Friday, 2 January 2015

[wanabidii] MWINYI ALIVYOANDIKA BARUA KWA NYERERE YA KUJIUZULU UWAZIRI

Wakati Taifa likipita katika kipindi kigumu cha kupima uadilifu wa viongozi, safu hii imefanikiwa kupata barua ya kujiuzulu ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali Hassan Mwinyi, ikithibitisha jinsi kiongozi huyo alivyo juu kwa viwango vya utiifu na uadilifu.

Katika barua hiyo, inaonyesha jinsi Mwinyi alivyojiuzulu kwa unyenyekevu Januari 22, 1977 wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Ndani.Kiongozi huyo ambaye mwaka 1985 alikuja kupanda ngazi kuwa Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika barua aliyomwandikia rais wake, Mwalimu Julius Nyerere, anaeleza jinsi binafsi alivyoguswa na mauaji ya watu wanalioshukiwa kuwa wachawi katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza mwaka 1975.

Kwa maneno yake Mwinyi alisema: "Kisiasa nakiri kuwa nahusika, siwezi kukwepa kwa sababu dhamana yangu ya uwaziri inaambatana na wajibu unaonitaka nijue yanayotendeka wizarani na pia niweze kudhibiti na kuhakikisha mwenendo mwema wa Jeshi la Polisi Tanzania."

Mwinyi alijikuta katika matatizo hayo baada ya Jeshi la Polisi Tanzania kuendesha operesheni ya kusaka wauaji wa wachawi katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga na alikiri kwa kusema:

"…vyombo vinavyohusika na utekelezaji, polisi ikiwemo, vilivuka mipaka ya wajibu wao na vikajipa madaraka ya kuogelea katika vitendo viovu vya kishenzi, kinyama na kikatili hata baadhi ya watu waliokamatwa kwa kushukiwa tu kwamba wanahusika wakafa na wengine wakapata vilema vya kudumu."

Ingawa Mwinyi aliweka bayana kwa bosi wake Mwalimu Nyerere kwamba kijinai asingehusika kwani hakushiriki wala kushauri, kuagiza wala kuelekeza mambo hayo yafanywe hivyo, aliandika barua isiyo na kinyongo kabisa na yenye unyenyekevu mkubwa kwa Rais Nyerere.

Kwa unyeyekevu mkubwa, Mwinyi alisema: "Kwa hiyo, Mwalimu, nakuomba mambo matatu. Kwanza naomba radhi mimi nafsi yangu na pia naomba radhi kwa niaba ya askari wote walio wema. Pili, naomba vilevile uelewe sehemu yangu katika kosa hili. Tatu, kwa fedheha hii, naomba unikubalie kujiuzulu."

Barua hiyo ya Mwinyi ya kujiuzulu inaweka mizania mpya kabisa ya uadilifu katika uwajibikaji wa viongozi wa umma wanapoingia matatani na kutakiwa kujiuzulu.

Mzee Mwinyi kwa maudhui ya barua yake ya mwaka 1977 halikuwa jambo la ajabu kuja kuwa Rais wa Tanzania miaka minane baadaye, huku akionekana kama kiongozi aliyeshinda vishawishi na kila aina ya hila kwenye uongozi wake.

Miongoni mwa viongozi wakuu waliowahi kujiuzulu katika miaka ya hivi karibuni ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, Edward Lowassa, pamoja na mawaziri wawili waliopata kusimamia Wizara ya Nishati na Madini kwa nyakati tofauti za utawala wa awamu hiyo, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.

Wengine ni waliokuwa Mawaziri wa Mali Asili na Utalii, Khamisi Kagasheki na Ezekiel Maige, Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi wa JKT, Shamsi Vuai Nahodha.

Viongozi hao, ingawa barua zao za kujiuzulu kwa Rais Jakaya Kikwete hazijapata kuwekwa hadharani, lakini kwa kauli na maelezo yao bungeni wakati wanatangaza kujiuzulu walionyesha kuwa walionewa tu kufikishwa katika hatua hiyo.

Kwa mfano, Lowassa alisema wazi "ameonewa na kudhalilishwa sana" kuhusu suala la mkataba tata wa kuzalisha umeme wa dharura ambao ulitolewa kwa kampuni feki ya Richmond.Tangu kujiuzulu kwa Lowassa na wenzake, umezuka mpasuko mkubwa miongoni mwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), vita ikipiganwa kuonyesha kwamba kujiuzulu kwa viongozi hao ulikuwa ni uonevu.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment