Saturday 1 September 2012

[wanabidii] BARUA YA WAZI KWA RAIS WA DOLA YA ZANZIBAR DR. ALI MUHAMMED SHEIN

BARUA YA WAZI KWA RAIS WA DOLA YA ZANZIBAR DR. ALI MUHAMMED SHEIN

BISMILLAHI 'RRAHMANI 'RRAHIM

Kila sifa njema zinamstahikia Allah, Subhanah wa Taala, isofichika
kwake dhulma wala harudishi dua ya mwenye kudhulumiwa. Rehma na amani
zimshukie Mtume Muhmmad (s.a.w) kipenzi chake na cha umma, mtetezi wa
waliodhulimiwa hata kabla ya kupewa Utume.

Mhishimiwa Rais,

Kwa mapenzi makubwa, baada ya kuisoma kwa utulivu khutuba yako ya siku
tukufu ya Iddil Alfitri, nimelazimika kuandika barua hii kufuatana na
kauli mbiu ya Mtume Muhammad (s.a.w) inayosema:

"…Dini ni nasaha…nasaha kwa Allah (S.w.T) na ni nasaha kwa Mtume
(s.a.w.) na kwa viongozi wa Waislamu na kwa watu wote…"

Mh. Rais;
Ni kweli nchi yeti ya Zanzibar imechafuliwa jina lake kuwa ni nchi ya
amani kama ilivyogeuzwa nchi yetu na ndugu zetu na kufanywa kuwa ni
koloni lao baada ya mkoloni Mwingereza kutupa uhuru mwaka 1963 na kuwa
na kiti chetu Umoja wa Mataifa huku walimwengu wote wakishuhudia; kiti
ambacho kwa uwezo wake Allah atakirejesha karibuni na wewe ukiwa rais
wa Zanzibar au uliyemwakilisha kuweza kuketi juu yake Insha'allah na
sisi wananchi wako wa Zanzibar tukifurahikia jambo hilo adhimu.

Mh.Rais;
Ni kweli nchi yetu inatiwa dosari lakini si kweli kuwa wananchi wa
Zanzibar ndio wanaosababisha dosari hiyo na doa hilo la uvunjifu wa
amani; ushahidi wa maneno haya tutaupata tukirejea na kutizama kwa
jicho la uadilifu na insafu katika matukio tafauti. Kwa hakika
tukifanya hivyo tutagundua bila ya taabu kuwa Jeshi la Polisi la
Tanzania ndio wahusika wakuu na waanzilishi wa vurugu na uvunjifu wa
amani ya nchi yetu ya Zanzibar kwa mara zote tatu, nikimaanisha
machafuko yaliyotokea tarehe 25-26/5/2012 mjini Zanzibar na yale ya
kuhujumu waumini na kunajisi misiskiti tarehe 17/6/2012, Donge,
Mahonda na Mkokotoni pamoja na hujuma ya tarehe 20/7/2012 msikitini
pia dhidi ya Waislamu walokusanyika msikiti wa Mbuyuni kuwasalia ndugu
zao waliofariki kwa ajali ya meli ya Mv. Skaget. Waislamu tulihujumiwa
ndani ya msikiti. Jeshi la polisi halikusita hapo bali liliwaingilia
wananchi wanyonge mpaka ndani ya nyumba zao na kuwatendea matendo
haramiya ya chuki na uhuni na katika waliotendewa matendo hayo maovu
walikuwa wanawake na watoto wachanga. Polisi hao wakhalifu wa sharia
waharibifu wa amani walifika hadi ya kutupa mabomu ya madawa makali
ndani ya majumba ya raia bila ya kujali athari zitakazowasibu watoto
wachanga na wanawake wenye kunyonyesha. Iwapo jeshi la polisi
lililopewa jukumu la kulinda sharia, kuweka amani na kuwahami wananchi
na mali zao ndio wenye kuvunja shariakwa kuwahujumu watu bila ya
sababu, wananchi na haki zao zitalindwa na nani?

