Wednesday 8 August 2012

[wanabidii] MAFANIKIO KUELEKEA MWISHO WA MICHANGO MIKUBWA YA SHEREHE

Ndugu zangu,

Disemba 2010, niliandika waraka wa kuhimiza kubadili desturi ya
kuchangisha mamilioni ya fedha kwa ajili ya kufanya sherehe kubwa, nikitoa
mifano hai jinsi michango hii inavyowaumiza baadhi ya wachangaji, na
kuathiri maisha yao. Vile vile nilielezea umuhimu wa wasomi kuwa chachu na
viongozi wa kubadili desturi ambazo zinaleta madhara, ikiwemo ya kuchangia
sherehe kubwa. Ikumbukwe kuwa desturi ikishajengeka, inajijengea uhalali
wake na kuibadili kunahitaji msukumo.

Nafurahi kuwa karibu kila aliyechangia mjadala ule aliuunga mkono, na pia
kwamba kuna ambao walishaanza siku nyingi kuacha kuchanga na kufanya
kampeni hii hata kabla ya waraka wangu (ona kiambatanisho).

Napenda pia kuwafahamisha kuwa, nimefanikiwa kutimiza ahadi yangu, na sasa
nashiriki kuchangia tu sherehe ndani ya familia. Taratibu idadi ya kadi
za michango ninazopata imeshuka na sasa imekaribia 0. Pia kuna watu wengi
wanaonizunguka ambao wameniambia kuwa kadi za michango wanazopata
zimepungua. Kuna watu nafahamu walikuwa wakigawa kadi kwa kila wamjuaye
miaka ya nyuma, lakini sasa wanapooza au kuozesha wanachagua nani wampe
kadi. Pia watu ninaowafahamu wanaopata kadi na kuacha kuzichangia bila
kuona aibu wameongezeka. Kwa hiyo tumepiga hatua. Natamani tungekuwa na
utafiti wa kisayansi kuona hii desturi inavyobadilika.

Nashukuru sana kwamba kuacha kuchangia harusi hakujaniletea matatizo
yeyote ya kuharibu mahusiano na watu wengine. Kuna watu sikuchangia harusi
zao na za wanao na uhusiano wetu umezidi kuimarika. Kwani kutoa kwa ajili
ya kujenga mahusiano lazima iwe kwa kuchangia sherehe tu? La hasha. Kuna
wachache wamekuwa wakinialika kwenye sherehe zao ingawa sijachanga – kwa
sababu ya ukaribu wetu – nami nakwenda kwa sababu ya ukaribu. Na mimi
nikiwa na sherehe nitakualika si kwa sababu umenichangia, ila kwa kuwa
ningependa uwepo kama mtu wa karibu.

Leo napenda kuwashirikisha mawazo yaliyotolewa katika huu mjadala.
Unaposoma na hata unapoongea na watu mtaani, unaona kuwa jamii imelichoka
hili jambo, na ingependa libadilike, ila tu baadhi wanaogopa. Wako
wachache wanapenda liendelee, ama kwa sababu kweli wanaamini ni jambo
zuri, ama kwa sababu linawasaidia wao moja kwa moja. Hawa hatuna la
kufanya mbali na kuwanyima michango wabadilike kidogokidogo.

Kuna ambao wanasema sherehe zinasaidia uchumi. Kwani fedha isipotumika kwa
sherehe si itatumika kufanya kazi nyingine ambazo zitajenga uchumi ambazo
hazifanyiki kwa kuwa fedha zinakwenda kwenye sherehe kubwa? Kiuchumi
tunasema kila kitu kina "opportunity cost". Unachokitumia huku unashidwa
kukitumia kule" Wanaochanga wangetumia fedha hizo kwenye ada, kujenga
nyumba, kukarabati choo kilichoharibika, kuboresha lishe nyumbani, nk.
Hivi navyo vinajenga uchumi.

Naomba kuwasilisha

Na tafadhali sambaza, na tushirikishe uzoefu wako


--
"Give your energy to things that give you energy.",

"Learn enough to begin and then learn as you go."


Dr. Donath R.Olomi
Chief Executive Officer
Institute of Management and Entrepreneurship Development (IMED)
Mwalimu House 7th Floor, Ilala
P.O. Box 35036 Dar es Salaam, Tanzania E-mail: info@imedtz.org, website:
www.imedtz.org
Mobile +255-754-296660

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment