Thursday 6 September 2012

[wanabidii] Mjengwablog Inachangisha Pole Ya Kumsaidia Mjane Wa Daud Mwangosi Kuendesha Biashara Ndogo...


Ndugu zangu, 


 Daud Mwangosi ambaye pia alikuwa ' Mwanakijiji' mwenzetu hapa  Mjengwablog hatunaye tena.

Nimemfahamu Daud Mwangosi  tangu mwaka 2004 nilipofika Iringa. Tangu wakati huo, amekuwa akiinipa ushirikiano mkubwa kwenye kazi ya kutangaza shughuli za kijamii kwenye  Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi. Ni  kwa kupiga picha za televisheni na kurusha habari kwenda Channel Ten; Iwe ni kwenda naye Ilula au Njombe, Daud Mwangosi  alikuwa tayari kila nilipomwomba aongozane nami kwa shughuli ya kijamii.

Mara nyingi nilimkuta Daud ofisini kwake  ( Picha ya kwanza juu) akichapa kazi na   huku mkewe akimsaidia kazi nyingine. Daud Mwangosi alikuwa mbunifu. Alikuwa ni mwenye kiu ya kujifunza mambo mapya kwenye teknolojia ya habari na mawasiliano.

Najua Daud Mwangosi alikuwa na  malengo ya kuendeleza shughuli zake za ujasiriamali.  Mbali ya mambo mengine, alikuwa na Photocopy machine ya kumwongezea kipato  ambayo iliharibika mwaka jana. Akawa na ndoto ya kuwa na studio ndogo ya kupiga picha za vipande ( Passport Size). Yote ni katika kumwongezea kipato kutunza familia yake.

Leo Daud Mwangosi hayuko nasi. Ameacha familia, mjane  na watoto wanne;  Itika Mwangosi ( Mjane) Nehemia Mwangosi ( 17) Kidato cha Nne Malangali Sekondari, Hetzgovina Mwangosi  (12) Bathsheba Mwangosi (9) na Moria Mwangosi ( 2)
Namini Daud Mwangosi angependa shughuli alizokuwa akizifanya ziendelee na zije kuwasaidia watoto wake pia.

Jana na leo nimewasiliana na mjane wa marehemu Mwangosi ambaye bado yuko Tukuyu. Nikamwambia kuna ' Wanakijiji ' wa Mjengwablog walioguswa na msiba wa Mwangosi na wangependa kutoa pole yao imsaidie katika kupata mwanzo kutoka hapa alipo sasa. Mjane wa Mwangosi amefarijika sana kusikia habari hizo. 

Kwa vile tayari ameahidiwa msaada wa kusomeshewa watoto. Msaada anaouhitaji kwa sasa ni kupata photocopy machine ( Used)  na kodi ya pango la ofisi. Jumla yake kwa yote hayo mawili haitazidi shilingi za Kitanzania milioni mbili na laki mbili. Hivyo msaada anaouomba kwa wenye mapenzi mema ni shilingi 2, 200,000 ( Shilingi milioni mbili na laki mbili). Shughuli hizo zitamsaidia kujikimu.

Kutokana na hali aliyo nayo sasa, Mwenyekiti wenu napendekeza nichukue jukumu la kuratibu michango hiyo.  Shime tushirikiane kufanikisha hili ili tumsitiri mjane wa mwenzetu Daud Mwangosi.
 Napendekeza ifikapo mwisho wa mwezi huu  ( Septemba) tuwe tumefanikisha zoezi hili kwa yeyote aliye nacho, hata kama ni shilingi elfu tano, ni msaada mkubwa.

Mjengwablog bado tuna rekodi nzuri katika kuchangishana kuwasaidia  wenye kuhitaji. Itakumbukwa, huko nyuma,  kwa pamoja, tulifanikisha kukusanya michango ile ya watoto wa Somalia na kuikabidhi UNICEF, Dar es Salaam. Ni zaidi ya shilingi milioni mbili.
Tulifanikisha mchango wa kusaidia ukarabati  wa maktaba ya Kijamii kijijini Mahango, Madibira. Zaidi ya shilingi milioni nne.
Sasa ni zamu ya kumchangia mjane wa mwenzetu Daud Mwangosi. Kinachohitajika ni milioni mbili na laki mbili.
Naam, kutoa ni moyo, usambe ni utajiri.
 Mwenyekiti wenu na familia yangu naanza kwa kuchangia shilingi laki moja.
Na kama kawaida, taarifa za waliochanga na kiasi kilichopatikana kitawekwa kwenye blogu kwa kila mmoja kuona.

Namna ya kuwasilisha michango: Tumia M-Mpesa, Tigo Pesa, Airtel Money au NMB Mobile. Kwa namba 0754 678 252, 0712 95 61 31, 0788 111 765 ( Kwa walio nje mnaweza kutuma kwa Western Union, jina la mpokeaji- Maggid Mjengwa)

Natanguliza Shukrani.

Maggid Mjengwa,
Iringa.

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

0 comments:

Post a Comment