Wednesday 18 December 2013

[wanabidii] POSHO KWA WAWAKILISHI WA WANANCHI NI KIKWAZO CHA MAENDELEO YA TAIFA

Na.Damas Makangale
--
Ingawaje Tanzania inaitwa nchi masikini pamoja na kwamba wahisani na wadau wa maendeleo wanasema ni nchi inayoendelea lakini kwa ujumla na kwa yeyote anayeijua nchi yetu kwa maana ya hali ya maisha ya wananchi wake, ni jambo la hatari kwa kikundi kidogo cha watu waliokalia ofisi za umma na kujipangia utaratibu fulani wa kujinufaisha.

Kikundi hiki kidogo tena kilichochaguliwa na wananchi kama wawakilishi wao (wabunge) na ndio watunga sheria kujinufaisha kwa jasho la walipa kodi kwa kisingizio cha sheria ambazo wametunga wao wenyewe kwa kujipendelea.

Ni aibu zaidi kusikia kwamba wabunge wengi na hata baadhi ya mawaziri kukejeli juhudi binafsi za baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania wenye kuogopa kodi za wananchi na kutaka mabilioni hayo kuelekezwa katika miradi ya maendeleo ya wananchi kwa maslahi mapana ya taifa.

Tumeamua kusema hayo bila kuficha kwamba ni muhimu kwa Serikali pamoja na Bunge kufikiri upya mtindo huu wa kifisadi wa kulipana posho ya kukaa (Sitting Allowance) wakati wana mishahara mikubwa kuzidi wafanyakazi wenye kufanya kazi usiku na mchana kama vile madaktari wanaosubiri kulipwa posho ya (overtime) ya shilingi elfu kumi ambayo hukaa hadi miezi mitatu mpaka sita haijalipwa.

Tunasema na kusisitiza kuwa ujira wa vikao ambavyo ni kazi halali za ubunge ni mshahara na si posho! Posho ni wizi wa fedha za umma mchana kweupe kwa sababu kazi ya Mbunge ni uwakilishi na pale anapokaa kwenye vikao vya bunge na kamati mbalimbali anatimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi iweje alipwe Posho? 

Mwaka juzi kwenda mwaka jana 2011/2012 Serikali ililiomba Bunge kupitisha sh bilioni 987 kwa ajili ya psoho mbalimbali za watumishi wa Serikali wakiwamo wabunge. Hii ni hatari kwa mustakabali wa taifa changa kama Tanzania.

Huu ni kweli kwamba mabilioni ya shilingi zikiwa ni kodi za wananchi kila mwaka wa fedha yanatengwa kwa ajili ya posho tu, na hata mwaka jana Benki ya Dunia na wahisani wa maendeleo walihoji uwepo wa posho za kukaa kwa watumishi wa serikali na wabunge lakini bado tatizo hili la kuzoea posho linaitafuna nchi yetu bila huruma.

Serikali kupitia wizara ya fedha mwaka 2011/2012 iliahidi kwamba posho ambazo hazina tija zitaondolewa kauli iliyoonekana kama mwanzo wa mageuzi ya kweli, lakini leo asubuhi niliposikia kipindi cha tuongee magazeti juu ya Wabunge kutafuna posho ovyo wote wa chama tawala na upinzani ni ishara kwamba serikali ilitaka kauli ile ieleweke kinyume nyume.

Gazeti la kila wiki la Raia Mwema limeongoza leo na habari za wabunge kutafuna posho hovyo hovyo na Mbunge kijana Joshua Nasari amekiri kwamba alichukua posho ya kwenda safari Malaysia lakini ikatokea dharula ya Harambee jimboni kwake akaona ni busara kujumuika na wananchi wake bravo kwake.

Bila kutafuna maneno Tanzania ni nchi maskini, kwani kipato cha mwaka cha mwananchi wa kawaida ni Sh 770,463 hivi, wastani wa kama Sh 2,140 kwa siku, kwa mantiki hiyo Mtanzania wa kawaida kuishi katika maisha ya leo kwa kipato hiko ni kwa kudra za mwenyezi mungu kama si rushwa dogo dogo zinazomwezesha kumaliza mwaka. 

Lakini wakati wananchi walio wengi wakiishi katika umaskini wa kutupa, wapo watu waliaomua kusaka nafasi za uongozi katika nchi hii si kwa nia ya kusaidiana na wananchi kutokomeza umaskini ulioelemea taifa hili, ila kujitenga nao kwa kutengeneza utaratibu mbaya na kandamizi wa kujilipa mafao manono kama hizi zinazoitwa posho za vikao za wabunge.

Kwa maelezo yoyote yale, posho hizi si halali hasa zinapolipwa na taifa maskini kama Tanzania ambalo haliwezi hata kujitegemea kwa kuwa na bajeti yake walau kwa mwaka mmoja tu bila kutembeza bakuli kwa wafadhili ili kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa mtanzania yeyote makini atakubaliana nasi kwamba walioweka utaratibu huu ama walipotea njia kwa ama walitanguliza mbele maslahi binafsi lakini wananchi wameamka na wanajua kinachoendelea na wanawasubiri 2015 kwenye uchaguzi watawaita wabunge wa posho na vitambi vya posho kama si mchemsho na kiti moto na bia kaeni chonjo uchaguzi unakuja!

Na kuna taarifa za kutisha kwamba siku hizi hata kazi ambazo ni wajibu wa watumishi wa umma kuzifanya watu hawafanyi mpaka kuwepo na posho (Bahasha) yaani ofisa wa serikali kukaa kwenye kikao cha kazi ambayo ni wajibu wake, anadai mshiko tumekwisha!
Kwa utaratibu huu watanzania itatuchukua muda mrefu mpaka kuja kupata maendeleo ya kweli na hakuna jambo lolote linalokwamisha uwezo wa serikali kutimiza wajibu wake zaidi ya maposho yasiyo kuwa na kichwa wala miguu ndugu zangu tukafanye kazi tuliotumwa na wananchi tuache rongo rongo za posho zisizo kuwa na tija kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Naomba kuwasilisha !
Damas Makangale
Mhariri Mkuu

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment