Sunday 1 December 2013

[wanabidii] Maoni, ushauri kwa Wahusika wa 'sintofahamu' ndani ya CHADEMA

Nikiwa kama Mtanzania ambaye kwa sehemu moja au nyingine nawajibika katika utumishi wa jamii, nimeona vema nitoe mawazo yangu kidogo kuhusu kinachoendelea ndani ya  CHADEMA kama taasisi. Mimi sio mwanasiasa kwa maana ya kimajukumu wala kiutendaji lakini ni sehemu ya siasa za nchi yetu kwa cheo changu cha Uraia wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wengi wetu tunafahamu au tumesikia sintofahamu inayoendelea katika CHADEMA kama taasisi. Pamoja na ukweli kuwa huenda sisi ambao tuko nje ya taasisi hii hatujui kwa undani yanayoendelea ndani ya chama hicho, lakini kwa sehemu kubwa wahusika wa taasisi hii wamekua wakitoa habari nyingi tunazokutana nazo kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na kwa jinsi hiyo picha ya kinachoendelea iko wazi kwa sehemu kubwa. 

Kwa mfuatiliaji yeyote wa mambo ya siasa na uongozi katika nchi yetu anaelewa vema uendeshwaji wa taasisi za kisasa katika nchi yetu. Kwa wiki kadhaa sasa nimekua nikifuatilia kwa karibu habari na mijadala iliyokua ikiendelea pamoja na kauli mbalimbali za wanachama, viongozi na wabunge wa chama wa CHADEMA. Kwa mtazamo wangu kuna mambo 
kadhaa yanakanganya na mengine yako wazi kabisa kwa maana ya chanzo cha mgogoro.  Mambo mengi yamekua wazi zaidi hasa baada ya waraka wa kimkakati katika kuleta mabadiliko katika uongozi wa chama hicho kuwekwa hadharani na kufuatiwa na yaliyojiri katika mkutano wa kamati kuu na muendelezo wake. 

Nianze kwa kusema kuwa, migogoro ni afya katika kundi na jamii yoyote ile. Migogoro ni chachu ya fikra chanya na pana katika kuibua tofauti zenye kujenga na kuondoa nadharia ya amani iliyolala katika kundi na taasisi. Migogoro ni afya kubwa kwa sababu inapotokea ndio unakua wakati muafaka wa kutuwezesha kufahamiana kwa undani kuwa sisi ni watu wa aina gani; nini kimehifadhiwa ndani ya mioyo na dhamira zetu; na kwa nini tunafanya na kutenda mambo fulanifulani. Migogoro huondoa wingu linalozuia kutabaniasha taswira halisi ya ndani kati utu wa mwanadamu usio kamili.

Migogoro inakua tatizo tu katika mazingira makubwa matatu:

  1. Moja ni pale tunapouangalia zaidi wasifu wa muhusika katika mgogoro (personality) na kuushambulia utu wake  na hivyo kujikuta tunapambana naye zaidi badala ya chanzo na mgogoro wenyewe. 

  2. Pili ni pale tunapotatua migogoro kwa matukio badala kwa kuangalia chanzo cha mgogoro. Hili limekua tatizo kubwa sana katika nchi yetu. Mara nyingi tunahangaika zaidi na mtukukio na kuacha kujikita katika msingi wa matukio huku tukiwa tumedharau ukweli kuwa huwezi kuelezea utatu na uchachu wa chungwa bila kuhusisha na mti wake pamoja na ulivyotunzwa kabla na wakati wa kubeba machungwa husika. 

  3. Tatu, migogoro inakua tatizo pale ambapo wahusika katika mgogoro wanapokosa hekina na ufahamu sahihi wa kushughulikia migogoro.

Mara nyingi tumekua tukiiona migogoro ndani ya vyama vya siasa hasa vya upinzani ikifanywa kuwa matukio makubwa. Na mara zote migogoro hii imejikita katika kumjadili mtu au kundi la watu zaidi ya hija zilizoibua mgogoro. Taasisi hizi za kisiasa zinajikuta katika mamambano ya utu na kuacha kabisa mambo ya msingi ya kuzisaidia kujijenga na kujiimarisha katika malengo ya msingi wa uanzishwaji wake. Nchi yetu imekua nchi ya kujadili na kuendeshwa na matukio (hasa katika siasa na uongozi) badala ya mambo ya msingi yenye kuleta tija kwa kizazi cha sasa na cha baadaye. Na matukio haya yanakua hayana uzito wa kutosha bila kuwa na mtu au jina la mtu ambalo hufanywa shabaha. Hiki ndicho kinachowakumba CHADEMA mara kwa mara. Katika yote haya mimi ninaona mambo yafuatayo kama  matatizo ya msingi yanayokikabili CDM kama taasisi:

  1. Nakiona chama husika kuwa kwenye wakati mgumu wa kukubali kuiweka nadharia ya demokrasia kwa ujumla wake katika vitendo. Kama taasisi ambayo bado inakua huku ikiwa imebeba majukumu kadhaa ya kiuongozi katika taifa, jambo hili linaweza lisiwe la kushangaza sana lakini inategemewa kuwa baada ya miaka zaidi ya 20 sasa, lazima kuwa na dhamira njema za kuongeza wigo wa kidemokrasia katika taasisi.

  2. Kama ilivyo kwa vyama vingine vya upinzani, wengi walioingia humo kama wanachama wameingia kwa malengo binafsi zaidi na ni wachache ambao wameamua kuwa wanachama wa vyama vya upinzani kwa malengo ya kutafuta njia mbadala ya kisiasa na kiuongozi katika kulisaidia taifa letu. Ni changamoto kuwa na taasisi ambayo wengi wa walioko ndani wana malengo binafsi ya uongozi au kupata fursa ambazo zinapatikana ndani ya chama au nje kupitia chama

  3. Kutokana na hoja 2 za kwanza hapo juu, chama hiki kiko katika wakati mgumu wa kufanya kazi kama taasisi na badala yake imekua kama vile baadhi ya watu ndani ya chama ndio wenye nguvu na majina yao kuwa maarufu kuliko taasisi. Ujasiri huu wa watu hawa ndani ya chama ndio unaokipa chama wakati mgumu kwani kila mmoja anataka kujiimarisha yeye kama taasisi badala ya kukijenga chama kama taasisi.

  4. Tatizo la tatu hapo juu linakifanya chama kiwe na watu wengi walioko busy na mikakati ya kujijenga wao binafsi badala ya kujenga taasisi. Ni kweli kuwa hakuna mtu yeyote asiyekua na mikakati ya kujijenga kama mtu binafsi lakini ni lazima mikakati hii itanguliwe na mitakati ya kitaasisi na kijamii maana hivi vikifanikiwa ni rahisi na mtu binafsi kufanikisha malengo yake. Kinyume chake huwa ni majanga. Ni lazima tuwaze kufananikiwa kama taifa kwanza kabla ya kuwaza kujifanikisha mtu mmoja mmoja ...na hili tatizo ni majanga makubwa katika taifa letu. ..Kila mmoja anaanza na mimi kwanza wengine baadaye iwapo kutakua na kitakachobakia.

  5. Tatizo la kimfumo wa kitaasisi ni kubwa na linaonekana zaidi pale ambapo kwenye chama hicho karibu kila mmoja ni msemaji wa hisia/maamzi/mtizamo na mipango ya chama. Ukienda kwenye mitandao unaona kabisa jinsi ambavyo wanachama wenye ushawishi ndani ya chama hicho huwa wepesi sana kutoa kauli zainazobeba sura ya kitaasisi kama vile wanakisemea chama.

  6. Kuwa na wanachama wengi kwenye chama ambao wamejikita katika kutafuta kujijenga wao binafsi, kumepelekea wanachama hawa (na hata viongozi wao) kutazamana kwa hisia za kutaka kuzibiana. Na matokeo yake taasisi imejikuta ina watu amboa wanawindana, wanaharibiana, wanashindana, wanapambana na hata kuvunjiana heshima latika kutafuta kufanikisha malengo binafsi. 

  7. Hoja ya sita inaweza kuthibitishwa na jinsi ambavyo tangu sintofahamu iliyokikuta chama itokee, unashangazwa na wingi wa wanachama na viongozi wa chama hicho wanaoonesha chuki ya hali ya juu kwa walioshutumiwa kuwa ni wakosaji. Inasumbua kweli kuona jinsi ambavyo kukikosea chama (iwapo kuna kosa) kunabadilika kuwa ni kukosea watu binafsi na hivyo kujenga hoja ya kuonesha chuki na uadui wa hali ya juu na hata kushindwa kuheshimiana.

  8. Taasisi yoyote imara lazima iwe na mpango mkakati wa muda mrefu wa jinsi ya kutatua matatizo yanayojitokeza bila kujali ukubwa au udogo wake. Ni lazima taasisi ijijengee utamaduni wa kutatua migogoro kwa haraka na kuimaliza bila kuiacha kukua na kubadilika majanga kwa taasisi. CDM wana changamoto hii.

Ningepewa nafasi ya kuishauri taasisi hii na viongozi wake pamoja na wale wanaonekana kama maadui na wasaliti wa ndani wa taasisi (kama ni kweli) ningewaambia yafuatayo:

  1. Chama hiki kijiwekee malengo yenye mipango ya kutekelezeka katika kukijenga kama taasisi. Pamoja na mambo mengine, lazima ibuni njia na miundombinu ya kiutawala na kujiendesha ili utaasisi wake uwe dhahiri, wa kweli na wazi kwa jimii

  2. Lazima taasisi hii iwe na mkakati wa kudumu wa namna nzuri ya kupata viongozi wanaoaminishwa siri za chama na uendeshwaji wake. Tatizo la majina na umaarufu kua na nguvu kuliko taasisi ambalo nimelitaja hapo juu, limejitokeza sana CDM hasa pale watu maarufu wanapotoka vyama vingine au huko walipokua na kupewa madara makubwa ambayo ni wazi wanakua hawana mizizi ya kutosha katika kuyasimamia. Mara nyingine wageni hawa wanaokaribishwa moja kwa moja hadi jikoni na chumbani, huwa wanakuja na malengo yao ambayo mara nyingi yanakua sio ya kikimarisha chama

  3. Chama hiki kikubali kuiweka ndaharia ya uongozi wa uwajibikaji katika matendo. Badala ya kutumia nguvu kubwa katika kujibizana, kuzibana midomo na kujibu hoja zinazoonesha manung'uniko, malalamiko na shutuma; vionngozi wake watumie nguvu kubwa kufanya mambo ya vitendo huku wakijitahidi kusikiliza na kufanyia kazi malalamiko ya wale wanaowangoza.

  4. Ni vema kama taasisi ikubali kujitathmini katika kuukubali ukweli hata kama unauma na haupendezi kwa baadhi ya watu au vingozi. Hii ni njia pekee itakayoweza kukifanya kielewe nini jamii inachotaka kuingoza inataka na kutegemea kutoka kwao

  5. Kuna msemo usemao, "usianze kutafuta soko la ngozi ya simba kabla hujamuua kwanza maana mwisho wa siku unaweza kujikuta simba ndio kakuua wewe"....kwa lugha yao husema, "Don't sell a skin before you kill a lion". Taasisi hii isishangilie ushindi au kujiona washindi kabla hawajakabidhiwa ushindi. Ni vema kuwa na subira katika harakati zake katika kuuendea ushindi iwapo uko dhahiri. Subira hii ina mambo mengi ya msingi kujijenga zaidi, kujiimarisha zaidi na kujitawala zaidi. Viongozi wasijenge kiburi cha kukubalika na kujiona wajuaji bila kutaka kujua nini watu wanategema kwao.

  6. Wanachama na viongozi wa taasisi husika waache kuwapa uzito wanachama au viongozi fulani kuliko chama na badala yake kuwa na usawa wa kuheshimiana katika ujenzi wa taasisi. Ni hatari sana kumwangalia mtu mmoja au kikundi cha watu wachache kama msingi wa ukuaji na kusimama kwa taasisi kwani hakuna mwanadamu mwenye mkataba na Mungu wa kuishi hadi jioni au kesho asubuhi. Mojawapo wa mikakati wa kulitendea kazi hili ni kuhakikisha dhana ya uongozi ni ya wazi, ya kubadilishana kwa moyo wa amani, na yenye uwajibikaji mkubwa kwa wanaoongozwa

  7. Ni lazima wahusika wote ndani ya chama wajitahidi sana kuchuja kile wanachokiongea kwenye umma...bila kujali ni kwenye vyombo vya habari, mitandao ya kijamii au kwingine popote pale. Hii itawezekana tu pale ambapo wale ambao ama wamejipa au wamepewa umaarufu na ushujaa katika chama watajiona umuhim wao ni sawa na wa wengine...na tofauti ziko tu kwenye utendaji na uwajibikaji tu na sio ubora. Chama kiwe na nidhamu katika kuyaongelea mambo ya chama kwani ni hatari kuwa na nyumba ambayo baba, mama, watoto na hata ndugu na wafanyakazi walio ndani wote ni wa semaji wa familia

  8. Taasisi hii ijitahidi kung'oa mzizi wa uadui, majungu na mashindano ndani ya chama. Badala ya kubomoana, kama kuna anayeonekana ana neema, vipaji na mtazamo wa kujenga taasisi na nchi kuliko wengine, basi huyu apokee msaada wa kila aina katika kumfanya kuwa bora zaidi ili hatimaye aweze kuwa msaada wa kuiinua taasisi na wale wa nje ya taasiso kwa maana ya nchi yetu.

  9. Wanachama wa taasisi hii watenganishe maswala ya kitaasisi na ya kibinafsi. Hakuna mantiki ya mtu kusemekana kakikosea chama au katiba ya chama halafu akageuka ni adui wa kushambuliwa, kutukanwa, kudharauliwa na kutothaminiwa. Haifa kuwa na chama ambacho mama akilaumiwa na chama au wanachama, mume wake ambaye sio kiongozi wa chama anaibuka na kujibizana na wahusika. Ni ngumu kuwa na chama ambacho baba akishindwa kuwajibika kwenye uongozi wake mke wake au watoto wake wanatoka na kukisema chama au kutoa ufafanuzi. Ni lazima kutenganisha mambo ya familia na taasisi.

  10. Taasisi hii na wanachama wake wajitahidi sana kuwa na malengo ya pamoja na kuyafanyia kazi pamoja. Katika nadharia ya uongozi na menejimenti, umoja na mshikamano miongoni mwa viongozi ni jambo la muhim sana bila kujali tofuati za utu wao. Kila kiongozi ndani ya taasisi ni vema ajione ni sehemu ya taasisi na ajizuie kwa gharama zozote zile kujitambulisha yeye binafsi nje ya utambulisho wa taasisi yake huku akijua hata kama anaweza kufanya alifanyalo kwa utambulisho wake,mwisho wa siku anaiaibisha au kuijengea heshima taasisi yake

  11. Ni hatari sana kwa taasisi kudharau mchango wa wanachama na viongozi wake kwa sababu tu kuna makosa wamefanya. Katika ubinadamu wa kawaida ni udhaifu mkubwa sana kufuta mema yote ya mtu kwa sababu ya kosa au kuonesha upande wa pili tusioupenda. Pamoja na majukumu mengine, taasisi lazima itumike kusaidia wanachama na viongozi wake kuwa bora zaidi na wanapoonesha kasoro zisizokubalika basi wajikite zaidi katika kuwarejesha badala ya kuwaona hawajawahi kuwa na faidia na ni hasara kwa chama

  12. Mwisho kabisa, nikishauri  chama hiki kuangalia vema namna wanavyokwenda kutatua sintofahamu iliyoko katikati yao. Wajaribu kutizama kwa undani uzito wa makosa ambayo yameonekana kwa baadhi ya viongozi wao (kama ni kweli) ambao nina hakika wamekua sehemu na mchango mkubwa sana wa kilipofikia chama sasa hivi. Pamoja na makosa yao (kama wanayo), wakumbukwe pia kwa mema na michango yao na kwamba kuna wakati walisimama kwa niaba ya chama kwa namna ambayo hakuna mtu mwingine yeyote yule angefanya. Mara zote, kuridhiana na kukubaliana ni bora zaidi ya kushutumiana, kulaumiana, kulumbana, kuchafuana na kuhukumiana. 

Kuna kitu nimejifunza na kukiona toka kwa Rais Kikwete ambaye. Mara kadhaa kumekua na mabishano na malumbano ambayo yamefikia hata watu kuvunjiana heshima katika uongozi wa kisiasa na wa nchi yetu. Mara kadhaa kumekua na sintofahamu katika uwanja wa kimataifa pia. Lakini Baba huyu katika uumini wake wa diplomasia ya maridhiano na kutafuta suhulu kupitia mijadala, amekua akitafuta kurejesha mahusiano mema na aliotofautiana nao, waliomkosea, wanamlamu na hata ambao kwa mtazamo wake wanaotaka kumuonea bila sababu za kweli. Kama CHADEMA kimeawahi kutafuta maridhiano na taasisi au watu wengine nje ya taasisi yao, hata katika hili la ndani ya chama chao, wanaweza kuliweka sawa na maisha yakasonga mbele wakiwa wamoja na wenye nguvu zaidi. 

Mimi sio mwanachama wa taasisi hii wala sijawahi kukutana uso kwa uso na wanaoshutumiwa wala kuwa na mawasiliano nao kama viongozi.  Nimewafahamu kwa kazi yao na uwajibikaji wao katika taasisi yao na kama vile ambavyo inawezekana kuna wengi wanakubali mchango wao katika kuijenga taasisi, hata mimi nimeshawishika na mchango wao katika mambo ya msingi ndani na nje ya taasisi yao. Hivyo maoni yangu hayajajikita katika kuwatetea bali katika ukweli uliofungwa na nadharia ya ubinadamu unaokuba kuwa kutokamilika kwetu sio msingi wa utambulisho wetu. Pamoja na hili, iwapo kuna mambo ya msingi wale wanaoshutumiwa wameharibu, ni wajibu wao kujitazama na kukubali fikra mpya zinazolenga kuwasaidia kuwa watu bora zaidi. 

Huenda wanapata vita zaidi kutokana na ugumu wao katika kukubali fikra na misimamo tofauti na waliyonayo au kujitambulisha kuwa bora zaidi ya wengine hasa pale kunapotokea mambo ya msingi yenye kuhitaji mustakabali wa pamoja.

Mwalim MM
mathewmndeme@gmail.com

Sakata la CHADEMA_ Ushauri huru kwa wahusika.docx
Download File



--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment