Wednesday 13 March 2013

[wanabidii] BUNGE LISILOKUWA NA MENO!


KIKAO kilichomalizika­ cha Bunge kimetuacha tena na mawazo mapya na wengine wetu kuturudisha nyuma miaka mingi.
 
Kwa namna mambo yalivyokwenda inaelekea Spika Anne Makinda na naibu wake, Job Ndugai, bado wanaamini katika zile zama za chama kushika hatamu.
 
Hizi ni zile zama ambapo kiongozi wa chama katika ngazi yoyote alionekana mwenye mamlaka makubwa na katika ngazi ya taifa ilifikia mahali wanazuoni wakaanza kulumbana kati ya chama na Bunge ni kipi chenye maamuzi ya mwisho na watu wa aina ya Pius Msekwa walitetea sana hoja ya chama kushika hatamu.
 
Kwa wakati ule wa chama kimoja hilo halikuwa jambo la ajabu sana. Lakini katika mfumo wa vyama vingi anapotokea yeyote akadhani chama chake kina nafasi kubwa kuliko nguvu ya wananchi basi ajue ana mawazo mgando na uwezo wake wa kufikiri unatia shaka.
 
Tumewahi kulalamika hali hii ya wabunge kuendekeza vyama vyao kwa viwango vya kuwasaliti wapiga kura wao.
 
Na wanaoangukia katika mtego huu mara nyingi ni wabunge wa Chama Cha Mapinduzi ambao bila weledi wanadhani wana jukumu la kuibeba serikali ya chama chao hata kama kwa kufanya hivyo wanazima hoja za msingi za kuwakwamua wananchi.
 
Na jambo hili hujionesha mara nyingi wabunge hao wanapopewa nafasi ya kuzungumza bungeni. Huanza kwa mapambio na kutoa sifa ambazo kwa hakika unaweza kusema wanaivika serikali kilemba cha ukoka.
 
Wanajipendekeza­ kiasi cha kusema wanaunga mkono hoja za serikali asilimia mia kwa mia lakini kabla ya kumaliza hotuba lazima watazungumza matatizo ambayo kama wanajua maana ya asilimia mia kwa mia basi wasingekuwa tena na nyongeza kwenye hotuba zao.
 
Inawezekana kabisa wabunge hasa wa Chama Cha Mapinduzi wanalazimika kuwa na chembe chembe za unafiki kutokana na ukweli kwamba kitumbua chao kinategemea maamuzi ya chama. Hii pia ni kwa wabunge wa vyama vingine lakini leo sina mjadala kuhusu hao wengine.
 
Baada ya kuona na kusikia yaliyotokea bungeni katika kikao kilichomalizika­, inafika mahali unathubutu kuhoji ikiwa wabunge wa CCM na viongozi wao wanafikiri kwa akili zao wenyewe na kwa manufaa ya waliowapigia kura au bado wamezama katika kusema "zidumu fikra za mwenyekiti".
 
Hoja kama ya John Mnyika kuhusu tatizo la maji si hoja inayopaswa kubezwa na mtu yeyote anayejigamba kuwa na akili timamu. Asiyejua tatizo la maji ni fisadi aliyejitenga na kuishi peponi bila kujua raia wa kawaida wana matatizo gani. Kwa jambo hilo tu linatosha kumuondolea sifa ya kuwa kiongozi tena mwakilishi wa watu. Wabunge wanaoshangilia au kuzomea kwa kuangalia mtoa hoja badala ya kufanya tafakuri ya hoja wameingia bungeni kwa makosa.
 
Wangestahili zaidi kufanya kazi nyingine yoyote inayohitaji kupayuka bila kutia akili.
Yapo matukio mengi mno ambayo Bunge la sasa hivi limeonekana dhahiri kuibeba serikali badala ya kufanya kazi yake ya kuisimamia na kuibana. Na kuna mtiririko wa matukio ambapo Bunge limetafuta sababu za kiufundi kuzuia mbubujiko wa fikra huru kujadili jambo.
 
Bunge limetumia visingizio kama suala la kuwapo mahakamani au serikali kuwa inashugulikia jambo na kuzima hoja za msingi ambazo bila shaka zingeifanya serikali ijikute imesimamia vidole gumba!
 
Katika mazingira hayo Bunge limegeuka kuwa ngao ya serikali kupitia kwa watu aina ya William Lukuvi wanaonekana kuifurahia mbeleko hiyo.
 
Ukimdekeza sana mtoto anaweza kuwa mjinga. Hali si tofauti sana kwa serikali. Kama serikali inafahamu kwamba haiwajibiki na haitawajibishwa­ na chombo chochote lazima itabweteka na matokeo yake wengi tayari tumeanza kuyaona.
 
Kama serikali inafahamu kwamba Bunge limegeuka baraza ambalo hata likitoa maelekezo imebaki ni utashi wa serikali kuyatimiza au kuyakataa. Na mijadala mikubwa ambayo kimsingi ingetikisa nchi imeachwa kunyauka bila chochote kutokea.
 
Na kama Bunge halina uwezo au linajinyima uwezo wa kuiwajibisha serikali, uwepo wa Bunge ni maigizo na ni afadhali lisiwepo kabisa.
 
Unaweza kujiuliza kwa viwango hivi vya kuzuia uchokonozi bungeni kumekuwa na faida gani hasa katika kuendesha nchi yetu? Kama viongozi wa Bunge ndio vinara wa kuzuia fikra pevu za kuikosoa serikali kwa kujidai wanatumia kanuni basi ni heri kutokuwa na kanuni hizo.
 
Ni bahati mbaya mno unapoona anayeongoza Bunge akifikiri kwamba wajibu wake wa kwanza ni kwa chama chake. Na aina hii ya Bunge limefanya hata baadhi ya mambo ya kisheria kuwa kama maigizo tu.
 
Chukulia mfano wa kumthibitisha waziri mkuu bungeni. Kimsingi katika Bunge la aina ya Bunge letu, rais akishamteua waziri mkuu hoja ya kuthibitishwa bungeni imebaki kama igizo tu.
 
Na hata waziri mkuu anapokuwa bungeni tumeshuhudia mara kadhaa akipewa kinga na spika ili asijibu maswali ambayo yanaonekana kama kumtundika msalabani.
 
Na haya yanafanyika kwa sababu tayari kuna udhaifu mkubwa unaofahamika katika serikali. Na udhaifu huu unatokana na ulegelege wa Chama Cha Mapinduzi ambacho kiukweli kimeshindwa kuunda serikali thabiti. Imekuwa serikali inayojikuta imewekwa kwenye kona na wapinzani.
 
Imekuwa serikali inayojaribu kufurukuta ili walau ionekane ipo na kuzima kashfa moja baada ya nyingine. Ni katika Bunge la aina hii ndiyo maana serikali inaweza kuchomoka katika mambo ya aibu kama kusafirisha wanyama, kuficha hela nje ya nchi, kutowajibika kwa mauaji ya raia bila kujali wana hatia au la.
 
Ni Bunge la aina hii ambalo linaweza kunywea pale hoja nzito inapojibiwa kisiasa kwa kusema serikali ipo katika mchakato au serikali ni sikivu au pambio lingine lolote liwalo. Ndipo tulipofikishwa na wabunge wetu.
 
Nguvu na mamlaka ya Bunge yamebaki katika kurasa na maandishi ya katiba bila nguvu hizo kujidhihirisha katika utendaji. Ndiyo maana hata watendaji wengine wakijua kuna udhaifu huo wameweza hata kuwatuhumu wabunge kula rushwa.
 
Ndiyo maana Bunge hili ambalo linapaswa kuwakilisha wananchi linashindwa kuhoji pale risasi ya serikali inapotumika kunyofoa uhai wa mwananchi.
 
Ni Bunge ambalo halina nguvu au linajipunja lenyewe nguvu zake, linaweza kufanya kazi ya propaganda za kuisifu serikali badala ya kuinyooshea kidole pale inapoharibu.
Na kama Bunge letu halitafanya juhudi za makusudi kuvunja ndoa yake na serikali basi kazi ya Bunge itakuwa haina maana na ni afadhali waende likizo isiyo na malipo.
Nawasilisha.

0 comments:

Post a Comment