TAMKO LA JUMUIYA YA WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO MACHINGA JUU YA UAMUZI WA BUNGE KWENYE SUALA LA AKAUNTI YA TEGETA ESCROW KWA VIONGOZI WA SERIKALI NA ATHARI ZAKE
Ndugu wanahabari,
Toka kuanza na hata kuhitimishwa kwa mjadala katika bunge letu kama wa Tanzania tumesikia na kuona mengi, baada ya kutafakari mengi tulioyaona na kuyasikia, kwa pamoja kama kundi katika jamii tunadhani tunayo haki ya kutoa maoni yetu kwa namna swala zima tunaloliona. Si nia ya maoni haya kupinga au kukosoa maoni na mtazamo wa yeyote katika swala hili na pia si nia ya taarifa hii kupinga maoni au uamuzi wa bunge katika swala hili. Bila shaka tunakubaliana na uamuzi wa bunge kwa kuwa sote kama wa Tanzania tunalo jukumu kubwa la kupiga vita vitendo vya ufisadi na rushwa vinavyozidi kulitafuna taifa letu kila kukicha. Hii ndio sababu tunaliunga mkono bunge.
Pamoja na ukweli huo, lakini bado tunayo mashaka makubwa juu ya namna uamuzi wa bunge ulivyopatikana, bado tumeachwa na maswali mengi ambayo yanatia shaka kwamba huenda uamuzi uliofikiwa sio sahihi na wenye uonevu kwa baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali, pia tunaona kivuli kikubwa cha chuki za baadhi ya wafanyabiashara wakubwa kwa baadhi ya viongozi wetu na hasa waziri prof Muhongo, wafanyabiashara hawa bungeni wakiwakilishwa na baadhi ya wabunge kutokana na fadhila mbalimbali wanazopewa na wafanyabiashara hawa, kwa hakika prof Muhongo ameandamwa sana. Pia tumeona upepo mkali na kivuli kikubwa cha misukumo ya kisiasa ikitawala pia mjadala mzima pamoja na mazingira yote hasa katika kipindi hiki tunapokaribia kushiriki katika zoezi la uchaguzi mkuu wan chi yetu mwaka 2015.
Kwa kuwa hivi sasa swala hili limeachwa mikononi mwa Rais mwenyewe kama mamlaka kamili ya uteuzi na nidhamu kwa viongozi na watendaji wa serikali kufanya uchunguzi na hatimae kutoa uamuzi juu ya utekelezwaji wa maazimio ya Buinge. Kutokana na hali hiyo, na katika hatua hii tunaomba mh rais aachwe afanye kazi yake na kutoa uamuzi wake bila kuingiliwa na mtu yeyote, sisi tunaamini mh rais atafanya maamuzi yake kwa Haki, bila kumuonea yeyote huku akiepuka misukumo ya chuki na upepo mkali wa kisiasa kwa ajili ya makundi ya watu mbalimbali wanaojiandaa na uchaguzi mkuu mwaka 2015. Kufikia hapa pia tunaamini mh Rais atapata nafasi ya kusikiliza maoni yetu na kujaribu kutafuta majibu ya maswali kadhaa ambayo kwetu sisi bado hayajapatiwa majibu. Baadhi ya maswali yetu sisi ni haya yafuatayo:-
1. Je pesa zilizowekwa katika akaunti ya Tegeta Escrow ni pesa za serikali? Kama ni pesa za serikali kwa nini ziwekwe katika akauti ya escrow? Na kwa,ba pesa hizo zimelipwa kwa IPTL au zimeibiwa? Na kama zimeibiwa, nani alieiba?
2. Je IPTL ilistahili kulipwa capacity charge au haikustahili kulipwa?
3. Katika sakata hili, nani alipaswa kutuambia ukweli wa Tanzania juu ya kiasi gani hasa cha deni la capacity charge tunachodaiwa na IPTL hadi kufikia angalau kufikia tarehe 31/11/2014 ili tujue iwapo kiasi kilicholipwa ni kikubwa kuliko kile tunachodaiwa au kiasi kilicholipwa bado ni kidogo kuliko kile tunachodaiwa.(je ni kamati ya bunge ya hesabu za serikali? Je ni serikali yenyewe kupitia wizara ya nishati na madini? Bunge zima? Ni nani alikuwa na wajibu huu?
4. Kama kulikuwa na mgogogoro baina ya wamiliki wa IPTL hadi kupelekea kuamua kufungua akaunti hii ya tegeta Escrow kufunguliwa ili kuhifadhi malimbikizo ya malipo ya capacity charge hadi mgogoro wa wanahisa utakapoisha. Je ? hukumu ya jaji utamwa ilipotoka na kuipa haki PAP kusimamia mali na madeni yote ya IPTL je kuna mwanahisa yeyote aliekwenda mahakamani kupinga uamuzi wa jaji utamwa? Katika muda uliowekwa kisheria? Na kama hakuna aliepinga hukumu hiyo, AG alifanya kosa lipi kushauri malipo hayo yafanyike?
5. Katika sakata hili tumeshuhudia pasina hata chembe ya shaka kwamba ipo chuki binafsi dhidi ya waziri Prof Muhongo. Bila shaka chimbuko la chuki hii inatokana na misimamo mikali na thabiti ya mh prof Muhongo katika sekta anazozisimamia (nishati na madini) tumemshuhudia mara kadhaa waziri akiwakana waziwazi wawekezaji uchwara katika sekta ya gesi asilia, tunaamini prof muhongo alifanya hivyo baada ya kuangalia rekodi mbalimbali na historia ya uwekezaji wa watu hawa katika nchi hii je ni wawekezaji au madalali? Kauli na misimamo ya prof muhongo zimemfanya achukiwe kwani hakuna mtu atakaesema kweli akaachwa kuwa salama. Ikumbukwe kwamba baadhi ya wafanyabiashara hawa ndani ya bunge wanao watu ambao wamekubali kuwakilisha chuki zao dhidi ya prof muhongo kwa ujira wa kupewa fadhila za aina mbalimbali (wengine inasemekana watoto wao wanasomeshwa nje ya nchi kwa kulipiwa na wafanyabiashara hawa) tunaomba vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi yetu vichunguze na kufuatilia kwa undani swala hili.
6. Kwetu sisi kama wajasiliamali wadogo tunadhani na tunayo imani na prof muhongo kwani katika kipindi chake cha uongozi tumeona mambo yafuatayo:
(a) Hali ya kushuka kwa gharama za kuunganishiwa umeme majumbani na katika sehemu za biashara.
(b) Kupungua kwa muda wa kuomba umeme na kupatiwa huduma za umeme
(c) Kuanza kupatikana kwa umeme wa uhakika mijini na vijijini jambo ambalo limerahisisha sana shughuli zetu za ujasiliamali kwani hakuna maendeleo bila umeme.
Kutokana na hali hiyo, sisi kama sehemu tu ya wananchi tunaomba prof muhongo pamoja na viongozi wengine wote waliotajwa kuhusika katika swala hili, tunaomba uchunguzi wa kina ufanyike juu ya kuhusika kwao na kama kuna makosa yoyote waliofanya na hata kuwajibika kuchukuliwa hatua zilizopendekezwa na bunge. Na kwa kuwa tuliona bunge lenyewe likigawanyika juu ya kukubali ripoti ya kamati ya bunge ya hesabu za serikali, tumeona jinsi ripoti ya serikali ilivyokanusha kwa ufasaha hoja zote zilizopo katika taarifa ya kamati ya bunge, katika mjadala pia tumeshuhudia pia wabunge wakigawanyika kwa kiasi kikubwa na kuwepo kwa tetesi za makundi mbalimbali yalivyokuwa yamenufaika kwa namna mbalimbali na mjadala wa swala hili, kutokana na hali hii tunashauri kama upo uwezekano ni vema serikali ikaalika vyombo va uchunguzi vya nje ya nchi kufanya uchunguzi huru wa swala hili.
Mwisho tunamuomba mwenyezi mungu amjalie rais wetu hekima kama za mfalme suleimani katika kutafuta ufumbuzi wa swala hili kwa haki na asinyongwe mtu bila haki. Mara zote mh rais amekuwa akituasa kuwa na akili kama za mbayuwayu kwamba usikilize kila kitu kisha uchanganye na zako ili kupata jibu makini na la uhakika.
IMETOLEWA TAREHE 5/12/2014 NA JUMUIYA YA WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 comments:
Post a Comment