Na Abraham Byamungu
Biblia inasema mwenye nacho ataongezewa na asiye nacho hata kile kidogo alichokuwa nacho atanyang'anywa - Mathayo 25:29.
Huu mstari huwatatiza wengi. Wengi hujiuliza, sasa huyu hana kitu inakuwaje ananyang'anywa kidogo alichokuwa nacho? Kidogo hicho amekitoa wapi?
Baada ya tafakari ya muda mrefu juu ya neno hili, Mungu aliweza kunifunulia tafsiri kwamba hakuna hasiye nacho. Kila mtu Mungu humjalia kwa kadiri anavyostahili; sasa ni juu ya mtu huyo kukitumia vyema kile alichopewa.
Mfano wa asiyenacho kunyang'anywa ni kwamba huyo hujiona hana kitu ndipo Mungu mtoaji huamuru basi anyang'anywe hicho alichonacho kwa sababu ya udanganyifu wake kwa kusema hana kitu. Kinyume chake kwa yule anayejitambua kwamba anacho kitu na kumpa Mungu sifa, basi Mungu hutoa baraka ili mtu huyo aongezewe!
Maandiko haya ni mfano halisi unaohakisi fikra na maisha yetu watanzania. Mungu ametupa kila lililojema ndani ya nchi yetu. Ametupa madini, ardhi yenye rutuba, maji ya kila aina (bahari, maziwa, mito, mabwawa), mbuga za wanyama, misitu, hali ya hewa safi, milima, mabonde na mambo mengine mengi mazuri ambayo yanazidi kuongezeka kila kukicha. Bahati mbaya sana watanzania tumekumbwa na ugonjwa wa 'asiyenacho' na kumkufuru Mungu kwa kujiona hatuna kitu hivyo kanuni ile ile inaendelea kututafuna, 'tunanyang'anywa na kupewa wale wanaojitambua'!
Tumeendelea kulia juu ya umaskini wetu na kuwaangukia wale tunaodhani wanacho; nao bila hiyana wamekuja kutimiza agizo la Mungu kwamba maadamu tumekiri hatuna kitu basi kile watakacho kikuta sio chetu hivyo ni halali kuondoka nacho.
Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sura ya 9(k) inatamka kwamba nchi inatawalika kufuata misingi ya demokrasia na ujamaa. Sina tatizo sehemu hii ya katiba mpaka hapo labda kwa mawazo ya wengi sehemu itakapo badilika kwenye katiba mpya na huenda neno 'ujamaa' au sehemu nzima ikabaki kama ilivyo. Ujamaa una misingi mizuri ya umoja na upendo.
Sasa hili la ujamaa liko kwenye jamii zetu na mioyoni mwetu pia. Katika jamii nyingi za kitanzania chakula kikisalia kinakuwa 'kiporo' kwa ajili ya kesho hususani kwa watoto. Kwa familia zenye upendo na kwa misingi ya kijamaa, huita hata watoto wa jirani ili kiporo kiliwe na kuisha, kisiwe kiporo tena kwani kitaharibika. Sasa masikitiko yangu ni kwamba rasilimali zetu tumezigeuza kiporo na hivyo tunahitaji watu 'majirani' kutoka nje tusaidiane kiporo hiki. Ndio, rasilimali zimekuwa kiporo hata kabla hatujala na kusaza; na mbaya zaidi tunaita watoto wa jirani ambao ni walafi kupindukia!
Utaratibu wa kiporo ni kwamba yule aliye mkubwa anakula kidogo na kuwaachia wadogo. Maajabu ni kwamba hawa watoto wakubwa kutoka kwa jirani sio tu wanaenda sambamba na watoto wenyeji, ambao ndio wametoa mwaliko, bali wanamaliza kabisa na nafasi inapopatikana wanawashika wenyeji wao mkono! Haidhuru hiki ni kiporo!
Kesho tutaenda kwa jirani tena na kulalamika kuwa hatuna kitu zaidi ya kiporo chetu, 'Tanzania has abundance of natural resources which are yet to be utilized'. Msisitizo ni kuwa sisi hatuna kitu na wasitegemee chochote kutoka kwetu na pia sisi hatuhitaji chochote kutoka kwao zaidi ya kutuongoza kukishughulikia kiporo hicho. Ndio tutasema hatuna kitu, hatuna wasomi, hatuna ujuzi, zana hatuna, hatuna teknolojia, na zaidi sana hatuna uelewa juu ya thamani ya rasilimali zetu.
Masikitiko yangu ni pale ikifika siku hata hicho kiporo kikaisha. Picha iliyojaa uchungu na huzuni inanijia, namuona 'baba' ameweka mikono nyuma akienda kwa jirani na kumwaambia hatuna kitu na kile kiporo tulichozoea kuwaita watoto wake waje washiriki nasi sasa hakipo! Tuamke sasa majuto ni mjukuu.
Haya yote yametokea, yanatokea na huenda yakaendelea kutokea kwa sababu hatujitambui. Hatuijui thamani yetu, zaidi sana kosa letu kubwa ni kujiona kuwa sisi sio kitu. Wasomi kimya, wataalamu tafiti zao mpaka pesa na msaada kutoka kwa jirani, walio bahatika kupata elimu wameikumbatia na imebaki vichwani mwao badala ya kuieneza kwa jamii, wachache 'walalahai' waliofanikiwa kujikwamua ndio wametoka hivyo na familia zao hawajui watu baki wanaamkaje, na mwisho ukombozi wa matatizo yetu tumewatwisha watu wachache kisa 'wanaharakati' kama vile wao hawana roho za nyama!
Natoa wito kwa watanzania wote kuitambua thamani yetu na mali alizotujalia mwenyezi Mungu. Tunaomba viongozi tuliowaweka madarakani watuongoze vema katika hili. Tukienda nje ya mipaka yetu tusimame imara, tujivunie tunu hizi na tuzitangaze kwa faida yetu. Kwenye mikataba ya rasilimali zetu, tuangalie maslahi yetu kwanza na daima tusikubali chini ya masilahi ya wote-watanzania na wageni yazingatiwe, 'win-win'. Hapa naomba nisisitize kwamba tunapoingia mikataba, wajibu wetu ni kuangalia na kutetea maslahi ya watanzania na tuache upande wa pili ufanye ya kwake. Watanzania tumeumizwa sana na kauli mambo ya haibu kwamba baada ya miaka 50 ya Uhuru bado mikataba ya kubadilishana 'shanga' kwa 'dhahabu' inaendelea. Kauli za wataalamu wetu hawakuwa makini kwenye mikataba ni jambo lililozoeleka kwenye masikio ya watanzania.
Tujifunze kwa familia za majirani, Marekani na washirika wake. Ukifuatilia kauli mbalimbali za Rais yoyote wa wakati wowote na wa kutoka upande wowote wa itikadi aliyewahi kutawala Marekani, kauli mbiu na sera huwa hazibadiliki 'kwa faida ya raia wa Marekani'. Kauli zenye mlengo huo kamwe hazibadiliki hata kama Rais huyo anahutubia kwenye majukwaa ya kimataifa. Mara nyingi imekuwa kawaida ya dunia kutafsiri kwamba lile lililo jema kwa Marekani basi ni jema kwetu pia, jambo ambalo sio sahihi mara zote na hivyo kupelekea 'sisi kukosa wao kupata'. Imeendelea kuwa hivyo kwa sababu dunia, kuondoa majirani hawa, imekiuka kanuni ya kwanza ya mikataba ambayo ni kuangalia maslahi yako kwanza kwani usipofanya hivyo hakuna atakayefanya kwa ajili yako!
Sisi sio kwamba hatuna kitu, bali tuna kitu tena chenye thamani, hivyo tunahitaji kukitambua ili tuongezewe! Sisi tuna mali wao wana mahitaji, tusijinyenyekeze! Tuko sawa katika mizania ya kibiashara, tuzungumze kama wenye mali na tuwasikilize wale walio wateja wetu kwa kutumia kanuni za kimasoko. Pale ambapo tunafaida ya ziada kwa vitu hadimu, tuitumie vizuri nguvu ya soko, 'monopoly' kujinufaisha. Tusipotimiza vema wajibu wetu, wenzetu watatimiza wa kwao na hakuna atakaye tuonea huruma siku tukiwa wateja wao.
Mungu ibariki Tanzania!
Source: http://www.wavuti.com/#ixzz2OfoyCHDO --
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
0 comments:
Post a Comment