Wednesday 18 December 2013

RE: [wanabidii] Kwa CCM tatizo si CHADEMA ni Mbowe

Kwa mpenda mabadiliko wa kweli pasipo fitina huu ndio ukweli.

 

 

Always darkness will never comprehend light


From: wanabidii@googlegroups.com [wanabidii@googlegroups.com] on behalf of Josephat Isango [joseisango@yahoo.com]
Sent: Wednesday, December 18, 2013 2:43 PM
To: mabadilikotanzania@googlegroups.com; wanabidii@googlegroups.com
Subject: [wanabidii] Kwa CCM tatizo si CHADEMA ni Mbowe

Kwa CCM tatizo si CHADEMA ni Mbowe

15/12/2013   | Makala | 0 comments | 145 views

NDUGU wasomaji, ninapenda sana kuwapa pole kwa kifo cha shujaa wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi Nelson Ndlahla Mandela. Kila gazeti, runinga na redio zimeelezea wasifu wake kiasi cha kufurahisha.
Hata hivyo, mimi niseme tu kwamba kwa Mandela tunajifunza neno moja dunia nzima; "hakuna utawala dhalimu popote duniani utakaoruhusu haki ipatikane kirahisi."
Kwa hakika hawa wote wanaomsifia Mandela kwa namna alivyovumilia mateso akipigania haki za wanyonge Afrika Kusini na duniani kote kwa taathira yake, wengi wao kati ya wale wenye mamlaka wanawatesa sana wananchi wazalendo wanaopigania haki zao na za wenzao.
Hayo yapo sana Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine nyingi Afrika na duniani kote.
Hivi leo sambamba na habari za kifo cha nguli huyu wa siasa duniani, hapa Tanzania kunaendelea habari za sakata la Zitto Kabwe na Dk. Kitila Mkumbo kunyang'anywa vyeo vyao CHADEMA na Kamati Kuu.
Mengi yamesemwa kuhusu namna wanachama hawa wa CHADEMA walivyochukuliwa hatua hizo na jinsi walivyozistahili. Yametokeza makundi yakibishana sana kuhusu hatua hii ya Kamati Kuu.
Wapo waliofurahia na kupongeza hatua hiyo. Hapa baina yao wapo waliohoji ni kwa nini chama hicho kilichelewa kuchukua hatua hiyo kwani walikuwa wanajua ukweli kwamba watu hawa kwa ukosefu huo wa nidhamu walistahili kuondoka mapema zaidi.
Wengine waliona mwenendo wa Zitto katika siasa za ukombozi ulivyobadilika na kujiaminisha kabisa kwamba kuna "kitu" kimemdhuru na kuharibu kabisa kasi yake ya awali.
Sitaacha kuwasemea wale walioamini kwamba matendo ya Zitto yanathibitisha wazi kwamba anasaliti harakati za ukombozi kwani amekuwa akihujumu shughuli za CHADEMA na pia yeye binafsi haonekani katika kukurukakara za chama.
"Mbona wabunge wote wamekumbwa na kadhia nyingi dhidi ya polisi na lukuki wana kesi mahakamani, lakini Zitto yeye hana kesi hata moja na wala hatujasikia akiparurana na polisi?" mmojawao aliniuliza.
Haidhuru. Hebu leo nije na taarifa ya uchunguzi juu ya sababu hasa ya vita iliyoko CHADEMA. Haiwezekani chama cha siasa kiwe kinapigwa vita bila sababu. Hiki si ugonjwa wala si janga inakuwaje kipigwe vita kubwa namna hiyo?
Inakuwaje vyama vingine havipigwi vita kama CHADEMA na ndani ya chama hicho kinachopigwa vita na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni nini?
Kihistoria kila chama cha siasa kilichopata nguvu katika enzi yake kilipigwa vita za aina mbalimbali na hatimaye kuporomoshwa kama si kuanguka kabisa. Ikumbukwe kwamba enzi za NCCR- Mageuzi chama kiliimarika na kuwa tishio kabisa dhidi nya CCM.
Wengi waliamini kwamba CCM ilikuwa katika dakika zake za mwisho. Mwaka 1997,  NCCR-Mageuzi ikapigwa dafrao. Wanachama wengi akiwepo mwenyekiti wake wa wakati huo wakaondoka.
Baada ya dafrao hilo, chama kilipoteza umaarufu na hakikuwa masikioni wala machoni mwa Watanzania kama ilivyokuwa kabla ya dhoruba.
Nyota ya Chama cha Wananchi (CUF) ilianza kung'ara sana, watu walikiona ndiyo mbadala wa CCM.
Uhai wa CCM ulikuwa shakani. CUF kilipigwa vita sana. Zilipigwa propaganda nyingi dhidi ya CUF. Serikali na CCM walipiga propaganda nyingi kwamba chama kile kilikuwa cha Kiislamu.
Ilifikia hatua Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) wa wakati huo Omari Mahita, akaenda kwenye vyombo vya habari akionyesha majambia yaliyoletwa nchini na kutangaza kwamba yalikuwa mali ya CUF.
Kelele nyingi zilipigwa dhidi ya Maalim Seif aliyekuwa akiwania urais wa Zanzibar kwa lengo la kukidhoofisha chama hicho. Walifanikiwa kabisa kuimaliza CUF huku Tanzania Bara na kule Unguja, lakini bado kule Pemba huwaambii lolote wananchi juu ya chama hicho.
CHADEMA kilikuwa chama kipole. Kilisifiwa sana na viongozi wa serikali na CCM. Aliyeanza kukisifia alikuwa Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere. Wengi ndani ya serikali katika miaka ya 1990 waliitamka CHADEMA kwamba ni chama kinachoongozwa kwa busara nyingi.
Viongozi wake walisifiwa sana kwamba hawana hata tamaa ya kugombea urais. Ikumbukwe kwamba katika uchaguzi mkuu wa 1995 hakikuweka mgombea urais na hata majimboni waligombea sehemu chache sana.
CHADEMA kilivishawishi vyama vingine viunganishe nguvu na kuachiana majimbo kama njia ya kuiondoa CCM. Mwaka huo 1995 nguvu za chama hicho katika urais ziliwekezwa kwa mgombea urais wa chama cha NCCR Mageuzi.
Kiliamua bila ajizi kumpigia kampeni mgombea urais huyo kila walipokuwa wakiamini kwamba hiyo ndiyo ilikuwa njia njema ya kuishinda CCM.
Mwaka 2000 CHADEMA haikuweka mgombea urais pia. Ilijipima na kuona kwamba haijakua vya kutosha. Kipindi hiki nguvu yake ikazihamishia kwa mgombea wa urais wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.
Kipindi hiki pia CHADEMA kiliamini katika kuhakikisha kwamba kinaachiana majimbo ili kuishinda CCM.
Mwaka 2005 CHADEMA kiliamua kuweka mgombea urais. Aligombea kijana mkakamavu Freeman Mbowe.
Katika kinyang'anyiro kile cha moto, Mbowe aliyekuwa mwenyekiti wa chama kipindi hicho alikuja na mbinu ya kutumia helkopta katika kampeni zake. Hii ilimfanya afanye mikutano mingi kwa siku na hivyo kuwakimbiza sana wagombea wenzake, akiwepo mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete.
Inakadiriwa kwamba Mbowe alifanya mikutano ya kampeni 582 wakati wagombea wenzake 9 kwa pamoja hawakufikisha mikutano 300.
Kwa kampeni zile ambazo kwa hakika CCM hawakujua mpango nyuma ya pazia wa CHADEMA, ndizo zilizokifanya chama kikawa maarufu na kuanza kufahamika nchini kote.
Hii ilikuwa mbinu iliyowekwa na watu wachache chini ya kamanda Mbowe. Alijua wazi kwamba CCM haijajiandaa kuachia madaraka hata kama itashindwa kwa uhalali kiasi gani.
Mbowe alijua kwamba atapata kura nyingi na pia atawasaidia wagombea wengi wa ubunge na udiwani kushinda kutokana na kishindo cha chama. Jambo hili lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa sana.
Kura za urais alizozipata Mbowe hadi leo hakuna ajuaye nini kilitokea. Ilikuwaje akapata laki sita tu? Eti alishindwa hata na Lipumba wa CUF.
Ushahidi wa uongo mkubwa uliofanywa katika kutoa matokeo ya uchaguzi wa rais mwaka ule 2005 ni matokeo ya chaguzi ndogo zilizofuata. Kule Kiteto, CHADEMA ilipata kura 24,000 ikitanguliwa na CCM iliyokuwa na kura 29,000.
CUF haikugombea kabisa kwa kushindwa hata kupata mgombea. Kule Busanda, CCM ilipata kura 25,000 hivi wakati CHADEMA ilipata kura takriban 21,000. CUF haikupata kura 1,000.
Hayo yalitokea pia kule Tarime, Biharamulo ambako tofauti kati ya kura za CCM na CHADEMA zilikuwa 880 tu. Kila mahali CHADEMA kilishika nafasi ya pili karibu sana na CCM kikifuatiwa na vyama vingine kwa mbali sana.
