Tuesday 7 August 2012

[wanabidii] Msimamo wa Tanzania Kuhusu Mpaka kwenye Ziwa Nyasa

HIVI NDIVYO ALIVYOSEMA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA
KIMATAIFA KWENYE HOTUBA YAKE BUNGENI .


MSIMAMO WA TANZANIA KATIKA MASUALA MBALIMBALI
64. Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukishuhudia mabadiliko mbalimbali ya
kiuchumi, kisiasa na kijamii duniani kote ambayo wakati mwingine
yanahitaji nchi kuonesha msimamo wake kwa baadhi ya masuala hayo. Moja
ya sifa kubwa ambayo Mwasisi wa Taifa hili Hayati Mwalimu Nyerere
aliyotuachia ni kuweka misimamo kwenye misingi tunayoiamini kama
Taifa. Kutokana na hali hiyo, Tanzania kama nchi huru imeweza kuwa na
misimamo yake kuhusiana na masuala hayo kama yanavyoelezewa hapa
chini.

Suala la Mpaka Kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa
65. Mheshimiwa Spika, lipo tatizo la muda mrefu kati yetu na nchi
jirani ya Malawi linalohusiana na mpaka kwenye Ziwa Nyasa. Tatizo
lenyewe ni kwamba Malawi wanadai kuwa Ziwa lote Kaskazini ya Msumbiji
kuelekea Ruvuma na Mbeya ni mali yao kwa mujibu wa Mkataba wa
Heligoland uliowekwa saini tarehe 1 Julai 1890.

66. Mheshimiwa Spika, Tanzania kwa upande wetu tunasema kuwa mpaka wa
kweli kati yetu na Malawi unapita katikati ya Ziwa hivyo kufanya eneo
lote la kaskazini mashariki ya Ziwa kati ya Latitude digree 9° na
digree 11° kuwa mali ya Tanzania kwa mujibu wa Mkataba huo huo wa
Heligoland (Ango-German Agreement) wa mwaka 1890 ambao ulikubali kuwa
kwa vile kuna maeneo ya mpaka ambayo hayana mantiki, pande
zinazohusika zikutane na kurekebisha kwa kuunda "Border Commissions".
Aidha, tunazo ramani ambazo Waingereza wenyewe (ambao wakati huo
walikuwa wakitawala Nyasaland na Tanganyika) walikubaliana kurekebisha
na hivyo kusogeza mpaka katikati kama ulivyo mpaka kati ya Malawi na
Msumbiji.

67. Mheshimiwa Spika, kutokana na tatizo hili, mwaka 2005 Marehemu
Rais Bingu wa Mutharika, alimwandikia Rais wa awamu ya tatu Mheshimiwa
Mkapa akimtaka waunde Kamati ya kuliangalia tatizo hilo na kulipatia
ufumbuzi. Awamu ya Nne ikaendeleza kwa kuunda Kamati ya Mawaziri wa
Mambo ya Nje kuliangalia tatizo na kulitolea mapendekezo. Kama
zilivyokutana mwaka 2010, mwaka 2012 zilikutana tena ili kuendeleza
mazungumzo ya mwaka 2010 na pia kujadili matukio ya kuonekana kwa
ndege ndogo ndogo za utafiti wa mafuta na gesi kwenye Ziwa Nyasa
zikitafiti hadi pwani ya Ziwa hilo upande wa Tanzania.

68. Mheshimiwa Spika, baada ya majadiliano makubwa kati yetu na
Malawi, Serikali yetu iliwataka wenzetu wa Serikali ya Malawi pamoja
na kampuni za utafiti au uchimbaji kusitisha mara moja shughuli zote
za utafiti hadi majadiliano yatakapokamilika. Ni matumaini yetu kuwa
wenzetu wa Malawi wametuelewa. Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa
mgogoro huu mbele ya safari kutatuliwa na Msuluhishi badala ya sisi
wenyewe.

69. Mheshimiwa Spika, sehemu ya pili ya mgogoro bado iko mezani kwa
majadiliano. Kufuatia maelekezo ya Marais wa pande mbili, Mawaziri wa
Mambo ya Nje na wataalamu wetu wa masuala ya mipaka, ulinzi na usalama
tulikutana Dar es Salaam tarehe 27 Julai, 2012 kujadili kwa kina
mgogoro na kuupatia suluhu ya kudumu. Majadiliano yanaendelea vizuri
na tumekubaliana kuwa wakati tukiendelea na mazungumzo, nchi zote
zijiepushe na shughuli zozote kwenye Ziwa Nyasa ambazo zinaweza
kutafsiriwa kuathiri maslahi ya nchi mojawapo. Kwa makubaliano haya,
naomba niwatoe hofu wananchi wa mikoa ya Mbeya na Ruvuma kuhusu hali
ya usalama mpakani mwa nchi yetu na Malawi. Chini ya uongozi wa
Serikali ya CCM, wananchi wa Tanzania daima watakuwa salama dhidi ya
tishio lolote la dhahiri au la kificho la kiusalama. Tumefanya hivyo
tokea uhuru na hatutachelea kufanya vinginevyo wakati wote tukiwa
madarakani. Hili limeelezewa katika Ibara ya Nane, aya ya 191 na 192
ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 - 2015.

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment