Sunday 2 September 2012

[wanabidii] Taarifa Ya Jeshi la Polisi Kabla ya Vurugu Baina ya Wafuasi wa Chadema katika kijiji cha Nyololo, Mufindi,Iringa

JESHI la polisi mkoa wa Iringa limesema limezuia mikutano ya vyama vya siasa kwa vyama vyote na sio kwa chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) pekee hivyo laonya vyama vyote kutii sheria bila shuruti.

Hata hivyo jeshi hilo la Polisi limesema kuwa halifanyi kazi kwa matakwa ya chama chochote cha siasa na kuwa si kweli kama wanavyodai viongozi wa Chadema kuwa jeshi la polisi linatumiwa na chama cha mapinduzi (CCM) kuzuia mikutano hiyo.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Michael Kamuanda ametoa kauli hiyo leo ofisini kwake alipozungumza na waandisha wa habari kuhusu zuio la mkutano wa Chadema uliopangwa kuanza leo katika wilaya ya Mufindi.

" Nawatangazia wanasiasa na vyama vyote vya siasa pamoja na wananchi wa mkoa wa Iringa kuwa hakutakuwa na mikutano ya kisiasa kutokana na shughuli za sensa zinazoendelea ....hivyo basi nawaomba wananchi wote kutoshiriki mikutano yoyote ya kisiasa itakayoitishwa na wanasiasa "alisisitiza

Kuwa mikutano hiyo imezuiliwa kwa kipindi hiki cha sensa kilichoongezwa hadi hapo tamko litakapotolewa tena na msajili wa vyama vya siasa John Tendwa kama alivyokwisha kutoa tamko la kuzuia shughuli hizo za vyama vya siasa kwa kipindi hiki cha sensa.

"Wananchi wote wa mkoa wa Iringa mnaombwa kutii sheria bila shuruti hii ni amri ....nawaombeni sana wananchi kutodanganywa na wanasiasa kwa kuvunja sheria "aliongeza kamanda huyo wa polisi.

Hata hivyo alisema kuwa kimsingi zoezi la sensa lilipaswa kuhitimishwa Septemba mosi mwaka huu ila kutokana na serikali kuongeza muda wa zoezi hilo bado jeshi hilo la polisi linazingatia maagizo ya Msajili wa vyama vya siasa kama alivyoyatoa kwa jeshi hilo.

Kamanda Kamuanda alisema kuwa jeshi hilo la polisi wala msajili wa vyama vya siasa hajazuia vyama vya siasa kuendelea na vikao vyao vya ndani kwa kipindi hiki na kuwa hata Chadema wakiwa mkoani Iringa wameendelea kufanya vikao vyao vya ndani katika kata mbali mbali za mkoa wa Iringa na hakuna mtu aliyewazuia kuendelea kufanya hivyo.

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

0 comments:

Post a Comment