Huu ndiyo uthibitisho kwamba matokeo ya urais mwaka 2005 ambapo Kikwete alishinda kwa mbali akifuatiwa na Lipumba wa CUF na wa tatu alikuwa Mbowe wa CHADEMA aliyepata takriban nusu ya kura za Lipumba hayakuakisi hali halisi ya umaarufu na uthabiti wa vyama vilivyoingia katika kinyang'anyiro. Kiukweli tuseme wazi matokeo yale yalikuwa na uongo mwingi.
Hoja yangu kwenu wasomaji leo ni kuchimbua sababu za chuki kubwa ya CCM kwa CHADEMA na ukweli wa kile wanachokichukia CHADEMA.
Tumejiridhisha kwamba kila chama cha siasa kilichoshika kasi na kuimarika kiasi cha kutishia usalama wa CCM kilikumbwa na mshikemshike mkubwa kutoka kwa chama hicho tawala ambao ulikifanya chama hicho kuyumba sana na vyote viliporomoka.
Baadhi ya mbinu zilizotumika kuporomosha vyama hivyo ni kuingizwa kwa migogoro baina ya viongozi wa ngazi za juu (hasa Mwenyekiti na Katibu Mkuu), matumizi ya fedha kupoza kasi za viongozi wa juu wa vyama hivyo na bakshishi zilizowafanya wakubali kuachana na mpango wa kuviimarisha vyama vyao.
Kusema kweli kwa mujibu wa CCM ni lazima chama chochote cha siasa kikipata nguvu kifanyiwe kila mbinu kukiporomosha. Hii ni mbinu pekee iliyobaki kwa CCM kubaki salama.
CCM kimejithibitishia kwamba hakiwezi tena kuwatumikia wananchi na kuwaondolea matatizo waliyo nayo. CCM si chama cha kuwatumikia Watanzania tena bali ni chama cha kila kiongozi kujitajirisha na kupora mali za umma.
Ili wasihojiwe na ili kupunguza nafasi ya kushindwa katika uchaguzi wanafanya kwa bidii kubwa kuua upinzani. Wanataka wabaki wao wenyewe wakiwa na nguvu ya kufanya siasa na kuwanyima wananchi chama mbadala chenye hadhi ya kuchagulika.
Mbowe alikabidhiwa chama kama mwenyekiti akikikuta kina wabunge wanne wa kuchaguliwa na idadi ya madiwani wasiofika 100.
Miaka sita baadaye chini ya uenyekiti wake tayari chama kina wabunge 49, madiwani zaidi ya 500 na wenyeviti kwa maelfu wa vijiji na mitaa. Chama kimejenga mtandao katika vijiji vyote nchi nzima.
Kuanzia kaskazini hadi kusini mashariki hadi magharibi CHADEMA inafahamika. Kikubwa zaidi ni kwamba inafahamika kama chama mtetezi wa wanyonge na kinachopambana na ufisadi na rushwa.
Ugunduzi wa kutumia helkopta katika uchaguzi nchini uliofanywa na Mbowe umefanya watoto na watu wazima nchini wakiona helkopta hata kama ni ya Msalaba Mwekundu au ya Jeshi la Polisi wanajua hiyo ni "CHADEMA inapita".
Mavazi ya kombati ambayo Mbowe amekuwa akiyavaa kuanzia katika kampeni za uchaguzi wa mwaka 2005 yamewavutia sana vijana wa Tanzania. Hata watu wazima wengi wanayapenda.
Kwa hakika kombati ni alama ya CHADEMA kokote. Wapo ambao si wanachama wenye kadi, lakini wanajitambulisha mapenzi yao kwa chama kwa kuvaa kombati.
Kaulimbiu ya 'People's Power' ambayo hadi leo Watanzania wanaifurahia, wengi wanaitumia kama namna ya kuonyesha kwamba umma una mamlaka zaidi kuliko viongozi. Umma ukiamua inabidi watawala wakubali.
Mfumo wa kuendesha operesheni za chama kuanzia ile ya Sangara, M4C na sasa CHADEMA ni msingi pamoja na ugatuaji wa madaraka kutoka makao makuu Dar es Salaam hadi kwenda kwenye kanda ni vichache kati ya mbinu za Mbowe kuibana CCM.
Katika matukio makubwa ambayo hayatasahaulika kirahisi, ni pale wabunge wa kambi rasmi ya upinzani walipotoka nje ya ukumbi wa Bunge kama namna ya kumpa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ujumbe kwamba matokeo ya uchaguzi yalikuwa yamechakachuliwa, katiba ni mbovu na mahitaji ya Tume Huru ya Uchaguzi.
Si jambo la mchezo kusimamia tukio hilo. Inahitaji moyo sana. Lakini Mbowe aliwaongoza wabunge wenzake kwa ujasiri kutoka mbele ya rais. Tukio hilo ndiyo hasa lilimsababisha rais kuamua kuanzisha mchakato wa kutengeneza katiba mpya.
Kwa kifupi CCM inatawala nchi wakati CHADEMA inaongoza taifa. Yote haya yametokana na bidii, kujituma, ujasiri na uzalendo wa Freeman Mbowe.
Katika kuua nguvu za CHADEMA, CCM wamejitahidi sana kuwagawa Mbowe na Katibu Mkuu wake Dk. Willibrod Slaa. Yamefanyika mengi sana kuwachonganisha hawa watu muhimu wawili.
Kimsingi Dk. Slaa na Mbowe wamejitambulisha kama timu iliyoshikana na isiyoingilika na kuchonganishwa kirahisi. Imedhihirika kwamba huwezi kumshambulia Dk. Slaa, Mbowe akuache salama, vivyo hivyo huwezi kumgusa Mbowe usishambuliwe na Dk. Slaa.
CCM na serikali yake wamejitahidi sana kuwatenganisha bila mafanikio. Wamejitahidi sana kuyumbisha uongozi wao imeshindikana. Wamejitahidi kuwaghilibu kwa kuwanunua na kuwapa bakshishi haikuwezekana.
Wamewatisha na kuwafungulia kesi nyingi za jinai, bado haikufua dafu. Hawa watu si warahisi kuwanunua. Mbowe ni mfanyabiashara maarufu atanunuliwa kwa bei gani? Hana njaa wala hakuna jipya katika kula raha ambalo hajui.
Amezaliwa katika familia tajiri iliyojitosheleza. Hawezi kupagawa kwa maisha yoyote yanayoahidiwa na watu wasio na historia kama yake walioko CCM na serikalini.
Sasa mipango ya mapinduzi ndani ya chama inafanywa na kufadhiliwa na CCM na serikali yake. Wamejazwa mamluki na wasaliti wengi ndani ya CHADEMA kwa lengo la kuwaondoa madarakani ili CCM iwe salama.
Mamluki hawa wamejazana kuanzia makao makuu, Kamati Kuu, uongozi wa mikoa hadi wilaya zote nchini.
Wanatangaza kwamba chama kimegubikwa na ukabila, ukanda na udini. Hizo ni propaganda za CCM zenye lengo la kuwaondoa watu walioshindwa kuwarubuni na kuwanunua ili waweke watu ambao wananunulika kirahisi.
Wanataka waweke watu ambao watafuata maagizo ya CCM na serikali yake namna ya kuendesha siasa za upinzani.
Kwa hakika leo kama CCM ikifanikiwa kumwondoa Mbowe, Dk. Slaa na CHADEMA basi itapumua kwamba kikwazo kikubwa cha kupoka demokrasia kimeondoka.
Ni vizuri kujiuliza kama Mbowe amefanya kazi nzuri kuiimarisha CHADEMA na kuifanya kufikia hatua sasa tunajiamini kwamba inakwenda kuiondoa CCM madarakani, kwanini wanatokeza watu wanaopiga kelele sana kwamba aondoke?
Kwanini wapiga kelele hawa wanasaidiwa sana na CCM? Mbona vyombo vya habari vinavyowatetea sana ni vya CCM na watu wake?
Tunajua na ni ukweli usio na chembe ya uongo kwamba tatizo kwa CCM sio CHADEMA bali ni Freeman Mbowe.
Tulianza na Mungu tunaendelea na Mungu na tutamaliza na Mungu. Kwa mkono wa Mungu tutashinda.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
*************************************************************************************** *************************************************************************************** This e-mail and any attachments are proprietary to NMB PLC. Any unauthorized use or interception is illegal. The views and opinions expressed are those of the sender, unless clearly stated as being those of NMB PLC. This e-mail is only addressed to the addressee and NMB PLC shall not be responsible for any further publication of the contents of this e-mail. If this e-mail is not addressed to you, you may not copy, distribute or disclose the contents to anyone nor act on its contents. If you received this in error, please inform the sender and delete this e-mail from your computer.

0 comments:

Post a Comment