Thursday 6 September 2012

[wanabidii] Mwandishi Ni Mjumbe, Hauawi - Makala Yangu Raia Mwema Jana Jumatano

Na Maggid Mjengwa,

HUWEZI kutawala miili ya watu ukaacha mioyo yao. Ndiyo, mjumbe hauawi, ni kauli ya hekima ya tangu enzi za wahenga wetu.

Mwandishi wa habari na Mwenyekiti wa Chama cha Wandishi wa Habari mkoani Iringa, Daud Mwangosi ameuawa. Polisi wanatuhumiwa kuhusika na mauaji hayo.


Jumapili ya Septemba 2, 2012 itabaki katika kumbukumbu za Watanzania kwa mamilioni kwa kufikiwa na taarifa za kutisha za mauaji ya mwandishi wa habari. Haya yanaingia katika historia kuwa ni mauaji ya kwanza kwa mwandishi wa habari kufanyika hadharani tangu nchi hii ipate Uhuru.

Wengi watakuja kukumbuka walikuwa wapi na walifanya nini siku walipopata taarifa hizo za kutisha. Binafsi, taarifa ile ya mauaji ya Daud Mwangosi siku ile ya Jumapili ya huzuni kwa Taifa ilinikuta nikiwa Iringa, umbali wa mwendo wa saa moja  kwa gari kufika eneo la tukio, Nyololo, Mufindi.


Jioni ile nilikuwa nikifundisha soka ya watoto. Mara baada ya kupata taarifa zile kwa simu,  nilisitisha mazoezi yale ya watoto. Nikawapa taarifa zile.  Nilipowaambia kuwa nimepata taarifa sasa hivi kuwa mwandishi wa habari ameuawa Mafinga, mtoto mmoja akaniangalia na kuniuliza; " Kwanini?"

Ndiyo, swali la mtoto yule ndilo umma wa Watanzania unapaswa kujiuliza sasa; KWA NINI?


Mwandishi wa habari ni mjumbe katika jamii. Anapokuwa akifanya kazi yake hapaswi kuwa na hofu ya kudhuriwa kwa kukusudia na waliopata mafunzo ya  kutumia silaha.  Ndivyo ilivyo kwa watumishi wa Msalaba Mwekundu, wanapokuwa kazini kwenye maeneo hata ya vita.


Askari asiyejua kutofautisha kati ya mwanahabari aliyeshika kamera, mtu wa Msalaba Mwekundu aliyeshika mkoba wa Huduma ya  Kwanza na raia anayefanya vurugu au adui aliyeshika silaha vitani, huyo hawezi kuwa ni askari makini.


Polisi katika nchi ni  moja ya viungo muhimu vya dola kuu. Polisi ni mkono mrefu wa dola ( State's extended arm). Inapofika mahali, mkono huu muhimu unapoonyesha udhaifu wa ndani katika mfumo wa utendaji kazi wake, basi, umma nao unakosa imani na mkono huu mrefu. Ndipo hata raia wa kawaida niliyemsikia kwenye runinga ya ITV akitamka; " Kama polisi si makini, basi ni heri wasiwepo watuache wenyewe tuendeshe mambo yetu, maana sisi wananchi tunaishi kwa amani na utulivu".

Kauli kama hizi ni kiashiria cha umma unaopungukiwa imani na dola na viungo vyake, ikiwamo polisi. Hili haliwezi kuwa jambo jema.


Na hakika, kama  Taifa,  tunafanya makosa kuamini,  kuwa  nchi yetu ni ya amani kwa vile wananchi wetu hawagombani.


Kama watu hawagombani basi maana yake ni nchi ina amani yaweza kuwa tafsiri potofu ya maana nzima ya amani.  Maana, kama watu hawagombani mahali pasipo na haki, usawa na uadilifu wa viongozi; mahali palipojaa dhuluma,unyanyasaji na maovu mengine  wanayotendewa au wanaotendeana wanajamii,  basi, amani hiyo itakuwa ni ya muda tu.


Maana, kwa watu wenye kuishi kwenye mazingira hayo bila kugombana wala kutokea uvunjifu wa amani, hiyo  itakuwa na maana ifuatayo; ama watu hao hawaelewi kuwa wanaishi katika mazingira hayo ya dhuluma na maovu mengine wanayotendewa au kutendeana, au wamejawa na  hofu.


Hivyo basi, kwa hilo la mwisho, itakuwa ni amani iliyojengeka katika misingi ya hofu. Na hofu hiyo haiwezi kuwa ya kudumu. Kuna siku mwanadamu hufikia ukomo wa kuhofia. Ukimwandama sana mjusi, mwisho hugeuka nyoka! Ndipo hapo tunapoona nchi zinalipuka na watu kuchinjana.


Tumefika mahali hata wawakilishi wa wananchi kwa maana ya wabunge , wanatiwa mbaroni na polisi katika mazingira ya kudhalilisha, tulishuhudia hili likimtokea Mbunge wa Viti Maalumu, CUF, Tabora Mjini.  Mbunge ni mwakilishi wa wananchi. Mbunge ni mjumbe aliyetumwa na wananchi. Ana kinga ya kikatiba.

Kwa polisi kumdhalilisha  mjumbe wa wananchi ina maana pia ya kuwadhalilisha waliomtuma. Haya ni matendo ya aibu.


Kilichomtokea mwandishi Daud Mwangosi ni aibu pia ya Taifa hata kimataifa. Kupunguza aibu hii ni kufanyika kwa uchunguzi huru, na kwa wote watakaobainika kuhusika na aibu hii wachukuliwe  hatua za kisheria. Na wenye kustahili kuwajibika wawajibike kulinda heshima ya  serikali iliyo madarakani.

Hii ni nchi yetu. Katika tofauti zetu hizi za kiitikadi tusifike mahali tukashindwa kuongea kama Watanzania kwa kutanguliza maslahi ya Tanzania. Kuna umma uliopo na unaokuja. Umma  unaotegemea sana busara katika uongozi wetu.


Tuanze sasa kujenga utamaduni wa kuitumikia nchi yetu kwa kufanya na kuamua yale yenye maslahi kwa Tanzania. Hivi vyama vya siasa vipo leo na kesho havipo. Vinakuja na kuondoka, lakini Tanzania kama nchi itakuwapo daima.


Tusifike mahali  tukabaki tunawaangalia wanasiasa wetu, kwa maslahi yao binafsi, ya makundi yao na vyama vyao,  wakashinikiza au kuelekeza yale  yenye kuchochea machafuko makubwa ya kijamii. Ni wajibu wa viongozi wa kisiasa kutanguliza busara katika kila maamuzi wayafanyao.


Na tunafanyaje pale tunapowaona viongozi  wa kisiasa na watendaji wakifanya maamuzi yasiyo na busara na kusababisha Watanzania wenzetu kupoteza uhai na hata kuchochea machafuko?

Jibu; Kama Watanzania wazawa na wazalendo wa nchi hii, tuna wajibu wa kuyalaani matendo yao maovu.


Na katika nchi zetu hizi, ni kazi rahisi sana kuanzisha vurugu  na kujenga mazingira ya chuki na  uhasama, lakini ni kazi kubwa sana kumaliza vurugu na kuondosha mazingira hayo ya chuki na uhasama. Na nchi yetu kamwe haiwezi kupiga hatua za maana za maendeleo katikati ya mazingira ya vurugu, chuki na uhasama, uwe wa vyama vya siasa au wanajamii.


Kihistoria, Watanzania tumeishi kwa amani na upendo bila kuwa na chuki na uhasama miongoni mwetu unaotokana na tofauti zetu za kidini na kikabila. Tunaziona sasa, dalili za baadhi ya wanasiasa, kwa malengo ya kisiasa,  kutaka kupandikiza miongoni mwetu uhasama na chuki kwa kutumia tofauti zetu za kidini na kikabila, tofauti zetu za kiitikadi.  Wanafanya hivyo mara ile wanaposhindwa kujenga hoja za kisiasa kwenye majukwaa ya kisiasa. Hawa ni watu hatari sana kwa maslahi ya taifa letu.


Katika nchi zetu hizi, ni wanasiasa wa aina hii ambao, katika kufanikisha malengo yao,  huwa tayari hata kuwalipa vijana wasio na ajira na kuwavutisha bangi ili washiriki vurugu za kisiasa, kidini na kikabila.  Tumeyaona hayo Liberia, Ivory Coast na hata katika nchi jirani na kwetu.


Tusipokuwa makini, yako karibu kupisha hodi kwenye nchi yetu, kama si tayari kuwa yameshaingia ndani ya nchi yetu.

Hii ni nchi yetu. Tutafanya makosa makubwa kuwaachia viongozi wa kisiasa pekee, jukumu la kulinda maslahi ya nchi yetu.  Tunapita sasa katika kipindi kigumu tangu tupate Uhuru.


Dunia imebadilika, na nchi yetu inapitia kwenye kipindi cha mabadiliko. Hakuna  mtu au chama cha siasa kinachoweza kuyazuia mabadiliko  haya. Kufanya hivyo ni kutuletea machafuko na kuvunja amani yetu. Tuna jukumu la kufanya tunayoweza, na kwa kutanguliza busara, kuipitisha salama nchi yetu katika kipindi hiki cha mabadiliko.

Maana, tukiingia kwenye machafuko, basi, hakutakuwa na mshindi, maana, sote tutashindwa.


Mungu Ibariki Tanzania Mungu Ibariki Afrika.
0788 111 765
http://mjengwablog.com

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

0 comments:

Post a Comment