MWIGULLU NI MTU MWEMA.
GAZETI CHANGAMOTO.
Wiki iliyopita niliahidi kuwa nitazungumzia mahusiano ambayo yamekuwa yakitajwa kuwepo kati yangu na baadhi ya watu mbalimbali hususani wana habari na wanasiasa. Kwa kweli wakati mwingine hata mimi mwenyewe nilishtushwa sana na namna magazeti yalivyokuwa yakiandika uongo wa mchana kweupe dhidi ya watu na mimi. Kati ya watu wengi ambao nimekuwa nikihusishwa nao ni Mwigullu Nchemba, wakati ule mbunge na naibu katibu mkuu wa CCM taifa.
Ukiacha kusikia na kusoma magazeti nilikuwa sijawahi kumuona Mwigullu kwa karibu mpaka siku moja tukiwa Igunga mwaka 2011 wakati wa uchaguzi mdogo. Alikuwa kiongozi wa kampeni za CCM. Siku moja nilikuta katika saloon ya kunyoa nywele akiwa hapo pamoja na Julius Mtatiro wa CUF.kulikuwa na mjafala mkubwa sana unaohusu mambo ya uchaguzi ule. Mwigullu na Mtatiro ndiyo walikuwa wazungumzaji wakuu na vijana waliwasikiliza.
Nilipofika niligundua upande wa Chadema haukuwa na mzungumzaji na hawa walikuwa wakivutia kwenye vyama vyao.nikaona ninawajibika kutetea chama changu. Nikaanza kuongea na ajabu kumbe vijana wengi waliokuwa hapo walikuwa wafuasi wa chadema wakawa wananishangilia sana kiasi cha kutowaruhusu akina Mtatiro kuongea tena. Hata hivyo hapakuwa na utambulisho wowote kwa hiyo japo mimi nilimfahamu Mwigullu lakini yeye hakunifahamu mimi.Mtatiro tulikuja kuendelea kuwasiliana na hata kukutana mara kadhaa baada ya uchaguzi wa Igunga.
Wakati wa Krismass nilikutana tena na Mwigullu dar es salaam mlimani city akiwa na familia yake akifanya manunuzi ya sikukuu.alikuwa pia na Laurence Masha. Yeye nadhani anaweza hata asikumbuke matukio haya. Tulisalimiana na nikajitambulisha kwake na kumkumbusha tukio la Igunga kwenye saloon.akanikumbuka na hapo tukawa tumeongelea mambo kadhaa ya uchaguzi wa Igunga kisha tukaachana. Unaweza kuona kuwa mpaka hapo wala huwezi kusema tulifahamiana.
Muda uliofuatia nikawa nabishana naye sana kwenye mitandao na hasa kwenye kundi la TANURU LA FIKRA la facebook ambako naye alikuwa mchangiaji.
Nilikuja kukutana tena ana kwa ana na Mwigullu siku kadhaa baada ya sakata la video ya Lwakatare. Ni sahihi kuwa Mwigullu amewahi kunitumia elfu 50 kwa M Pesa. Kwa nini alinitumia fedha hiyo na malengo ya kukutana kwetu wakati huo hayawezi kuandikwa sasa kwa sababu ya kesi iliyoko mahakamani. Lakini hakika siyo kwa malengo ambayo yamekuwa yanaandikwa magazetini. Kesi ikimalizika mahakamani, kila jambo litakuwa wazi.
Tangu matukio hayo Mwigullu amekuwa anatangazwa na Chadema na baadhi ya watu kama mtu mbaya ama gaidi, ama mtu hatari kwa mabadiliko ya nchi hii. Sina lengo la kumtetea juu ya tuhuma hizo maana yeye na mimi ni binadamu. Ninachosema ni kuwa kwangu mimi kadri nilivyomfahamu wakati ule na sasa nimemjua kama mtu mwema.
Sambamba na Mwigullu kulikuwa pia na maneno kuwa mimi Ludovick ni mtumishi wa Usalama wa Taifa. Nimewahi kusema kwa ufupi tu kuwa hayo ni majungu na propaganda za kisiasa na ninaweza kusema kwa hakika kuwa zilikuwa zikisambazwa makusudi na baadhi ya watu waliokusudia kuuchanganya umma. Ukiacha maneno hayo ya usalama wa taifa sijui chochote zaidi kuhusu idara hiyo achilia mbali kuwa mtumishi wake.
Historia yangu na nilikosoma iko wazi na ni ya moja kwa moja.hakuna jambo lolote kwenye masomo yangu ambalo limekuwa kificho wala hakuna wakati wowote kwenye maisha yangu ambalo halifahamiki sawasawa kujenga nadharia kwamba muda huo labda ndiyo nimeutumia kwa mafunzo ya idara hii.
Katika uongo, majungu na propaganda hizo, gazeti moja lilifikia kuandika kuwa nimewahi kuishi na kufanya kazi Vatican makao ya papa wa kanisa katoliki duniani. Huu licha ya kuwa ulikuwa uongo ulionyesha pia uwezo mdogo na wa hovyo wa baadhi ya waandishi wetu wa habari. Mimi sijawahi hata kufika Uganda nchi ambayo iko jirani kabisa na kijijini kwetu.
Lakini wakati wengi hawakujua ni kwa nini waliotangaza kuwa mimi ni mtumishi wa usalama wa taifa mimi ninayo mawazo kuwa walifanya hivyo kutokana na Paniki ya kuogopa kuhusishwa na tukio la kujeruhiwa vibaya kwa Absalom kibanda. Walikuwa wanadhani wanafanya "pre emptive" mesures! Kwa kweli walikuwa wameogopa kivuli chao tu.
Huko mbele nitasimulia ni kwa namna gani na kwa malengo gani nilihusishwa na matukio hayo tena na chama changu mwenyewe. Ilivyo ni kuwa mimi nimefunguliwa jalada la uchunguzi dhidi ya tukio lile na ninaamini uchunguzi wa dola unaendelea. Kwa hiyo mambo ya kusema mimi ni mtumishi wa usalama wa taifa ni uzushi na ujinga wa waliokuwa wakivumisha hivyo.
Katika mlolongo wa mambo niliyozushiwa ama kusingiziwa ni pamoja na kuwa nilijipenyeza, kuwa karibu na waandishi wa habari na wahariri wa magazeti. Je madai haya yenyewe yana ukweli kiasi gani? Wiki ijayo nitaendelea kuelezea hayo na mahusiano yangu na mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora.
Itaendelea wiki ijayo...
Mawasiliano 0757 314961.
--Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 comments:
Post a Comment