Tuesday, 3 December 2013

[wanabidii] Naliona anguko la Zitto Kabwe!

by Absalom Kibanda

NAOMBA nianze makala yangu hii kwa kuwaomba radhi sana wasomaji wa safu hii, ambao wiki iliyopita niliahidi kuendelea na hoja yangu kuhusu tatizo la ushabiki wa kisiasa, ambalo limekuwa likiliandama taifa hili kwa miaka mingi sasa.


Nimelazimika kuomba radhi kutokana na ukweli kwamba, nimejikuta nikipaswa kuachana na mada hiyo ya ushabiki wa kisiasa, baada ya kuibuka kwa moja ya mambo mazito katika siasa za ushindani na hususan katika medani ya ujenzi wa demokrasia madhubuti ndani ya vyama vya siasa vya upinzani.


Kikubwa kilichosababisha nifikie uamuzi huo, ni tukio kubwa na la kihistoria lililojitokeza wiki hii, ambalo mwanzo wake uko ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho hakuna shaka kwamba, afya yake ya kisiasa ya jana, leo na kesho ina mchango mkubwa katika maendeleo ya kisiasa katika taifa letu.


Tukio hili ambalo baadhi ya watu wanaweza wakaliona kuwa ni dogo na pengine lisilo na maana kubwa, ni lile la uamuzi wa mwanasiasa mchanga na kipenzi cha watu, Zitto Zubeir Kabwe, kuamua kujitoa mhanga na kugombea nafasi ya uenyekiti wa taifa wa CHADEMA.


Niseme bayana kwamba, uamuzi huo wa Zitto, mwanasiasa kijana aliyejizolea umaarufu mkubwa tangu alipoingia katika siasa za kitaifa ndani ya Bunge mwaka 2005, unaonekana waziwazi kuitikisa CHADEMA, na kwa kiwango kikubwa kugusa hisia za viongozi na wanachama wake na wale walio nje ya chama hicho.


Kikubwa kinachoonekana kuzusha maswali vichwani mwa watu wengi, nikiwamo mimi mwenyewe, ni uamuzi wa kijana huyo kuamua kugombea nafasi hiyo pasipo kujali iwapo Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe anayemaliza muda wake atachukua fomu au la.


Ingawa watu wanaofahamu ujasiri wa Zitto katika kuchukua maamuzi mazito tangu akiwa shuleni na baadaye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wanaweza wakawa hawajashtushwa na uamuzi wa kijana huyo, ni wazi kwamba, hatua yake ya safari hii itakuwa imewafanya waanze kujiuliza mara mbili mbili kulikoni!

Katika hili la uenyekiti wa taifa wa CHADEMA, naweza kusema waziwazi kwamba, hata kwangu mimi ambaye mara kadhaa nimepata fursa ya kushiriki katika mawazo na maamuzi kadha wa kadha ya Zitto, nimejikuta nikishtushwa na namna alivyofikia uamuzi huu na kuutekeleza.


Ingawa nilikuwa nikijua japo kwa sehemu ndogo kuwa, Zitto alikuwa akipita katika tanuri gumu la kimaamuzi juu ya ama kugombea uenyekiti wa CHADEMA au kutogombea, bado sikuweza kujiaminisha kwamba, kijana huyu niliyemuunga mkono wakati wote alipokuwa akisimamia baadhi ya mambo makubwa ya kisiasa, angefikia hitimisho la kuwashtua watu wengi kwa uamuzi wake huu.


Watu wanaojua masuala ya CHADEMA ni mashahidi wazuri kwamba, uamuzi huu wa Zitto kuchukua fomu kupambana na Mbowe ambaye yeye mwenyewe (Zitto), mara zote amekuwa akimtambulisha kuwa ni 'mentor' wake wa kisiasa ndani ya chama hicho cha upinzani, tena kwa staili ya kumshtukiza, umesababisha mtafaruku mkubwa wa mawazo.


Ni wazi kwamba, uamuzi huu wa Zitto kuchukua fomu, kwa kiwango kikubwa umekuwa ni wa faraja kubwa kwa wana CCM, ambao siku zote wamekuwa wakitaka kuiona CHADEMA ikisambaratika na kukipa fursa chama hicho tawala kupumua.


Watu tunaolifahamu hilo kwa ndani, tunatambua vyema kwamba, kwa CCM na kwa maofisa usalama wa taifa waliolelewa katika mfumo wa siasa za chama kimoja, kuanguka au kuporomoka kwa uimara wa CHADEMA wa leo hii, ni jambo la kuliwekea mikakati na kwa kiwango kikubwa kulishangilia.


Kwa wana CCM na wapambe wao hao wa 'kiusalama', hatua yoyote ya kuwang'oa kutoka katika madaraka ya CHADEMA au ya kuwadhibiti watu wa aina ya Mbowe, Dk. Willbrod Slaa, John Mnyika na wanasiasa wengine madhubuti wengi tu wa ndani ya chama hicho cha upinzani, ni ya kushangiliwa na kuungwa mkono.


Ni wazi kwamba CHADEMA chini ya uenyekiti wa Mbowe na ukatibu mkuu wa Dk. Slaa, pamoja na kuwapo kwa kasoro zake nyingi za kiutendaji, kiutawala, kimfumo, kisera na pengine hata kiitikadi, imepiga hatua kubwa katika medani ya ushindani wa kisiasa ndani ya nchi hii.


Watu wanaofuatilia historia ya CHADEMA ya siku na miaka ya hivi karibuni, ni mashahidi wazuri kwamba, chama hicho kimeweza kujijengea misingi bora na imara kisiasa, kiasi cha watu wengi kukijengea imani na matumaini makubwa kwamba, kinaweza kikafanya mambo makubwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwakani.


Dalili hizi za CHADEMA kujijengea uhalali ambao umejidhihirisha wakati wa chaguzi mbalimbali ndogo zilizofanyika katika miaka ya hivi karibuni, kama zile za Tunduru, Kiteto, Tarime, Mbeya Vijijini, Busanda na Biharamulo, zimekuwa zikikifanya CCM na majemedari wake wa mikakati kujipanga na kukesha wakikiwinda, usiku na mchana.


Mawindo hayo dhidi ya CHADEMA yamekuwa yakijionyesha waziwazi kupitia katika vyombo vya habari, ambako kila mara taarifa za kupikwa na kufinyangwa dhidi ya chama hicho na viongozi wake, kama akina Mbowe, zimekuwa zikiandikwa mfululizo na kupewa uzito mkubwa.


Kwa ustadi mkubwa wa kufinyanga uongo, mawakala wa CCM wamefanya kila linalowezekana kumchimba Mbowe wakitumia falsafa ya Kibiblia isemayo; 'Mpige mchungaji, kondoo watawanyike' ili kufanikisha malengo yao haya ambayo matokeo yake hayatamgharibu mwenyekiti huyo pekee yake, au chama anachokiongoza, bali mafanikio yote tuliyopata kidemokrasia kama taifa.


Ni kwa sababu hiyo basi, Mbowe amepewa sifa mbaya kila wakati, akihusishwa na ukabila, ufisadi, udikteta, ubinafsi na kila aina ya sifa mbaya, lengo likiwa ni lile lile la kukivuruga chama hicho na kudumaza nguvu ya kiushindani ya vyama vya upinzani.


Mbinu hiyo haramu ya kutumia vyombo vya habari kumchafua Mbowe iliposhindikana, hata wakati ule ikafikia hatua ya kutumia hoja za aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Chacha Wangwe, mawakala hao wa CCM wakaja na mbinu nyingine mbadala.


Mbinu hii haikuwa nyingine bali ile ya kujaribu kuwagombanisha na kuwachonganisha viongozi wa kitaifa wa chama hicho kwa mbinu na staili tofauti.


Wakati fulani mwaka jana, Zitto alipofanya mahojiano na gazeti hili na kuulizwa kuhusu kusambazwa kwa habari za viongozi wa CHADEMA kugombanishwa, alikiri kulifahamu hili.


Wakati huo (Desemba mwaka 2007), vyombo kadhaa vya habari vilianza kuandika habari za kumpamba Zitto, zikimsifu kwa kuwa mwanasiasa kijana machachari na ambaye uwezo wake wa kiuongozi ulikuwa ukikizidi chama hicho na pengine viongozi wengine wa chama hicho.


Taarifa hizi za vyombo vya habari zilinikutanisha na Zitto na tukazijadili naye kwa muda mrefu kabla ya wote wawili kukubaliana kwamba, zilikuwa na lengo la kukihujumu CHADEMA na kuua dhana nzima ya upinzani hapa nchini.


Tulipofikia hatua ya kukubaliana naye, alifanya mahojiano na gazeti hili na akatoa tamko zito ambalo kwa kiwango kikubwa lilisababisha mawakala wa CCM kuachana na ajenda hiyo. Kwa maneno yake mwenyewe wakati huo akirejea taarifa za vyombo mbalimbali vya habari alisema: ''Tumegundua kuwapo kwa juhudi za makusudi za kutaka kutugombanisha CHADEMA. Hiki ni chama makini, kimezibaini njama hizo na kwa hakika hakiwezi kusambaratishwa.


"…CHADEMA ndiyo imenipa umaarufu mimi… mimi si maarufu kuliko chama. CHADEMA ni taasisi, ni chama ambacho kina misingi ya uanzishwaji wake.


"…(Wanasema) eti nilishinda kwa umaarufu wangu binafsi, si kweli. Niligombea ubunge nikitokea shule, sikuwa najulikana. Nilikuta 'grassroots network' ya chama, (chama) hakikujengwa na mimi.


"CHADEMA ilijengwa na uongozi uliokuwepo, nilikuta uongozi 'intact' (imara). Katika kila kijiji kulikuwa na uongozi na hata katika vitongoji vyote. Wakati naingia kugombea ubunge kulikuwa na wanachama wa CHADEMA wenye kadi wanaofikia 10,800 katika jimbo zima. Hawa sikuwatafuta mimi, niliwakuta na ndio waliofanikisha ushindi wangu.


"…Katika mazingira kama haya utasemaje kuwa mimi ni maarufu kuliko chama wakati chama ndicho kimenipa umaarufu?

"…CHADEMA ni chama ambacho wenyeviti wake wastaafu wanaendelea kuenziwa na kuhudhuria vikao vyote vya chama… 'institutional memory' ipo kuliko katika vyama vingine vya upinzani.


"…Alipohama (Dk. Aman Walid) Kabourou, wengi walidhani ndiyo mwisho wa CHADEMA Kigoma, lakini leo hii CHADEMA ni moto Kigoma kuliko ilivyokuwa awali."

Ni jambo la ajabu kwamba, karibu miaka miwili tangu Zitto mwenyewe akiri kutambua kuwapo kwa njama hizo za kumkosanisha na viongozi wenzake na pengine kukihujumu chama chao, anaonekana akiingia katika mtego ambao miaka kadhaa iliyopita ulipata kukinasa chama kingine cha NCCR Mageuzi kiasi cha kukifanya leo hii kushindwa kufurukuta hata kufananishwa na baadhi ya watu kuwa ni sawa na shirika lisilo la kiserikali (NGo).


Ni jambo la kusikitisha sana kwamba, leo inapofikia hatua ya mwanasiasa kijana aliyekuwa akionekana kuwa moja ya mazao ya kuigwa ndani ya kambi ya upinzani tangu kukwama kwa akina James Mbatia, Mabere Marando, Augustine Mrema na wenzao wengine wengi, akifuata mkondo ule ule, basi ni wazi Watanzania wanaweza wakajikuta wakilazimika kukata tamaa zaidi na zaidi.


Ingawa ni kweli kwamba pengine nyuma ya Zitto wako watu wengi ndani ya CHADEMA na nje, waliojitoa mhanga kumuunga mkono katika mapambano haya, mwanasiasa huyo anapaswa kutambua wazi kwamba, uamuzi wake huu wa sasa, unamuandalia anguko ambalo si mimi wala mwingine yeyote atamwepusha nalo.


Ni wazi kwamba katika umri wa miaka 33 aliyonayo Zitto na tena akiwa na akili zinazochemka na afya njema, mwanasiasa huyo mchanga anayo fursa kubwa mbele ya safari ya kuwa mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA na Mungu akipenda kupanda zaidi ya hapo alipo leo.


Anapaswa kujifunza kuwa na subira waliyonayo vijana wengi ndani ya CCM na serikalini, ambao pamoja na kuwa na fursa nyingi za harakaharaka, wameamua kuwa watulivu na wenye subira, wakiwa na uhakika kuwa, wakati wao utafika.


Wakati atakapokuwa akiyatafakari hayo, Zitto anapaswa kuyarejea maneno aliyoyatoa Rais Jakaya Kikwete siku alipoteuliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM pale Dodoma, Mei mwaka 2005, alipokiri yeye mwenyewe kwamba lilikuwa jambo jema kwake kuukosa urais mwaka 1995.


Naliona anguko la kihistoria la Zitto.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment