Friday 31 October 2014

[wanabidii] Serikali isikwepe kulipa malimbikizo ya madeni MSD kuokoa maisha ya Watanzania!

Taarifa kwa Vyombo Vya Habari, 30 Octoba 2014

 

Serikali isikwepe kulipa malimbikizo ya madeni MSD kuokoa maisha ya Watanzania!

 

Sikika imesikitishwa na tamko lililotolewa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, kuhusiana na kushindwa kwa vituo vya huduma za afya kununua dawa MSD kutokana na kuongezeka kwa deni. Ni wazi kuwa waziri hajalipa tatizo hili uzito unaotakiwa na kutambua kuwa baadhi ya wagonjwa wanaweza kupoteza maisha kutokana na tatizo hili.

 

Sikika inatambua kuwa, mapato yatokanayo na uchangiaji katika huduma za afya ni moja tu ya vyanzo vinavyotumika katika kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini. Na pia inatambua kuwa chanzo hiki pekee hakiwezi kuziba pengo kubwa la ufinyu wa bajeti ya dawa na vifaa tiba muhimu ambao hauendani na mahitaji halisi. Kwa mfano, makadirio ya mahitaji ya dawa nchini kwa mwaka wa fedha 2014/15 ni shilingi bilioni 500 lakini bajeti iliyopangwa na kupitishwa ni shilingi bilioni 70.5 ambayo inakidhi mahitaji kwa asilimia 14 tu!

 

Sikika inapenda kuikumbusha Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii kuwa, takribani asilimia 75 ya wagonjwa  wanaopata huduma katika hospitali za Manispaa wapo katika kundi la msamaha wa huduma za afya. Kundi hili linahusisha wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, wazee, watu wenye magonjwa sugu, watu wasiojiweza pamoja na watu wenye ulemavu. Hii inamaanisha kuwa Serikali inategemea asilimia 25 tu ya wagonjwa wanaoweza kuchangia huduma  kama chanzo  kikuu cha fedha za dawa zitokanazo na uchangiaji. Serikali inatakiwa kuwajibika katika hili na sio kuwatupia mzigo wananchi wachache.

 

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii atambue kuwa, kuzitaka hospitali kulipa deni la MSD kwa kutumia fedha za uchangiaji badala ya kutumia fedha hizo kununua dawa kutokana na ufinyu wa bajeti, ni chanzo cha kuzifanya hospitali hizo kuendelea  kukopa zaidi na hivyo kuendelea kukuza tatizo badala ya kutafuta suluhu. Tunamkumbusha kwamba hili ni tatizo linalotokana mfululizo wa upangaji wa bajeti finyu kwa makusudi. Baadhi ya hospitali hizi zimekuwa zikitumia fedha za uchangiaji kununua dawa lakini bado zina madeni. Kwa hiyo, agizo la Waziri halitakuwa na tija katika kutatua tatizo hili kwa sasa.

 

Hii sio mara ya kwanza kwa Wizara ya Afya kuzitaka hospitali kupeleka MSD asilimia 50 ya mapato yao uchangiaji. Agizo hili limekuwa likijirudia tangu mwaka 2012 bila ya kuwa na usimamizi katika utekelezaji na ufuatiliaji. Kwa mfano, mwezi Julai 2014, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii aliziagiza hospitali zote kupeleka MSD asilimia 50 ya mapato yao. Kwa kuwa agizo hili limekuwa likishindwa kutatua tatizo la upatikanaji wa dawa, tulitarajia mbinu mbadala kutoka serikalini.

 

Sikika ingependa pia kujua ni jinsi gani hospitali ya Taifa, za rufaa na maalumu ambazo zinachangia asilimia kubwa ya deni (67%) katika kundi la madeni ya vituo vya huduma za afya zitalipa deni hilo, kwani agizo la waziri lililenga hospitali za wilaya na mikoa pekee. Vile vile, tungependa kujua Wizara imeweka mipango gani katika kulipa deni lake ambalo ni zaidi ya asilimia 70 ya deni lote ambalo MSD wanadai. Deni hilo la Wizara linatokana na gharama za kugomboa, kuhifadhi na kusambaza bidhaa za miradi misonge (vertical programs).

 

Mbali na hilo, tamko la Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa Umma la tarehe 27 Oktoba 2014 linaeleza kuwa, Serikali imekuwa ikilipa Deni la MSD kwa awamu. Hata hivyo, Waziri hakuweka wazi kwamba pamoja na kulipa kwa awamu, deni limekuwa likiongezeka kwa sababu serikali inalipa kiwango kidogo na kukopa kiwango kikubwa. Kwa mfano, mwaka 2013 deni lilikuwa kiasi cha Tsh. bilioni 76.4 lakini kufikia Septemba 2014 deni limekuwa na kufikia kiasi cha Tsh. bilioni 102 ingawa serikali ilifanya malipo ya Tsh. bilioni 10 .

 

Sikika ingependa kupata ufafanuzi kutoka kwa Waziri wa Afya na Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Mh. Mwigulu Nchemba ambaye hivi karibuni alinukuliwa na baadhi ya magazeti akisema kuwa kiasi cha fedha zilizotolewa kwa ajili ya dawa katika mwaka 2013/14 ilikuwa Tsh. bilioni 47 lakini ni Tsh. bilioni 7 tu ndizo zilitumika katika kununua dawa. Sikika, pamoja na watanzania wote, ingependa kujua ni wapi  fedha hizi zimepelekwa na ni kwa sababu zipi  hususan katika kipindi hiki cha uhaba wa dawa na vifaa  tiba katika vituo vya huduma za afya.

 

Sikika pia ingependa kutoa ufafanuzi kwa umma kwamba misaada iliyositishwa na wafadhili ni kwenye bajeti ya kuu tu (General Budget support) na si kwenye mfuko wa pamoja wa sekta ya afya (Health Basket Fund). Kwa kipindi cha Julai-Septemba 2014, zaidi ya Tsh bilioni 20 zilitolewa na wafadhili kwa ajili ya kusaidia halmashauri zote nchini ambapo kwa kawaida, theluthi moja ya fedha hizo inapaswa kutumika kwa ajili ya manununzi ya dawa na vifaa tiba muhimu.

 

Sikika inatambua juhudi za serikali kujumuisha sekta ya afya katika mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN), ambao kwa kiasi unaweza kuchangia kupunguza uhaba  sugu wa  dawa na vifaa tiba katika vituo vya huduma za afya vya umma. Hata hivyo, mpango huo utaanza kutekelezwa rasmi mwaka wa fedha 2015/16, hivyo hauwezi kutatua tatizo la sasa la dawa. Waziri atambue kwamba wagonjwa wanateseka na pengine baadhi kufariki kwa sababu ya ukosefu huu wa dawa na vifaa tiba.

 

Mwisho, Sikika inaitaka Wizara ya afya na Ustawi wa Jamii kuchukua hatua za haraka katika kutatua tatizo hili sugu la ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya huduma za afya vya umma. Uhaba wa dawa unawanyima wananchi kupata haki ya huduma bora za afya ambazo huweza kusababisha vifo. Serikali inapaswa kulipa deni la MSD na kuwezesha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa dharura na haraka. Sio haki kwa serikali yoyote kuacha wananchi wake wakiteseka ama kupoteza maisha kutokanana sababu zinazoweza kuzuilika.

Mr. Irenei Kiria,


Executive Director of Sikika,

P. O. Box 12183 Dar es Salaam,

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

0 comments:

Post a Comment