Saturday 28 June 2014

[wanabidii] UJANA, UNABII NA UJASIRIAMALI

UTANGULIZI


Ujana maji ya moto, huchemka na kupoa; na Ujana ni moshi, ukienda haurudi: hii ni misemo inayotumika kuelezea umuhimu wa ujana. Ni kipindi cha mpito katika maisha ya mwanadamu. Sio kwamba vipindi vingine si vya mpito; la hasha! Hata utoto ni kipindi cha mpito na ndio maana mtoto anakua na baadae kuwa kijana na mwisho wake anazeeka. Lakini kipindi cha ujana kina ladha yake, asikwambie mtu. Kama unabishi, kaa na wazee; watakusimulia mambo waliyofanya wakati wa ujana wao enzi hizo!!


Vijana wanatakiwa katika kila sekta. Hata serikali inategemea sana nguvu za vijana; Kanisa halikadhalika. Tatizo tunalokumbana nalo ni taswira ya kijana tumtakaye hasa kijana Mkatoliki. Kujenga taswira ni rahisi lakini kupata uhalisia wa taswira hiyo ni kazi ngumu hasa katika nyakati hizi zenye changamoto kama za udini, uchumi dhaifu, ukabila, tamaa, ubinafsi n.k.


Biblia imeweka mkazo sana kwa vijana. Kijana Katika Biblia Takatatifu amejengewa picha mbali mbali kama ifuatavyo;

1.      Ujana ni wakati muafaka wa kumtumikia Mungu (Muhubiri 12;1). Bwana wetu Yesu Kristu alimtumikia Mungu Baba yake wakati wa ujana. Amepaa mbinguni akiwa na miaka 33 baada ya kuikamilisha kwa asilimia miamoja kazi aliyotumwa hapa duniani. Ni mfano mzuri wa kuigwa kwetu vijana katika mwaka huu wa imani.

2.      Vijana wananguvu ya kumshinda shetani (1Yohane2:3(c); 4(c)) Kijana anawindwa na shetani ili kumtumikisha. Lakini Mungu kamwekea kijana baraka tele na ulinzi ili amshinde shetani.

Pamoja na hayo, kijana ni windo la thamani kwa shetani. Muda wote shetani anamtafuta kijana ili amtumikishe. Matamanio ni mengi wakati wa ujana. Karibia kila sehemu, kilio kikubwa ni mmomonyoko wa maadili kwa vijana. Dunia na Kanisa kwa ujumla linagugumia maumivu yatokanayo na mmomonyoko wa maadili hasa kwa vijana. Matukio ya kusikitisha kama mauaji, ujangili, madawa ya kulevya, uvaaji mbaya, utoaji mimba n.k ni mambo ambayo yanaongezeka kila kukicha. Swali ni "Je, vijana hatuyatambui haya?" "Je, hatujui athari zake?" au hakuna mifano ya kutosha kuweza kututia hofu nasi tusiingie?"


Ki ukweli maswali ni mengi kuliko majibu. Je, vijana tumefananishwa na mfano wa Yesu alioutoa kuwa tunaimbiwa hatuchezi, tunaombolezewa hatulii? (Mathayo 11:16-18; Luka 7:31-32).  Hali sio mbaya kiasi hicho lakini hairidhishi pia. Vijana tunataka maono; Unabii, ushuhuda. Vijana tunataka kugusa ndio tuamini.


KWANINI VIJANA HATUNA MSUKUMO NA MAMBO YA KANISA HUKU TUKISHABIKIA MAMBO YA DUNIA?


Kwa utafiti mdogo nilioufanya baada ya kupata mada hii, nimebaini kuwa vijana wanakatishwa tamaa na mambo kadha wa kadha yakiwemo yafuatayo;

i.                    Kukosa nafasi za uongozi; Mara nyingi nafasi za uongozi katika Kanisa zinashikiliwa na wazee ambao mara nyingi ni walalamishi juu ya maisha na miendeno ya vijana na wakati mwingine kuhamishia shutuma hizo katika familia. Vijana niliofanya nao mahojiano wanaonesha kukerwa na shutuma kwani wanaona kuwa wazee hawatambui mabadiliko ya wakati. Si kila kitu cha kisasa ni utovu wa maadili.

ii.                  Mahubiri kutolenga mahitaji ya vijana. Kila rika lina mahitaji yake; mahubiri ya wazee ni tofauti na ya vijana na ni tofauti na ya watoto. Hivyo kama ibada za Misa zingetenganishwa zingeweza kuwa na mvuto kwa vijana.

iii.                Ukosefu wa viongozi na walezi wa vijana. Vijana tunakosa viongozi na walezi wa kutuongoza katika shughuli na harakati za kimaadili. Mara nyingi hata wale walio onesha nia ya kuwa walezi hawana muda na sisi.  Watatoa misaada ya jezi, T-shirts na pesa za makongamano lakini hawatashiriki  katika shughuli za vijana.

iv.                Kuongezeka kwa tuhuma za utovu wa nidhamu kwa viongozi na watumishi wa Kanisa. Hali hii inawatatanisha sana vijana ambao hawajakomaa katika imani na kuamua kuachana na masuala ya Kanisa. Kiteolojia sio sababu ya msingi mtu kuacha imani yake kwa hisia za dhambi za mtu mwingine lakini ndio hali halisi ya maisha ya sasa.

Vijana tuna maamuzi ya haraka na wakati mwingine hatutafakari kwa kina ili kupambanua mambo; kwani kwetu "Ujanja ni kupata kuwahi hata jogoo huamka mapema!" Ni katika harakati hizi manabii wa kisasa wametukamata.


JE, VIJANA TUNATAMBUA UNABII?


Biblia inafafanua unabii kuwa umekuja ili mwanadamu anene na kutenda ya Mungu akiongozwa na Roho Mtakatifu na sio mambo yake mwenyewe (2 Petro 1:21). Biblia imetupa ahadi tele juu ya manufaa ya kutegemea maagizo ya Mungu. Imetupa maagizo ya namna ya kuishi kwa kumpendeza Mungu na mwanadamu. Kitabu cha Kumbukumbu la Torati sura ya 28, tunapewa ahadi za kuishi maagizo ya Mungu pamoja na laana zitokanazo na kukiuka maagizo hayo.


Kwa aina ya unabii wa sasa ni tishio kwa imani yetu sisi vijana. Kama isemavyo Biblia takatifu, unabii upo ili kunena ya Mungu kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu. Hivyo basi, lazima nabii aoneshe kuwa anaongozwa na Roho huyo kwa matendo na matunda ya kazi yake. Matunda ya Roho Mtakatifu twayajua; Upendo, Kiasi, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhiri, uaminifu  na upole.

Unataka kujua kipimo kitakachokusaidia kujua kama mtumishi au mkristo fulani ana Roho Mtakatifu au hapana? Hatupimi uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu kwa kuangalia aina ya miujiza anayofanya… hatupimi uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu kwa kiwango cha maombi yaliyojibiwa pale alipoomba… Hatupimi uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu kwa vile ananena kwa lugha… anaweza kuwa amebakiza "tone" kwa nje na Roho alishazimishwa na kuondoka! Tunaupima uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu kwa uhalisi na uwazi wa tunda la roho maishani mwake… Kama hana upendo wa ki-Mungu; kiasi cha kusitiri wingi wa dhambi, kama hana furaha; bila kujali mambo yako safi au la, kama hana amani ya ki-Mungu isiyoondolewa na changamoto za maisha; kama hana uvumilivu na hawezi kuwabeba wengine na kuwastahi japo kweli wanamuudhi au kumuumiza, kama hana utu wema maisha yake yamejaa matendo mema kwa watu wote na hasa jamii ya waaminio; kama hana fadhili: hawezi kuwafadhili wengine walio katika ugumu au maeneo ambako mkono wake unaweza kufika, kama hana uaminifu kwenye mambo ya Mungu na ya wanadamu, kama hana upole; amejaa ukali, hasira, jazba na gadhabu, kama hana kiasi [uwezo wa kujizuia]; hana mipaka, hawezi kuudhibiti mwili wake, ulimi wake na hana nidhamu ya maisha. Mtu ambaye haya matunda 9 ya Roho Mtakatifu hayaonekani kwake, huo ni ushahidi wa nje kuonesha kuwa ndani hakuna 'mti- Roho Mtakatifu' uzaao hayo matunda yapasayo kuonekana nje na kuonesha aina ya mti-Roho Mtakatifu ulio ndani!


Hivyo ili kutambua unabii wa kweli hatupaswi kuwa mbali na matunda haya. Japokuwa watanena kwa lugha wanazojua wao, watatamka Neno la Mungu kwa sauti kubwa na mbwembwe, wataangusha watu kwa nguvu wazijuazo, watahubiri barabarani na vichochoroni, nabii lazima aoneshe matunda ya Roho Mtakatifu. Nabii lazima atimize matakwa ya Mungu na kwa Kanisa lake.


Hitaji la kwanza kwa Kanisa la Mungu ni kuwa na ukweli, kwani Mungu ni ukweli na neno lake ni ukweli (Yohana 17:17). Roho Mtakatifu ni Roho wa ukweli (Yohana 14:17; 15:26). Roho Mtakatifu anatuongoza katika ukweli na ukweli unatuweka huru. Roho Mtakatifu anafanya kazi miongoni mwa uongozi ambao ndio waelekezi wa maajabu ya Mungu katika ukweli. Kwa hivyo Roho Mtakatifu ni ukweli na anaendeleza mpango wa Mungu kupitia kanisa lake. Yatupasa sisi vijana tutafute nabii wa ukweli katika Kanisa la ukweli.


Hitaji la pili ni Upendo; nabii hahubiri chuki, mafarakano, utengano na uhasama. Katika ujumbe wake kwa Korintho, Paulo anatuambia kwamba upendo haupotoki. Amri zote za Mungu zimeainishwa kwa imani kama ilivyoandikwa kwenye Amri mbili kuu za Mungu. Hizi nguzo mbili za sheria ambazo ni upendo wa Mungu na upendo wa mwanadamu mwenzetu.


UNABII WA KIZAZI CHA LEO


Kumeibuka wimbi kubwa la unabii. Kila kukicha anafunuliwa nabii mpya, mchungaji mpya, muhubiri mpya, mtume mpya na watumishi wa Mungu ndio hawahesabiki. Dini sasa ni ufunuo, ahadi, na utajiri. Wapo wanaotumia Neno la Mungu, na kujenga makanisa, mahekalu n.k. Tunahitaji kuwajua manabii hawa.

Unabii na manabii wa uongo wanapingana na nguvu za Mungu. Manabii wa uongo wanajitafutia umaarufu ilihali mtumishi wa Mungu anapaswa kuwa mtumishi wa wote katika mwili wa Kristo. Wanapenda kutambulika kwa majina yao. Utasikia mimi nasali kwa nabii fulani, nimepata uponyaji baada ya mtume fulani kuniombea. Mungu ametenda kupitika mtumishi wake.


Lakini kwa kasi ya ajabu, shetani kaja kututafuta mitaani. Kila upitapo hasa jiji la Dar es salaam utasalimiwa na mabango kadhaa ya waganga na watabiri. Hawa wana yao. Wao wanatibu mambo mengi. Mbali na kuongeza nguvu za kiume na kuongeza hamu ya tendo la ndoa, siku hizi wanatibu akili darasani, kutafuta kazi, kupata mpenzi, kujiunga na free mason, pete za majini, utajiri wa haraka na wanauza jini pesa. Hawa ndio manabii wa kisasa kutoka Nigeria, Sumbawanga, Kigoma na Shinyanga. Ukijiunga nao utatembelea Gambushi. Unabii huu hauna matunda ya Roho Mtakatifu. Wanaweza kuwa na matendo yanayompendeza Mungu lakini wamejaa chuki, ubinafsi, uchoyo, vurugu na hawana subira. Ni matendo haya ambayo tunaiga na kurithishana. Inashangaza kuona hata serikali yetu inaingia katika mkumbo huu wa "Big Results Now" Matokeo Makubwa Sasa, kiashiria kikubwa cha ukosefu wa weledi na subira.

Je, ni wangapi wanatembelea kwenye nyumba hizi? Je, Imani halisi ya Kikatoliki imekomea wapi? Sababu inayowasukuma watu kwenye nyumba hizi; vijana kwa wazee ni kukosa majibu ya matatizo yao ya muda mrefu. Nani asiyejua kuwa kwa sasa ili upate kazi lazima alama za masomo darasani ziwe za juu, ili kufundisha chuo lazima uwe na GPA kubwa? Ukisoma hata kama una degree tatu kupata kazi ni shida? Kijana gani anathaminika mtaani kama hana maisha mazuri; gari, nyumba, simu nzuri, anavaa na kupendeza n.k?. Mambo haya humfanya kijana kupoteza mwelekeo wa liturujia na hata ibada mara nyingi huwa ni wakati wa uhitaji na shida kama uhitaji wa kazi, mchumba au magumu mbalimbali.


Haya ni mambo ambayo pamoja na kuihubiri imani yetu, ni lazima kama Kanisa lije na mbinu mbadala ya kutatua matatizo haya. Ili kumkomboa kijana sio lazima kumpa pesa, anahitaji elimu mahususi ya kujitambua (Soft skills). Hili walijaribu kulifanya CPT mwaka jana na bado wanaendelea nalo. Ni changamoto hizi ambazo zinahitaji uinjilishaji mpya; kuzijibu changamoto hizi sio kwa maneno tu bali kwa vitendo. Hii ni kwasababu ya imani tuliyonayo kwa muda wote wa uwepo wa Kanisa lazima ijikite katika maendeleo ya mwanadamu. Muda wote mafundisho ya Kanisa lazima yasimamie misingi imara ya kimaendeleo yaliyo na mizizi katika uchungaji na unabii unaotenda ya Mungu.


Hata uwepo wetu hapa tukijadili hatima ya imani yetu ni ushahidi tosha kuwa kuna kitu hakiendi sawa. Lazima tukubaliane na ukweli huo kuwa kuna haja ya kupanua wigo na kuangalia fursa na makandokando ya imani yetu huku tukitafakari kwa kina njia sahihi kwa ajiri ya kuzijibu changamoto mbalimbali za wakati huu.


UJASIRIAMALI


Mara kwa mara vijana tumekuwa tukihaha kujikwamua kimaisha. Vijana tumekuwa tukisaka fursa mbali mbali ambazo zinaweza kutusaidia kutoka hapa tulipo na kusonga mbele ili kufikia malengo yetu. Swali linaloumiza vichwa ni uhalali wa njia hizi. Linapokuja suala la "UJASIRIAMALI" kila mtu anatafsiri yake. Japokuwa chama cha wanataaluma wa Kanisa (CPT) muda wote wamesisitiza taaluma halali, lakini wimbi la UJASIRIAMALI unaotakatisha pesa haramu limeshika kasi. Udanganyifu katika mizani ya kupimia, usafirishaji wa dawa za kulevya, unyang'anyi kwa kutumia siraha, biashara ya viungo vya binadamu, ujangiri, n,k ni vitendo ambayo vinakemewa moja kwa moja na jamii lakini vijana wamezama huko na hawana mpango wa kutoka.


Tatazo tunalokumbana nalo kama vijana ni kudhani kuwa elimu ni kila kitu. Kweli elimu ni ufunguo wa maisha lakini sio suluhisho la maisha. Tunahitaji malezi mahususi (Transformation). Malezi ni ya msingi kutolewa kabla ya kujenga taaluma ili kijana aweze kujitambua kuwa anaweza taaluma gani badala ya kuvamia taaluma. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kunatofauti kubwa kati ya tabia ya mtu, uwezo binafsi, na taaluma azipatazo katika mfumo wa elimu.


Zipo fursa kadhaa ambazo hazikemewi na jamii lakini sio salama kwa vijana. Fursa hizi ni zile ambazo zinatambulika kwa lugha ya mitaani kama "JOTO HASIRA" ambazo zinawazalisha akina "Yahaya" wengi tu mitaani. Vijana tunatumiwa kama chambo cha kuvulia maslahi ya wakubwa. Matumizi ya vijana katika siasa, maandamano, kujichukulia sheria mikononi kwa kigezo cha kuchoshwa na mfumo ni baadhi tu ya viashiria vya uvunjifu wa amani huku tukipoteza vijana wenzetu katika harakati za kutimiza ndoto zao.


Sio kweli kwamba vijana hatutambui athari za kujiingiza katika harakati hizi, lakini unakuta hatuna mbadala wa maisha. Vituo vya Kanisa maalumu kwa ajili ya kuendeleza vijana kwa stadi mbalimbali kama Home-craft, useremala, ufumaji n.k vimekua kwa vijana ambao hawakupata fursa ya kuendelea na elimu ya juu na sio wahitimu wa vyuo. Pia vituo hivi vinakumbwa na changamoto mbalimbali kama ukosefu wa vifaa vya kisasa kuendana na teknolojia ya sasa, uhaba au ukosefu wa wakufunzi waliobobea na wanaoendana na mabadiriko ya sasa pamoja na ada ambayo inakua kikwazo kwa vijana wanaotaka kujiendeleza. Hata mafunzo yatolewayo katika vituo hivi pamoja na fani zake ni zile ambazo kwa kiasi fulani tayari zina ushindani au zimepoteza nafasi katika jamii. Mara nyingi vituo hivi hutoa kozi za ufumaji, ushonaji, upishi na uselemara; kozi ambazo zimevamiwa na masoko ya China na bidhaa bora za viwandani. Kanisa linapaswa kufanya badiriko na kuwekeza katika kozi kama biashara, viwanda vya nguo kama vitenge, uzalishaji wa vyakula kwa kiwango cha ushindani kama viwanda vya Baharesa na Azania, ufugaji n,k huku wakitumia tekinolojia ya kisasa.


Ukosefu wa nafasi za ajira katika taasisi za Kanisa kama shule, hospitali, benki n.k unatukatisha tamaa vijana na kuona kama Kanisa halitusaidii. Muda mwingi Kanisa limetaka kututumia vijana katika shughuli za kujitolea bila kutambua changamoto tunazokumbana nazo za kimaisha. Yalipasa Kanisa la sasa lirejee katika waraka wa Mwenyeheri Baba Mtakatifu John Paul II wa mwaka 1987 juu ya Sollicitudo Rei Socialis (The Social Concern of the Church).


Pia Kanisa liwekeze katika nyanja za kiuchumi ambazo zinaweza kuwa fursa za ajira kwa vijana wanaohitimu katika vyuo na elimu kwa ngazi tofauti. Kanisa kwa muda mrefu limewekeza katika sekta za elimu na afya tu. Lakini ni vyema kuwekeza katika viwanda vya Uzalishaji kama wa vyakula, kwa kiwango kikubwa tofauti na cha sasa kinachosimamiwa na watawa kwa ajili ya matumizi ya parokiani tu. Fursa nyingine ni katika taasisi kama benki, biashara, ujenzi, n.k kuanzia ngazi ya jimbo ili kuweza kumeza nguvu kazi ya vijana. Kuna haja ya kufanya marekebisho makubwa katika taasisi za kanisa hasa za kiparokia na kuzifanya za kiushindani kwa kuweka taasisi kama utawala, uhasibu, masoko, miradi na uwekezaji n.k ili kuongeza uzalishaji na kuweza hata kupanua wigo wa ajira lakini wenye tija.


Malipo duni yatolewayo katika taasisi za kanisa yamewakatisha tamaa vijana kukimbilia ajira katika taasisi hizi. Ni bora Kanisa likatambua ugumu wa maisha na kurekebisha malipo yao. Kwa hali ya sasa ya mfumuko wa bei maisha ni magumu mno. Chumba cha kupanga ni kati ya Tsh 30,000 hadi 70,000 kwa mwezi na unatakiwa kulipa kwa miezi sita hadi mwaka, nauli ni kati ya 400 hadi 600 kwa kituo, maji ni kati ya 100 hadi 500 kwa ndoo, na Chakula ni kati ya 1000 kwa kilo ya sembe hadi 2500 kwa maharage. Mishahara ya Kanisa ni kati ya 80,000 na 300,000 kwa mwezi. Maboresho ya mishahara katika Kanisa yatasaidia vijana kutojiingiza katika ajira ambazo zitawashawishi kushiriki matendo kama rushwa, na ukosefu wa uaminifu na pia kutoa mbadala wa ajira kwa serikali.


Ukosefu wa mtaji nalo limekuwa ni tatizo kwa vijana. Mara nyingi tumekuwa na shauku ya kujiajiri lakini tunakosa mitaji. Masharti ya mikopo ni magumu. Taasisi za fedha kama Mkombozi hazina dirisha maalum kwa ajili ya vijana wakatoliki. Tunatambua na kuthamini jitihada za baadhi ya parokia kuanzisha SACCOSS lakini vijana hatujafaidika kwa sababu ya kukosa mwongozo wa nini tufanye na elimu mahususi ya ujariamali. Ni parokia chache  kama za Luhanga ambazo kwa kipindi furani wameendesha mafunzo bure ya utengenezaji wa batiki kwa watoto wa kike. Je, katika hali kama hii, tutashindwaje kwenda kwenye makanisa yanayohaidi pesa?


HITIMISHO

Ni dhahiri kuwa Kanisa lipo makini sana na vijana. Tunatambua na kuthamini jitihada mbali mbali ambazo viongozi wa Kanisa kila mara wamezionesha ili kumjenga kijana katika misingi ya imani. Jambo la kutafakari kwa pamoja ni je, jamii gani tunataka kujenga, tuna vijana wa aina gani, wenye maono ya aina gani? na kwa sisi vijana tujiulize, je, tunataka kuwa watu wa aina gani? Tukipata majibu ya maswali haya kwa pamoja tunaweza kuanza kuwaza mambo mengi yanayoweza kutusaidia kufika tutakapo. IMANI KWA VIJANA NI PAMOJA NA KUPATA MAJIBU YA MSTAKABALI WA MAISHA YAO.


ASANTENI SANA NA MUNGU AIMARISHE IMANI YETU

MATHIAS KABYEMERA-CPT JIMBO KUU LA DAR ES SALAAM NA MRATIBU TMCS TAIFA 


--

Yona Fares Maro

Institut d'études de sécurité - SA


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment