Thursday 16 August 2012

[wanabidii] Kuhusu habari ya gazeti la Rai, "UCHIMBAJI WA URANI SERIKALI YAONYWA"

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA NISHATI NA MADINI

TAARIFA KWA UMMA

Tarehe 16 Agosti, 2012 gazeti la Rai Toleo Na.986 katika ukurasa wake
wa kwanza na watatu lilichapisha taarifa yenye kichwa cha habari
"UCHIMBAJI WA URANI SERIKALI YAONYWA" na kuwa kumezuka sakata lingine
ambapo kampuni ya kigeni imeanza kuchimba madini hatari aina ya urani
kwa kile wachunguzi wanasema ni kinyume cha sheria. Gazeti hilo
liliendelea kuandika kwamba Tanzania haina sera ya urani na kwamba
hata kama Serikali imeruhusu uchimbaji huo, ni kinyume cha sheria kwa
sababu hata Serikali yenyewe haijatunga sheria ya uchimbaji urani.
Tunasema habari hii inamalengo ya kuupotosha umma.

Mwandishi wa habari hii bila ya kutaja jina lake anaeleza kuwa
hakuweza kuwasiliana na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini licha
ya yeye kuwaandikia ujumbe kitu ambacho hakina ukweli. Kutokana na
unyeti wa habari yenyewe mwandishi alipaswa kuhakikisha anapata
taarifa kamili kutoka Wizarani na siyo kutoa taarifa kwa matakwa
binafsi.

Habari hii imelenga zaidi katika kupotosha umma badala ya kuelimisha
kama ambavyo mwandishi ameshindwa kueleza kwa ufasaha ni nini hasa
kusudio lake. Tunaheshimu Uhuru wa vyombo vya Habari na tungependa
kama kuna suala lolote linalohitaji ufafanuzi, Wizara ipo tayari muda
wowote kutoa maelezo badala ya kukimbilia kuandika habari
zinazojichanganya na kusababisha usumbufu kwa wananchi.

Tunatumia fursa hii kwa mara nyingine kuufahamisha umma kuwa kama
Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini Mhe: Prof Sospeter Muhongo
alivyosema kwenye hotuba ya bajeti ya mwaka huu kuwa pamoja na kuwepo
kwa maeneo mbalimbali hapa nchini yenye madini ya urani ni maeneo
mawili yaani Wilaya ya Namtumbo na Monyoni ndiyo yaliodhibitishwa kuwa
na kiasi cha kutosha kuweza kuchimbwa kibiashara na si kweli kuwa
uchimbaji umeanza.
Eneo la Namtumbo lipo ndani ya Hifadhi ya Taifa na Serikali
iliwasilisha maombi UNESCO ya kurekebisha mipaka ya eneo la hifadhi ya
Dunia ili kuongeza eneo la mradi, ombi liliridhiwa katika kikao cha
UNESCO cha tarehe 02/Julai,2012 kilichofanyika Saint Petersburg
(Urusi).

Aidha, Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na Kanuni za Madini ya Mionzi
Ayonisha za Mwaka 2010 - the Mining (Radioactive Minerals)
Regulations, 2010 chini ya Sheria ya Madini, 2010 zinatumika katika
kusimamia shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini ya urani
nchini. Sheria na Kanuni zote zilizotungwa na zitakazoendelea kutungwa
zinazohusiana na usimamizi wa madini ya urani pamoja na mambo mengine
zinalenga kuzingatia miongozo/taratibu za Shirika la Kimataifa la
Nguvu za Atomiki (IAEA) za usimamizi wa madini hayo zinazohakikisha
kuwa uchimbaji hauleti athari kwa binadamu na mazingira.

Tunaendelea kuwashauri waandishi wa habari kuwa sisi kama wizara na
chombo cha Serikali tunawajibu wa kuelimisha umma juu shughuli
mbalimbali za wizara hivyo tunawashauri kuwa tushirikiane kwa maslahi
ya taifa badala ya kutoa habari zenye malengo binafsi.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Nishati na Madini

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment