Thursday, 2 August 2012

[wanabidii] USHAURI KUHUSU TUZO ZA MITANDAO YA KIJAMII INAYOTOLEWA NA VODACOM TANZANIA

August 01, 2012, Mbeya,
Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza kwa dhati kabisa
washindi wa tuzo za kwanza za umahiri wa dijitali zilizoandaliwa na
kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom, nchini Tanzania (The Vodacom
Awards for Digital Excellence – VADE). Na kwa upekee kabisa, napenda
niwataje washindi hao ambao ni wafuatao:

Mikocheni Report, Issa Michuzi, Wanamuziki Tanzania, Kipanya.co.tz,
Vijana FM, Millardayo.com, Taste of Tanzania, Jamii Forums, Mambo
Magazine pamoja na DJ Fetty Blog.

Toka kutangazwa kwao, msimamo wangu umekuwa ni kwamba, sina tatizo na
washindi, maana mwisho wa siku naamini hawakujichagua wao wenyewe.
Lakini niongeze pia kuwa, huenda sina tatizo na waliowachagua washindi
hao, kwani ni wazi walichagua washindi kulingana na vigezo ambavyo
viliwekwa na ndio maana waandaaji hawakuwa na lolote la kusema pindi
walipotajwa washindi hao, zaidi ya kuwapa tuzo zao.

Na baada ya hapo, bilashaka sasa ninabakia na upande ambao nina
matatizo nao. Upande wa waandaaji wa tuzo hizi, na hapa nikimaanisha
kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom.

Kwangu mimi, utoaji wa tuzo hizi, umekuwa ni mwendelezo wa usanii
ambao umekuwa ukifanywa na kampuni hii katika kuhakikisha kuwa
wanatumia udhaifu wa kisheria, weledi na mshikamano baina ya waandishi
wa habari wa mtandaoni, kujinufaisha zaidi wao badala ya kuwanufaisha
wanahabari hawa ambao ni wazi wamekuwa wakiwafanyia kazi kubwa sana.

Yapo mambo kadhaa ambayo binafsi nimeyaona kuwa ni usanii mkubwa sana
ambao umefanywa na Vodacom hapa na wala haikuwa kwa lengo la kuinua
wahusika au tasnia ya uandishi wa mtandaoni kwa ujumla wake na
miongoni mwayo ni pamoja na vigezo ambayo vilitumika katika utoaji wa
tuzo hizo.

1. kati ya vigezo ambavyo nilisikia kuwa walivitumia, ni pamoja na
blog au blogger husika kuwa na blog ambayo habari anazoziweka
hazitokani na kutafsiri kutoka mitandao yoyote ile iwe ya ndani au nje
ya nchi wala kuwa imechukuliwa toka blog zingine.

Miongoni mwa blog ambazo zilishinda kama ambavyo nimezitaja hapo juu,
zipo ambazo zimekuwa zikiandika kazi za wasanii wa nje ambazo wenyewe
wamekuwa wakitamka kabisa maneno "…kwa mujibu wa mtandao fulani, redio
fulani, jarida fulani nk" Je, Vodacom hawakuliona hili kuwa ni kinyume
na vigezo vyao hapo?

2. Nimesoma mahali kuwa Vodacom waliliasisi wazo hili mwezi uliopita,
kwa maana ya mwezi Julai mwaka huu, ingawa linaelezwa pia kuwa
lilikuwa wazo la muda mrefu na kisha mwezi huo huo tuzo hizo
zikatolewa.
Je, Vodacom wanaweza kutusaidia kujua ni jinsi gani waliwashirikisha
blogger katika kuandaa tuzo zenyewe, kwa maana ya kuweka vigezo,
sababu ya vigezo hivyo, mechanism ya kuhakikisha kuwa vigezo
vinafuatiliwa (hasa linapokuja suala la takwimu), na mambo mengine ya
namna hiyo?

3. Katika kuangalia kile walichosema kuwa habari kwenye hizo blog
zinatakiwa ziwe zimeandikwa na mtu mwenye ujuzi nazo, je walikuwa na
mechanism gani pia katika kuhakikisha hili? Maana Vodacom ni kampuni
ya simu, haina wataalamu wala weledi wa masuala ya habari.

Upo uwezekano mkubwa sana kuwa walitumia kitengo chao cha mawasiliano
na umma au kitengo chao cha habari nk, (kulingana na wanavyokiita
wao), lakini pia upo ukweli wa wazi kuwa kitengo hiki sawa na kile cha
masoko, vimekuwa vitengo vyenye kuonyesha waziwazi udhaifu wao katika
utendaji kazi wao kiasi cha kuzua maswali miongoni mwa wenye
kuvifuatilia.

Hebu tujiulize, si hawa hawa Vodacom ambao walizua mjadala mkubwa sana
baada ya kuwa miongoni mwa wadhamini wa blog ambayo ilikuwa ikitajwa
kuwa imejaa matusi mengine ambayo hayafai hata kusimuliwa mbele za
watu waliostaarabika? Watu wa habari kama wapo, na kama walishindwa
kubaini mapungufu ya kilichokuwa kimejaa katikablog hiyo, leo hii
wanawezaje kutushawishi kuwa walikuwa bora katika kuibua na kutekeleza
wazo la VADE? Na wale wa masoko nao halikadhalika?

Je, Vodacom kweli walishindwa kuwa waungwana walau hata kushirikisha
waasisi wa fani hii katika Tanzania, wakiwemo akina Ndesanjo Macha,
Jeff, na wengineo ambao tunawajua kuwa bila wao leo hii Watanzania
bado tungekuwa tunasikia tu kitu blog katika vyombo vya habari?

Ni aibu sana kwa kampuni kubwa kama hii kuchukulia suala la tuzo kama
mechi fulani ya wanywapombe wanaoamua kujifurahisha katika kile
wanachokipachika jina la Bonanza. Aibu kwasababu, hata utoaji wa tuzo
wenyewe, lilikuwa tukio ambalo lilikuwa jepesi jepesi mno. Halikuwa na
mwamko wa namna hiyo, na pengine ni kutokana na ukweli kuwa wenyewe
walishajua kuwa wamefanya madudu kwahiyo ili kuepuka aibu, basi
wasiifanye kuwa issue kubwa.

Na ni katika muktadha huu basi ambako binafsi najiuliza, Je, Vodacom,
wameona kuwa kilicho cha muhimu kwao ni kujitangaza tu bila hata
kujali kuwa kujitangaza kwenyewe kunahusisha kuwa watupu? Lakini pia
nageuka upande wa waandishi wa habari hususan ambao wamezitwaa tuzo
hizo.

Mmejisikiaje kupata kitu ambacho kama wana taaluma mnaelewa wazi na
nafsi zenu zinawaeleza kuwa mmefanywa kombe lililofunikwa ili
mwanaharamu fulani apite na aendelee na hamsini zake?

Inawezekana kabisa kuwa wazo lilikuwa zuri, na hakika ninaafiki sio tu
kuwa wazo lilikuwa zuri, bali lilikuwa zuri sana, lakini utekelezwaji
wa wazo hili, umekuwa ni tukio la aibu ambalo binafsi ninaamini kabisa
kuwa Vodacom, watatakiwa kukaa na kujitathmini juu ya namna
wanavyowatumia waandishi wa habari.

Ni hadi pale tutakapofikia mahali pa kutambuana na kuthaminiana ndipo
tutaweza kusonga mbele kimaendeleo, kinyume na hapo, hii tabia ya
wengine kuwa wanyonge na wengine kuwa mahiri katika kutumia udhaifu wa
wengine kitaaluma, kiumoja na hata kiueledi, itafikia mahali
itatuumbua hadharani kweupeeeeee!! Kama ambavyo imeshaanza kujionyesha
sasa ambapo nasikia kuwa mmoja wa washindi, ambaye ni Michuzi,
amerejesha tuzo hiyo kwa waandaaji. Sijui kwa kuikataa, kuona
haimstahili anataka wambadilishie wampe nyingine au vipi.

Niko tayari kukosolewa pale ambapo siko sahihi
Ramadhan Msangi
CEO – Jukwaa Huru Media

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment