Thursday, 30 October 2014

[wanabidii] Shyrose Banji azua kizaazaa, Wabunge EALA wataka ang’oke.

MVUTANO mkubwa unaoendelea ndani ya Bunge la Afrika Mashariki (EALA) umekwamisha shughuli za Bunge hilo kutokana na baadhi ya wabunge kugomea, wakitaka kwanza Mbunge kutoka Tanzania, Shyrose Bhanji achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kile wanachodai kuwa ni utovu wa nidhamu.

Shyrose, anatuhumiwa kutoa lugha chafu kwa baadhi ya wabunge wenzake na viongozi wakuu wa nchi za Rwanda, Uganda na Kenya, wakati wa ziara ya viongozi wa EALA iliyofanyika Brussels, Ubelgiji wiki mbili zilizopita.

Kutokana na tuhuma hizo, wabunge wenzake wanamshinikiza Spika wa EALA, Margaret Zziwa aruhusu mjadala kuhusu Shyrose, lakini kiongozi huyo hakuwa amekubaliana na suala hilo, hivyo kusababisha miswada ya sheria na taarifa za kamati ambazo zilipangwa kujadiliwa na vikao vya Bunge hilo kuwekwa kando.

Tanzania daima ilishuhudia mwenendo mzima wa kikao cha Bunge hilo juzi, majira ya saa 8:30 mchana (saa za Rwanda), ambako Spika Zziwa alitoa taarifa kwamba, suala la utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wabunge lilikuwa likishughulikiwa na Tume ya Bunge.

"Tulifanya kikao Jumanne iliyopita, Oktoba 21, 2014 na pia Jumatano, Oktoba 22, 2014 suala hilo lilijadiliwa kwa pamoja na mawaziri wa Afrika Mashariki. Kutokana na tuhuma husika kuwa nzito, hatukuweza kupata hitimisho," alisema Zziwa.

Kwa maelezo ya Spika huyo, tume yake ilitarajiwa kukutana tena jana huku akiahidi kwamba, uamuzi ambao ungelifanywa, taarifa zake zingetolewa kwa wabunge.

Baada ya maelezo hayo, Zziwa alitoa maelekezo ya kuanza kwa mchakato wa kupitisha muswada wa sheria ya Ushirika ya Afrika Mashariki, lakini kabla ya suala hilo kuingia katika hatua ya kupata maelezo ya kamati husika, ilitolewa hoja ya kutaka shughuli hiyo isitishwe ili kutoa fursa ya kujadiliwa kwa kanuni na miongozo ya Bunge hilo.

Hoja hiyo iliyotolewa na Judith Pareno, iliungwa mkono na wabunge wengi, hivyo Spika Zziwa kuelekeza kwamba kuanzia jana mjadala kuhusu kanuni ungepewa nafasi ya kwanza.

Hata hivyo, baada ya mwongozo huo, ilitolewa hoja nyingine kwamba Bunge liahirishwe ili kuwapa fursa wabunge muda wa kujiandaa, hoja ambayo pia ilipitishwa hivyo kusababisha kikao hicho kudumu kwa dakika 25 tu.

Baadaye akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge la Rwanda vinakofanyika vikao vya EALA, Pareno alisema lengo la hoja yake ni kuwezesha Bunge hilo kuendeshwa kwa kuzingatia utawala bora.

Watanzania wakutana

Kuahirishwa kwa kikao cha Jumanne kabla ya muda uliotarajiwa, kulitoa fursa kwa wabunge wa Tanzania EALA, kukutana kwa faragha ili kupata ukweli kuhusu suala hilo kutoka kwa Shyrose mwenyewe ambaye pia ni Katibu wa wabunge hao.

Kikao hicho cha dharura kilidumu kwa takribani saa tatu, lakini habari zinasema hakukuwa na muafaka wa pamoja ambao ulifikiwa kuhusu suala hilo, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa misimamo iliyokinzana miongoni mwao.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Shyrose alisema kuwa anashangazwa na tuhuma zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii juu yake na kwamba, alikuwa hajapokea taarifa rasmi kutoka kwa uongozi wa EALA ili aweze kujibu.

"Hata mimi nasikia mengi sana tu lakini hadi sasa sijaletewa wala sijaambiwa chochote, lakini kama ni za kweli wanaonituhumu waziwasilishe kwangu kwa maandishi na mimi nipo tayari kuzijibu," alisema Shyrose.

Mmoja wa wabunge wa Tanzania, Makongoro Nyerere, alisema hawakuweza kuwa na mjadala wenye afya katika kikao chao, kwani ni kweli kwamba hakukuwa na orodha ya tuhuma zinazomkabili Shyrose.

"Sisi tungekuwa na cha kusema kama tungekuwa na hizo tuhuma rasmi na pengine ni vizuri kujua ni nani anamtuhumu, yaani mlalamikaji ni nani tofauti na sasa ambapo tunasikia manung'unuko tu, watu wananung'unika, ukiwauliza nani mlalamikaji hakuna anayejitokeza," alisema Nyerere.

Mwelekeo wa hatma ya Shyrose, ulitarajiwa kufahamika jana jioni baada ya Spika Zziwa kutoa taarifa ya tume, ambayo ilipanga kukutana jana asubuhi.

Mbunge Peter Mathuki kutoka Kenya, alisema mgogoro unaoendelea ndani ya EALA umewagawa wabunge na kwamba, hali ya kutoheshimiana miongoni mwao ni sababu kubwa ya athari zinazojitokeza sasa katika uendeshaji wake.

Vikao vya Bunge la Afrika Mshariki vinavyoendelea jijini Kigali Rwanda, vilianza Oktoba 20 na vinatarajiwa kumalizika leo, huku likiwa limeshindwa kukamilisha kazi hata moja kati ya zote zilizokuwa zimepangwa kwenye orodha yake.

Source: Tanzania Daima

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment