Sunday 2 September 2012

[wanabidii] Majibu ya Samwel Sitta Kuhusu Tuhuma alizozushiwa na Dr Slaa

Nimesikitishwa na kauli za jazba na mwangwi wa kiwewe za Mhe Dr W
Slaa alipokuwa Iringa juzi hadi kuniita mnafiki, mwongo, mtu wa hatari
n.k

Hali hii inatia mashaka juu ya uwezo wa kiongozi huyo wa kisiasa
kuhimili kukosolewa ambayo ni sifa muhimu ya maisha ya mwanasiasa
yeyote hususani anapojinadi kuwa anaweza kuchukua madaraka ya
kuiongoza nchi.

Kauli zisizo na staha alizozitoa Dr Slaa dhidi yangu kama vile sifai
hata uongozi wa kata zinadhihirisha mambo mawili:

Dr Slaa ni dicteta. Hana uvumilivu. Ana hulka ya kujiskia kwamba
mawazo yake hayapingwi.
Ni mzushi asiyeogopa kusema na kupindisha mantiki ya jambo ili tu
kushinda hoja. Iweje mtu aliyenibembeleza nigombee uraisi kupitia
chama chake mwaka juzi leo aseme sifai kuongoza hata kata kwasababu tu
nimetamka ukweli juu ya udhaifu wa chama chake cha siasa?

Niliyoyasema pale Karagwe majuzi katika uchambuzi wangu wa vyama vya
siasa nchini ni kwamba CHADEMA wamekuwa hodari wa kukosoa na
kuishambulia CCM na serikali zake lakini wanasau kuwa ili wawe mbadala
kwa kuiongoza nchi hawana budi kurutubisha safu yao ya uongozi nawe na
watu wakutosha kuweza kushika madaraka ya ngazi mbalimbali za uongozi
wa Taifa. Kuukataa ukweli kwamba safu ya uongozi wa CHADEMA ni
nyembamba ni kujidanganya tu.Kupita mikoani kutangaza kwamba matatizo
yote ya wananchi yanatokana na CCM ni kazi rahisi na ina mvuto wake
kisiasa lakini mwanasiasa makini hana budi kwenda mbele zaidi ya
hapo.
Hana budi kutuambia wapiga kura mipango ya chama chake inayoeleweka na
inayotekelezeka na iliyo makini kukabiliana na changamoto mbalimbali
za maendeleo ya nchi. Ahadi za alinacha za tiba bure, elimu bure bila
kuonyesha vyanzo halisi vya mapato ni porojo tu. Kusema kwamba
raslimali za nchi kama vile gesi asilia, madini, makaa ya mawe, utalii
zinatosha kuondoa umaskini ni nadharia tupu ambayo uhalisia wake hauna
budi kubainishwa kwa mikakati dhahiri na thabiti ya kiutawala
(uendeshaji) inayoweza kuchuma utajiri huo kwa ufanisi, kwa uendelevu
na kwa faida ya wengi1. Kuhusu mwenyekiti Mh Mbowe – MB

Katika hotuba yangu sikukejeli uzoefu wa Mhe Mbowe, wala sijasema Mhe
Mbowe ni mcheza disko. Niliuchambua wasifu wa viongozi wa CHADEMA na
kutamka uzoefu wa Mhe Mbowe katika vitega uchumi vya burudani hii
siyo kudharau bali ni kutamka ukweli tu.Huwezi kuuelezea wasifu wa Mhe
Mbowe bila kuelezea mchango wake mkubwa katika tasnia ya
burudani.Mmoja wa maraisi maarufu wa marekani (USA)alikuwa ni mcheza
sinema Ronald Reagan.Na hapa Tanzania tulikuwa na mzee R. Kawawa
ambaye alianzia katika tasnia ya uigizaji, kwa hiyo Mhe Mbowe au Dr.W.
Slaa anaweza akawa Rais wetu kwa maana ya kupigiwa kura za uchaguzi wa
demokrasia.Kumudu au kutoyamudu madaraka hayo ni suala tofauti.
Tathmini yangu ilihusu safu nzima ya uongozi wa CHADEMA kwa ujumla
wao.Ni safu nyembamba mno.2. Kujiunga na CHADEMA

Kama alivyosema Dr. Slaa Chadema walifanya jitihada ya kunishawishi
niingie CHADEMA 2010 na niwe mgombea wao wa Urais. Jambo hili
nililitafakari na kutafuta ushauri kwa watu wangu wa karibu na
nikabaini kwamba:-

CHADEMA wana migawanyiko yao ya uongozi tena ni ya hatari
kwasababu ni ya kikanda za nchi – yaani nani anatoka wapi.

Kutokana na yaliomo katika ilani yao ya uchaguzi 2010 – 2015
nilibaini mambo ya kiitikadi ambayo siyakubali kama vile sera ya
majimbo. Sera ya majimbo inawezekana katika nchi ambazo ni tajiri na
pia isiyo na tofauti kubwa ya hali ya maisha baina ya kanda mbalimbali
za nchi kama vile Marekani (USA). Kuleta majimbo Tanzania ambako kuna
tofauti kubwa za kimaendeleo baina ya Kaskazini, Mashariki, kati,
Kusini na Magharibi ni kusababisha nchi ichanike vipande vipande.

Huduma bure za elimu kuanzia chekechea hadi chuo kikuu na huduma
bure za afya kwa wote ni ndoto na ni ghilba kwa wananchi. Isitoshe
siamini kwamba kazi ya Serikali yoyote Duniani ni kuwalea Wananchi kwa
umaskini huku ukiwaahidi huduma za bure badala ya kuwaendeleza
wajitume na waongeze kipato ili wamudu gharama za maisha. Kwa hiyo
nisingeweza kuwa mgombea Uraisi ndani ya chama ambacho itikadi zake za
msingi sikubaliani nazo.

Baada ya hapo nisingeweza eti baada ya uchaguzi Mkuu niombe kugombea
Uspika kupitia chama cha CHADEMA.3. Kuhusu CCJ

Kama ilivyo kawaida kwa vyama vya siasa kutafuta wagombea bora, CCJ ni
miongoni mwa vyama vilivyonifuata mimi na baadhi ya wanasiasa wakati
wa maandilizi ya uchaguzi mkuu. jambo hili si la siri wala la ajabu na
Nimelizungumza hili mara nyingi. Isitokee katika mfumo wa vyama vingi
vya siasa mtu kutoka chama kumoja cha siasa na kujiunga na chama
kingine haiwezi kusemwa kuwa ni uhaini. Na kama Ningeridhika na mambo
yao ningejiunga na CCJ mwaka 2010 lakini sikufanya hivyo. Pia ni
uzushi usio na msingi kunihusisha na uanzishaji wa chama hicho.
Waanzilishi wa chama hicho cha siasa wanajulikana na wapo hai, ni haki
ya kikatiba ya kila Mtanzania kuanzisha au kujiunga Binafsi na chama
chochote cha siasa.4. Madai mengine

Eti nilitamka kwamba ningehamia chadema na Wabunge wa CCM 55 ni porojo
za Dr. Slaa kama ulivyo usemi ningeihama CCM siku chache kabla ya
kuvunjwa Bunge la 9.

Inashangaza kwa Dr Slaa kukejeli uendeshaji wa bunge la 9 ambalo ndilo
lililowapa fursa watu kama yeye kujulikana na kujipatia umaarufu.

Haya madai ya mimi nikiwa Spika kukwamisha uchunguzi wa Meremeta na
Richmond ni kutokana na hisia tu za chuki. Taratibu za Kibunge
hazimwezeshi Spika kuwa Dikteta anayeamua nini kijadiliwe na nini
kisijadiliwe. Yote yapo katika kanunu za Bunge. Maamuzi ya Bunge si
lazima yawe ni ya Spika.

Kuhusu ofisi ya Mbunge jimboni Urambo mahasimu wangu ndani ya CCM na
nje yake wameng'ang'ania kwa makusudi maalum kuiita ofisi ile kuwa ni
ya Spika. Michoro yake na gharama zake hata ukijumuisha samani
haifikii tarakimu za ajabu wanazotaja mahasimu wangu kujenga hoja
istoshe ofisi hiyo haina maslahi yeyote binafsi kwangu Aidha viongozi
wengine waliofikia hadhi za juu mathlani ya uwaziri mkuu nao
wamejengewa majimboni ofisi zinazolingana na hiyo

Porojo nyingine binafsi kama vile kumuhusisha mke wangu kumpigia simu
Dr Slaa kumsihi anisaidie kisiasa ni upuuzi wa aina yake
unaodhihirisha umahiri wa Dr.Slaa katika siasa za kiwango cha chini.

5. HITIMISHO

Mimi nikiwa mwanasiasa mzoefu na mkongwe nimetoa ushauri na
nitaendelea kutoa ushauri kwa makundi mbalimbali nchini.Kuniambia
naingilia mambo ya CHADEMA ni kichekesho.Wakiwa wao ni chama cha siasa
kinachoendesha harakati za kuwania kuchukua madaraka ya kuongoza nchi
ambayo mimi ni raia wasitazamie kuwa sisi wapiga kura tutaacha
kuwachambua.Wanalo tatizo kubwa la safu nyembamba mno ya uongozi,
Kulingana na majukumu ya kuendesha nchi.

Kujilinganisha na safu ya uongozi ya Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere
ni mzaha wako wapi akina R.M Kawawa, Pauli Bomani, George Kahama, Amir
Jamal, Solomoni Eliufoo, Tewa Saidi, Tewa Abdallah, Fundikira wa
CHADEMA? Kutembea nchi nzima kuhamasisha chuki dhidi ya serikali
iliopo madarakani ni jambo jepesi lakini Watanzania walio makini
wanahitaji maelezo ya mipango mbadala ya uchumi kuinua hali za maisha
yao na kuiona safu ya uongozi itakayowezesha kwa dhati kubuni na
kusimamia mikakati endelevu ya kuondoa umaskini kujenga uchumi imara
na kuimarisha umoja wa watanzania

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment