilimia 60, sasa kati ya fedha hizo, asilimia 10 ni miradi ya wanawake na vijana, ambayo kama tutaisimamia vyema na kuielekeza kwenye miradi endelevu kama hii italeta tija.
"Kama wahisani hawa wamejitokeza na wamekuja kutoka Hispania, sisi kama serikali nasi tunapaswa kuunga mkono jitihada hizi ambazo zina tija kubwa," alisema Naibu Mstahiki Meya.
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 comments:
Post a Comment