Monday, 30 December 2013

[wanabidii] Jeshi la Polisi laanza operesheni dhidi ya wanaotumia vibaya mawasiliano simu na internet

Hatimaye, Jeshi la Polisi nchini, limeanzisha operesheni maalumu ya kuwabaini na kisha kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kama vile Twitter, Facebook pamoja na laini za simu.

Jeshi la Polisi limeamaua kuchukua hatua hiyo baada ya kuona teknolojia hizo zinatumiwa vibaya na watumiaji ikiwa ni pamoja na kuhamasisha vitendo vya uvunjifu wa amani ya nchi, kutishia usalama wa maisha ya watu na kutengeneza njama ovu za matukio ya kijambazi. 

Baadhi ya hatua ambazo jeshi hilo limepanga kuwachukulia wote watakaobainika kutumia vibaya mitandao hiyo ni pamoja 
na kuwapeleka mahakamani.

Akizungumza na NIPASHE jana, Mratibu Msaidizi wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Jeshi hilo, Kitengo cha Cyber Crime, Joshua Mwasungasa, alisema operesheni hiyo ni endelevu kwa nchi nzima, lakini kwa sasa wameanza na Jiji la Dar es Salaam kuanzia mwezi huu hadi Aprili, mwakani.

Alisema jeshi hilo linafanya operesheni hiyo kwa ushirikiano na kampuni mbalimbali za simu pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), na kwamba wote watakaobainika kutumia mitandao hiyo kwa matukio yoyote ya kiuhalifu, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kupelekwa mahakamani bila kujali hali au mahali alipo mtuhumiwa.

Kwa mujibu wa Mwasungasa, wanayo idadi ya watuhumiwa wanaotumia vibaya teknolojia hizo za mawasiliano, lakini alisema asingeweza kuiweka wazi ili isivuruge zoezi hilo ambalo wanaendelea nalo kwa sasa na kwamba wameamua kuanzisha operesheni hiyo mapema kwa ajili ya kuzuia athari kubwa ambayo ingeweza kujitokeza hapo baadaye baada ya kuonekana kwa dalili za vitisho vya uvunjifu wa amani kutokana na watu wanaotumia vibaya teknolojia hizo.

"Zoezi hili si la muda mfupi, ni la muda mrefu. Hatuwezi kusubiri mpaka uharibifu utokee ndipo tuanze. Tumeona vyema tuanze sasa kwani kuna 'threats' (vitisho) mbalimbali vinakuja kutokana na matumizi mabaya ya laini za simu na mitandao ya kijamii. Ni lazima tuwe na 'Line Patrol' kabla ya kitu kutokea na kuleta uvunjifu wa amani," alisema na kuongeza:

"Kutumia laini za simu kwa mambo ya kiuchochezi ni kosa kisheria, na Sheria ipo ya EPCO inayosimamia matumizi ya mtandao hiyo. Kama mtu anatumia mtandao wa simu kwa kukashifu mtu ni kosa, na siyo simu tu bali hata mitandao ya kijamii. 

Kutokana na hili, tumeanzisha operesheni maalumu inayoitwa 'Line Patrol' kwenye simu na mitandao ya kijamii na endapo tutakutana na kitu ambacho kinakiuka sheria ya matumizi ya mitandao hiyo, tutamchukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kupelekwa mahakamani mhusika."

Aliongeza kuwa mtu yeyote atakayetuma meseji za uchochezi kwa mwingine kupitia mitandao hiyo ya mawasiliano, atakuwa hatiani na yule atakayepokea na kurusha kwa mwingine bila kuifuta, naye pia atakuwa ameshiriki vitendo hivyo vya uhalifu kwani atakuwa ameingizwa na kuonekana kuwa ni mmiliki wa meseji hizo za kiuhalifu.

Alitaja baadhi ya matumizi mabaya ya mitandao hiyo kuwa ni pamoja na kuzungumza au kuandika ujumbe wa uchochezi, kukashfu, kutengeneza njama za matukio ya uhalifu na kuchochea uvunjifu wa amani.

Aliwaasa Watanzania kuwa makini na matumizi ya teknolojia hizo kwani kwa mujibu wa sheria zinazosimamia matumizi ya mitandao hiyo ya EPCO, mtu yeyote akipokea ujumbe wa uchochezi bila kuufuta na kuurusha kwa mwingine, tayari ameshakuwa mmiliki wa kosa hilo. 

Alisema baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza ya uchunguzi huo katika Jiji la Dar es Salaam ifikapo Aprili, mwakani, watafanya tathmini na kisha kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika, na kisha kuendelea na maeneo mengine.

Aliongeza kuwa katika zoezi hilo, pia wanalenga kutoa elimu kwa Watanzania na watumiaji ambao hawana uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya mitandao hiyo kwani wengi wameingizwa kwenye matukio ya uhalifu kwa sababu ya kutokuwa na elimu hiyo.
Kutolewa kwa taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi, kunafuatia malalamiko mengi kutoka kwa watumiaji wa mitandao nchini kutokana na kukashfiwa, kutishiwa usalama wa maisha yao na kudhalilishwa.

Baadhi ya viongozi ambao kwa siku za hivi karibuni walipewa vitisho kupitia mitandao hiyo ni pamoja wabunge akiwamo Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema; Mbunge wa Viti Maalum, Esther Bulaya; Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai. 

NIPASHE lilizungumza na Cyber Crime baada ya TCRA hivi karibuni kusema kuwa wanaoshughulika na udhibiti wa mitandao ya mawasiliano ikiwamo hiyo ya kijamii, ni Jeshi la Polisi. 


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment