Thursday 6 September 2012

[wanabidii] Re: siasa uchwara kwenye haki za walemavu..

nakubaliana na wewe kim kwamba dhana kwamba ''watu wote ni sawa'' ni dhana dhaifu ya kibwanyenye kwa sababu yapo makundi mengi ya jamii yamewekwa pembeni katika kuupata ''usawa''..lakini tusife moyo..tuendelee kupambana..''haki haidondoki kama ''mana'' waliyodondoshewa waisraeli..haki hupiganiwa''
On Wednesday, September 5, 2012 11:10:30 PM UTC+3, Ado Shaibu wrote:

  1. SIASA UCHWARA ZIKOME KWENYE USIMAMIZI WA HAKI ZA WALEMAVU.
    Ado Shaibu.
    Makala yangu ya wiki iliyopita(kwenye gazeti la RAI) kuhusu uwezo na nafasi ya walemavu kwenye tasnia ya elimu imevuta hisia za wengi. Katika makala ile nilionesha jinsi ambavyo walemavu wanaweza kufaulu vyema kwenye mitihani na kuwa wataalamu wabobezi katika taaluma mbalimbali kama mazingira rafiki na vitendea kazi hitaji
    ka vitatolewa kwa walemavu. Nilitoa mfano wa Faridi Adallah ambaye licha ya ulemavu wa macho, ameongoza mitihani ya kidato cha sita mwaka huu kwenye kundi la sayansi ya jamii na lugha.
    Pia nilitoa mfano wa Sudi Andanenga, mshairi maarufu ambaye kwa mtizamo wangu, yeye ni zaidi ya malenga. Andanenga ni shaha wa malenga!. Mfano mwingine nilioutoa ni wa viongozi walemavu wanaofanya vizuri kwenye medani ya siasa kama Said Baruwany (Mbunge wa Lindi kwa tiketi ya CUF) na Alshaimaa Kwegir (Mbunge wa vitu maalumu-CCM na mjumbe wa Tume ya kukusanya na Kuratibu Maoni ya Katiba Mpya.)
    Licha ya simulizi hizo za kutia moyo nilizozitoa, sehemu kubwa ya watu waliowasiliana na mimi kwa njia ya barua pepe na simu wana mtizamo tofauti.Wengi wanaona habari ya walemavu wachache waliofanikisha kwenye taaluma anuai, licha ya kusisimua, bado ni tone dogo ambalo haliwezi kukata kiu ya madhila wanayokumbana nayo walemavu kwenye elimu na nyanja nyingine hapa nchini.
    Mwitiko huo wa wasomaji ulinisukuma kufanya utafiti zaidi.Kama alivyowahi kusisitiza Mao Tse Tung, no research, no right to speak (Bila kufanya utafiti, mtu hana haki ya kuzungumza).Kabla sijasonga mbele ni vyema niwashukuru wadau wa Kituo cha Taarifa kuhusu Ulemavu(CID), kituo cha CCBRT na kitengo cha maktaba cha Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kuwezesha utafiti wangu.
    Baada ya kuzungumza na wadau muhimu wa haki za walemavu, hitimisho nililolipata ni kushamiri kwa ubabaishaji kwenye utoaji na usimamizi wa haki za walemavu. Wanaleksikolojia wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam wanatujuza kwamba ubabaishaji ni kubambia mambo; kulifanya jambo bila weledi au kulijua barabara. Kwa kweli hata haki za walemavu zinatekelezwa kwa kubambanywa na kubabaisha tu; hakuna uhakika wala uthabiti.
    Yapo maeneo mengi ambayo mtu anaweza kuyapigia mfano, lakini mimi nitagusia maeneo machache niliyoyatafiti.
    Mosi, hebu tutazame ubabaishaji katika agizo la kuwafutia ada walemavu. Tarehe 27.8.1999, katika kipindi maalum cha BBC, rais Benjamin Mkapa alitoa ahadi ya kuwafutia ada walemavu. Dhamiri hii ya rais Mkapa ilitokana na ukweli kwamba hali ya walemavu ni duni sana. Wakati watu waio na ulemavu wanahangaikia malazi, mavazi, chakula na mahitaji mengine ya msingi,walemavu wana changamoto maradufu.Wanapaswa pia kutafuta baiskeli maalum za viwete, fimbo na miwani za walemavu wa macho, dawa za ngozi kwa albino n.k.
    Mahitaji hayo ya lazima yanafanya maisha ya walemavu kuwa magumu zaidi. Katika ripoti ya haki za binadamu iliyoandaliwa na Kituo cha Msaada wa Sheria Zanzibar, inakadiriwa kwamba kaya nyingi za walemavu zinaishi chini ya dola moja. Pia ikumbukwe kwamba uwezo wa walemavu kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji mali kwa uthabiti ni mdogo mno. Familia za walemavu pia zinasongwa na jukumu la kutoa uangalizi wa karibu kwa walemavu. Haya yote yanafifisha pato la familia. Hivyo basi, uamuzi wa kuwafutia ada walemavu ulikuwa uamuzi wa kiungwana na wakizalendo.
    Ili kurasimisha ahadi ya rais, tarehe 2 septemba 2009, katibu mkuu wa rais (wakati huo mh D.S.L Foka) alitoa waraka maalum wenye kumbukumbu namba SHC/PP.447 kwenda kwa waziri wa elimu na waziri wa tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) akiwaamuru ''kutekekeleza agizo la kuwasamehe walemavu ada''.
    Naye katibu mkuu wa wizara ya elimu(wakati huo mh.A.R.M.S Rajabu)alitoa waraka maalum wa serikali wenye kumbukumbu namba C/BA:308/495/01/3.Katika waraka wake mh Rajabu alimtaka waziri wa TAMISEMI ''kuwaagiza watendaji wa halmashauri za wilaya kutekeleza agizo rais la kufuta ada kwa walemavu''.
    Je baada ya urasimishaji wote huu wa agizo la rais, walemavu walifutiwa ada kama ilivyoagizwa? Kwa hakika, ahadi hii ya rais iliishia kwenye makabrasha ya serikali.Ubabaishaishaji nilioouzungumza ukachukua nafasi yake! Watendaji wa halmashauri nyingi za wilaya hawakutekeleza agizo la rais la kuwafutia ada walemavu.Ni halmashauri chache sana zinajikongoja kutekeleza agizo hilo lenye tija kwa walemavu.
    Hebu tujiulize kidogo. Ni walemavu wangapi wameathirika kwa ubabaishaji huu wa watendaji wa serikali? Ni walemavu wangapi wameshindwa kwenda shule kwa umasikini wa familia zao au kukosa ushirikiano wa kifedha kutoka kwa wazazi wenye mtizamo potofu wa kutowapeleka walemavu shule?
    Binafsi nina mifano kadhaa. Frank weston nilikosoma kidato cha kwanza hadi cha nne, nilimshuhudia Issa Shaibu, kiziwi aliyeacha shule akiwa kidato cha pili kutokana na changamoto ya ada na matatizo mengine ambayo nitayaeleza kwenye hitimisho langu.
    Wakati naendelea kufanya utafiti wa mada hii, nilikutana na Charles kunji, albino aliyekatisha masomo yake ya kidato cha tano (Shule ya Sekondari Mzinga) kwa kukosa ada. Hao ni baadhi tu. Kwa hakika wapo wahanga wengi wa ubabaishaji huu. Kulingana na takwimu zilizotolewa kwenye ripoti ya haki za binadamu inayotolewa na LHRC, mpaka mwaka 2010,Tanzania ilikuwa na wastani wa walemavu 3,456,900.Takwimu hizo pia zinaonesha kwamba asilimia58.5 ya walemavu walijiunga na elimu ya msingi. Cha kushangaza,ni asilimia7.6 tu ya walemavu walijiunga na elimu ya sekondari!
    Rai yangu: serikali itekeleze mara moja waraka wa mwaka1999 wa katibu mkuu kiongozi unaowataka watendaji wa serikali katika ngazi ya halmashauri kuangalia uwezekano wakuwafutia walemavu ada.Pia Asasi Zisizo za Serikali(AZISE) zifuatilie suala hili kwa karibu ili haki hii iliyoahidiwa na serikali miaka mingi iliyopita, itekelezwe kwa uthabiti.
    Eneo la pili ambalo ubabaishaji unajidhihirisha kwa uwazi ni haki ya walemavu ya kupata taarifa. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, katika ibara ya 18(d) inatoa haki ya kupata taarifa kwa kila mtu.kwa upande wa zanzibar, katiba ya zanzibar ya mwaka 1984 kama ilivyorekebishwa mwaka 2010 inasisitiza,katika ibara ya18(2), umuhimu wa kila raia kupewa taarifa wakati wote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi.
    Kwa mtizamo wangu haki ya kupata taarifa ni chachandu inayokoleza haki nyingine ziweze kupatikana kwa urahisi.Mathalani,mtu kama hana taarifa ya kutosha kuhusu namna ya kujikinga na gonjwa jipya la mlipuko au hatari ya kutokea tetemeko la ardhi na mafuriko,haki yake ya kuishi inaweza kuwa mashakani. Hebu tuangazie mfano mwingine. Mtu asipopata taarifa za kutosha kuhusu ajira au elimu, anawezaje kufanikisha haki na wajibu wake wa kufanya kazi na kujielimisha?
    Kwa upande wa walemavu, Mkataba wa kimataifa wa Haki za Wenye Ulemavu wa mwaka 2006 (ibara ya 21) unatoa wajibu kwa serikali kuhakikisha walemavu wanapata haki yao ya kupata habari na taarifa muhimu kwa njia wanayoielewa. Hapa nchini, Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka2010 katika ibara ya 18(d) imesisitiza suala la umuhimu wa taarifa kuwa katika namna ambayo walemavu wanaielewa kama vile maandishi ya nukta nundu (braille)kwa vipofu.
    Sasa tujiulize. Je matakwa haya ya haki ya walemavu kupata taarifa yanayosisitizwa na sheria za kimataifa na kulindwa na sheria zetu yanatekelezwa ipasavyo? Thubutu! Kama kuna eneo limejaa ubabaiwashaji basi hili linaongoza.Anayebisha afunge safari mpaka kitengo cha elimu maalum pale wizarani,bodi ya mikopo ya elimu ya Juu (HESLB) na Tume ya Vyuo vikuu(TCU) Kisha awaulize ''mabosi'' wa vitengo hivi kama wameandaa hata nakala kumi za taarifa zao muhimu za jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu kwa ajili ya walemavu wa macho(yaani katika muundo wa braile).Nakuhakikishia,wakikukabidhi hata nakala moja fahamu dunia inakaribia kufika mwisho na masihi yu njiani! Hawana hata nakala moja!
    Wito wangu:Wadau wote, hasa kitengo cha elimu maalumu cha wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi, waikabili changamoto hii. Nafahamu ni ndoto za alinacha kuamini kwamba, kufumba na kufumbua, taasisi zote za umma zitaweza kuandaa taarifa zao katika braile.Hilo linahitaji muda kidogo.Lakini hili la kuwanyima walemavu taarifa muhimu za kujiunga na vyuo katika njia wanayoielewa linapaswa kuchukuliwa hatua upesi! Hivi inagharimu shilingi ngapi kuandaa hata nakala mia za miongozo ya bodi ya mikopo na TCU zilizo katika muundo wa braille?
    Mlima wa kero za walemavu ni mrefu na ni vigumu mtu kuupanda wote. Sisemi kila kero itatuliwe leo au kesho. Yako mambo yanahitaji muda.Tatizo letu ni kutopangilia vyema vipaumbele vyetu.katika makala zangu mbili nimesisitiza sana suala la elimu kwa walemavu kwa sababu naamini kama haki hii itatekelezwa ipasavyo, haki nyinginezo kama vile ajira, afya, makazi n.k zitarahisishwa. Mamia ya walemavu tunaowaona barabarani wakiomba ni kutokana na mkazo wetu duni katika uboreshaji wa haki ya elimu kwa walemavu.
    Lakini haki ya elimu itatekelezwaje katika lindi hili la ubabaishaji? Nauliza, haki ya elimu kwa walemavu itafanikishwa vipi katika taifa lenye chuo kikuu kimoja tu(Sebastian Kulowa College-SEKUCO) kinachoandaa walimu wa ngazi ya shahada wa kuwafundisha wanafunzi walemavu? Mwishowe, wanafunzi walemavu kama ndugu yangu Issa Shaibu (kiziwi) wanaishia kupelekwa shule kama Frankweston (wilaya ya Tunduru) Zisizo na mwalimu hata mmoja mwenye ujuzi wa kufundisha walemavu. Unatarajia nini?
    Fanya tafakuri ya kina,kisha chukua hatua!
    Mwandishi anapatikana kwa namba ya simu 0653619906 na barua pepe: adoado75@hotmail.com

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

0 comments:

Post a Comment