Mh.Rais;
Matokeo ya ukiukwaji wa sharia na haki za binadamu yaliyopelekea
kuiharibia nchi yetu ya Zanzibar sifa yake ya amani na utulivu
yamesababishwa na jeshi la polisi la Tanzania lililoacha kutekeleza
wajibu wake wa kutunza amani ya nchi yetu Zanzibar . La kusikitisha
zaidi ni kuwepo baadhi ya watendaji wako wa karibu wanaopotosha ukweli
na kuifanyia khiyana nchi yetu ya Zanzibar kwa kufikisha kwako taarifa
za uongo zilizopelekea kuitia doa na kuiharibu khutuba yako ilojaa
maneno matukufu ya Allah Subhanah wa Taala pamoja na mafunzo kutoka
Sunna za Mtume (s.a.w), khutuba ambayo ilitarajiwa kukemea dhulma za
jeshi la polisi dhidi ya Waiislam na nyumba tukufu za Allah (S.w.T)
iliyohujumiwa pamoja na wanawake na watoto wachanga ndani ya majumba
kama ulivotetea makanisa na kubainisha hatari na ubaya wa walioyachoma
makanisa hayo kwa lengo la kutaka kuanzisha fitna baina ya Waislam na
jirani zao Wakristo waliokaribishwa nchini Zanzibar na kuishi pamoja
nao miaka mingi kwa amani kiasi ambacho haijawahi kutokea Muislamu
kulitusi kanisa licha kulichoma moto, kwani hayo ni kinyume na mafunzo
ya dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Mh.Rais;
Watu wanaokuwa karibu na Rais ni watu muhimu sana katika kufanikisha
dhana ya uadilifu na utawala bora na wa haki usioogopa kukemea maovu
hata kama walotenda au kuteleza ni Jeshi la Polisi kwani pia wao ni
binaadamu siajabu kutenda makosa kwa maksudi seuze kuteleza, Allah
Sbhanah wa Taala anatwambia: "…Enyi mloamini kuweni wasimamizi wa
Allah wenye kushuhudia ukweli hata kama ni dhidi ya nafsi zenu…" Kwa
hivyo, kosa kubwa zaidi ni kuuficha ukweli au kumpotosha kiongozi wa
nchi hadi kufikia kuwashushia sifa wasiostahiki, wahuni ambao
waliwatendea ya uhuni na dhulma kubwa hata wanawake na watoto. Ni
khatari wadhulumiwa wanapofikishwa kumshtakia Mfalme wa Mbingu na
Ardhi juu ya dhulma wanazotendewa. Isitoshe, khiyana ya watu kamaa hao
wa karibu na viongozi kila inapojikariri khiyana hiyo inajenga hisiya
kwa wenyeji wa nchi hii ambao wengi wao ni Waislamu kuwa wanabaguliwa,
na sio wao tu bali hata kudharauliwa nyumba zao tukufu za ibada na
kuthaminiwa makanisa peke yake. Sisi Waislamu hatutaki nyumba zozote
za ibada zidharauliwe. Nyumba zote za ibada lazima ziwekewe hishima
zinazostahiki.

Mh.Rais;
Kwa heshma zote naomba zichunguzwe sana sifa mbili kwa watu wote wa
karibu na viongozi, sifa mbazo ni hatari kuzikosa tena zinaweza
kuiangamiza nchi yetu tukufu ya Zanzibar . Sifa hizo si nyengine illa
ni ukweli na uaminifu ambazo ni kinyume na uwongo na khiyana.

Yarabbi Muumba Mbingu na Ardhi, usieshindwa na jambo, tunakuomba
muhifadhi Rais wetu, turejeshee nchi yetu kwa salama na amani, DOLA
HURU YA ZANZIBAR, wastiri wanawake na watoto wachanga majumbani na
Wazanzibari wote tunaodhulumiwa kwa kudai uhuru wa nchi yetu ya
Zanzibar uloporwa na jirani zetu, ndugu zetu baada ya kutoka kwa
wakoloni.

Amir Mkuu, Jumuiya ya Maimamu Zanzibar
Farid Hadi Ahmed

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment