Wednesday 13 March 2013

[wanabidii] MBINU ZAO CHAFU ZIMEDUNDA!

ENZI zile za Luteni Yusuph Makamba, CCM walikwepa sana kutumia polisi moja kwa moja. Hata hawakuwaamini kabisa polisi. Mfano, nakumbuka jinsi Makamba wakati wa uchaguzi mdogo wa 2008 kule Tarime alipotangaza kwamba polisi wa Tarime mchana ni CCM, lakini usiku wanageuka kuwa CHADEMA.

Nadhani hiyo ndiyo iliyowapa akili walipokwenda Busanda hawakutaka tena kushughulika na polisi. Wakakusanya wavuta bangi kwenye mitaa ya Manzese na kuwapa mazoezi kisha kuwapeleka Busanda wakiwa wamevalia kininja na kazi yao ikawa moja tu: kutembeza kipigo kwa kila aliyejidai kuipigia debe CHADEMA.

Walitembeza ubabe mpaka wakatangazwa washindi wa uchaguzi ule Busanda. Wakati CHADEMA bado hawajashtuka wakaenda na mbinu hizo hizo Biharamulo na kwenyewe wakatangazwa kwa nguvu kuwa washindi.
Mbinu nyingine ninayoikumbuka sana ni ile ya kununua wapinzani. Nakumbuka walivyomnunua Tambwe Hizza na Frank Magoba kutoka CUF, Aman Kabourou na Shaibu Akwilombe kutoka CHADEMA na wengineo.
Tambwe akapewa kazi ya propaganda kuipiga CUF na upinzani kwa ujumla.

Akwilombe kazi ilikuwa moja tu ya kuwaonesha Watanzania kwamba CHADEMA ni chama cha watu wawili tu: Mtei na Ndesamburo. Nakumbuka ilivyokuwa kwenye uchaguzi mdogo wa Tarime 2008. Makamba akapanda jukwaani, akawaambia Wana Tarime: "Mnaponyoosha vidole viwili hewani eleweni maana yake nini. Maana yake CHADEMA ni chama cha watu wawili, yaani Mtei na Ndesamburo.

Sasa nitamleta jukwaani Shaibu Akwilombe ili awathibitishie hilo". Akwilombe akapanda jukwaani na kuanza kuhutubia: "Ndugu zangu watu wa Tarime, mara ya mwisho nilipokuja Tarime, nilikuwa na Mbowe, Zitto, …." Mara Makamba akamkatisha akisema, "Akwilombeeee, ninachotaka mimi uwaeleze kwamba chama cha CHADEMA ni cha watu wawili". Akwilombe akasema: "Nakuja huko mheshimiwa katibu mkuu". Akaendelea: "Waheshimiwa Wana wa Tarime, wakati huo nilikuwa Naibu Katibu mkuu wa CHADEMA". Makamba akaingilia kati tena, "Aaaha! Akwilombe waeleze CHADEMA ni chama cha nani?". Ilikuwa kama kichekesho vile, mgosi bwana!

Lakini kama kuna kazi kubwa aliifanya Makamba ni kuimarisha kitengo cha makao makuu cha propaganda. Kile kitengo kazi yake ilikuwa kupika majungu, uongo, uzushi, na kila aina ya kashfa kwa wapinzani na kuzisambaza kila leo.

Bahati mbaya alipoondoka, katika kile kinachoweza kutafsiriwa kama kutaka kufuta kabisa nyayo zake, waliomfuatia walikifuta kitengo kile na kumfuta kazi yule mgosi mwenzie aliyemweka pale.
Waliofuatia walikuja na mbinu ya kutumia polisi. Wanakwenda wanazuia maandamano ya CHADEMA, wanaua watu ili wananchi waogope kuambatana na chama hicho. Tena wakawa wanapiga propaganda kwamba chama hicho ndicho kinachowaua watu.

Mungu si Athumani, kule Iringa wakati wanamuua Mwangosi kamera ya mwandishi ikawanasa na kuwaumbua.
Mwisho, ikabidi mwenyekiti wako wa taifa awatangazie viongozi waliokurithi kwamba wasitumie polisi maana Watanzania wamekwisha kuwashtukia na sasa kadiri wenzao wanavyouawa na polisi ndivyo wanavyozidi kukiunga mkono chama cha cha upinzani.

Wakaja na ya kutumia mawaziri wa serikali. Wakataka kurejea ya mwaka 47 ya kuwapeleka mawaziri mikoani kutangaza jinsi serikali ilivyofanya mambo mengi mazuri. Wakaishia kuzomewa na mradi huo ukafa kifo cha mende.
Sijui kwa nini hawajamuuliza Makamba maana hata hiyo mbinu aliwahi kuijaribu mwaka 2007 kunadi uzuri wa bajeti ya Zakhia Meghji, wakaishia kupopolewa mawe!

Hivi karibuni wakaja na mbinu ya mwaka ambayo ni ghali sana, lakini kama mgonjwa yuko ICU unafanyaje?
Nayo ni mbinu ya kununua muda wa hewani kwenye vituo vyote vya televisheni nchini na kutangaza jinsi serikali ya awamu ya nne ilivyoleta maendeleo.

Hiyo ndiyo mbinu aliyoingia nayo Kapteni mstaafu Abdullahman Kinana. Naona kama kapteni kuna vitu anafanya ambavyo vinaonekana vya kitoto vile! Yaani mwananchi asione maendeleo kwa macho yake pale kijijini anapoishi ama mtaani anakoishi ama kwenye mji anaoishi mpaka wewe uje umwoneshe picha kwenye kioo cha runinga?
Je, ukichukua picha za Dubai ukazitumia kuwadanganya watu wa Musoma kwamba ndivyo mji wa Kigoma Ujiji unavyoonekana leo?

Mimi sijui kama hata kuna wananchi katika enzi hizi za dijitali wataacha kuangalia mdahalo wa wagombea urais wa Kenya wakaenda kuangalia porojo za Kapteni Kinana.

Hiyo mbinu nayo imekufa. Hela za chama zinaendelea kuteketea lakini ukitaka kujua hivyo vipindi haviangaliwi na watu japo wanajitahidi kutoa matangazo 'live' ya Bunge na kuweka vipindi hivyo, hebu waulize wanapokea maoni mangapi kwa siku ya wananchi wanaoshukuru kwa kuoneshwa maendeleo ya 'picha'?

Mbinu ya hivi karibuni kabisa ambayo nayo imeingia mchanga ni ya kutumia uongozi wa Bunge. Spika na Naibu Spika wawabane kabisa wapinzani wasipumue na kupata nafasi hata kiduchu ya kupenyeza hoja zao zenye nguvu.
Ha ha ha ha! Hiyo nayo imeingia mchanga. Umati uliojitokeza kwenye mkutano wa CHADEMA Jumapili pale Mwembeyanga kupinga uongozi wa Bunge sijui wanautazamaje. Tunaaminishwa kwamba Makinda ameshapigiwa simu 200 na sms 400 za kumpinga alichokifanya bungeni na kumtaka ajiuzulu.

Sijui kama ni kweli lakini muhimu ni kwamba hata hiyo nayo 'imebumba'. Wafanyeje sasa, wameshajaribu hata kurudia mbinu za Makamba lakini imeshindikana.

Moja, mbinu ya kununua wapinzani imechuja. Wazungu wanasema ni obsolete (imepitwa na teknolojia). Siku hizi hakuna tena wapinzani wa maana wanaodiriki kununuliwa na kuja CCM.

Ndiyo maana kina Kafulila na Danda Juju walioichoka CHADEMA walikwenda NCCR. Siku hizi ni bora kutoka chama kimoja cha upinzani kwenda kingine cha upinzani.

Wamegundua kwamba mnapowarudisha kwenu mnawapepea joto kwa muda mfupi tu halafu mnawatupa jalalani.
Wamejifunza kwa yaliyomkuta Lamwai, Kabourou, Akwilombe, Hizza, Magoba, Ngawaia, Nsanzugwako, Shitambala na wengineo.

Wamerejea CCM na kuuawa kisiasa, hawasikiki tena! Nani tena atafanya huo mchezo? Mimi nilishaazimia siku yakinishinda CHADEMA, kuliko niende CCM ni bora niache siasa.

Mbinu ya kutumia maninja nayo imekwama kwa kuwa CHADEMA sasa wana Red Brigade kali kuliko Green Guard.
Waliishuhudia Igunga na Arumeru Mashariki mpaka wakasema CHADEMA Igunga iliingiza magaidi kutoka Libya na Arumeru Mashariki walileta Mungiki.

Pia wakati wao wamekifuta kitengo cha propaganda na kumkabidhi Nape kazi ya propaganda, CHADEMA wameimarisha Kurugenzi ya Habari na Uenezi.

Siku hizi Nape yuko bize kusambaza propaganda, Mnyika yuko bize kusambaza habari njema za matumaini kwa Watanzania kupitia CHADEMA.

Ama kweli siku ya kufa nyani miti yote huteleza. Pole Kapteni Kinana. Luteni Makamba wanakukumbuka sana ila wanaona aibu kukurudisha!

0 comments:

Post a Comment