Monday 30 December 2013

[wanabidii] Taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuhusu kusitishwa kwa “Operesheni Tokomeza Ujangili”

Itakumbukwa kuwa Serikali iliamua kuanzisha "Operesheni Tokomeza Ujangili" kufuatia kukithiri kwa vitendo vya ujangili katika maeneo yote yaliyotengwa kisheria kama Mapori ya Akiba; Hifadhi za Taifa na Hifadhi za Misitu katika miaka ya karibuni. Hata hivyo, Serikali iliamua kusitisha operesheni hiyo kwa muda.

Kufuatia kusitishwa kwa Operesheni Tokomeza, matukio ya uvunjaji wa sheria za hifadhi kama vile uingizaji holela wa mifugo katika maeneo ya hifadhi; ujangili wa tembo pamoja na uvunaji wa miti katika hifadhi za misitu yanaonekana 
kushamiri. Aidha, kumekuwa na ongezeko la kuvamiwa watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii na hata kuwasababisha madhara yakiwemo vifo na majeraha. Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na:

  • Majangili kuua takriban tembo 60 katika Hifadhi/Mapori ya Selous, Rungwa, Burigi na Katavi na Ngorongoro. Hawa ni takriban tembo wawili kwa siku. Ikumbukwe kuwa wakati wa kipindi chote cha operesheni kilichodumu kwa mwezi mmoja ni tembo wawili tu waliokuwa wameuawa. 

  • Watumishi wa Pori la Akiba Mkungunero (Kondoa) waliokuwa doria kuvamiwa na kundi la watu wapatao 80 waliokuwa na mikuki na silaha nyingine za jadi tarehe 24 Desemba, 2013. 

  • Kuuawa kwa Askari mmoja wa wanyamapori aliyejulikana kwa jina la Ramadhani Magengere (40) na mwingine, Bwana Yahaya Ramadhani (34), kujeruhiwa vibaya na Wafugaji walioingiza mifugo ndani ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Jumuiya (WMA) Ukutu (au JUKUMU) iliyoko Morogoro vijijini tarehe 6 Decemba, 2013. 

  • Mtumishi mmoja wa wanyamapori, Sajidi Majidi, kujeruhiwa kwa kuchomwa mkuki kichwani na kuvunjwa mkono na wafugaji walioingiza ng'ombe katika Eneo la Ramsar la Kilombero tarehe 14 Novemba, 2013. 

  • Kukamatwa kwa gari lililokuwa na mizoga 20 ya swala wilayani Simanjiro siku za karibuni

  • Kuanzishwa kwa kambi ya majangili katika Pori la Akiba Burigi ambapo vitendo vya ujangili vinaendeshwa. Majangili waliokuwa na silaha za moto walikimbia na kuacha nyuma nyani 30 waliokuwa wamewaua baada ya kukurupushwa na askari wa wanyamapori.

  • Kuongezeka wimbi la uvamizi na ufugaji wa mifugo ndani ya mapori ya akiba na hifadhi za misitu iliyopo magharibi mwa nchi yetu, hasa Burigi-Biharamulo-Kimisi, malagarasi-Moyowosi, Rukwa Lukwati, Luwanda, Ugalla, Ibanda-Rumanyika, Minziro na Katavi.

Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kuwakumbusha wananchi kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 pamoja na Sheria zinazosimamia maeneo ya Hifadhi za Taifa na Misitu kuwa hairuhusiwi wananchi kuingia katika maeneo haya bila kibali ikiwa ni pamoja na uingizaji wa mifugo kwa ajili malisho. Aidha, bado vitendo vya ujangili haviruhusiwi chini ya sheria hizi. Kifungu cha 15 ni marufuku mtu yeyote kuingia kwenye pori la akiba bila kibali. Aidha, Sheria hiyo inakataza kuwa na silaha yoyote ndani ya Pori la Akiba bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori [kifungu cha 17]; kuwinda, kuua, kukamata au kujeruhi mnyama [Kifungu cha 19] na kuchunga ng'ombe ndani ya Pori la Akiba [Kifungu cha 21]. 

Ikumbukwe kuwa matukio yaliyotokea bungeni Dodoma, hayajatengua Sheria yoyote ya Wanyamapori au Misitu. Hamna maamuzi yoyote ya Bunge yaliyohalalisha ukiukwaji wa Sheria za Uhifadhi. Hivyo, wananchi wanatakiwa kutii na kufuata Sheria hizo kama zilivyo. Tahadhari inatolewa kuwa Serikali haitasita kumchukulia hatua kali yeyote atakayekiuka Sheria ya Wanyamapori kwa makusudi. Tunawaomba wananchi wasikubali kudanganywa na mtu yeyote yule kuvunja Sheria za nchi.

Aidha, nachukua nafasi hii kuwaagiza watumishi wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii wahakikishe kuwa wanaendelea kutekeleza majukumu yao ya ulinzi wa maeneo ya Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba na Misitu ya Hifadhi bila kutetereka. Sanjari na hilo wasisite kuchukua hatua stahiki dhidi ya mhalifu yeyote mradi tu wanazingatia Sheria, Kanuni na taratibu. Utekelezaji huu wa sheria ufanyike bila kuathiri haki za msingi za binadamu.

Serikali ina maadili na miiko inayotawala utendaji kazi wa watumishi wake wote wakiwemo wale wa maliasili. Wizara ya Maliasili itaendelea kuwakumbusha watumishi wake juu ya maadili na miiko hii kupitia mafunzo ya mara kwa mara na mbinu nyingine. Aidha, Wizara itaendelea kuboresha miongozo inayohusu maadili na miiko hii ili iweze kuendana na wakati.

Mwisho, Serikali inasisitiza kuwa, kwa kutumia vyombo vyake, itaendelea kutekeleza majukumu yake na kusimamia ipasavyo Sheria ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayeshiriki moja kwa moja au kusaidia vitendo vya ujangili ili kunusuru rasilimali za Taifa. Jukumu la uhifadhi wa maliasili zetu liko pale pale, ni letu na lazima litekelezwe kwa manufaa ya kizazi hiki na vizazi vijavyo.

Imetolewa na:

Mh. Lazaro Nyalandu, MB.
NAIBU WAZIRI, MALIASILI NA UTALII
Desemba 29, 2013.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment